MIONGO sita iliyopita, uchumi wa Zanzibar, ulitegemea zao la karafuu. Lakini, kadri miaka ilivyosonga mbele, uzalishaji wa zao hilo ulikuwa unapungua.
Hivyo, ilibidi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kutafuta njia mbadala ya kukuza uchumi wa nchi. Mbadala uliopatikana ni kuendeleza utalii ili kujenga uchumi.
Serikali ya awamu ya nane,chini ya Rais Dk. Hussein Mwinyi,ilipoingia madarakani 2020,ilikuja na Ajenda ya Uchumi wa Buluu.Hili ni eneo pana linalohusu uvuvi,utalii na mengineyo.
Katika kipindi hiki kifupi cha utekelezaji wa uchumi wa buluu, Rais Dk. Mwinyi ,kila uchao akiwa ndani na nje ya nchi amekuwa akifafanua kwa kueleza faida za uchumi wa buluu na kuomba wawekezaji kuwekeza katika eneo hilo.
Ajenda ya Uchumi wa Buluu inazidi kueleweka, kwani Zanzibar inaendelea kupata wawekezaji, hasa katika sekta ya utalii. Uwekezaji wa utalii unafanywa katika visiwa vikubwa vya Unguja na Pemba, lakini umesogea kwenye visiwa vidogo.
SEKTA MAMA
Mapema mwaka huu, katika kuelekea sherehe za miaka 61 ya Mapinduzi matukufu ya Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi, alisema sekta ya utalii kwa sasa inachangia takrbani asilimia 30 ya pato la Taifa la Zanzibar na ndiyo maana inachukuliwa kama sekta mama.
Sekta ya utalii inaendelea kushamiri na kustawi na kuimarisha uchumi wa Zanzibar, ambao kwa asilimia 45 pato lake linatokana na utalii.
Juhudi zinafanywa kuendeleza na kuboresha vivutio vya utalii katika visiwa vya Unguja na Pemba. Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, Aboud Suleiman Jumbe anasema idadi ya watalii wanaoingia kisiwa cha Pemba imeongezeka.
Alisema kuongezeka kwa idadi ya watalii wanaoingia Pemba kunakifanya kisiwa hicho kukua kiuchumi.Alisema hali hiyo inatokana na uwepo wa vivutio vingi vya utalii.
MKAKATI PEMBA
Katibu Mkuu anasema katika mpango mkakati wa kukifungua kisiwa cha Pemba, watalii wengi wanakwenda kuangalia raslimali za maliasili zilizopo maeneo mbalimbali kisiwani humo.
Baadhi ya maeneo yanayopata watalii wengi kisiwani Pemba ni pamoja na mji uliozama wa Ras Mkumbuu na mabaki ya majahazi yaliyopigwa na dhoruba.
Maeneo ya Mkamandume na mji huo wa kihistoria wa Mkumbuu katika kisiwa cha Pemba,yameimarishwa kwa kuwekewa maelezo yanayoonyesha historia ya mambo ya kale kwa watawala mbalimbali.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mudrik Ramadhan Soraga, aliliambia Baraza la Wawakilishi wakati wa kikao chake mwezi uliopita kwamba wizara imeyakarabati magofu ya Bi Hole.Aliongeza kwamba baadhi ya majengo ya kale yaliyopo Pemba wameanza kuyarudisha kataika uhalisia wake.
POPO WA PEMBA (POPOBAWA)
Katika mikakati ya kukifungua kisiwa cha Pemba,Serikali imechukua jitihada za dhati kuwalinda popo wanaopatikana kisiwani humo wasitoweke.
Umuhimu wa kuwalinda popo wa Pemba ambao wanafahamika kama’ Popo Bawa’ ni kwa sababu duniani kote hawapatikani,isipokuwa Pemba pekee.
Popo wa Pemba ni wakubwa,ambapo mmoja akiinuliwa ukubwa wa mabawa yake unafikia mita moja na nusu,hivyo wamekuwa ni kivutio kikubwa kwa watalii.
Serikali imesema imekuwa ikinufaika na popo hao kutokana na wageni kuingia kisiwani Pemba kuwaangalia na wengine kuwafanyia utafiti.Jambo hili linakuza utalii wa Zanzibar.
Mkurugenzi wa Idara ya Misitu Zanzibar, Said Juma Ali,amekaririwa akisema katika nchi zenye visiwa duniani,kuna kila aina yake ya popo.
MISALI YAONGOZA
Kisiwa kidogo cha Misali,katika hifadhi ya Pecca,Pemba,kinaongoza kwa kutembelewa na watalii wanaotoka moja kwa moja kutoka Mombasa,nchini Kenya.Watalii hao wanatembelea hapo kufanya utalii wa kuzamia baharini.
Serikali ya Mapinduzi ina mipango ya kuongeza thamani ya ukuaji wa soko la utalii kwa kuwashawishi watalii kutembelea maeneo ya vivutio vya utalii.Ili kufanikisha hilo, mradi wa teksi ya baharini unatarajiwa kuanza mwezi ujao wa Aprili.
TEKSI BAHARINI
Mradi huo ukikamilika utaongeza thamani ya michezo ya baharini, fukwe za visiwa vidogo vya Bawe,Pungume, Kwale, Changu na Mnemba. Imeelezwa mradi utarahisisha safari za baharini katika mzunguko wa visiwa vya Unguja na Pemba.
Watu watazitumia teksi hizo kutembelea maeneo mbalimbali yenye vivutio vya utalii na hivyo kukuza utalii wa ndani kwa wananchi.
Pamoja na kuboresha vivutio vya utalii,serikali inatilia mkazo mafunzo kwa watembeza watalii,ili waweze kutoa taarifa sahihi kwa wageni,bila upotoshaji.
MAFUNZO
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale amelieleza Baraza la Wawakili kwamba watembeza utalii hupatiwa mwongozo wanaoutumia kwa shughuli zao,kutoa elimu katika mambo ya utalii.
Ili kulinda mila na desturi za Mzanzibari,serikali inawataka waongoza watalii kufuata sheria na utaratibu.
Waongoza watalii wanatakiwa kuwa mabalozi wa kusambaza elimu waliyopata kutekeleza azma ya serikali ya kuona utalii unaendeshwa kwa weledi na kukuza uchumi wa nchi.Mafunzo hayo yameshatolewa katika maeneo ya utalii yakiwemo Paje,Matemwe,Jambiani na Maruhubi.
ULINZI WA AFYA ZA WATALII
Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuhakikisha inalinda afya za watalii,inashirikiana na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kutoa mafunzo ya tiba ya dharura kwa watembeza watalii.
Katika ushirikiano huo, JKCI, imeshatoa mafunzo ya siku mbili kwa waongoza watalii Zanzibar kuwawezesha kutoa kutoa huduma kwa wagonjwa wa dharura.Lengo ni kuwajengea uwezo wa kutoa msaada haraka ,huduma ya kwanza inapohitajika.
Waongoza utalii wakiweza kutoa huduma ya kwanza itasaidia kuimarisha na kukuza uchumi wan chi kwa kuingiza idadi kubwa ya watalii.
Katika kuipa mbele biashara ya utalii,Serikali ya Mapinduzi inachukua hatua za kukiimarisha Chuo cha Utalii Maruhubi.Taasisi ya kuendeleza utalii ya Ufaransa imeonyesha nia ya kuleta watalamu wakiwemo walimu kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa chuo hicho.
Taasisi nyingine inayotajwa kusaidia kutoa mafunzo katika Chuo cha Utalii ni Taasisi ya Tony Blairn ya Uingereza.Nayo imeonyesha nia ya kushirikiana na Chuo cha Utalii kutoa mafunzo kwa wanafunzi ili kuhakikisha wanafikia vigezo vya kimataifa.
MASHIRIKA YA NDEGE
Katibu Mkuu Jumbe anasema uwekezaji katika visiwa vidogo umefikia zaidi ya 16,usiopungua dola za Marekani milioni 500 na miradi 1,600 ya utalii.Anaongeza mashirika ndege yanayoleta watalii Zanzibar ni zaidi ya 80 yakiwemo ya KLM la Uholanzi,Air France na mengine ya kikanda.Siku wanazokaa watalii Zanzibar zimeongezeka kutoka sita hadi nane.
Benki ya Exim Tanzania nayo inashirikiana na Serikali ya Mapinduzi kukuza na kuendeleza sekta ya utalii Zanzibar.Benki itashirikiana na wadau wa sekjta hiyo kuwezesha waendeshaji shughuli za utalii kufanya malipo na ada za kuingia hifadhini kwa haraka,usalama na urahisi.
Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim,Shani Kinswaga anasema nia ni kuweka mikakati ya kuimarisha zaidi nafasi ya Zanzibar kuwa moja ya vivutio bora vya utalii duniani.
![]() |
Mzee Joe Nakajumo |
Mawasiliano: Whatsapp 0784291434
email nakajumoj@gmail.com
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇