Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi kwa kutumia mashine ya Echocardiogram (ECHO) yanayoendelea katika Taasisi hiyo Jijini Dar Es Salaam. Mafunzo hayo yaliyoudhuriwa na wataalam wa afya zaidi ya 100 yamefanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini.
Na: Genofeva Matemu – Dar es Salaam
19/08/2022 Wataalam wa afya zaidi ya 100 kutoka hospitali binafsi
na hospitali za umma wameshiriki mafunzo yakimataifa ya siku mbili ya upimaji wa
jinsi moyo unavyofanya kazi kwa kutumia mashine ya Echocardiogram (ECHO) ambayo
yamefanyika kwa mara ya kwanza hapa nchini.
Akizungumza na waandhishi wa Habari wakati wa uzinduzi wa mafunzo
hayo leo Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete
(JKCI) Prof. Mohamed Janabi alisema kuwa mafunzo hayo yanatolewa na wakufunzi na
wabobezi wakuu wa magonjwa ya moyo kutoka nchini Marekani.
Prof. Janabi alisema kuwa lengo la mafunzo hayo nikuongeza ujuzi
kwa wataalam wa afya ili kusaidia na kupunguza wagonjwa ambao wanaingia gharama
kutoka mikoani kwenda JKCI kwa ajili ya kufanyiwa kipimo cha Echo kwani wakiweza
kuwagundua katika maeneo yao ya kazi wataweza kuchagua wagonjwa wanaohitaji kufanyiwa
matibabu zaidi na kuwatuma JKCI.
“Tumekua tukifanya mafunzo kama hayo huko nyuma lakini kwa kutumia
wataalamu wetu wa ndani ndio maana leo tunasema haya ni mafunzo yetu ya kwanza
yakimataifa kwasababu tuna wabobezi na wataalam zaidi katika uchunguzi wa jinsi
moyo unavyofanya kazi (ECHO) kutoka nchini Marekani”,
“Kwetu sisi wataalam wakutoa huduma za matibabu ya moyo,
hatuwezi kufanya upasuaji wa aina yoyote bila kufanya kipimo cha Echo hivyo ujuzi
tutakaoupata hapa utasaidia zaidi kuboresha huduma zetu na kuchagua wagonjwa wapi waende kwenye upasuaji
na wangapi wanaweza kutumia dawa bila ya kufanyiwa upasuaji”, aliseama Prof.
Janabi
Prof. Janabi alisema kuwa mafunzo ya upimaji wa jinsi moyo unavyofanyakazi
kwa kutumia mashine ya Echocardiogram (ECHO) yataendelea kutolewa kila mwaka kwa
wataalam wote wa afya bila kubagua waliopo katika hospitali za umma na zile za binafsi
ili kujifundisha mbinu mpya za kugundua matatizo ya moyo awali kabla ya tatizo kuwa
kubwa.
Mshiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Mbunge wa viti maalum Mhe.
Dkt. Alice Kaijage alisema kuwa ameshiriki mafunzo ya upimaji wa jinsi moyo unavyofanya
kazi kwa kutumia mashine ya Echocardiogram (ECHO) ili aweze kupata mbinu mpya na
zakisasa katika kutoa huduma za matibabu ya moyo.
“Nikiwa bungeni tuna kituo cha afya hivyo kwanjia moja ama nyingine
naweza kusaidiana na wenzangu kama mtaalamu kupima moyo unavyofanya kazi kwa wagonjwa
wanaofika katika kituo hicho lakini pia kupitia taaluma yangu natakiwa kuongeza
ujuzi ili niweze kuendana na maendeleo ya sayansi na teknolojia”
Kwa upande wake Mkufunzi kutoka Taasisi ya Piedmont Health
iliyopo Atlanta Georgia nchini Marekali Dkt. Mani Vannan alisema kuwa anaamini katika
mafunzo ya mara kwa mara katika taaluma ya afya na nimoja ya matamanio yake kuona
wataalam wa afya wanashiriki mafunzo ya kuongeza taaluma zao kila wanapopata fursa.
“Naamini Taasisi hii inamisingi mizuri katika taaluma ya upimaji
wa jinsi moyo unavyofanya kazi kwa kutumia mashine ya Echocardiogram (ECHO),
madhumuni ya mafunzo haya nikuifanya nchi hii kuwa kituo cha ubora katika utoaji
wa huduma za kibingwa za vipimo na matibabu ya moyo”, alisema Dkt. Mani
Naye Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Tiba Shirikishi katika Taasisi
ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Delila Kimambo alisema kuwa kipimo cha
kuangalia jinsi moyo unavyofanyakazi ni moja ya huduma za tiba shirikishi ambayo
nimuhimu kwa mtaalam wa afya kujua matatizo aliyonayo mgonjwa na kumpa mwelekeo
wa huduma gani mgonjwa anastahili kupewa.
“Mgonjwa yeyote wa moyo nilazima afanyiwe kipimo cha
kuangalia jinsi moyo unavyofanya kazi (ECHO), ni kipimo muhimu ambacho wataalam
waliopo hapa leo wanapaswa kukifahamu kwa undani zaidi ndio maana tumeandaa mafunzo
haya ili tuwakumbushe na kuwafundisha waweze kutoa huduma hiyo katika ubora zaidi”,
“Unapofanya kipimo cha Echo vyema zaidi unamsaidia mgonjwa kupata
huduma bora zaidi, kumpa taarifa sahihi itakayomsaidia katika matibabu yake pamoja
na kujua tatizo lake kama linahitaji dawa ama upasuaji”, alisema Dkt. Delila
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇