Na: Genofeva Matemu – JKCI
18/08/2022 Naibu Waziri wa Afya wa nchini Malawi ametembelea
Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kuona huduma za matibabu ya
moyo zinazotolewa pamoja na kujifunza mifumo ya Tehama inayotumika katika uendeshaji
wa huduma za matibabu katika Taasisi hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam
kwa niaba ya Waziri wa Afya Naibu Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Godwin Mollel
alisema kuwa ugeni wa naibu waziri wa afya kutoka nchini Malawi umelenga kupata
uelewa wa huduma zinazotolewa na JKCI pamoja na kujifunza mifumo ya Tehama
ambayo Tanzania inaitumia kwenye sekta ya afya ili nao waende kuboresha mifumo
ya afya nchini mwao.
Mhe. Mollel alisema kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa katika
taaluma ya afya na vifaa tiba imeleta tija kubwa kwani sasa nchi za Afrika na
nchi ambazo zinaizunguka Tanzania zimeanza kujifunza kupitia Tanzania na kuona
badala ya kuwapeleka wagonjwa wao India, Ulaya na Marekani waanze kuwaleta hapa
nchini.
“Upande wa upasuaji mdogo
wa moyo kupitia tundu dogo kwenye paja wataalamu wetu wameweza kufanya aina
tofauti tofauti za upasuaji ambapo hadi sasa asilimia 92 ya upasuaji mdogo wa
moyo unafanywa na wataalamu na asilimia nane iliyobaki inafanywa na wataalam
kutoka nje ya Tanzania ambapo tunawachukua wataalam hao kuja hapa kwetu
kwasababu vifaa tunavyo tunachotaka kutoka kwao ni ujuzi ambao utatuwezesha
kwenda hatua ya juu zaidi”,
“Upasuaji mkubwa wa kufungua kifua asilimia 85 za upasuaji
huo inafanywa na wataalam wa afya wazawa huku asilimia 15 za upasuaji huo
inafanywa na wataalam wa afya kutoka nje ya nchi ambao wamekuwa wakituachia
ujuzi kwa wataalamu wetu”, alisema Dkt. Mollel
Mhe. Dkt. Mollel alisema kuwa hivi sasa Taasisi ya Moyo
inapokea wagonjwa kutoka nchi 25 duniani ikiwemo Visiwa vya Comoro, Zambia,
Kenya, Congo, Malawi na nyinginezo hii inatokana na Uongozi wa Mhe. Rais Samia
ambaye tokea Mwanzo alisema kuwa anaifungua nchi kwa maana ya kufungua fursa ya
ujuzi, utalii wa kimatibabu na uduma za kibobezi za afya zinazopatikana hapa Tanzania.
Mhe. Dkt Mollel alisema kuwa Mhe. Samia Suluhu Hassan Rais wa
Jamhuri ya Muuungano wa Tanzania amewekeza kwenye eneo la afya ambapo Afrika
hadi sasa zipo nchi chache ambazo zinafanya upasuaji wa moyo mbalimbali hivyo
kuzivutia nchi ningine kama Malawi kuona ni vyema leo kuja kujifunza kwetu.
“Mhe. Naibu waziri wa Afya kutoka Nchini Malawi Mhe. Enock
Phale amekuja hapa kwetu kwa ajili ya kuona huduma tunazizitoa na kujifunza
mifumo ya Tehama tunayoitumia katika sekta ya afya hii inaonyesha adhma ya Mhe.
Samia ya utalii wa kimatibabu inavyotekelezeka”,
Tukiwa wabunifu wakutosha kwa kuwatengenezea wataalamu wetu
ujuzi na kuvisimamia vizuri vifaa vyetu tukapata wagonjwa wengi kutoka nje ya
Tanzania mapato ya Taasisi zetu yataongezeka hivyo kuziwezesha Taasisi zetu
kujiendesha zenyewe na kupunguza kuitegemea serikali”, alisema Dkt. Mollel
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi alisema kuwa ugeni wa Naibu Waziri wa Afya
wa nchini Malawi umelenga kujifundisha JKCI inachokifanya na itawasaidiaje kama
nchi na wao kuweza kufika Tanzania ilipo katika Sekta ya Afya.
“Malawi wanapita njia ambayo sisi tumepita huko nyuma ambapo
wagonjwa wote wa moyo, figo, saratani, mifupa na magonjwa ya damu tulikua tunawapeleka
India, Afrika ya Kusini, Ulaya na Marekani lakini baada ya uwekezaji huu mkubwa
uliofanywa na Serikali JKCI imepunguza kupeleka wagonjwa wa moyo nje ya nchi
kwa asilimia 95”,
“Katika hii miezi mitatu tumeshapata ugeni kutoka Afrika ya
Mashariki, ugeni kutoka Zambia, na tukapata ugeni kutoka Mozambique, hii ni
nchi ya nne sasa inakuja JKCI kwa ajili ya kuona nini tunafanya ili na wao
wakafanye kama sisi”, alisema Prof. Janabi
Aidha Prof. Janabi alisema kuwa Serikali ina nia kubwa katika
utalii tiba hivyo katika lile lengo la kufikisha watalii milioni 5 sekta ya
afya chini ya usimamizi wa Wizara imekusudia afya ichangie katika kuleta
watalii kupitia huduma bora na bobezi za matibabu yanayotolewa hapa nchini
yakiwemo matibabu ya moyo.
“Tunaishukuru Serikali kwa ushirikiano waliotupatia kwa
kuwekeza wataalamu na vifaa tiba vya kisasa katika Taasisi yetu, sisi kama
wataalam kazi yetu ni moja tu ya kuwahudumia wananchi wa Tanzania na nchi za
jirani za SADC ikiwemo kutangaza utalii kupitia afya”, alisema Prof. Janabi
Naye Naibu waziri wa afya Nchini Malawi Mhe. Enock Phale alisema
kuwa amekuja Tanzania kwa ajili ya kujifunza Tanzania imewezaje kufanikiwa
katika kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo na kuangalia namna ambavyo
nchi yake itaweza kuwaleta wagonjwa wa moyo badala ya kuwapeleka nchi za India
na Ulaya.
“Natamani na sisi Malawi tuwe kituo cha ubora katika kutoa huduma
za matibabu ya moyo kwani sasa tunatumia fedha nyingi kuwapeleka wagonjwa wetu
nchini India kwa ajili ya matibabu ya moyo wakati majirani zetu hapa
mmefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kutoa huduma za matibabu ya moyo”,
“Naamini kwa kuwaleta wagonjwa hapa Tanzania kutapunguza
gharama za matibabu, Malawi ni nchi wanachama wa SADC hivyo kupitia mwavuli huo
tunaenda kufanikiwa kwa wagonjwa wetu kuja kutibiwa hapa JKCI”, alisema Mhe.
Phale
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇