LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 31, 2024

MAMA MARIA NYERERE ALISHIRIKI MAFUNZO YA MGAMBO, KAWAWA: KAZI YA ULINZI NI WOTE

“KAZI ya ulinzi ni ya wote”. Ni kauli iliyotolewa na Waziri Mkuu, Bw. Rashidi Kawawa miaka 51 iliyopita alipofunga mafunzo ya mgambo wilayani Mwanza.

Akifunga  mafunzo hayo, Mei 28, mwaka 1973, Kawawa alisema mafunzo ya walinzi wa mgambo hayatakoma mpaka wazalendo  wote wa Tanzania waelewe jinsi ya kuilinda  siasa ya nchi kifikira na kitaalam.

Suala la mafunzo ya ulinzi kwa wananchi lilihimizwa na kutiliwa mkazo  baada ya nchi kupata Uhuru na hasa katika miaka ya 1970.

Wananchi wengi walihamisika kupata mafunzo ya ulinzi ambayo  hadi sasa yanajulikana kama mafunzo ya mgambo.Mafunzo haya hutolewa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania.

JESHI LA MGAMBO
Kimsingi, wanamgambo wanawekwa katika  kundi la Jeshi la Akiba. Ikumbukwe kwamba katika miaka baada ya Uhuru na kuendelea hadi miaka ya 1980, Tanzania ilisimama kidete katika kushiriki vita vya ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika.

Ushiriki katika vita, uliifanya Tanzania iwe na maadui wakiwemo, wakoloni, makaburu na walowezi   waliozikalia nchi za, Shelisheli, Msumbiji, Zimbabwe, Afrika Kusini, Angola, Namibia na nyinginezo katika bara la Afrika.

Kama nilivyosema, hamasa ilikuwa kubwa ya Watanzania kujiunga mafunzo ya mgambo. Aidha viongozi wa taasisi za serikali na mashirika ya umma, pamoja na wafanyakazi walilazimika kujiunga mafunzo ya mgambo.

Hata hivyo, kuna baadhi ya Watanzania, walikuwa na utashi binafsi kujiunga na mafunzo, kwa sababu yalikuwa na faida.

Kwanza unajenga afya kutokana na mazoezi ya ukakamavu,unapata mafunzo ya kiintelijinsia, mbinu za ulinzi na taratibu nyingine za kijeshi. Lakini pia mafunzo ya mgambo yaliwajengea zaidi uzalendo na uadilifu kwa wale walioshiriki.

WANAMGAMBO IKULU
Mama Maria Nyerere, mke wa Rais wa Awamu ya Kwanza, Baba wa Taifa, Hayati Rais Julius Nyerere, naye kwa utashi na ridhaa yake alijiunga mafunzo ya mgambo mwaka1973, akiwa Ikulu, Dar es Salaam.

Katika kikundi cha kwanza cha wanamgambo wa Ikulu, alikuwemo Mama Maria Nyerere. Kikundi kilipata mafunzo ya wiki 13 kutoka Kikosi cha Tano cha Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Gwaride la kumaliza mafunzo kwa wanamgambo wa Ikulu, lilifanyika Juni Mosi, mwaka1973 katika viwanja vya Ikulu, Dar es Salaam.

Wanamgambo walipita na kutoa heshima kwa Rais Nyerere katika  sherehe ya kumaliza rasmi mafunzo yao. Miongoni mwao alikuwemo Mama Maria Nyerere, ambaye alimaliza vizuri mafunzo na kutunikiwa cheo cha Kamanda wa Platuni.

KAMANDA PLATUNI
Platuni tano zikiongozwa na Mama Maria Nyerere zilipita mbele ya Rais ambapo kiongozi wa Platuni, Mama Maria, aliamrisha platuni yake na wote wakageuka kwa pamoja kutoa heshima kwa Rais huku wakienda kwa mwendo wa haraka.

MWANAMGAMBO BUTIKU
Baada ya hapo, wanamgambo walitoa kiapo cha utii kwa Rais, TANU na Serikali. Kiongozi wa wanamgambo, Bw. Joseph Butiku, alisoma risala kwa niaba ya wenzake. Alisema walijifunza  mbinu za kivita na mambo ya ulinzi kutoka kwa wakufunzi wa Kikosi hicho cha Tano cha JWTZ.

Katika miaka ya 1970, lilikuwa ni jambo la kawaida kwa viongozi kushiriki mafunzo ya kijeshi. Kwa mara ya kwanza katika historia ya Tanzania, viongozi 44 wa TANU na Umoja wa Vijana wa TANU, walimaliza mafunzo ya kijeshi katika Chuo kilichokuwa kipya cha Kijeshi cha Viongozi wa Chama, Monduli, mkoani Arusha.

MAKATIBU WANOLEWA JESHINI
Viongozi hao walikuwa makatibu tawala wa Chama na Umoja wa Vijana wa TANU na walimaliza masomo ya  juu ya siasa na ulinzi kwa miezi saba, Mei 31, mwaka 1973.

Uimarishaji wa ulinzi na usalama, mbali ya watu kupata mafunzo rasmi, Chama cha TANU, kiliweka utaratibu wa kuwa na mabalozi, kila nyumba kumi. Mlinzi wa mgambo mwenye makazi katika eneo la nyumba kumi, pia alisaidia kuhakikisha usalama.

Siku hizi, wanafahamika kama wajumbe. Hawa walihakikisha mgeni ye yote aliyefika katika utawala wake wa nyumba kumi anajitambulisha na kueleza  sababu za ugeni wake.Hatua hii kwa kiasi fulani iliimarisha usalama.

Kwa  sasa, kuanzia miaka ya hivi karibuni, utaratibu wa mgeni kujisajili kwa mjumbe umekufa  katika maeneo mengi ya nchi. Mgeni anaingia, anakaribishwa na mwenyeji wake  na kuondoka au kuendelea kuishi, bila taarifa  ya mjumbe.

Jumatatu, Januari 22, kwa wiki hii iliyomalizika, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, alifungua Mkutano wa saba wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama na Makamanda, katika kambi ya Lugalo, Dar es Salaam.

ANGALIZO LA JWTZ
Katika hotuba yake ya kumkaribisha Amiri Jeshi Mkuu, Rais Samia, Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania Jenerali Jacob John Mkunda, alisema hali ya ulinzi na usalama ni shwari, licha ya kuwepo matishio ya ugaidi na itikadi kali ambapo wanamtandao wa kigaidi wamekuwa wakiwatumia vijana wenye umri wa kati ya  miaka 15 hadi 35 kusafirishwa kwenda kujiunga na vikundi vya kigaidi nchi za Jamhuri ya Kidemokrasi Congo(DRC), Msumbiji na Somalia.

Jenerali Mkunda alitaja changamoto nyingine ni uwepo wakimbizi na waomba hifadhi wa muda mrefu katika mikoa yetu ya magharibi. Tanzania imekuwa ikipokea maombi ya waomba hifadhi na wakimbizi kutoka nchi za Burundi tangu 1972, Rwanda mwaka 1994 na DRC mwaka 1996.

Mkuu wa Majeshi alisema kuanzia Januari hadi Disemba mwaka jana, 2023, waomba hifadhi 138,149, walipokelewa nchini ambao sehemu kubwa ni kutoka Burundi na DRC.

Jenerali Mkunda, alisema, wao Jeshi ni maoni yao ni kwamba kuendelea kuwepo kwa muda mrefu kwa waomba hifadhi na wakimbizi nchini ni tishio la usalama.

Alisema taarifa zilizopo ni kwamba baadhi ya waomba hifadhi au wakimbizi au familia zao, wameajiriwa serikalini kwa nafasi mbalimbali na wengine wamepewa teuzi serikalini katika nyadhifa zenye maamuzi.

KAULI YA RAIS SAMIA
Rais Samia, alisema amelipokea angalizo la Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama,juu ya uwepo wa wakimbizi waliojichomeka na kupata nafasi na kwa sasa Serikali inaendelea na mchakato wa  kuwachambua.

Amiri Jeshi Mkuu,alivitaka vyombo vya ulinzi na usalama, kushirikiana katika kuwadhibiti baadhi ya vijana nchini, wanaotoroka kwenda nje ya nchi kujiunga na vikundi vya ugaidi,uharamia na dawa za kulevya.

Rais Samia amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kudhibiti vijana hao. Hapa agizo hilo la Rais, linatuhusu sote raia wa kawaida, kwa sababu vijana hawa tunaishi nao katika makazi kwenye mitaa.

Mlinzi wa kwanza wa kuvisadia vyombo vya usalama anapaswa kuwa mwananchi wa mtaani ayeushiba uzalendo. Huyu anafahamu nyendo za kila siku za vijana wa aina hiyo.

Hali kadhalika kwa waomba hifadhi na wakimbizi wanaojipenyeza kuingia serikalini, raia Mtanzania mtaani, kwa vyote vile anajua chimbuko na historia ya watu hao, wajibu uliopo ni kuisadia serikali kuwachekecha kwa sababu baadhi tunaishi nao mtaani.

Wajumbe wa nyumba kumi nao wanapaswa kutafakari kauli ya Rais Dk. Samia na warejee katika utaratibu wa kuhoji wageni katika eneo lao ili kuwatambua wema na wabaya.

Imeandaliwa na;

Joe Nakajumo Aliyewahi kuwa Mhariri wa Habari Uhuru Publications Ltd Simu: 0784291434, email: nakajumoj@gmail.com


 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages