Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Manejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Msaafu) George Huruma Mkuchika (Mb) akizungumza wakati wa Mahafali ya 28 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika katika Kampasi ya Mbeya.
………………………………………………………………..
James Mwanamyoto – Dodoma
Waajiri katika Taasisi za Umma wenye watumishi ambao hawajapata mafunzo ya namna Serikali inavyofanya kazi, wametakiwa kuwapeleka watumishi hao kupata mafunzo Chuo cha Utumishi wa Umma mapema iwezekanavyo kabla ya kuchukuliwa hatua kwa kupuuza Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma 2009, kanuni ya G.1 (8).
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst.) Mhe. George Huruma Mkuchika (Mb) alipokuwa akisisitiza umuhimu wa Watumishi wa Umma kupata mafunzo ya namna Serikali inavyofanya kazi ikiwa ni pamoja na kupewa elimu juu ya miiko ya kiutendaji katika Utumishi wa Umma.
Mhe. Mkuchika amesema, Serikali haitosita kumchukulia hatua za kinidhamu mwaajiri yeyote ambaye hatawapeleka watumishi wake Chuo cha Utumishi wa Umma kupata mafunzo ya namna Serikali inavyofanya kazi kwani mafunzo hayo yanalenga kuwaongezea ufanisi wa kiutendaji.
“Kanuni G.1 (8) ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma 2009 inasema; kila mwajiri anawajibika kupanga na kusimamia mafunzo elekezi kwa watumishi wapya walioajiriwa, hivyo mtumishi wa umma akishaajiriwa kabla ya kuanza kutekeleza majukumu yake anapaswa kupata mafunzo ya namna Serikali inavyofanya kazi, kwa mantiki hiyo ni kosa kwa mwajiri kutompatia fursa hiyo ya mafunzo”, Mhe. Mkuchika amesisitiza.
Mhe. Mkuchika amefafanua kuwa, zamani hakukuwa na fursa kubwa ya watumishi kupata nafasi ya kujifunza utendaji kazi Serikalini katika Chuo cha Utumishi wa Umma, lakini hivi sasa chuo kina kampasi 6 ambazo ni Dar es Salaam, Mtwara, Tanga, Singida, Mbeya na Tabora hivyo ni wajibu wa waajiri kuwapeleka watumishi katika kampasi hizo.
Aidha, Mhe. Mkuchika amewapongeza Watumishi wa Umma kwa kazi nzuri ya ukusanyaji wa mapato, ambao umewezesha uboreshwaji wa miundombinu katika sekta za Afya, Elimu, Barabara na Reli hivyo kuboresha utoaji huduma kwa umma.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇