Na. WAF - Dar es Salaam
Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuhakikisha upatikanaji na ugawaji wa kingatiba zinapatikana na kuzigawa katika jamii kwenye maeneo yaliyo athirika na Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele nchini.
Hayo ameyasema Mfamasia wa Mpango wa Taifa wa Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTD) kutoka Wizara ya Afya Bi. Neema Nagu baada ya kumalizika kwa kikao kazi cha kupitia mpango kazi wa magonjwa hayo kwa mwaka 2021/22 kilichofanyika jijini Dar es Salaam.
"Katika kikao hiki pia tumepitia mpango wa mwaka 2022/23 ili kuonesha mpango wa Taifa wa kuendelea kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele hadi kufikia 2030 tuwe tumeyamaliza magonjwa haya kama alivyoagiza Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan." Amesema Bi. Nagu
Azimio hilo lililosainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan mnamo Januari 27, 2022 linaazimia hadi ifikapo mwaka 2030 magonjwa hayo yawe yametokomezwa nchini.
"Kama Wizara ya Afya na kama Mpango wa Taifa wa kudhibiti Magonjwa haya tumejipanga vizuri katika ugawaji wa kingatiba kwenye jamii lengo likiwa ni kuharibu mnyororo wa vimelea vinavyo ambukiza magonjwa haya." Amesema Bi. Nagu
Pia, Bi. Nagu amesema katika ugawaji wa kingatiba hizo wanazingatia kugawa kwa watoto wenye umri wa kuenda shule kuanzia miaka 5-14 na kwenye jamii yote katika maeneo yaliyoathirika ili kuhakikisha Mwananchi amepata kingatiba kwakuwa hata akiwa amepata vimelea kwenye mwili wake basi dawa hizo hutumika kama tiba.
Hata hivyo, Bi. Nagu amewataka wananchi kujitokeza pindi kingatiba hizo zinapotolewa katika maeneo yaliyoathirika ili kufikia azma ya Serikali kupitia Wizara ya Afya kutokomeza magonjwa hayo ifikapo 2030.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇