MAHAKAMA
Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa amri kuwa hakuna shabiki yetote
atakayeruhusiwa kuingia mahakamani hapo kusikiliza rufaa iliyokatwa na
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake saba kupinga hukumu
iliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Jaji Mfawidhi wa Kanda hiyo, Lameck Mlacha ametoa amri hiyo leo Aprili 28,2020 wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kutajwa.
Amri
hiyo imetolewa ikiwa ni njia moja wapo ya kuepukana na mikusanyiko
katika kipindi hiki ambacho nchi inapopambana na ugonjwa hatari la
Corona .
"Siku
ya usikilizwaji wa kesi wanaotakiwa kuwepo ni warufani wenyewe nane,
mawakili wao na mawakili wa upande wa wajibu rufani" amesema Jaji
Mlacha.
Hata hivyo, Jaji Mlacha amepanga kesi hiyo kuanza kusikilizwa mbele ya Jaji Elvin Mgeta Mei 13, mwaka huu.
Katika
rufaa hiyo namba 76 ya mwaka 2020 wakata rufani ni Mbowe, wengine ni
Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu-Zanzibar,
Salum Mwalimu, Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, Mbunge wa Tarime
Mjini, Esther Matiko, Halima Mdee (Kawe), John Heche (Tarime Vijijini)
na Ester Bulaya (Bunda).
Machi
10, 2020 Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliwahukumu warufani hapo
pamoja na Dk Vicent Mashinji aliyehamia CCM mwaka huu akitokea Chadema
alikokuwa katibu mkuu.
Hakimu
Mkazi Mkuu, Thomas Simba aliwahukumu kulipa faini ya Sh milioni 350 au
kifungo cha miezi mitano jela baada ya kuwatia hatiani kwa makosa 12
kati ya 13 yaliokuwa yakiwakabili.
Warufani hao kwa nyakati tofauti walilipa faini hiyo na kukwepa kifungo.
Mbowe na wenzake wanapinga
hukumu
iliyotolewa na Mahakama ya Kisutu kwamba imefanya makosa ya kisheria
kufikia maamuzi ya kesi ya msingi bila ya upande wa mashitaka
kuthibitisha pasipo shaka.
Wanadai Mahakama ya Kisutu ilikosea kisheria kushindwa kufanya mchanganuo mzuri kwa kufuata ushahidi uliotolewa.
Pia
wanadai mahakama imeshindwa kuainisha viini vya makosa dhidi ya
mashitaka na kuwahukumu bila kuzingatia utetezi wa washitakiwa.
Wanadai
mahakama imeshindwa kuzingatia ushahidi kwa kushindwa kuangalia uwepo
au ushiriki wa baadhi ya washitakiwa kwenye mkutano na kuwahukumu kwenye
mashitaka ya 2,3 na 4.
Warufani
hao wanadai mahakama hiyo ilikosea kupokea vielelezo vya kielektroniki
ambavyo ni video, imekosea kisheria kuzingatia mashitaka ya 11,12 na 13
yamewafanya washitakiwa washindwe kujitetea.
Mahakama
ilikosea kisheria kuangalia maneno yaliyotolewa katika mashitaka ya
5,6,7,8,9,10 kwamba hayawezi kuhesabika kuwa makosa ya jinai kwa mujibu
wa maamuzi yaliyotolewa katika kesi ya Hussein Katanga dhidi ya Jamhuri
(1974) ukurasa wa 97 wa hukumu hiyo.
Pia wanadai hakukuwa na maelekezo ya awali yaliyofanyika sambamba na kupuuzwa kwa haki ya uwakilishi.
Wanadai
mahakama imekosea katika kutoa adhabu dhidi ya warufani ya kulipa
faini ambayo ilikuwa inajitegemea wakati adhabu ya kifungo ilikuwa
inaenda kwa pamoja hali hiyo imesababisha kuleta mkanganyiko wa
kisheria.
Hata hivyo, warufani hao wanaiomba mahakama iamuru hukumu na adhabu iliyotolewa dhidi ya warufani ifutwe.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇