Charles James, Michuzi TV
WAKALA wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) umetakiwa kuhakikisha unajiendesha kibiashara pamoja na kutoa huduma bora kwa watanzania.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Kilimo, Joseph Hasunga leo jijini Dodoma alipokua akizindua Bodi ya Ushauri ya NFRA ambapo ameutaka wakala huo kufanya manunuzi kipindi hiki cha mavuno.
Ameutaka wakala huo kufanya manunuzi ya mazao kwa ajili ya kuhifadhi kama akiba kwenye maghala ya serikali lakini pia kwa ajili ya biashara kwa kutafuta masoko ndani na nje ya Nchi.
Waziri Hasunga amesema wakala huo una jukumu la kuhifadhi mazao ya kila aina na siyo kuchagua mazao ya kuhifadhi akitolea mfano Mahindi kuwa ndiyo yamekua yakipewa kipaumbele kulinganisha na mengine.
" Wakala wa hifadhi ya chakula mna wajibu wa kujiendesha kibiashara na kukuza mapato yetu kama zilivyo Taasisi zingine. Sitegemei kuona NFRA inahifadhi tu vyakula, mnapaswa mfanye biashara pia.
Mwaka huu kuna fursa za masoko mengi ya chakula. Kenya walipata changamoto ya Nzige hivyo uzalishaji wao hauwezi kuwa mzuri lazima watahitaji chakula kwetu, kuna Uganda, Malawi, Rwanda, Zambia, Zimbabwe na Congo wote hawa wanategemea chakula kutoka kwetu," Amesema Hasunga.
Ameitaka NFRA kuzitumia Balozi za Tanzania zilizopo kwenye Nchi zingine kutafuta soko la biashara ili waweze kuingia mikataba ya kuuza vyakula kwa wingi.
" Niwaagize pia kufuatilia maeneo ambayo yamekua yakiathirika na maafa mbalimbali kama Mvua na Maafuriko ni jukumu lenu kufanya utafiti huko na kuwapelekea chakula kwa bei nafuu," Amesema Hasunga.
Hasunga ameitaka bodi hiyo pia kufuatilia kwa kina mahesabu ya kifedha ya wakala, Mali na madeni ambayo Wakala inayo pamoja na fedha walizonazo ikiwa ni pamoja na kujua idadi ya watumishi na stahiki za mishahara na posho zao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Yustas Kongolle amemshukuru Waziri Hasunga kwa kuwaamini yeye na wajumbe wa bodi hiyo kiasi cha kuwateua kuhudumu kwa miaka mitatu huku akisema watafanya kazi kwa bidii.
" Kuaminiwa na Wizara maana yake Nchi imetuamini, tunaahidi kufanya kazi kwa bidii na kutimiza maagizo yote ambayo tumeelekezwa kufanya ikiwa ni pamoja na kuifanya NFRA ijiendeshe kibiashara," Amesema Mhandisi Kongolle.
Waziri
wa Kilimo, Josephat Hasunga akimkabidhi vitendea kazi Mwenyekiti wa
Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Mhandisi Yustas
Kongolle leo jijini Dodoma baada ya kuizindua bodi hiyo.
Waziri
wa Kilimo, Josephat Hasunga akizungumza kwenye mkutano wake na wajumbe
wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)
jijini Dodoma.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Taifa ya Ushauri wa Wakala wa Hifadhi ya Chakula, Mhandisi
Yustas Kongolle wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo jijini Dodoma leo.
Waziri
wa Kilimo, Joseph at Hasunga akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa
bodi ya ushauri ya wakala wa hifadhi ya chakula (NFRA) baada ya
kuzindua bodi hiyo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇