Na Bashir Nkoromo, CCM Blog
Bila shaka inajulikana kwamba zipo changamoto zinazompata mwanamke anapofiwa na mume wake ikiwemo msongo wa mawazo na kushindwa kumudu maisha ikiwemo kutunza familia, kutokana na upweke anaobaki nao, hivyo huo ndio wakati anaohitaji sana kupendwa na kutiwa moyo na jamii.
Lakini kinyume chake, umekuwa ndio wakati wa kutengwa, kunyanyaswa hasa ndugu, jamaa na marafiki, ikiwa ni pamoja na kunyang’anywa mali zilizokuwa za familia na kufukuzwa katika nyumba aliyokuwa akiishi na mume wake.
Mjane amekuwa mtu wa kuonewa na kuumizwa katika jamii, wengi wamenyanyasika kijinsia pamoja na kuathiriwa kabisa kisaikologia, na hata baadhi kupoteza maisha kutokana na mkandamizo na msongo wa mawazo baada ya kufiwa na mume wake.
Ni kutokana na kutambua hivyo ndiyo sababu Serikali ya Tanzania imekuwa ikiungana na Mataifa mengine Duniani kufanya jitihada mbalimbali za kuwasaidia Wajane ili waondokane na changamoto hizo.
Moja ya hatua ambazo Tanzania imekuwa ikifanya ni kutambua Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani ambayo huadhimishwa Julai 23 ya kila mwaka, ambapo inafanya hivyo kwa kutambua kuwa siku hiyo ni jukwaa ninalowaleta pamoja wajane na kuwapa fursa ya kushiriki na kubaini changamoto wanazokumbana nazo na hata kuimarisha ushirikiano kwa ajili ya ufumbuzi wa changamoto hizo.
Pia Tanzania huitumia siku hiyo kukuza hamasa, mshikamano na uelewa ndani ya jamii ili kuacha ukiukaji wa haki za binadamu kwa wajane na kutoa fursa ya pamoja kwa Taifa katika kubaini changamoto za wajane na namna ya kukabiliana nazo.
Wakati Tanzania ikishiriki kufanya Maadhimisho hayo ya siku ya Wajane Duniani, Mataifa mengine duniani nayo huiadhimisha, ikiitumia kukemea vurugu, ubaguzi na unyanyasaji dhidi ya wajane huku maadhimisho hayo yakitumika pia kama sehemu ya kupongeza mchango wa wajane katika mataifa husika na duniani kwa jumla.
Katika Maadhimisho yaliyofanyika mwezi uliopita wa Julai 23, 2022, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alitoa tamko, akisema kila mtu atafakari changamoto za kiuchumi na matatizo wanayopitia wajane na kuhakikisha kwamba hawaachwi nyuma.
Akasema, hakuna mwanamke anayepaswa kupoteza hadhi, utu, ustawi au kipato eti kwa sababu amefiwa na mumewe.
Katibu Mkuu huyo wa UN akashangaa kwamba suala hilo ni dhahiri lakini bado mamilioni ya wanawake duniani wanakumbwa na manyanyaso, ukatili na hata kuenguliwa kwenye urithi wa mali wanapofiwa na waume zao.
Katika kuonyesha kuwa licha ya changamoto zinazowakumba wajane baadhi yao wanajitambua, hapa Tanzania Wanacho Chama cha wajane ambacho walikianzisha, ili kuwaweka pamoja kwa lengo la kutambuana, kufahamiana, kujua changamoto anazopitia mjane, na kutafuta ufumbuzi wa kuzitatua, ikiwemo za kusomesha watoto, kupatiwa elimu ya sheria, afya, saikolojia, biashara na ujasiriamali.
Vilevile chama hicho kikishirikiana na taasisi nyingine, kinajihusisha na kutoa elimu kwa jamii ili iwatambue wajane, kuwapenda, kuwathamini na kuwasaidia kwa namna moja ama nyingine, pia kujitoa kwa hali na mali kusaidia kupambana na changamoto anazopitia mjane.
Pamoja na jitihada hizo za Kitaifa na Kimataifa za kumkomboa Mjane, lakini ijulikane kwamba hata mjane husika akiondokewa na madhila yanayomfanya asiishi maisha ya utu kamili, ili mjane huyo aweze kuishi maisha ya 'ujane nje ya ujane', itategemea uwezo wake binafsi atakaokuwa nao hasa katika kujiongeza ili kuendeleza rasilimali zilizoachwa na mwenza wake, ziwe chache au nyingi.
Wajane wanaokwama kunyanyuliwa na juhudi za Kitaifa na Kimataifa katika kuwakomboa ni wale ambao wanakuwa hawajiongezi, siyo wabunifu na wapambanaji katika maisha jambo ambalo husababisha rasilimali zilizoachwa na wenza wao kudumaa au kutoweka kabisa na mjane kubaki akihangaika yeye na watoto au wanafamilia ambao ni tegemezi (kama anao).
Lakini wapo wajane wapambanaji, ambao baada ya wenza wao kufariki dunia, hujiongeza na huchakarika vya kutosha hadi kuhakikisha kwamba pamoja na kuwa ni mjane lakini maisha yanaendelea vizuri akiwa mjane nje ya ujane', ukiacha upweke ambao kwa kawaida huwa ni pengo ambalo haliwezi kuzibika.
SALOME KOMBA:
Mmoja wa wajane aliyeweza kuishi maisha ya 'mjane nje ya ujane' ni Mjane wa aliyekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Mkurugenzi wa Kikundi cha Hamasa cha CCM cha Tanzania One Thetre (TOT) Hayati Kapteni John Damiano Komba.
Huyo siyo mwingine, ni Bi. Salome Komba ambaye licha ya Mwenza wake huyo Hayati Kapteni John Komba kumwacha na familia ya watoto, wajukuu na wengine wanaomtegemea ameweza kujiongeza na kupambana akitumia hekima burasa na maarifa kuhakikisha maisha yanaendelea.
Baada ya Kapteni John Komba kufariki dunia Februar 28, 2015, Bi Salome ambaye ni mwalimu mstaafu alishika usemi wa 'ukishikwa shikamana', akaingia katika ujasiriamali, mtaji wake wa kwanza ukiwa ni kuendeleza rasmilimali alizokuwa akizimiliki yeye na Mumewe Kapteni John Komba.
Miongoni mwa rasilimali alizoziendeleza Mama huyu na kuonesha 'kumlida' kwa kiasi fulani yeye na familia, baada ya kifo cha memewe mwaka 2015, ni makazi alikoachwa na Mumewe, eneo la Mbezi Beach kwa Komba, Kata ya Kawe, Wilayani Kinondoni Jijini Dar es Salaam, ambapo kwa kujiongeza aliamua kujena katika eneo hilo Jengo la Kibiashara lenye mvuto wa aina yake.
Bi. Salome anasema, pamoja na jengo hilo kuwa na fremu za maduka ya bidhaa mbalimbali na saluni za kunyoa na kurembesha nyewele, kikubwa ni kwamba katika jengo hilo ameweka ukumbi mkubwa wa kisasa kwa ajili ya kutoa huduma za kuukodisha kwa wanaohitaji kuutumia kufanyia sherehe za aina zote, kama harusi, mikutano ikiwemo ya Makongamano, semina na shughuli nyinginezo zinazohusisha kukutana watu wengi.
"Baada ya kuona nimebaki peke yangu, nikaona sasa mkombozi niliyebaki naye wa kwanza ni kutumia kwa usahihi rasilimali hii ya makazi niliyoachwa nayo na Hayati Mume wangu.
Katika kujiongeza nikaamua kujenga jengo la Kibiashara hapa mbele ya nyumbani, kwa ajili ya kukodisha fremu za maduka, lakini lengo kubwa haikuwa fremu tu, ila kuweka ukumbi wa kisasa wa kukodisha kwa wanaohitaji kufanyia sherehe kama za harusi, mikutano na semina.
Sasa ukumbi huu upo na umeanza kufanyakazi tangu mwaka jana wa 2021 baada ya kuujenga tangu mwaka 2019, ukumbi huu unaitwa Salome Social Hall, ni ukumbi wenye hadhi ya kutumiwa na watu wastaarabu. Haupo mbali na Barabara Kuu ya kwenda Tegeta hadi Bagamoyo kutokea Mwenge kupitia Lugalo. ni kiasi kama cha mita tano tu hivi, kutoka Barabarani, na ni rahisi kufikika maana upo mkabala na Kituo cha Daladala kinachojulikana kwa jina maarufu 'Kwa Komba' na tunalo eneo kubwa la kuegesha magari.
Ni ukumbi uliopo kwenye ya mandhari ya kuvutia, lakini pia licha ya kutumia feni na viyoyozi, ukumbi huu upo ghorofani hivyo una uwezo wa kuingiza hewa moja kwa moja kutoka Bahari ya Hindi, maana haupo mbali na ufukwe wa Mbezi Beach, na pia wanaohitaji kupatiwa huduma ya mapambo, keki za matukio, vinywaji na vyakula aina zote vinapatikana ukumbini", akasema Bi Salome Komba.
Bi Salome akaendelea kusema, "Pamoja na lengo kubwa la kujenga jengo hili lenye ukumbi huu, ili litufae kuendeshea maisha yangu, watoto, familia na ndugu na jamaa ninaoishi nao, nilijiwa na wazo hili la kujenga jengo hili na kuweka ukumbi ili pia kuwa kumbukumbu ya mume wangu ambaye alinishauri kufanya hivyo siku chache kabla ya kifo chake".
Bi Salome, akawaomba viongozi wa CCM, Wanachama wote wa CCM, Wasiokuwa wana CCM na wadau wote hasa waliokuwa mashabiki wa marehemu mumewe Kapteni Komba kwenda kufanyia shughuli zao kwenye ukumbi huo wa Salome Sociall Hall kwa kuukodi kwa gharama nafuu ikiwa ni sehemu ya kumuenzi Hayati Kapteni Komba.
Kuhusu yeye kuwa mjane, Bi Salome akasema, “Niliona nitakaa chini na kujiita mjane hadi lini, nikaona nijiongeze kwa kujenga ukumbi huu kama alivyonishauri Mume wangu wakati wa uhai wake.
Lakini kwa kuwa mimi sasa ni mjane ambaye machungu ya ujane nayajua, nimekuwa nikitumia sehemu ya mapato ninayopata kwenye biashara hii ya ukumbi kuwasaidia wajane wenzangu, watu wenye uhitaji maalum na watoto wanaoishi katika mazingira magumu".
Bi. Salome, akatoa neno kwa Wajane wenzake akisema, "Nawaomba na wajane wenzangu waache kukaa chini na kuendelea kujiita wajane tu, wajitahidi kupambana katika ujasiriamali ili maisha mengine yaendelee”.
CHANGAMOTO.
Bi Salome amesema kutokana na Hayati Kapteni John Komba kuwa kipenzi cha Viongozi mbalimbali hasa wa CCM na Wanachama wa CCM na hata wasiokuwa wana CCM, kutokana na haiba yake na kupendwa nyimbo zake alizokuwa akiimba wakati akiongoza TOT, sasa ukumbi wake huo umeanza 'kuhemewa'.
"Kwa kweli namshukuru Mungu, ukumbi huu sasa unapendwa na watu wa kila aina kuja kufanyia shughuli zao hapa, lakini sasa changamoto ninayoipata ni kwamba imefikia mahali ukumbi umekuwa mdogo, sasa kuna wateja wengine wanakuja wakitaka wafanye shughuli yao na watu hadi 300, lakini ukumbi huu una uwezo wa watu 200 tu.
Sasa hapa napambana kutafuta wafadhili, ili nikopeshwe fedha za kuongeza ukumbi huu ili uweze kuchukua hadi watu zaidi ya 300, maana nafasi ya eneo ipo, ila pesa tu ndiyo sina. Kwa kweli nimeshajaribu kupita huku na huko kupata wafadhili lakini bado sijafanikiwa.
Kuna wakati niliwahi kuzungumza na baadhi ya Viongozi wa Tanzania Bara na wa kule Zanzibar, baadhi wakaonyesha moyo wa kunisaidia kupata mikopo isiyo na riba au yenye riba nafuu lakini hadi sasa bado sijapata mrejesho chanya kutoka kwao, sifikirii kuwa wamenisahau ila nadhani bado wametingwa na majumu mengi ya kiuongozi.
Habari Picha👇
Mjane wa Hayati Kapteni John Komba, Bi Salome Komba akifarijiwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan alipofuatana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM William Lukuvi kumpa pole nyumbani kwake Mbezi Beach dar es Salaam, baada ya kifo cha mumewe. Wakati huo Rais Samia alikuwa bado ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM
Picha za Ukumbi wa Salome Social Hall👇
Mmiliki wa Salome Social Hall Bi Salome Komba akimpongeza Bibi Harusi, wakati wa harusi moja ya kufana iliyofanyika katika ukumbi huo, eneo la Mbezi Kwa Komba, Kata ya Kawe jijini Dar es Salaam, Jumamosi Agosti 20, 2022Mmiliki wa Salome Social Hall Bi Salome Komba akiwapongeza Maharusi, wakati wa harusi hiyo ya kufana iliyofanyika katika ukumbi huo, eneo la Mbezi Kwa Komba, Kata ya Kawe jijini Dar es Salaam, Jumamosi Agosti 20, 2022Mmiliki wa Salome Social Hall Bi Salome Komba akiwa na Maharusi na wapambe wao, wakati wa harusi hiyo ya kufana iliyofanyika katika ukumbi huo, eneo la Mbezi Kwa Komba, Kata ya Kawe jijini Dar es Salaam, Jumamosi Agosti 20, 2022Ukumbi unavyoonekana wakati maharusi wakiingia ukumbini
Ukumbi wanavyowazidishia Maharusi kumeremeta wakati wakiingia kwa shangwe katika ukumbi huo wa Salome SocialHall
Mlango wa kisasa kabisa wa kuingilia ukumbini
Vyakula katika hali nadhifu katika ukumbi huo.
Vyakula katika vyombo vya kisasa kabisa katika ukumbi huo.
Mkao ulivyo wa kistaarabu katika ukumbi huo.
Mpangilio wa ukaaji ulivyo wa kistaarabu ndani ya Salome Social Hall
Sehemy ya nje ya mlango wa kuingilia ukumbini.
Madhari ya ukumbi kabla ya wahusika kuingia
Mandhari ya ukumbi kabla ya wahusika kuingia
Eneo la kuketi maharusi linavyomeremeta kabla ya maharusi kuingia ukumbini
Mandhani ya upambwaji, meza na viti vya kisasa ukumbini.
Na muziki 'mnene' wa kutosha upo ukiukodi Salome Social Hall. ©August 2022 CCM Blog/Bashir Nkoromo
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇