LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 29, 2024

LISSU ACHA KUPOTOSHA, ICC SIO MAHAKAMA YA KIHIVYO WALA SIYO MAHAKAMA YA KUDAI MAPESA KAMA UNAVYODAI

Na Yahya Msangi, Togo
Mara kadhaa Lissu amejitapa kuishitaki serikali ya Tanzania ICC, Mara ya kwanza ilikuwa baada ya shambulio lake ambalo hadi leo inadaiwa mhusika mkuu aka dereva kamficha. Mara ya pili ni kipindi cha uchaguzi mwaka 2020, Lissu alidai akishindwa ataenda ICC akijitapa ana mwanasheria anayeitwa Amsterdam ndiye atapeleka suala lake ICC. Huyo Amsterdam akamwandikia Rais JPM na akatoa hicho kitisho. Lissu akatibiwa akapona na akarudi kugombea uraisi. Hakuna lolote kuhusu ICC. Na hata Amsterdam hatukumsikia tena.

Sasa Lissu kaanza tena vitisho vya ICC. Sababu eti kuna kesi dhidi ya Tigo kule Uingereza. Kesi bado inaendelea na hukumu haijatoka. Lakini Lissu tayari keshaona eti ushahidi uliotolewa mahakamani UK unamtosha kufungua kesi ICC dhidi ya serikali ya Tanzania.

Kwanza inampasa Lissu kutambua kuwa hata ikiwa kweli Tigo iliipa serikali mawasiliano ya simu yake sio kosa. Mataifa yote hufanya hivyo ili kulinda usalama wao. Nchini  Marekanai George Bush alipitisha sheria inayoruhudu shirika la usalama la Taifa kusikiliza simu za watu.

Hakuna Sheria yoyote ya kimataifa au mkataba wowote unaokataza a sovereign state kufanya hivyo. Hata hapa Tanzania hakuna sheria inayokataza idara ya usalama isisikilize simu za watu, isichungulie vyumbani mwa watu, isichungulie akaunti za watu. Ni kichaa tu anaweza kudhani uhalifu unaweza kuzuiwa au kushughulikiwa bila serikali kuchungulia!

Lakini nimweleze Lissu ICC ni nini maana nadhani ana uelewa mdogo. Tunaoshughulika Kimataifa kwenye migogoro duniani tuna first hand experience ya kazi za ICC.

ICC ni mahakama ya Kimataifa ambayo baadhi ya nchi ziliingia mkataba (Rome Statutes) kuhusu makosa aina nne (4) tu:

Kosa la kwanza ni Genocide (mauaji ya kimbari). Mfano Bosnia, Rwanda na Sasa Gaza. Taifa au mtu akitekeleza mauaji ya kimbari shauri lake liko chini ya ICC lakini mpaka lithibitishwe. Mfano ni Sudan. Japo Kuna madai ya mauaji ya kimbari bado ofisi ya mwendesha mashitaka mkuu wa ICC haijathibitisha pasipo shaka kwamba mauaji ya kimbari yamefanyika haswa jimbo la Darfur.

Ili mauaji ya kimbari yatimie lazima makosa haya yafanyike na pawe na ushahidi usio na shaka: wauawe au wadhuriwe watu wa Taifa, kabila au dini fulani. Pia shambulizi lilenge kuharibu maslahi yao kama wanadamu, kuzuia wasizae na kuhamisha watoto watengane na wazazi au walezi wao. Hili la mwisho ndio walilomshitaki Putin japo mizengwe pia ilikuwepo kwa shinikizo la wakubwa.

Kosa la pili ni Uhalifu dhidi ya binadamu (crime against humanity). Baadhi ya matendo yaliyowekwa chini ya kosa hili ni kuua, kubaka, kufunga, kupoteza watu, kugeuza watu kuwa watumwa, kutesa, kufukuza watu nchini, lakini inahitajika matendo hayo yaonyeshe kuna pattern au yanakuwa kawaida, madhani ndiyo maana kina CHADEMA wanajaribu kuonyesha utekaji na mauaji kuwa yamekuwa sehemu ya utendaji wa serikali. Wanachosahau ni kwamba lazima ionyeshe ushahidi kwamba unayemtuhimu anahusika.

Kwenye hili CHADEMA 'hawatatoboa'. Kuna ushahidi wa kutosha chama chao kina "pattern" ya kosa wanalotuhumu serikali. Kuna aliyekuwa Katibu Mkuu wao anayethibitisha walikuwa wanatekana na kuuana. Hakusema kwa kificho. Mwenyewe yupo na video ipo. Kuna kiongozi wao aliyeuawa na hawathubutu kudai serikali ichunguze.

Marehemu Chacha Wangwe! Kuna dereva aliyeshuhudia tukio la Lissu, kafichwa ila hukohuko Ulaya. Ikitokea kweli wakashawishi ofisi ya muendesha mashitaka ICC atume wachunguzi basi Slaa, Mnyika na Dereva watahojiwa na kifo cha Wangwe kitachunguzwa. Sidhani kama Chadema itasalimika.  Watakutwa na makosa wanalotuhumu serikali!

Uchunguzi wa ICC utaibua mambo ambayo Chadema wameyaficha kabatini. Mfano wachunguzi ICC watataka kujua kwa nini Katibu Mkuu wao alijificha Kanisani? Watamuuliza maswali yale yale anayoogopa. Ni nani alimpigia simu ndani ya basi alilokuwepo marehemu Ali Kibao? Wana uhusiano gani? Alijuaje ni abiria mwenzake ni kiongozi Chadema? Chadema watajikuta ni pweza aliyevuta mkaa kwa mkia!

Kosa la tatu ni makosa ya kivita. Haya ni pamoja na kutumia watoto vitani, kuua mateka, kushambulia raia wadio na silaha, kuharibu shule na mahospitali, kuharibu nyumba za ibada, kuharibu vituo vya sayansi na vya utamaduni, kushambulia  waandishi, watoa misaada na madaktari.

Kosa la nne ni kushambulia nchi nyingine (aggression). Ni pamoja na kuvamia na kuikalia nchi iliyo huru (sovereign state). Kwa hiyo ni kweli kaishiwa wafadhili lakini ni ndoto ya mwendawazimu kudhani kesi inavyoendelea London itampa utajiri.

Kosa la pili (crimes against humanity) ndio ambalo kwa mbali linamhusu. Ila atatakiwa yeye athibitishe chama chake hakihusiki na atoe ushahidi usio na punje ya mashaka kuwa serikali inahusika na imekuwa na huo utamaduni. ICC sio pahali pa kuropoka tu kuwa "Makonda" alinifuatiliaaaa! Itatakiwa utoe ushahidi. Kwenye kesi ya London dhidi ya Tigo  hakuna popote Makonda katajwa. Wala hakuna kokote serikali imetajwa kuhusika na tukio la Lissu. Kilichotajwa ni Tigo kutoa mawasiliano kwa serikali na hilo sio kosa. Na ikumbukwe kwenye kesi ya Tigo ni mfanyakazi anadai aliachishwa kazi kimakosa. Anadai fidia. Suala la Lissu ni katika tu kueleza sababu iliyomfukizisha kazi. Aliyefungua kesi hana shida na mambo ya Lissu.

Nihitimishe kwa kumfahamisha kuwa ICC sio mahakama yake. Inaweza kumtokea puani yeye na chama chake. Awahi tu kwa Amsterdam ampotoshe tena kama 2020. Japo nafasi ya shauri lake kukubaliwa ni finyu mno ningependa ICC walipokee waanze uchunguzi. Kama Chadema hawakulia.

Yahya Msangi

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages