LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jul 26, 2025

INEC YAZINDUA RATIBA YA UCHAGUZI MKUU 2025, IDADI YA WAPIGA KURA YAPAA KWA ASILIMIA 26.55 , POLISI WAKABIDHIWA MAJINA YA WALIOJIANDIKISHA MARA MBILI

Na Mwandishi Maalum, INEC, Dodoma

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imezindua ratiba ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 na kutangaza kuwa jumla ya wapigakura 37,655,559 wamejiandikisha kushiriki katika huo ikiwa ni ongezeko la asilimia 26.55 kutoka wapigakura milioni 29.7 waliokuwa wamejiandikisha mwaka 2020.

Mwenyekiti wa INEC, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani Jacob Mwambegele, ametoa taarifa hiyo leo Julai 26, 2025,  wakati wa hafla ya uzinduzi huo wa ratiba ya Uchaguzi Mkuu,
iliyofanyika Kao Kuu la Tume, Njedengwa jijini Dodoma, na kusema pia maandalizi ya uchaguzi huo yanaendelea vizuri kwa kuzingatia misingi ya uwazi, haki na sheria za nchi. 

 

Amesema kwa mujibu wa raiba hiyo Oktoba 29, 2025 ndio siku ya Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Madiwani kwa Tanzania Bara.

 

Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani  Jaji Mstaafu Mwambegele amesema Agosti 9, 2025 hadi Agosti 27, 2025 itakuwa utoaji wa fomu za uteuzi wa wagombea wa kiti cha Rais na Makamu wa Rais, Agosti 14, 2025 hadi Agosti 27, 2025 itakuwa utoaji wa fomu za uteuzi wa wagombea ubunge na udiwani na Agosti 27, 2025 itakuwa siku ya uteuzi wa wagombea Urais na Makamu wa Rais, uteuzi wa wagombea ubunge na uteuzi wa wagombea udiwani.

 

Amesema, Agosti 28, 2025 hadi Oktoba 28, 2025 kitakuwa kipindi cha kampeni za uchaguzi kwa Tanzania Bara, Agosti 28, 2025 hadi Oktoba 27, 2025 kitakuwa kipindi cha kampeni za Uchaguzi kwa Tanzania Zanzibar ili kupisha kura ya mapema na Oktoba 29, 2025 siku ya Jumatano itakuwa ndiyo Siku ya Kupiga Kura.

 

Amesema kwa upande wa Zanzibar, Wapiga Kura 725,876 wapo katika Daftari la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) na wapiga kura 278,751 wameandikishwa na INEC kwa kuwa hawakuwa na sifa za kuandikishwa na ZEC.

 

“Katika idadi ya wapiga kura 37,655,559 waliopo katika daftari, wapiga kura 36,650,932 wapo Tanzania Bara na wapiga kura 1,004,627 wapo Tanzania Zanzibar,” amesema Jaji Mwambegele.

 

Ameongeza kuwa kati ya wapiga kura hao, 18,943,455 ni wanawake sawa na asilimia 50.31 na wapiga kura 18,712,104 ni wanaume sawa na asilimia 49.69 na wapiga kura 49,174 ni watu wenye ulemavu.

 

Jaji Mwambegele amesema jumla ya vituo 99,911 vitatumika kupigia kura ambapo vituo 97,349 vitatumika kwa ajili ya kupigia kura kwa Tanzania Bara na vituo 2,562 vitatumika kwa ajili ya kupigia kura kwa Tanzania Zanzibar.

 

“Idadi hii ya vituo 99,911 ni sawa na ongezeko la asilimia 22.49 ya vituo vya kupigia kura 81,567 vilivyotumika katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020,” amesema.

 

Jaji Mwambegele ametoa mwito kwa wadau wote ikiwa ni pamoja na wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi kwa kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na maelekezo yatakayotolewa na Tume. 


Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi rasmi wa kalenda ya uchaguzi Mkuu 2025 katika hafla iliyofanyika Ofisi za Tume Njedengwa Jijini Dodoma Julai 26,2025. Pamoja nae ni Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye pia ni Katibu wa Tume, Ndg. Kailima Ramadhani.

Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufani Jacobs Mwambegele akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa kalenda ya uchaguzi Mkuu 2025 katika hafla iliyofanyika Ofisi za Tume Njedengwa Jijini Dodoma Julai 26,2025. Pamoja nae ni Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye pia ni Katibu wa Tume, Ndg. Kailima Ramadhani.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Ndg. Kailima Ramadhani akimkabidhi nakala ya orodha ya wananchi waliojiandikisha zaidi ya mara moja ambapo ni kinyume cha sharia ili Jeshi la Polisi liweze kuchukua hatua dhidi yao. Anaepokea nakala hiyo kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi ni Mkakuzi Msaidizi wa Polisi Zakaria Makanja Aron.




Baadhi ya viongozi kutoka vyama mbalimbali vya siasa vilivyohudhuria hafla ya uzinduzi wa uzinduzi rasmi wa kalenda ya uchaguzi Mkuu 2025 katika hafla iliyofanyika Ofisi za Tume Njedengwa Jijini Dodoma Julai 26,2025. Pamoja nae ni Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye pia ni Katibu wa Tume, Ndg. Kailima Ramadhani. (Picha zote na INEC). 

No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages