Na Mwandishi Maalum,Mpanda –Katavi
Idadi ya kubwa ya mahabusu wanaotuhumiwa kwa kesi za mauaji waliopo katika Gereza Mahabusu Mpanda, Mkoani Katavi, imewashangaza Makatibu Wakuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Utumishi na Utawala Bora na Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, ambapo sasa wanakusudia kuunda Timu Maalamu itakayofuatilia pamoja na mambo mengine kwa nini Mkoa huo una watuhumiwa wengi kiasi hicho.
Makatibu wakuu hao waliupata mshangao huo mwishoni mwa wiki wakati walipotembelea Gereza Mahabusu la Mpanda ambako walipata fursa ya kuzungumza na wafungwa na mahabusu wa gereza hilo.
Makatibu Wakuu Sifuni Mchome, Laurian Ndumbalo, na John Jingu wapo katika ziara ya kikazi ya kawaida ya kutembelea Mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi ambapo wamejionea hali halisi ya mnyororo wa utoaji HakiJinai,changamoto zinazowakabili watumishi wa serikali na changamoto za maendeleo na ustawi wa jamii.
“Hebu wenye kesi za wizi nyosheni mikono, wenye kesi za ubakaji nyosheni mikono, wenye kesi za mauaji nyosheni mikono ” akaamuru Katibu Mkuu Mchome.
Katika wafungwa na mahabusu walionyosha mikono yao kulingana na makosa yao, robo tatu ya mahabusu hao walikuwa ni watuhumiwa wa kesi za mauaji.
Alipowauliza tena kwa nini kuna idadi kubwa ya mahabusu wenye kesi za mauaji. Walijibu kwamba wengi wao wamembikiziwa kesi hizo, au walikamatwa katika zoazoa ya polisi na kubambikiziwa kesi hizo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Mkuu wa Gereza hilo SP Moses Mbesela , mahabusu wa kiume wenye kesi za mauaji na waliokuwa wanasubiria kikao walikuwa sabini na moja ( 71) na ambao kesi zao upelelezi unaendelea walikuwa themanini (80). Kwa upande wa Wanawake wenye kesi za mauaji na ambao wanasubiri kikao walikuwa sita (6) na wale ambao upelelezi unaendelea walikuwa watatu (3).
Kutokana na kauli hiyo, ndipo Katibu Mkuu Sifuni Mchome aliposema “ Cha msingi kuna matatizo hapa, tutaunda Timu Maalumu kuja hapa ili kuweza kuchambua kesi mbalimbali, kuna kesi nyingi za mauaji hapa”.
Akasema Timu hiyo pia itashughulikio malalamiko katika eneo la utawala bora na ustawi wajamii na akawashukuru wafungwa na mahababusu hao kwa michango ya hoja zao na kwa mifano michache ya kesi walizoziwasilisha kwao na kwamba watapata mahali pa kuanzia.
Kasema masuala mengine yatakayofuatiliwa ni pamoja na malalamiko ya kubambikiziwa kesi, uchukuaji wa mali za watuhumiwa na kwamba Timu hiyo itakapoundwa itafanya kazi yake kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Mchome, Timu hiyo maalumu itakuwa na wajumbe kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Kwa upande wake Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Laurian Ndumbalo atafuatilia na katika ngazi za juu baadhi ya malalamiko ya wafungwa na mahabusu, pamoja maombi yaliyowasilishwa na Mkuu wa Magereza Mkoa wa Katavi kuhusu upungufu mkubwa wa Maafisa na Askari magereza katika Mkoa huo.
Naye Katibu Mkuu, Maendeleo ya Jamaii, Jinsia, Wazee na Watoto, John Kingu yeye alisema, siyo jambo la kawaida kwa magereza moja kuwa na idadi kubwa kiasi hicho naye akaunga mkono kwamba kuna kila sababu ya kuunda Timu hiyo na kuangalia shida ipo wapi kwa sababu suala hilo linahusu ustawi wa jamii.
Makatibu Wakuu hao watatu wamemaliza ziara yao ya kikazi ya kawaida katika mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi ambapo na Jumatatu watamalizia ziara yao Mkoani Tabo
Imetolewa na Maura Mwingira
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇