Mar 18, 2025

WAZIRI AWESO MBONA 'SPIDI' NI NDOGO KWENYE HILI LA 'LUKU' ZA MAJI, UNAPIGWA MTAMA, AU?

Na Bashir Nkoromo
Hapana shaka Wizara ya Maji chini ya Waziri Aweso imefanya kazi ya kutukuta na kwa kweli inaendelea kufanya vema katika ujenzi wa miundombinu ya Usambazaji maji na usambazaji maji wenyewe hadi katika maeneo ambayo ilikuwa ni ndoto kupata maji safi na salama nchini.

Mfano Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), kwa mujibu wa taarifa ya Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka hiyo Mhandisi Mkama Bwire, aliyoitoa alipokuwa akizungumza  na waandishi wa habari Machi 11, 2025 jijini Dodoma, kuhusu mafanikio na mwelekeo wa mamlaka hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, katika kipindi cha kuanzia Julai 202, imeendelea na utekelezaji wa miradi zaidi ya 25 yenye thamani ya Sh. billioni 987.6.

Anasema, kati ya fedha hizo (Sh. Bilioni 987.6), miradi ya Sh. Bilioni 232.9 imekamilika na inatoa huduma kwa wananchi huku miradi yenye ya Sh Bilioni 754.7 ikiwa bado ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji na miradi iliyopo katika mipango ya muda mfupi na mrefu ya Sh. Trilioni 3.1 imebuniwa na iko katika hatua mbalimbali za maandalizi.

Kulingana na Mhandisi Bwire fedha hizo zinajumuisha gharama za usanifu, ujenzi, upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa majisafi, pamoja na ujenzi, upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya ukusanyaji, usafirishaji, upokeaji na uchakataji wa majitaka.

Miradi hiyo inatekelezwa kwa kutumia fedha za makusanyo ya DAWASA, Serikali kuu na mikopo ya masharti nafuu kutoka kwa Washirika wa Maendeleo, wakiwemo Benki ya Dunia, Serikali ya Korea Kusini (kupitia Benki ya Exim ya Korea) na Serikali ya India (kupitia Benki ya Exim ya India).

Kwa jumla ukipata picha hiyo ya mwenendo wa Dawasa ambayo inahudumia Jiji kubwa la Dar es Salaam na sehem ya mkoa wa Pwani, utakubali kuwa hata Mamlaka nyingine za Maji zinafanya vizuri, maana Waswahili husema "nguvu ya teke hutoka kwenye paja", hivyo kwa kuwa Dawasa inafanya vizuri, basi na nyingine zinafanya vizuri kwa sababu Mamlaka zote nguvu zake zinatokana na usimamizi mahiri wa Wizara ya Maji.

Sasa pamoja na Wizara kuzisimamia vema Mamlaka za Maji, zikitekeleza miradi ya mabilioni ya fedha lakini changamoto kubwa ipo kwenye mambo ya bili za maji, changamoto ambayo kwa muda mrefu, imezua 'uadui' baina ya Mamlaka za Maji na wananchi wanaotumia maji.

Uadui huu unatokana na kutokuwepo njia sahihi inayoweza kuridhisha mwananchi kwamba kiasi cha fedha cha bili anayopewa na Mamlaka husika kama Dawasa kinalingana na matumizi ya maji aliyotumia.

Hii ni kwa sababu, pamoja na viongozi Wakuu wa Wizara ya Maji akiwemo Waziri Aweso kusisitiza kwamba lazima msomaji mita ashirikishe mwananchi, lakini wananchi wengi nikiwemo mimi (mwandishi wa safu hii), huwa msoma mita hanishirikishi au kushirikisha yeyote anayemkuta nyumbani licha ya kwamba mita ipo ndani ya geti!

"Wasoma mita wawe waaminifu na wenye maadili, wanaposoma mita zao lazima wamshirikishe mwananchi, msoma mita asipokushirikisha mwananchi toa taarifa, tutawachulia hatua wote watakaobainikia kuchafua jina la mamlaka", ameshasikika mara nyingi Waziri Aweso akionya, lakini bado utekelezwaji wa agizo hilo ni nadra.

Kwa mfano, mwaka jana, kwa takriban miezi minne, mita ya Dawasa iliyopo nyumbani kwangu ilikuwa mbovu, msomaji akija kusoma anaichangamsha kwanza mita kwa kuiwashia moto wa makaratasi au kaa la moto, ndiyo anaosoma! akiona anashindwa anaondoka zake halafu kesho yake unastukia inatumwa kwa sms bili ya uniti zero (0), kwamba hukutumia maji!

Niliripoti kadhia hiyo lakini Dawasa hawakuchukua hatua yoyote, baadaye wakaja na mita mpya, wakaiweka ikiwa uniti ziro (0), halafu wakaondoka na ile mita mbovu ambayo wakati huo ilikuwa haisomi uniti kabisa.

Lahaula! Mwezi uliofuata Dawasa wakanitumia bili ya maelfu ya fedha wakichanganya na bili ya mita mpya!  Niliponana na msoma mita nikamuuliza, "wewe na mwenzako mlipokuja kufunga mita mpya, si mliniambia naanza upya, ukasema ndiyo, sasa imekuwaje natumiwa pamoja na bili ya maelfu, hayo maelfu mmeyapataje wakati mita ilikuwa mbovu?"

Msoma mita akasema; Mzee usijali wewe endelea kulipa bili ya mita mpya, mwaka wa fedha (Julai) ukipita hiyo bili ya maelfu inayounganishwa itafutwa. Tangu hapo ni mwaka wa pili na hiyo bili ya maelfu bado natumiwa!

Nilipoenda ofisi za Dawasa kuuliza kulikoni, wakasema, "Mzee baada ya mita mbovu kuletwa hapa ofisini tuliisoma tukaona ulitumia kiasi hicho. Nikawauliza, mbona taratibu zinaelekeza kuwa, usomwaji mita ufanyike mwananchi akishuhudia, sasa mbona ninyi hiyo mita mbovu mliisoma mkiwa peke yenu? Kwa nini baada ya kufanikiwa kuona 'digiti' hamkuniita nione mnavyoisoma?

Meneja Biashara wa hapo Dawasa akacheka! kisha akaniliuliza; "Kwa hiyo mzee unataka kusema katika kipindi hicho chote hukutumia maji? Nikawajibu; "Nilitumia, lakini sikutumia maji ya gharama mnayonitumia. Mimi ninachoona hapa ni kwamba hamkusoma ile mita mbovu bali mmekadiria tu na katika kutumia mtindo huo wa kukadiria uliopitwa na wakati pia mgenishirikisha, maana kwa kipindi hicho kuna vipindi tofauti ambayo baadhi ya wapangaji  hawakuwepo nyumbani na watoto walienda mikoani kusoma.

Meneja Biashara akasema", basi endelea kutumia maji ukilipa bili ya mita mpya, halafu tutakuita uje tujadili namna utakavyokuwa unalipa kidogo kidogo. Sasa hadi ninavyoandika safu hii hawajaniita na bili hiyo ya maelfu wanaendele kunitumia na sijui hatma yake.

Hayo yote nimeeleza kuonyesha changamoto ya mwenendo mzima wa namna ya usomaji mita na ulipaji bili za maji ulivyo, changamoto ambayo ninaamini asilimia 90 ya wapata huduma za maji kupitia Mamlaka za Maji wanakumbana nayo.

Kwa hiyo, ni vema Wizara ikaiangalia kwa makini kadhia hili na kuipatia tiba ya kudumu, tiba yenyewe siyo nyingine ni ya kulipia maji kwa mfumo wa kielektroniki kama ule wa Tanesco (LUKU), ving'amuzi vya televisheni au simu, au mita za malipo kabla.

Na tiba hii kwa sasa siyo ngeni maana ni miaka mingi imepita tangu kilio cha luku za maji kilipoanza kusikika na kuzungumzwa na  viongozi na watendaji wa wizara ya maji na hata Mkuu wa Nchi Rais Dk. Samia Suluhu Hassan. Hivi karibuni akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tanga, aliitaka wizara kuweka mfumo wa malipo ya maji kama Tanesco ilivyo na Luku.

Rais alisema wateja wa maji wanalalamika kubambikiwa bili kubwa, ikilinganishwa na kiasi cha maji walichotumia, akasema tuhuma hizo zimekuwa zikielekezwa kwa mamlaka za maji, hivyo kuondoa kadhia hiyo ni kuweka mfumo wa kielektroniki mithili ya Luku.

"Imefika wakati sasa Wizara ya maji muwaige wenzenu wa TANESCO kwa kufunga mita za maji za LUKU, ambazo zitamuwezesha mtumiaji wa maji kulipia kile anachotumia. Hii itasaidia wananchi kurudisha imani kwenu, kwani watakuwa wanajua kama matumizi ni sawa na kiasi cha pesa alicholipia", Alisema Rais.

Hata aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandishi Anthony Sanga, takriban miaka mitatu sasa alisema utaratibu wa LUKU za Maji ungeanza kutumika.

Kuhusu Dira za maji za malipo kabla, Juni 2021, Waziri Aweso, alisema Wizara ilikuwa imeanza mabadiliko kwa kuelekeza matumizi ya dira hizo, ili kuondokana na malalamiko ya bili bambikizi, pia kuendana na maendeleo ya teknolojia, na kuongeza kuwa nia ya mabadiliko hayo ilikuwa kumaliza malalamiko ya wananchi, kuhusu kusomewa dira za maji bila kushirikishwa.

Ikiwa ni hivyo, swali ni kwamba, kwa takriban miaka mitano sasa kauli kuhusu LUKU za Maji zimekuwa zikisemwa, lakini haziambani na vitendo vyenye 'spidi' je, Wizara ya Maji inakwama wapi? Kwa kuwa bili za maji zimekuwa ni changamoto kwa wananchi kulalamika kubambikiwa, sasa ugomvi huu kwa nini usimalizike?

Unaweza kujiuliza, kama Wizara ya Maji chini ya uongozi makini Waziri Aweso, imeweza kusimamia miradi ya maji kwa ufanisi hadi kilio cha ukosefu wa maji safi na salama kuwa nadra, inawezekanaje Wizara hiyohiyi ikashindwa kuongeza spidi ya kuwapatia wateja wa maji LUKU ya maji?

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Pages