JUKWAA HURU LA WAZALENDO LATOA TAMKO KUHUSU RAIS DK. MAGUFULI NA WABUNGE

Wednesday, November 25, 2015

Baada ya Rais Dk. John Magufuli kuonyesha dhamira yake ya thati kutaka kuliinua taifa la Tanzania kutoka katika lindi la umasikini katika nyanja mbalimbali, kwa kupunguza gharama zisizo za lazima ikiwemo fedha zinazoangamia katika posho, sherehe na safari za nje, Leo Jukwaa Huru la Wazalendo limejitokeza kumuunga mkono kwa kutoa tamko zito. Pichani, Mwenyekiti wa Jukwaa hilo, Ally Salum Hapi akizungumza na Waandishi wa habari leo katika hoteli ya Travertine, Magomeni jijini Dar es Salaam akiwa na Katibu wake, Mtela Mwampamba (kulia).

IFUATAYO NI TAMKO HILO KAMA LILIVYOSOMWA NA VIONGOZI HAO.

JUKWAA HURU LA WAZALENDO
TAMKO LA JUKWAA KWA VYOMBO VYA HABARI

Ndugu Wanahabari,

Mbele yenu sisi tuliowaita hapa ni Jukwaa Huru la Wazalendo ambalo limeitisha mkutano huu ili kufikisha yale tuliyoyakusudia kuwaeleza umma wa watanzania.


Sote tunatambua kuwa nchi yetu imetoka katika uchaguzi mkuu ambao umetupatia viongozi wapya wa awamu ya tano ya uongozi wa taifa letu chini ya Dr. John Pombe Joseph Magufuli. Tunapenda kuwapongeza watanzania wote kwa uchaguzi wa amani na utulivu. Aidha kwakua ndio mara yetu ya kwanza kuzungumza nanyi tunapenda kuwapongeza wanahabari wote kwa kazi nzuri ambayo mmekua mkiifanya kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu nchini. Tunawashukuru sana.

Mkutano wetu huu umebeba madhumuni makubwa mawili.
Kwanza ni kumpongeza Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa  hotuba yake aliyoitoa Bungeni siku ya ufunguzi wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 19/11/2015. Tunaiunga mkono Hotuba yake ambayo kwa kweli ilikuwa imebeba Uzalendo, Ujasiri, dira ya kweli ya maendeleo ya taifa letu na muuelekeo mpya wa Serikali ya awamu ya tano. Mambo yote aliyozungumzia Mh. Rais yamebeba maslahi mapana ya nchi yetu na yanalenga kuijenga Tanzania mpya ambayo waasisi wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Abeid Amani Karume walikusudia kuijenga.

Pili, pamoja na mambo mengi yaliyogusiwa na hotuba ya Mh. Rais, eneo la kubana matumizi na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kwa Serikali ni  moja katika mambo ambayo Jukwaa hili limeamua kuyaunga mkono kwa vitendo. Mh. Rais alitoa mchanganuo wa eneo moja tu la safari za nje na jinsi lilivyo ligharimu Taifa mabilioni ya shilingi na kuahidi kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wake itajikita katika kupunguza matumizi yasiyo ya lazima.

Aidha Mh. Rais ameanza kutekeleza kwa vitendo ahadi yake hiyo ya kupunguza matumizi yote yasiyo ya lazima Serikalini, ikiwemo hafla, warsha, makongamano na safari za nje.

Jukwaa Huru la Wazalendo, linatambua kuwa kwa miaka kadhaa mbunge wa Kigoma Mjini Mh. Zitto Kabwe amekuwa na msimamo wa kutokupokea posho za kitako tangu akiwa mbunge wa Kigoma Kaskazini katika Bunge la 10. Pamoja na mh. Zitto, Jukwaa pia limepokea taarifa za baadhi ya wabunge wa Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walioamua kuunga mkono juhudi za Mh. Rais za kupunguza matumizi yasiyo ya lazima serikalini kwa kukataa hadharani kupokea posho ya kitako ya mbunge (sitting allowance).

Mnamo tarehe 23/11/2015, mbunge wa Singida Magharibi (CCM) Mh. Elibariki Imanuel Kingu alimwandikia barua Katibu wa Bunge akieleza msimamo wake wa kukataa kulipwa posho ya kitako ya Bunge (sitting allowance) katika kipindi chote cha miaka mitano (2015 -  2020). Huyu anakuwa ni mbunge wa pili baada ya Mh. Zitto Kabwe kutoka hadharani na kukataa posho ambazo msingi wake ni unyonyaji wa wanyonge na ubadhirifu wa kodi za wananchi.


Jukwaa linapenda kumpongeza Mh. Kingu Mbunge kwa ujasiri wake na Uzalendo kwa Taifa lake, uliomfanya kuunga mkono juhudi za Mh. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa vitendo.
Jukwaa linatambua ya kwamba, mapambano ambayo Mh. Kingu Mbunge ameyaanzisha ni makubwa, magumu na yanahitaji kuungwa mkono na watanzania wote wanaoipenda nchi yao bila kujali itikadi za vyama. Tunafahamu, wapo baadhi ya wabunge wabinafsi na wasio na huruma na wanyonge wa Taifa letu ambao hawajafurahishwa na hatua hii ya wabunge kama Zitto na Kingu ya kukataa posho ya kitako. Baadhi ya wabunge wameanza kumpigia simu na kumtumia jumbe (sms) za vitisho mh. Elibariki Kingu (MB) na wengine wakibeza kuwa anatafuta cheo.

Jukwaa linalaani hatua za wabunge hao wanaopinga nia njema ya Mh. Elibariki Kingu na Mh. Zitto Kabwe kwa uamuzi wao wa kukataa posho za kinyonyaji na hivyo basi, Jukwaa linawaomba wananchi wote majimboni, kuwataka wabunge wao waliowachagua kueleza misimamo yao hadharani juu ya kuunga mkono hatua ya kukataa posho kama njia ya kupunguza matumizi ya Serikali yasiyo ya lazima.

Jukwaa linafahamu ya kwamba, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiye mwenye mamlaka ya mwisho ya kuidhinisha masharti ya kazi za kibunge na stahiki wanazopaswa kulipwa katika kazi hiyo.


Kwa heshima na unyenyekevu mkubwa, tunamuomba na kumshauri Mh. Rais John Pombe Magufuli atakapokuwa anaidhinisha masharti na stahiki hizo, atusaidie kuifuta kabisa posho ya kitako ya wabunge (sitting allowance).


Aidha, Jukwaa linamuomba mh. Rais kuzipitia na kutoa agizo la kufutwa kwa posho zote zisizo za lazima zinazolipwa kwa watumishi wa umma wa kada mbalimbali yakiwemo mashirika ya umma.

Jukwaa letu linatoa wito kwa wabunge wote bila kujali vyama vyao, kuungana na Mh. Kingu(MB) na Mh. Zitto(MB) katika kukataa malipo ya posho ya kitako ili kupunguza mzigo mkubwa ambao Serikali inaubeba kuhudumia wabunge. Fedha hizi ni vyema zielekezwe katika kutatua kero za wananchi vijijini kama vile ukosefu wa maji, madawati, vitanda vya Hospitali n.k.

Tunasisitiza kwamba, Ubunge ni Utumishi,na wala sio Utukufu. Kazi ya Mbunge ni kuwawakilisha wananchi wake na si kuwanyonya. Tufike mahali kama Taifa tuwe na nidhamu ya matumizi ya kodi za wananchi na mgawanyo sawa wa keki ya Taifa. Kuendelea kulipana posho hizo ni ishara ya unyonyaji, dhuluma na kuongeza pengo kati ya wenye nacho na wasionacho nchini. Jambo hili linakuza chuki na hasira miongoni mwa wananchi wa hali ya kawaida dhidi ya viongozi wao na serikali kwa ujumla.

Tunawaahidi kuwa Jukwaa litaendeleza harakati (movement) na vuguvugu hili kwa kuanzia na Bunge kwasababu ndio wawakilishi wa wananchi. Tutaendelea kupaza sauti zetu ili wabunge wengi zaidi Wazalendo wajitokeze na kukataaa posho hizi. Tunajua kuwa wapo miongoni mwao wabunge wazalendo ambao wataguswa na wito huu na kuuunga mkono hadharani.


Aidha tutaendelea kuwasemea kwa wananchi wabunge ambao bado hawataki kukataa posho hizi bila kujali vyama vyao. Tunawaomba wananchi kote nchini kutuunga mkono katika harakati hizi ili tuweze kuokoa mabilioni ya shilingi yanayopotea kila Bunge linapokaa Dodoma kupitia posho ya kitako (sitting allowance).
Ahsanteni sana.

ALLY SALUM HAPI  - MWENYEKITI (0714 193161
MTELA MWAMPAMBA  - KATIBU   (0755 178927)

MBUNGE AYSHAROSE AUNGA MKONO UAMUZI WA RAIS DK. MAGUFULI KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA UHURU MWAKA HUU

MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe, amesema Rais Dk. John Magufuli ni kiongozi mwenye kujali maslahi ya Watanzania hivyo maamuzi ya kuwataka wananchi kusherehekea kumbukumbu ya Uhuru kwa kufanya kazi na usafi, umeonyesha dhamira safi ya kiongozi huyo kwa wananchi.

Amesema, uamuzi huo umejali maslahi ya taifa kwa sababu fedha nyingi zingetumika kwenye masuala yasiyokuwa na ulazima kwa wananchi.


Pia, ametoa rai kwa watumishi na viongozi wenzake wa serikali kufanyakazi kwa kuwatumikia wananchi ili kuendana na kasi ya Rais Dk. Magufuli.


Akizungumza Dar es Salaam jana, Aysharose alisema, kuzuiliwa kwa fedha hizo kutumika kwenye sherehe za Uhuru ni sahihi kwa sababu baadhi ya watu wamekuwa wakijinufaisha.


Hivyo uamuzi ya Rais Dk. Magufuli ya kupangia fedha hizo matumizi  mengine hususan kuboresha huduma za afya ni wakuungwa mkono.


Aysharose alisema, badala ya fedha hizo kutumika kuwahudumia wageni, kupamba maeneo mbalimbali yatakayotumika kwenye sherehe hizo na kununulia mashati sasa zitatumika kwenye sekta ambayo inaumuhimu kwa maisha ya Watanzania.


“hospitali zetu bado hazina madawa ya kutosha, wahudumu wa afya pia wanafanyakazi kwenye mazingira magumu, shule hazina madawati ya kutosha lakini pia maslahi ya walimu sio mazuri hivyo fedha hizo zitasaidia kuboresha huduma hizo” alisisitiza.


Alisema anaunga mkono maamuzi hayo ya Rais kwa sababu fedha hizo zinakwenda kutatua changamoto wanazokabiliana nazo wananchi.


Mbunge huyo wa viti maalum alibainisha kuwa, baadhi ya watumishi wa umma wamekuwa wakitumia sherehe hizo kujinufaisha binafsi kwenye shughuli yenye kufanyika kwa siku moja.


“Hatuwezi kutumia fedha za walipakodi kwa matumizi yasiyokuwa endelevu hivyo kwa msingi huo, maamuzi ya Rais yamejikita kutumia fedha hizo kwa maendeleo endelevu” alibainisha.


Aysharose ambaye anawawakilisha wanawake wa mkoa wa Singida bungeni, alisema serikali ya awamu ya tano ni ya ukombozi kwa sababu Rais Dk. Magufuli ni imara na mwenye kujali maslahi ya wanyonge.


Alisema Rais. Dk. Magufuli ni mwajibikaji na hatowaonea huruma viongozi wabadhirifu na wala rushwa.


“Serikali ya wamu ya tano inaongozwa na kiongozi mwenye kujali maslahi ya wananchi, wenye uchungu kwa kutaka kufikia maendeleo ya kiuchumi na anadhamira safi ya kuwatumikia Watanzania kwa kuwakomboa wanyonge,” alisema.


Alisisitiza kuwa, Rais Dk. Magufuli, hatoweza kufumbia macho vitendo vitakavyorudisha nyuma maendeleo ya nchi hivyo watumishi wa umma wasiowajibika wanapaswa kukaa chonjo.


Juzi Rais Dk. Magufuli, alizuia kufanyika kwa sherehe za Uhuru Desemba 9 mwaka huu na kuamuru siku hiyo itumike kufanya kazi ikiwemo usafi kwenye maneneo mbalimbali nchini ili kukabiliana na ugonjwa wa kipindipindu.


Kwa mujibu wa agizo hilo la rais lililotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, Rais alisema wananchi hawapaswi kusherehekea miaka 54 ya Uhuru wa Tanzania Bara, huku wakiendelea kufariki kwa ugonjwa huo unaosababishwa na uchafu.


Aliamuru fedha zilizokuwa zitumike kugharamia sherehe hiyo zitapangiwa matumizi mengine ya maendeleo hususan kuboresha huduma za afya.


Uamuzi huo wa rais umeendelea kuungwa mkono na wananchi kwa sababu imechukuliwa ili fedha hizo zitumike kwenye masula muhimu zaidi yenye maslahi ya taifa.

MAKAMU WA RAIS MHE.SAMIA SULUHU HASSAN AKUTANA NA UONGOZI WA MTANDAO WA WANAWAKE TANZANIA

Tuesday, November 24, 2015


 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Uongozi wa Mtandao wa Wanawake Tanzania (WFT) wakati viongozi hao walipofika Ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam,leo Nov 24, 2015 kwa mazungumzo. Picha na OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi wa Mtandao wa Wanawake Tanzania (WFT) baada ya mazungumzo yao yao yaliyofanyika Ofisini kwa Makamu Ikulu jijini Dares Salaam, leo Nov 24, 2015. Picha na OMR
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo amekutana na uongozi wa Mtandao wa Wanawake na Katiba Tanzania (WFT) ambapo amezungumzia dhamira ya serikali katika kuyatafutia ufumbuzi matatizo mbali mbali yanayowakabili wanawake na watoto wa kike nchini.
Katika mazungumzo hayo Makamu wa Rais aliueleza ujumbe huo kuwa wakati wa kampeni aliahidi pamoja na kazi za kumsaidia Mhe. Rais bado kama mama atafuatilia kwa karibu utekelezaji wa ahadi ya kupatikana kwa maji safi na salama, kuboresha afya ya mama na mtoto, elimu na mazingira.
“Nilipokuwa kwenye kampeni nimejionea shida ya maji na wanawake ndiyo wanaopata tabu ya kutembea mwendo mrefu kutafuta maji. Kwa hiyo, pamoja na kazi zangu za kumsaidia Mhe. Rais nitasimamia miradi yote ya maji, alau tuhakikishe maji yanapatikana umbali wa mita 400 kutoka eneo wananchi wanakoishi au karibu zaidi”.
Alisema kinachofurahisha zaidi suala la maji liko kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na miradi mingi ikiwemo ya kuchimba visima virefu katika mikoa kama vile ya Singida na Dodoma iko kwenye mchakato na cha msingi ni kusimamia fedha zinatumika kuleta maji kama ilivyokusudiwa.
Kuhusu afya ya mama na mtoto alisema kazi hiyo ataianza hivi karibuni kwa kushirikiana na Mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotetea haki za wanawake ili kupunguza vifo vinavyosababishwa na mimba za utotoni.
“Hili tutajitahidi kulipunguza kwa kiasi kikubwa na hasa baada ya serikali ya Awamu ya Nne kusema kwamba shule ya msingi ya lazima ni kutoka darasa la kwanza hadi kidato cha nne”, alisema na kuongeza
“Katika kipindi hicho binti atakuwa amefikisha miaka 17, atakuwa tayari kukabiliana na mambo ya uzazi tofauti na ilivyo sasa ambapo anamaliza darasa la akiwa mdogo na matokeo yake anapata mimba katika umri mdogo. Mtusaidie kupiga debe huko nje utekelezaji uweze kufanikiwa.”
Hata hivyo, alisisitiza kusimamia suala la kuhakikisha zahanati, vituo vya afya na hospitali nchini zinakuwa na dawa na vifaa tiba vya kutosha katika wodi za wazazi kwa ajili ya kuhudumia akina mama na wananchi kwa ujumla ambao wengi wanaonekana ni watiifu kwa serikali yao.
Kwa upande wa elimu Mhe. Samia alisema atasimamia ujenzi wa mabweni kwa watoto wa kike na kuhakikisha mazingira yanatunzwa kwa sababu uharibifu wa mazingira ndiyo umekuwa chanzo cha upungufu wa maji nchini.
Aidha aliuambia ujumbe huo kuwa hivi sasa tuna mpango wa kuimarisha utendaji serikalini kuanzia serikali kuu hadi serikali za mitaa ili kinachopatikana kidogo kimfikie kila mwananchi.
“Tutaendelea kuaihirisha sherehe ili fedha hizo ziweze kutumika kwa mambo ya kijamii. Kwa msimamo huu amabao Mhe. Rais ameanza nao labda watu wote tushirikiane kwa kutatua matatizo yetu kwa gharama nafuu kwa ufanisi mkubwa.”
Mapema akizungumza kwa niaba ya wenzake Mwenyekiti wa Mtandao huo Prof Ruth Meena alimpongeza Mhe. Samia kwa kushika nafasi ya juu ya uongozi akiwa mwanamke wa kwanza kuweka historia katika Tanzania.
Alimweleza Mhe. Makamu wa Rais matarajio yao kwa serikali ya Awamu ya Tano kuwa itatetea misingi ya haki na usawa katika Nyanja zote.

Imetolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais
Dar es salaam
24/11/2015

MAPITIO YA MAGAZETI NA SIMU TV

Monday, November 23, 2015

 SIMU.TV: Kasi ya Rais Magufuli yaanza kuitikiwa huku watumishi wakiaswa kutii falsafa ya hapa kazi tu, Aliyeokolewa mgodini afariki dunia, kwa mapitio yadondoo za habari hizi magazetini:BOFYA HAPA

SIMU.TV:  UVCCM walia na UKAWA kumsusia Rais Magufuli, Mchujo NECTA kuanzia darasa la 2. Pata dondoo za magazeti ya leo:BOFYA HAPA

SIMU.TV: Wabunge wagonga mwamba kwa Rais Magufuli , Muhimbili hakukaliki, Mawaziri sura mpya zatawala. Dundika na Dondoo za magazeti ya leo.BOFYA HAPA

SIMU.TV: Yanga Wamzingua Mzungu Simba, St. George waamua kumrudisha Mart Noorj, Maguli aipaisha Kilimanjaro Stars Ethiopia;BOFYA HAPA

KINANA AONGOZA UJUMBE WA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA VYAMA VYA SIASA KUSINI MWA AFRIKA MJINI MAPUTO,MSUMBIJI


Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Komredi Abdulrahman Kinana katikati ya wiki iliyopita aliongoza ujumbe wa Tanzania nchini Msumbiji kuhudhuria mkutano wa Vyama vya Siasa Kusini Mwa Afrika. 
Mkutano huo uliohudhuriwa na baadhi ya Wenyeviti na Makatibu Wakuu wa vyama  hivyo, umemalizika mwishoni mwa wiki mjini Maputo kwa mafanikio makubwa.
Mkutano huo ulijadili masuala yaliyolenga kutatua changamoto mbalimbali za mataifa hayo na mipango ya maendeleo kwa ujumla.
Baadhi ya viongozi wa vyama hivyo vya siasa waliohudhuria ni pamoja na Mwenyekiti wa ANC ya Afrika Kusini Rais Jacob Zuma, Mwenyekiti wa FRELIMO ya Msumbiji Rais Filipe Nyusi, Mwenyekiti wa SWAPO ya Namibia Rais Hage Geingob pamoja na Komredi Kinana na ujumbe wake.
Ujumbe kutoka Tanzania ulioongozwa na Komredi Kinana umewajumuisha Katibu wa NEC anayeshughulikia Siasa na Mambo ya Nje Dkt. Asha-Rose Migiro pamoja na Makatibu Wakuu wa Jumuiya za CCM.
 Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman  Kinana (kulia)akiwa kwenye picha ya pamoja na Zuma Mwenyekiti wa ANC ya Afrika Kusini Rais Jacob  (kushoto) na Mwenyekiti wa FRELIMO ya Msumbiji Rais Philipe Nyusi  (katikati)


 Katibu Mkuu wa CCM Ndg Abdulrahman Kinana akijadiliana jambo na Mwenyekiti wa Chama cha SWAPO cha Namibia Rais Hage Gengob,  katika mkutano wa viongozi wa vyama vya siasa
Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana (kushoto) akizungumza kwenye mkutano wa viongozi wa vyama vya siasa vya Kusini mwa Afrika mjini Maputo, Msumbiji.

Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana akiwa na Makatibu Wakuu wa vyama vya ANC, FRELIMO, MPLA, SWAPO na ZANU PF mjini Maputo.


PICHA ZA KUMBUKUMBU BAADA YA RAIS DKT JOSEPH MAGUFULI KUZINDUA BUNGE DODOMA

Sunday, November 22, 2015

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akisalimiana na wabunge muda mfupi baada ya kuhutubia na kuzindua rasmi Bunge la 11 mjini Dodoma Jumamosi Novemba 20, 2015
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akisalimiana na Spika Mstaafu Mhe Pius Msekwa huku Spika Mstaafu mwingine Mhe Anne Makinda akisubiri zamu yake muda mfupi baada ya kuhutubia na kuzindua rasmi Bunge la 11 mjini Dodoma Jumamosi Novemba 20, 2015
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akisalimiana na mmoja wa wabunge muda mfupi baada ya kuhutubia na kuzindua rasmi Bunge la 11 mjini Dodoma Jumamosi Novemba 20, 2015
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Marais wastaafu Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na Mhe. Benjamin William Mkapa  muda mfupi baada ya kuhutubia na kuzindua rasmi Bunge la 11 mjini Dodoma Jumamosi Novemba 20, 2015
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika picha ya pamoja na viongozi wakuu na wabunge muda  mfupi baada ya kuhutubia na kuzindua rasmi Bunge la 11 mjini Dodoma Jumamosi Novemba 20, 2015
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akisikiliza kwa unyenyekevu mawaidha toka kwa Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Alhaj Ali Hassan Mwinyi muda mfupi baada ya kuhutubia na kuzindua rasmi Bunge la 11 mjini Dodoma Jumamosi Novemba 20, 2015
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akiwa na Rais wa Zanzibar Dkt Ali Mohamed Shein,  Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Alhaj Ali Hassan Mwinyi, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe  Pandu Ameir Kificho  muda mfupi baada ya kuhutubia na kuzindua rasmi Bunge la 11 mjini Dodoma Jumamosi Novemba 20, 2015
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Waziri Mkuu Mhe Majaliwa Kassim Majaliwa wakijichanganya na wabunge kwenye mchapalo muda  mfupi baada ya kuhutubia na kuzindua rasmi Bunge la 11 mjini Dodoma Jumamosi Novemba 20, 2015
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Dkt Jakaya Mrisho Kikwete na Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo Mhe Zitto Kabwe muda mfupi baada ya kuhutubia na kuzindua rasmi Bunge la 11 mjini Dodoma Jumamosi Novemba 20, 2015

Picha na Muhidin Issa Michuzi wa Ikulu

BOFYA HAPA KWA PICHA ZAIDI

HOTUBA YA MHE. RAIS MAGUFULI YA KUZINDUA BUNGE MJINI DODOMA IJUMAA NOVEMBA 20, 2014HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI, AKIFUNGUA RASMI BUNGE JIPYA LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, DODOMA,
20 NOVEMBA 2015

MAGUFULI AHUTUBIA NA KULIFUNGUA BUNGE LA 11

Saturday, November 21, 2015 Rais Magufuli, aliwashukuru wananchi kwa mara nyingine kwa kumuamini na kumchagua, ambapo ameahidi kuwa kiongozi atakayewatumikia watu wote bila kubagua, na kwamba lengo lake ni kuhakikisha nchi ya tanzania inasonga mbele kimaendeleo.

Rais Magufuli  kwenye hotuba yake pia akaeleza malalamiko aliyoyapokea kwa wananchi ambayo yeye anaona ni kero kwa wananchi, maeneo ambayo anasema ni lazima yashughulikiwe ipasavyo ili kuleta uaminifu kwa wananchi.

Kuhusu Uchumi rais Magufuli amesema kuwa serikali yake itakuwa ni serikali ya viwanda itakayosimamia sheria na kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi unasimama kwa kujenga na kuendelea viwanda ili kutengeneza ajira zaidi.

katika hotuba yake pia, rais magufuli hakuacha kugusia suala la katiba mpya, ambapo amesema atahakikisha serikali yake inasimamia mchakato huo na kwamba safari hii utakamilika kwa wakati.
Rais Magufuli pia akagusia suala la Muungano pamoja na hali ya kisiasa visiwani zanzibar ambapo amesema yeye ni muumini mkubwa wa muungano uliopo na kwamba anaamini mgogoro wa Zanzibar uliojtokeza unatatuliwa kwa amani.

Kabla ya kuanza kwa hotuba yake bungeni, rais Magufuli alishuhudia vioja vya upinzani ambao walikuwa wakipiga kelele wakati viongozi wa zanzibar walipokuwa wakiingia bungeni bungeni, ambapo baadae spika wa bunge Job Ndugai alilazimika kutumia kiti chake kuwafukuza nje ya ukumbi wa bunge ili kupisha hotuba ya rais kuanza, jambo ambalo upinzani ulitii na kutoka nje.

NAPE NNAUYE AFANYA MAZUNGUMZO NA BALOZI WA NORWAY MJINI DODOMA

Friday, November 20, 2015

 Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi CCM Taifa Nape Nnauye  akizungumza na Balozi wa Norway Nchini Bi. Hanne - Marie Kaarstad kwenye ofisi za CCM Makao Makuu mjini Dodoma.
  Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi CCM Taifa Nape Nnauye  akimsindikiza Balozi wa Norway Nchini Bi. Hanne - Marie Kaarstad aliyemtembelea leo kwenye ofisi za CCM Makao Makuu mjini Dodoma.
 Katibu wa NEC Itikadi na Uenezi CCM Taifa Nape Nnauye  akiagana na Balozi wa Norway Nchini Bi. Hanne - Marie Kaarstad kwenye ofisi za CCM Makao Makuu mjini Dodoma.

SHEREHE ZA KUAPISHWA WAZIRI MKUU WA AWAMU YA TANO VIWANJA VYA IKULU NDOGO CHAMWINO MJINI DODOMA.

 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli akimuapisha Kassim Majaliwa Kassim kuwa Waziri Mkuu wa Tanzania baada ya uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni, hafla ya kiapo ilifanyika leo Ikulu ya Chamwino Mkoa wa Dodoma
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli akimkabidhi hati ya kiapo Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa Kassim  baada ya uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni, hafla ya kiapo ilifanyika leo Ikulu ya Chamwino Mkoa wa Dodoma
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli (katikati)akiwa katika picha ya pamoja na familia ya Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa Kassim (watatu kushoto mstari wa nyuma) baada ka kuapishwa rasmi leo katika viwanja vya Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma,[Picha na Ikulu.]

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Makamo wa Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan (kushoto) na Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa Kassim (kulia) baada ya kuapishwa  rasmi kushika wadhifa wake huo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli katika Ikulu ya Chamwino Mkoani Dodoma leo.


IDADI YA WANAOPERUZI