Na Khadija Khamis –Maelezo Zanzibar 28/04/2020.
WIZARA ya Afya Zanzibar imepokea msaada wa vifaa mbali mbali vya
kuthibiti maambukizi ya Corona kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO)
vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 110.
Akipokea msaada huo, huko Wizara ya Afya Mnazimmoja Mkurugenzi Mkuu
wa Wizara ya Afya Zanzibar Dkt Jamala Adam Taib amelishukuru shirika
hilo kwa kutoa msaada ambao utawasaidia wafanyakazi kutekeleza kazi
zao kwa ufanisi pamoja na kujikinga na maambukizi ya Corona
Alifahamisha kuwa Shirika la Afya Duniani linaendelea kuiunga mkono
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuonyesha mashirikiano ya pamoja
katika udhibiti na ufuatiliaji wa mwenendo mzima tokea mwanzoni mwa
Mripuko wa maradhi hayo kuanza .
Nae Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani Ghirmay Ande Michel
wakati akikabidhi vifaa hivyo amesema vifaa hivyo vimekusudiwa kutumika
katika kitengo cha mwenendo wa Kuratibu Maradhi ya Mripuko yakiwemo
(COVID -19).
Amesema vifaa hivyo ni vitendea kazi ikiwemo komputa za kisasa vifaa
vya thamani,Barakoa,vipima joto ,cloves,nguo maalumu za kujikinga na
maambukizi ya maradhi ya Corona na vyenginevyo .
Alifahamisha kuwa Shirika la Afya Duniani litaendelea kutoa misaada
mbali mbali ya kujikinga na maambukizi ya Corona na (COVID-19) Kwa lengo
la kupambana na mripuko huo ambao umeikumba Dunia.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇