Na Mwandishi Maalum, Dodoma
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali itajenga shule mpya 1,026 ambapo kati ya hizo, shule 26 zitakuwa za bweni zenye uwezo wa kupokea wanafunzi kati ya 1,000 hadi 1,500 kwa kila mkoa na zitajengwa kwa awamu tatu.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Februari 13, 2021) katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa kuahirisha mkutano wa pili wa Bunge jijini Dodoma. Bunge limeahirishwa hadi Machi 30, mwaka huu.
Waziri Mkuu amesema shule nyingine mpya 1,000 za kutwa zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 400 kwa kila shule, zitajengwa chini ya mradi wa maboresho ya elimu ya sekondari yaani Secondary Education Quality Improvement Programme (SEQUIP) ambao utatekelezwa kwa muda wa miaka mitano (2020/2021 - 2025/2026).
Amesema Benki ya Dunia iliidhinisha mkopo wa kiasi cha dola za Marekani milioni 500 sawa na sh. trilioni 1.2 kwa ajili ya mradi huo, na kwamba ukikamilika, utakuwa ni mwarobaini kwa changamoto ya miundombinu ya shule za sekondari.
“Shule hizo zitajengwa kwenye kata 718 zisizo na sekondari za kata na kwenye maeneo yaliyoelemewa na idadi kubwa ya wanafunzi. Hivyo basi, nitumie nafasi hii kuwaelekeza viongozi na watendaji wa Serikali za Mitaa wasimamie kikamilifu utekelezaji wa mradi huu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa,” amesisitiza.
Wakati huohuo, akielezea suala la ukuzaji ujuzi miongoni mwa vijana, Waziri Mkuu amesema katika kipindi cha Julai, 2020 hadi Januari, 2021 vijana 10,178 wamepatiwa mafunzo na kutathminiwa ujuzi walioupata nje ya mfumo rasmi wa mafunzo nchi nzima ambapo vijana 9,736 wamefaulu na kupatiwa vyeti na Mamlaka ya Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA).
Amesema vyeti hivyo vinawawezesha vijana hao kutambulika, kujiendeleza kiujuzi, kujiajiri pamoja na kupata kazi katika taasisi na kampuni mbalimbali. “Vijana hao ni wenye ujuzi katika fani za uashi, useremala, ushonaji, ufundi bomba, uchomeleaji na uungaji vyuma, ufundi magari, ufundi umeme, ukarabati wa bodi za magari, upishi na uhudumu katika hoteli. Aidha, vijana 36 wamegharamiwa na Serikali kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo ya kilimo cha kisasa nchini Israel,” amesema.
“Katika nusu ya pili ya mwaka 2020/2021, vijana wapatao 4,616 watapatiwa mafunzo na kurasimishwa ujuzi walionao kupitia mfumo huu. Aidha, Januari 2021, vijana 1,203 wa vyuo vya elimu ya juu na kati wamehitimu mafunzo ya uzoefu wa kazi kupitia kampuni mbalimbali kulingana na fani walizosomea, na wahitimu 2,037 wamewezeshwa na wanaendelea kupata mafunzo ya uzoefu wa kazi katika taasisi binafsi na za umma ambayo yatachukua muda wa kipindi cha mwaka mmoja.”
Amesema wahitimu 2,421 wanaandaliwa ili waanze mafunzo Machi, 2021 katika fani za ushonaji nguo, useremala, uashi, uchorongaji vipuri, ufundi magari, umeme, bomba, terazo, upishi, na utoaji huduma za mahoteli, utengenezaji wa simu, majokofu, viyoyozi, upakaji rangi, uandishi wa alama, utengenezaji wa umeme wa magari, utengenezaji wa nywele na utanashati, uchoraji, n.k.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameeleza mikakati ya Serikali ya kuimarisha kilimo cha umwagiliaji nchini ambapo amesema katika kipindi cha mwaka 2015 hadi 2020, Serikali imefanikiwa kujenga na kukarabati skimu za umwagiliaji 179 ambazo zimeongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 461,000 mwaka 2015 hadi hekta 694,715 mwaka 2020 sawa na ongezeko la asilimia 50.7.
“Hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Taifa wa Umwagiliaji wa mwaka 2018 yaani Revised National Irrigation Master Plan (RNIMP 2018) ambao umeainisha hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliaji,” amesema.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imekamilisha ujenzi wa maghala 14 ya kuhifadhia mavuno katika skimu za umwagiliaji za Ngana na Makwale (Kyela), Magozi na Tungamalenga (Iringa), Mbuyuni-Kimani, Ipatagwa, Kongolo-Mswiswi na Motombaya (Mbarali), Lekitatu (Arusha), Mombo (Tanga), Uturo (Mbeya), Bagamoyo (Pwani), Mkindo na Mkula (Morogoro).
“Katika hatua ya kuongeza mnyororo wa thamani kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo, kati ya maghala hayo, maghala sita yamewekewa na vinu vya kukobolea mpunga,” ameongeza.
Ifuatayo ni Hotuba kamili ya Waziri Mkuu👇
HOTUBA YA MHESHIMIWA KASSIM M. MAJALIWA (MB.), WAZIRI MKUU WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, WAKATI AKIAHIRISHA MKUTANO WA PILI WA BUNGE LA 12, FEBRUARI 13, 2021
UTANGULIZI
1. Mheshimiwa
Spika, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema
kwa kutujalia afya njema hadi leo hii tunapohitimisha shughuli zote
zilizopangwa katika Mkutano huu wa Pili wa Bunge la Kumi na Mbili.
2. Mheshimiwa Spika, kwa
masikitiko makubwa naungana tena na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa salamu
za pole kwa Bunge lako Tukufu na kwa familia za waliokuwa Wabunge, Mheshimiwa
Martha Umbula Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara na Mheshimiwa Atashasta
Nditiye, Mbunge wa Muhambwe waliotangulia mbele za haki wakati wakiendelea
kulitumikia Taifa. Tunamwomba Mwenyezi
Mungu azipumzishe roho zao kwa amani.
3.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuwapa pole Watanzania
wenzangu waliopoteza ndugu, jamaa na marafiki na wengine kusababishiwa madhara
mbalimbali kutokana na ajali za barabarani na matukio mengine. Tunamuomba
Mwenyezi Mungu atupe subra na awape nafuu majeruhi wetu wapone haraka.
4.
Mheshimiwa
Spika, ninakushukuru sana wewe binafsi, Mheshimiwa Spika na Mheshimiwa Naibu
Spika kwa kusimamia kwa umahiri mkubwa majadiliano ya hoja kuhusu kujadili Hotuba
ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
aliyoitoa tarehe 13 Novemba, 2020 wakati akifungua Bunge la Kumi na Mbili sambamba
na Mpango wa Taifa wa Maendeleo.
5.
Mheshimiwa
Spika, ninawashukuru pia Waheshimiwa Wabunge kwa pongezi zenu kwa
Serikali na kwa michango yenu yenye dhamira ya dhati kabisa ya kuboresha
mipango na kazi zilizokusudiwa kutekelezwa na Serikali katika kipindi chote cha
miaka mitano. Mjadala huu umeendelea kuthibitisha uimara wa Bunge katika
kutekeleza wajibu wake wa Kikatiba wa kuishauri na kuisimamia Serikali
kikamilifu.
SHUGHULI ZA BUNGE
Maswali na Majibu
6.
Mheshimiwa
Spika, wakati wa mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge 164 na Mawaziri saba walichangia hoja ya kujadili Hotuba ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa tarehe 13 Novemba, 2020 wakati
akifungua Bunge la Kumi na Mbili. Aidha, Waheshimiwa Wabunge 126 walichangia Mpango wa Taifa wa
Maendeleo.
7.
Mheshimiwa
Spika, katika Mkutano huu jumla ya maswali 125 ya msingi na mengine 289
ya nyongeza yaliulizwa na Waheshimiwa Wabunge na kupatiwa majibu na
Serikali. Kadhalika, maswali 14 ya
papo kwa papo yaliulizwa na kujibiwa na Waziri Mkuu.
Kamati za Kudumu za Bunge
8.
Mheshimiwa Spika, natambua kuwa shughuli za utangulizi za
Mkutano huu zilianza tarehe 18 hadi 31 Januari 2021 kwa vikao vya Kamati za
Kudumu za Bunge sambamba na Chaguzi za Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati
za Kudumu za Bunge. Hivyo, nitumie fursa hii kuwapongeza wajumbe wote kwa kufanikisha
upatikanaji wa viongozi wa Kamati hizo ambao wameaminiwa na kuchaguliwa
kuongoza Kamati zetu.
9.
Mheshimiwa
Spika, ni matarajio yangu kwamba tutatumia nafasi hizo vizuri katika
kuleta ushirikiano, mshikamano na kufanya kazi pamoja kama wawakilishi wa
wananchi na kutekeleza majukumu yetu kwa kuisimamia na kuishauri Serikali.
10.
Mheshimiwa Spika, Serikali
kwa upande wake, itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kamati hizo ili
ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kuhakikisha tunaboresha utendaji
kazi na uwajibikaji hususan wakati huu tunapoelekea kwenye maandalizi ya Mpango
na Bajeti ya Mwaka 2021/2022.
11.
Mheshimiwa Spika, vilevile, nawashukuru sana Waheshimiwa
Mawaziri, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Naibu Mawaziri kwa kujibu vizuri
pamoja na kutoa ufafanuzi wa kina kuhusu hoja zilizowasilishwa na Waheshimiwa
Wabunge.
Miswada ya Serikali
12.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande mwingine, Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kujadili
Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2021 uliowasilishwa
na Serikali katika Mkutano huu.
Aidha,
Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Usajili wa Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu
wa Mwaka 2021 (The Accountants and
Auditors (Registration) (Amendment) Act, 2021) pamoja na Muswada
wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.2) wa Mwaka 2021 (The Written Laws (Miscellaneous Amendments)
(No.2) Act, 2021) ilisomwa kwa mara ya kwanza katika Mkutano huu.
13.
Mheshimiwa Spika, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa michango
yao mizuri wakati wa kujadili Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali wa Mwaka 2021 ambao kwa msingi wake ulikusudia kufanya marekebisho
katika Sheria ya Tafsiri ya Sheria (Sura ya 1), Sheria ya Mahakama za Mahakimu
(Sura ya 11) na Sheria ya Mahakama za Migogoro ya Ardhi (Sura ya 216). Lengo la
marekebisho hayo ni kuweka msingi wa lugha ya Mahakama, Mabaraza na vyombo
vingine vyenye jukumu la kutoa haki kuwa ni Kiswahili badala ya Kiingereza kwa
sababu Kiswahili ndiyo lugha ya Taifa, lugha ambayo inaeleweka na inatumika
katika shughuli zote za kijamii na za maendeleo nchini.
14.
Mheshimiwa Spika, marekebisho
haya yataimarisha mfumo wa upatikanaji haki kwa wananchi ambao wanakusudiwa
kuzitumia sheria husika. Serikali
itafanyia kazi maoni na ushauri uliotolewa nanyi Waheshimiwa Wabunge kwa lengo
la kuhakikisha utekelezaji wake unawanufaisha wananchi wote hapa nchini.
Mjadala
wa Hotuba ya Rais
15.
Mheshimiwa
Spika, katika mkutano huu moja ya agenda iliyochukua nafasi kubwa ni hoja
ya Serikali ya kujadili hotuba ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hoja hiyo tuliihitimisha vizuri na kwa
mafanikio makubwa.
16.
Mheshimiwa
Spika, kazi kubwa iliyoko mbele yetu ni kutekeleza yale tuliyokusudia
kama wajibu wetu. Hivyo basi, nitumie tena nafasi hii kuliahidi Bunge lako tukufu
kwamba michango ya Waheshimiwa Wabunge na maoni yao yatazingatiwa kwa
utekelezaji.
Mpango
wa Taifa wa Maendeleo
17.
Mheshimiwa
Spika, katika mkutano huu wa Bunge, Waheshimiwa Wabunge wamepata fursa ya
kujadili kuhusu tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano
(2016/2017-2020/2021), kujadili na kuidhinisha Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa
Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2021/2022-2025/2026) pamoja na kutoa maoni
na ushauri kuhusu Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na
Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2021/2022.
18.
Mheshimiwa
Spika, kipekee, naomba nimshukuru Mheshimiwa Dkt. Philip Isdor Mpango
(Mb.), Waziri wa Fedha na Mipango na Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb.),
Waziri wa Katiba na Sheria kwa kuwasilisha vizuri Mpango mbele ya Bunge lako
pamoja na Mheshimiwa Mwanaidi Ali Khamis (Mb.) Naibu Waziri wa Fedha na
Mipango, pamoja na Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri kwa ufafanuzi mzuri
walioutoa wakati wa kuhitimisha hoja hii.
UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI
YA MWAKA 2020/2021 KATIKA NUSU YA KWANZA JULAI – DESEMBA 2020
19.
Mheshimiwa Spika, Juni,
2020 Bunge lako tukufu liliidhinisha shilingi trilioni 34.88
ikiwa ni bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021. Kiasi hicho kinajumuisha, shilingi
trilioni 22.10
kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 12.78 kwa
ajili ya matumizi ya maendeleo.
20.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha
Julai hadi Desemba 2020, ridhaa ya matumizi iliyotolewa ilikuwa shilingi trilioni 13.12 sawa na asilimia 82.8 ya lengo. Kati ya kiasi kilichotolewa, shilingi
trilioni 10.52 ni fedha
za matumizi ya kawaida sawa na asilimia 95.2
na shilingi trilioni 2.60
ni fedha za maendeleo sawa na asilimia 54.2.
21.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa fedha za maendeleo, kiasi
cha shilingi bilioni
730.7 kutoka kwa washirika wa maendeleo zilizopelekwa
moja kwa moja kwenye utekelezaji wa miradi na hivyo kufanya utekelezaji wa
bajeti ya maendeleo kufikia asilimia
69.4. Kadhalika, kiasi cha
shilingi bilioni 254.6 kilitumika kulipa malimbikizo ya madai
yaliyohakikiwa ya watumishi, makandarasi na watoa huduma.
Mfumuko wa Bei
22.
Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei nchini umeendelea kuwa tulivu na
kubakia katika viwango vya chini. Kwa mfano, mfumuko wa bei kwa Desemba 2020 ulikuwa
asilimia 3.2 ikilinganishwa na asilimia 3.8 Desemba 2019. Kwa hiyo, katika
kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2020/2021, mfumuko wa bei ulikuwa wa
wastani wa asilimia 3.2, ndani ya lengo la muda wa kati la asilimia 5.0.
23.
Mheshimiwa Spika, kiwango hicho cha mfumuko wa bei kilitokana na
upatikanaji wa chakula cha kutosha katika masoko ya ndani na nchi jirani, bei
ndogo ya mafuta kwenye soko la dunia, utulivu wa thamani ya shilingi ya
Tanzania dhidi ya dola ya Marekani na sarafu nyingine duniani, na utekelezaji
madhubuti wa sera za fedha na bajeti.
Mafanikio, Changamoto na Mikakati katika utekelezaji wa
bajeti ya Serikali kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2020/2021
24.
Mheshimiwa Spika, wakati wa mkutano huu, Bunge lako tukufu lilipokea
na kujadili mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na
Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2021/2022 pamoja
na Mapendekezo ya Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa
Taifa wa Miaka Mitano 2021/2022 – 2025/2026.
25.
Mheshimiwa Spika, wakati tukiendelea na maandalizi ya utekelezaji wa
mipango hiyo kwa kipindi cha mwaka 2021/2022, nami nitumie nafasi hii kuwaeleza Waheshimiwa
Wabunge wenzangu na wananchi wote baadhi ya mambo makubwa na mafanikio
yaliyopatikana katika kipindi hicho cha nusu ya kwanza ya mwaka wa fedha wa
2020/2021.
26.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya
utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2020/2021 (yaani Julai
hadi Desemba 2020) yapo mafanikio mengi yaliyopatikana. Kadhalika, zipo
changamoto zilizoibuka na kuifanya Serikali kuja na mikakati ya kukabiliana na
changamoto hizo katika kipindi cha miezi sita ya pili ya mwaka ili kufikia
malengo yaliyowekwa kwa mwaka 2020/2021.
27.
Mheshimiwa Spika, niruhusu japo kwa uchache nieleze baadhi ya
mafanikio machache yaliyopatikana katika utekelezaji
wa bajeti ya Serikali kwa kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2020/2021. Aidha,
baadhi ya mafanikio ni muendelezo wa utekelezaji wa mipango ya maendeleo.
28.
Mheshimiwa Spika, mafanikio
hayo ni pamoja na Serikali kugharamia kwa mara ya kwanza Uchaguzi Mkuu wa mwaka
2020 kwa kutumia fedha za ndani ambapo shilingi bilioni 268.5 zilitumika. Serikali pia ililipa shilingi
bilioni 254.6 madeni ya wazabuni na watumishi yaliyohakikiwa; shilingi trilioni
3.64
mishahara ya watumishi; shilingi bilioni 124.8
kwa ajili ya kugharamia sera ya elimumsingi bila ada na shilingi bilioni 105.1
kwa ajili ya kugharamia
mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, uimarishaji wa vyuo vya ufundi stadi
(VETA) na kukuza ujuzi kwa vijana.
29.
Mheshimiwa Spika, mafanikio mengine ni kuendelea kutekeleza miradi
mbalimbali ya kimkakati kama ifuatavyo: -
- Ujenzi wa Reli ya Kati Kwa Kiwango cha Kimataifa (Standard Gauge Railway) ambapo ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km 300)
umefikia asilimia 90 na kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422)
umefikia asilimia 49.2. Aidha, tayari Serikali imesaini mkataba wa ujenzi
wa kipande cha Mwanza - Isaka (km 341) wenye thamani ya shilingi trilioni 3.07; na kuendelea kutafuta fedha kwa ajili ya
ujenzi wa vipande vya Makutupora – Tabora (km 294) na Tabora – Isaka (km
133). Shilingi bilioni 274.1 zimetumika katika
nusu ya kwanza ya mwaka 2020/2021. Baada ya kukamilika matengenezo hayo,
tutaanza kuunganisha vipande vya Tabora - Kigoma na Tabora – Mpanda.
- Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere (Megawati 2,115): Utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 25.8 ambapo shilingi
bilioni 128.9 zimetumika nusu
ya kwanza ya mwaka 2020/2021;
- Kuboresha Shirika la Ndege la
Tanzania: Serikali imekamilisha malipo ya mwisho ya ununuzi wa
ndege aina ya Bombadier Dash 8-Q400 na Boeing 787-8 Dreamliner na malipo
ya awali ya ununuzi wa ndege tatu (3), ambapo ndege mbili (2) ni aina ya
Airbus A220-300 na moja (1) ni Dash 8-Q400 De-Havilland na hivyo kuwezesha
Serikali kuwa na ndege mpya 11 kutoka ndege moja (1) iliyokuwepo mwaka
2015 na kuifanya ATCL kuwa na jumla ya ndege 12 ambapo ndege tatu (3)
zinatarajiwa kuwasili mwaka 2021/2022 ili ziweze kutoa huduma. Shilingi
bilioni 2.8 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/2021;
- Viwanja vya Ndege na Rada: Kukamilika kwa jengo la tatu la abiria katika Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) chenye uwezo wa kuhudumia abiria milioni
sita kwa mwaka; kuendelea na ujenzi wa viwanja vya Geita (asilimia 86),
Songea (asilimia 91) na Mtwara (asilimia 49.0); kukamilika kwa maandalizi
ya mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Msalato ambao
utagharimu dola za Marekani milioni 330, sawa na shilingi bilioni 759;
uzinduzi wa ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege vya Shinyanga, Kigoma,
Tabora na Sumbawanga vinavyogharimu Euro milioni 50 sawa na shilingi
bilioni 136.85; kuanza kwa ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege Musoma;
kukamilika kwa ukarabati wa karakana ya matengenezo ya ndege na kununuliwa
kwa magari mapya matatu (3) ya zimamoto yenye uwezo wa kubeba lita za maji
10,000 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA);
kupanuliwa kwa barabara ya kuruka na kutua ndege katika kiwanja cha ndege
cha Dodoma; kufungwa kwa mifumo ya kuongoza ndege (AGL) katika viwanja vya
ndege vya Dodoma, Tabora na Mwanza; na kupanuliwa na kukarabatiwa kwa
viwanja vya ndege vya Bukoba, Mwanza, Arusha, Nachingwea na Iringa. Shilingi bilioni 4.5
zimetumika katika nusu ya kwanza ya
mwaka 2020/2021;
- Usambazaji wa Umeme Vijijini kupitia mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini na
makao makuu ya wilaya (REA - III): Hadi Desemba 2020, jumla ya vijiji 10,018 kati ya
vijiji 12,317 sawa na asilimia 81.3 vilikuwa vimeunganishiwa umeme ambapo katika
kipindi cha nusu ya kwanza ya 2020/21 shilingi bilioni 171.9 zimetolewa na kazi inaendelea;
- Kuboresha usafiri wa
abiria na mizigo katika Maziwa Makuu:
Ziwa Victoria:
Kukamilika kwa ukarabati wa meli mbili za New Butiama Hapa
Kazi Tu na New Victoria Hapa Kazi Tu; kuendelea na ujenzi
wa meli mpya ya MV Mwanza Hapa kazi Tu yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na
tani 400 za mizigo; kukamilika kwa ujenzi wa Chelezo cha kujengea na kukarabati
meli katika Bandari ya Mwanza; kupatikana kwa mkandarasi kwa ajili ya ukarabati
wa meli za MV Umoja na MV Serengeti; kukamilika ukarabati wa meli za MV.
Clarias na ML. Wimbi.
Ziwa Tanganyika: kukamilika kwa mikataba kwa ajili ya Ujenzi wa Meli Mpya
yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na tani 400 pamoja na ukarabati wa meli ya MV
Liemba; na ukarabati wa meli ya MT Sangara kwenye Ziwa Tanganyika ambapo katika
nusu ya kwanza ya mwaka 2020/2021 shilingi bilioni
12.8 zimetumika. Tumeboresha bandari za Kibirizi, Sibwesa, Kagunga, Kabwe,
Kasanya na sasa tunajenga bandari Kalema ambapo shilingi bilioni 86.4
zimetumika;
Shughuli nyingine zilizokamilika ni: Ujenzi wa magati ya Lushamba, Ntama, Nyamirembe,
Magarine na Gati la majahazi Mwigobero; ununuzi wa vifaa vya kuhudumia mizigo
na meli; ukarabati wa majengo na ofisi za bandari za Ziwa Victoria; kuboresha
eneo la kushukia abiria Mwanza North; na ukarabati wa ‘Link Span’ ya bandari ya
Mwanza South;
Ziwa Nyasa: Kukamilika
kwa ujenzi wa matishari mawili (2) yenye uwezo wa kubeba tani 1000 kila moja;
na ujenzi wa meli moja mpya ya MV Mbeya II yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na
mizigo tani 200 umekamilika na imeanza kufanya kazi. Shilingi bilioni 1.5 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka
2020/2021;
- Ujenzi wa Barabara na Madaraja Makubwa: Kujengwa kwa mtandao wa
barabara kwa kiwango cha lami wenye urefu wa kilomita 3,537 (barabara kuu
na za mikoa kilomita 2,208.62 na barabara za halmashauri kilomita 1,328)
na hivyo kufanya mtandao wa barabara uliojengwa kwa kiwango cha lami hadi mwaka
2019/2020 kufikia kilomita 13,044 ambapo kilomita 10,939 ni barabara kuu
na kilomita 2,105 ni barabara za mikoa. Ujenzi huu umeongeza uwiano wa mtandao wa barabara za lami nchini
kutoka asilimia 6.8 mwaka 2015/2016 hadi asilimia 8.9 mwaka 2019/2020;
- Uendelezaji wa Mji wa Serikali Mtumba - Dodoma: Serikali imeanza maandalizi ya awamu ya pili ya ujenzi
wa majengo ya ofisi katika Mji wa Serikali Mtumba yatakayotosheleza
watumishi wote. Katika mwaka 2019/2020, Serikali imekamilisha usanifu wa
majengo husika. Aidha, mradi wa ujenzi wa barabara (km 51.2) kwa kiwango
cha lami katika Mji wa Serikali utakaogharimu jumla ya shilingi bilioni
89.13 unaendelea, ambapo malipo ya awali ya shilingi bilioni 13.21
yamefanyika na ujenzi umefikia asilimia 56;
- Miradi ya Vivuko: Kukamilisha ujenzi wa vivuko vipya vya Kigongo - Busisi (Mwanza),
Bugolora – Ukara (Mwanza) na Kayenze – Bezi (Mwanza). Aidha, ujenzi wa
kivuko kipya cha Nyamisati – Mafia (Pwani) na Chato – Nkome (Geita) umekamilika.
Vilevile, ujenzi wa boti mpya tano (5) za uokozi kwa ajili ya kisiwa cha
Ukerewe (Ilugwa, Nafuba na Gana), kivuko cha Magogoni – Kigamboni na Lindi
– Kitunda unaendelea. Pia, ukarabati mkubwa wa MV Kigamboni umekamilika na
ukarabati wa kivuko MV Sengerema umefikia asilimia 90;
- Mifugo: Kujenga
kiwanda kipya cha Kilimanjaro
International Leather Industries Company Ltd chenye uwezo wa kuzalisha
jozi na soli za viatu 1,200,000 kwa mwaka na kuchakata ngozi futi za mraba
13,000,000 kwa mwaka; kuimarisha kituo cha Taifa cha Uhimilishaji cha NAIC
kilichopo USA River, Arusha kwa kununua kifaa (Chiller) kwa ajili ya
mtambo wa kuzalisha kimiminika cha naitrojeni; kujengwa kwa viwanda vipya
vya kimkakati vya nyama vya Tanchoice
(Pwani), Elia Food Oversees
Limited (Arusha) na Binjiang
Company Limited (Shinyanga); kujengwa kwa kiwanda cha maziwa cha Galaxy Food and Beverage Company Limited (Arusha); kujengwa kwa kiwanda
cha kuzalisha chanjo cha Hester
Bioscience Africa Limited
(Pwani) chenye uwezo wa kuzalisha chanjo aina 37; na kuendelea kuboresha
huduma za malisho ya mifugo na majosho.
- Uvuvi: Kuongezeka kwa uzalishaji/uvunaji wa samaki katika maji ya asili
kutoka tani 362,645 zenye thamani ya shilingi trilioni 1.48 mwaka 2015/2016
hadi tani 497,567 za samaki zenye thamani ya shilingi trilioni 2.34 mwaka
2019/2020; kuongezeka kwa usindikaji wa minofu ya samaki aina ya Sangara
kutoka tani 23,000.58 mwaka 2015/2016 hadi tani 27,596.27 mwaka 2019/2020;
kuongezeka kwa huduma za usafirishaji wa mazao ya uvuvi kwenda masoko ya
Ulaya ambapo katika mwaka 2019/2020, jumla ya kilo 777,750.0 za mabondo
zilisafirishwa; kuongezeka kwa mauzo ya samaki na mazao ya uvuvi nje ya
nchi kutoka mauzo yenye thamani ya shilingi bilioni 379.25 mwaka 2015/2016
hadi shilingi bilioni 506.24 mwaka 2019/2020; na kuendelea na maandalizi
ya ujenzi wa bandari ya uvuvi (Mbegani). Katika nusu ya kwanza ya mwaka
2020/2021 shilingi milioni 606.7 zimetumika;
- Miradi ya
Maji: Kukamilika kwa miradi 1,423 ya maji iliyotekelezwa mijini na
vijijini. Baadhi ya miradi iliyotekelezwa na hatua zilizofikiwa ni: kukamilika
kwa miradi ya maji katika miji ya Geita, Njombe na Songwe na kuendelea kwa
ujenzi wa mradi wa maji katika mji wa Kigoma (asilimia 90); utekelezaji wa
mradi mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Isaka, Tinde,
Kagongwa, Tabora, Igunga, Uyui na Nzega umefikia asilimia 98; kukamilika kwa asilimia 76 ya ujenzi wa mradi wa maji
katika Jiji la Mwanza; kukamilika kwa asilimia 62 ya ujenzi wa mradi
wa maji katika Jiji la Arusha; na kuendelea na ujenzi wa mradi wa
maji wa Same – Mwanga – Korogwe
ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 65. Aidha, katika eneo
linalohudumiwa na DAWASA (mikoa ya Dar es Salaam na Pwani) utekelezaji wa
miradi umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 na umehusisha maeneo ya
Kibamba hadi Kisarawe, Mlandizi hadi Chalinze, Kisarawe-Pugu-Ukonga,
Mkuranga-Vikindu, Jet-Buza, Kisarawe, Kigamboni, Mkuranga, Chalinze, Mbezi
Luis hadi Kiluvya, Tegeta, Wazo, Madale, Mivumoni, Mabwepande na Bagamoyo
(maeneo ya Vikawe, Zinga, Mapinga na Kerege).
Kwa
ujumla miradi yote iliyotekelezwa imewezesha wananchi zaidi ya milioni 25
kupata huduma ya maji ambapo wastani wa idadi ya watu wanaopata huduma ya maji
safi na salama imeongezeka kutoka asilimia 74
mwaka 2015 hadi asilimia 84
mwaka 2020 kwa mijini na kutoka asilimia 47
mwaka 2015 hadi asilimia 70.1
mwaka 2020 kwa vijijini. Aidha, kwa Jiji la Dar es Salaam, upatikanaji wa maji
safi umeongezeka kutoka asilimia 72
mwaka 2015 hadi asilimia 90
Desemba, 2020. Shilingi bilioni 226.7 zimetumika katika nusu ya kwanza
ya 2020/2021. Kazi ya usambazaji maji vijijini inaendelea;
- Afya: Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi ya sekta ya afya ambayo
imefikia hatua mbalimbali ikiwemo: asilimia 98 ya ujenzi wa jengo la mama
na mtoto katika Hospitali ya Rufaa Mwananyamala; Ujenzi wa jengo la maabara
katika Hospitali ya Rufaa Njombe umefikia asilimia 73; ujenzi wa jengo la
mama na mtoto, upasuaji, radiolojia na maabara katika Hospitali ya Rufaa
Simiyu umefikia asilimia 50. Shilingi bilioni 64.6 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka
2020/2021 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya afya, ununuzi wa
vifaa, vitendanishi, dawa na chanjo; na
- Miradi ya
Kimkakati ya Kuongeza Mapato Katika Halmashauri: Katika
kuhakikisha kuwa Mamlaka za Serikali za Mitaa zinaongeza mapato kwa
kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao, Serikali ilitoa shilingi bilioni
91.4 kwa ajili ya kugharamia miradi 26. Kati ya fedha hizo, shilingi
bilioni 50.6 zilitolewa mwaka 2019/2020. Miradi ya ujenzi iliyotekelezwa
ni pamoja na; stendi za mabasi (9), machinjio (2), viwanda vidogo (3),
maegesho ya malori (2), masoko (9) na ghala la mazao (1). Katika kipindi
cha nusu ya kwanza ya 2020/2021, Serikali imetoa shilingi bilioni 19.9
kwa ajili ya kugharamia miradi ya kimkakati;
30.
Mheshimiwa Spika, licha ya mafanikio hayo makubwa ambayo nimejaribu
kueleza kwa uchache, vilevile, katika utekelezaji wa mpango na bajeti ya Serikali
kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2020/2021, zipo changamoto kadhaa zilizojitokeza.
Changamoto hizo ni pamoja na uharibifu wa
miundombinu ya barabara uliosababishwa na mafuriko; kupungua
kwa shughuli za kibiashara duniani kutokana na athari za mlipuko wa homa kali
ya mapafu; kasi
ndogo ya ukuaji wa uchumi;
na ukwepaji kodi kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu, hususan kupitia
biashara za magendo, kutokutoa na kudai stakabadhi za kielektroniki wakati
mauzo yanapofanyika na kasi ndogo ya ukusanyaji wa kodi ya majengo.
31.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha Januari hadi Juni 2021,
Serikali itaendelea kuchukua hatua na kutekeleza mikakati mbalimbali kwa lengo
la kuongeza mapato na kuimarisha usimamizi wa matumizi ili kufikia malengo kwa
kipindi kilichobaki cha mwaka 2020/2021. Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja
na kuendelea kuchukua hatua za tahadhari dhidi ya majanga na kufanya ukarabati
wa miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko na kuimarisha ukaguzi wake.
32.
Mheshimiwa Spika,
halikadhalika, Serikali itaendelea kusimamia nidhamu ya matumizi
ya fedha za umma kwa kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima; kuhakikisha nakisi ya
bajeti haizidi asilimia 3.0 ya Pato la Taifa na hivyo, kuendana na makubaliano
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki; kuelekeza fedha kwenye maeneo ya kipaumbele
yatakayochochea ukuaji wa uchumi; kuhakikisha miradi inayoendelea inapewa
kipaumbele kabla ya miradi mipya; kudhibiti ulimbikizaji wa madai; na kuongeza kasi
ya matumizi ya TEHAMA katika miamala na shughuli za Serikali.
33.
Mheshimiwa Spika,
sambamba na hayo, Serikali itatekeleza
mikakati mahususi ya kuongeza mapato kwa kufanya yafuatayo:-
Mosi: Kuimarisha mifumo ya usimamizi kwa kuhakikisha kuwa
wafanyabiashara wote wanatumia mashine za kutolea risiti za kielektroniki (EFD);
Pili: Kuimarisha ushirikiano kati ya mamlaka zinazokusanya mapato ya Serikali na
vyombo vya ulinzi na usalama katika kufanya doria maeneo ya mipaka ya nchi
kavu, baharini na kwenye maziwa ili kudhibiti biashara za magendo;
Tatu: Kukasimisha jukumu la kukusanya kodi
ya majengo kwa Halmashauri na Serikali za Mitaa.
34.
Mheshimiwa Spika, niwashukuru tena Waheshimiwa Wabunge kwa kuibua hoja
ambazo zilifanya mjadala wetu humu Bungeni kuwa wa kina na wenye kutoa
msisimko wa kiwango cha juu. Yote hayo, yalitokana na ukweli kwamba Waheshimiwa
Wabunge, waliibua hoja na kuchangia kwa umakini mkubwa kwa lengo kujenga na
kusaidia taifa letu.
35.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande mwingine kupitia hoja na michango yao, Waheshimiwa
Wabunge wamegusia masuala muhimu ikiwemo elimu, kilimo, uwezeshaji, uwekezaji, viwanda
na miundombinu ambayo yamekuwa kitovu cha mjadala na michango ya Waheshimiwa
Wabunge. Kwa msingi huo, naomba nitumie fursa hii adhimu kutolea ufafanuzi
baadhi ya masuala muhimu yaliyoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge.
ELIMU
Miundombinu ya Elimu
36.
Mheshimiwa Spika, kupitia Mkutano huu wa Pili wa Bunge lako tukufu,
Waheshimiwa Wabunge wameibua hoja nyingi kuhusu changamoto ya miundombinu ya
shule hususan sekondari, suala la ujuzi na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya
juu. Nyingi ya changamoto hizi, zinatokana na utekelezaji mzuri wa sera ya
Elimumsingi Bila Malipo sambamba na ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya
shule na vyuo ambao umechangia kuongezeka kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza na
hata darasa la kwanza kila mwaka.
37.
Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa
samani na miundombinu, Serikali imeweka mikakati mbalimbali ikiwemo ya muda
mfupi na muda mrefu. Lengo la Serikali ni kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu
mtihani wa Darasa la Saba wanajiunga na kidato cha kwanza bila kujali ni chaguo
la kwanza au la pili na kuhakikisha miundombinu yote na samani zote kwa ajili
ya kuwapokea wanafunzi hawa inakamilika ifikapo tarehe 28 Februari, 2021.
38.
Mheshimiwa Spika, Benki ya Dunia iliidhinisha mkopo wa kiasi cha
Dola za Marekani milioni 500 sawa na takriban shilingi za Tanzania trilioni 1.2
kwa ajili ya mradi wa maboresho ya elimu ya sekondari yaani (Secondary Education Quality Improvement Programme
- SEQUIP). Mradi huo, uliidhinishwa
mwaka jana licha ya kelele nyingi kutoka kwa watu wasiokuwa na uzalendo na nchi
hii.
39.
Mheshimiwa Spika, mradi huo, utakaotekelezwa kwa muda wa miaka
mitano (2020/2021 - 2025/2026) utakuwa ni mwarobaini kwa changamoto ya
miundombinu ya shule za sekondari kwani shule mpya 1,026 zitajengwa kote
nchini. Kati ya shule hizo, shule mpya 26 zitakuwa za Bweni zenye uwezo
wa kupokea wanafunzi kati ya 1,000 hadi 1,500 kwa kila mkoa na
zitajengwa kwa awamu tatu.
40.
Mheshimiwa Spika, kadhalika, Shule mpya 1,000 za kutwa zitajengwa
zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 400 kwa kila shule. Shule hizo
zitajengwa kwenye kata 718 zisizo na sekondari za kata na kwenye maeneo
yaliyoelemewa na idadi kubwa ya wanafunzi. Hivyo basi, nitumie nafasi hii
kuwaelekeza viongozi na watendaji wa Serikali za Mitaa wasimamie kikamilifu
utekelezaji wa mradi huu ili kufikia
malengo yaliyokusudiwa.
Mikopo ya Elimu ya Juu
41.
Mheshimiwa Spika, kuhusu mikopo ya elimu ya juu, kwa mwaka huu
2020/2021 Serikali imetoa mikopo kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza 55,287
ambapo wanafunzi 28,041 sawa na asilimia 5 wamehitimu elimu ya sekondari
katika shule mbalimbali za binafsi. Serikali itaendelea kuzingatia kigezo pekee
cha uhitaji wa mwombaji sambamba na kurahisisha matumizi ya mtandao katika
uombaji na utoaji wa mikopo.
42.
Mheshimiwa Spika, katika kuongeza ufanisi wa utoaji na urejeshaji wa
mikopo ya elimu ya juu, Serikali imefanya maboresho ya kisheria, kimfumo na
kiutendaji kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita (2015/2016 – 2019/2020).
Matunda ya maboresho hayo ni pamoja na kuongezeka kwa makusanyo kutoka wastani
wa shilingi 28.9 bilioni mwaka 2016/2017 hadi kufikia
wastani wa shilingi 192 bilioni mwaka 2019/2020.
43.
Mheshimiwa Spika, Serikalini inafarijika na inapokea kwa mikono miwili
michango yenye afya na tija kuhusu hatma ya mikopo inayotolewa na Serikali baada
ya miaka 15 ya uwepo wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu.
44.
Mheshimiwa Spika, nilihakikishie Bunge lako tukufu kwamba Serikali
kwa upande wake, ipo tayari kuendelea kujifunza kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge
na wananchi wote nchini kuhusu namna bora zaidi ya kuufanya mfuko huu uwe
endelevu na wenye manufaa katika ujenzi wa uchumi wa nchi yetu. Hivyo basi,
katika kuufanya mfuko huo uwe endelevu na himilivu; nitumie fursa hii kuelekeza
mambo yafuatayo;
Kwanza: Ninaitaka
Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ishirikiane na Bodi ya Mikopo ya
Wanafunzi wa Elimu ya Juu ili kuboresha huduma zake na kurahisisha urejeshwaji
wa mikopo kwa wanufaika waliojiari katika sekta binafsi, ikiwa ni pamoja na
kutoa elimu kwa umma kuhusu haki na wajibu wa mnufaika na mwajiri.
Pili: Ninawasihi wanufaika wote wa mikopo ya elimu ya juu,
ambao bado hawajajitokeza na kuanza kurejesha, wafanye hivyo mara moja;
Mwisho: Ninawataka
waajiri wote nchini katika sekta binafsi na sekta ya umma, watoe kipaumbele kwa
makato ya mikopo ya elimu ya juu kama yalivyo makato mengine ya kisheria; na
Ukuzaji
Ujuzi
45.
Mheshimiwa Spika, ukuzaji ujuzi ni miongoni mwa hoja iliyoungwa mkono
na Wabunge wengi wakati wa kuchangia hoja mbalimbali hususan ya elimu wakati wa
mkutano huu. Hivyo, nami nitumie nafasi hii kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba
katika kipindi cha Julai, 2020 hadi Januari, 2021 vijana 10,178
wamepatiwa mafunzo na kutathminiwa ujuzi walioupata nje ya mfumo rasmi wa
mafunzo nchi nzima ambapo vijana 9,736 wamefaulu na kupatiwa vyeti na
Mamlaka ya Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA).
46.
Mheshimiwa Spika, vyeti hivyo vinawawezesha kutambulika, kujiendeleza
kiujuzi, kujiajiri pamoja na kupata kazi katika taasisi na kampuni mbalimbali.
Vijana hao ni wenye ujuzi katika fani za uashi, useremala, ushonaji, ufundi
bomba, uchomeleaji na uungaji vyuma, ufundi magari, ufundi umeme, ukarabati wa
bodi za magari, upishi na uhudumu katika hoteli. Aidha, vijana 36 wamegharamiwa
na Serikali kwa ajili ya kuhudhuria mafunzo ya kilimo cha kisasa nchini Israel.
47.
Mheshimiwa Spika, katika nusu ya pili ya mwaka 2020/2021
vijana wapatao 4,616 watapatiwa mafunzo na kurasimishwa ujuzi walionao
kupitia mfumo huu. Aidha, mwezi Januari 2021, vijana 1,203 wa vyuo vya
elimu ya juu na kati wamehitimu mafunzo ya uzoefu wa kazi kupitia kampuni
mbalimbali kulingana na fani walizosomea, na Wahitimu 2,037 wamewezeshwa
na wanaendelea kupata mafunzo ya uzoefu wa kazi katika taasisi binafsi na za
umma ambayo yatachukua muda wa kipindi cha mwaka mmoja. Vilevile, Wahitimu 2,421
wanaandaliwa kwa ajili ya kuanza mafunzo mwezi Machi, 2021 katika fani za ushonaji nguo,
useremala, uashi, uchorongaji vipuri, ufundi magari, umeme, bomba, terazo, upishi,
na utoaji huduma za mahoteli, utengenezaji wa simu, majokofu, viyoyozi, upakaji
rangi, uandishi wa alama, utengenezaji wa umeme wa magari, utengenezaji wa
nywele na utanashati, uchoraji, n.k.
Barabara
48.
Mheshimiwa Spika, kumejitokeza mjadala unaohitaji uboreshaji
miundombinu ya barabara za mijini na hasa za vijijini. Vyombo vyetu vya
TANROADS na TARURA vinafanyia kazi na sasa tunakusudia kuongeza uwezo wa vyombo
hivyo. Kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge tumepokea ushauri wenu na tutaufanyia kazi
ili tuweze kufanya maboresho.
KILIMO
Hali ya Kilimo katika Msimu huu
wa kilimo
49.
Mheshimiwa Spika, katika msimu wa mvua wa mwaka 2020/2021, mvua za vuli zilizoanza mapema
mwezi Septemba zimeendelea kunyesha kwa kiwango cha juu ya wastani katika
maeneo mengi hasa ya Kanda ya Ziwa Victoria. Katika maeneo mengine ya Pwani ya
Kaskazini na Kanda ya Kaskazini Mashariki, mvua zilichelewa kuanza (Novemba) na
zimeendelea kunyesha hadi katika mwezi Januari, 2021.
50.
Mheshimiwa
Spika, kwa ujumla, hadi
kufikia mwishoni mwa mwezi Januari, mwenendo wa unyeshaji wa mvua hizo
umeendelea kwa kiwango cha juu ya wastani katika maeneo mengi. Mwelekeo
unaonesha kuwa mvua hizi zitachangia upatikanaji wa chakula katika kipindi cha
mwezi Februari na kuendelea kabla ya mavuno mengine kuanzia mwezi Mei, 2021. Vilevile,
hali ya malisho ya mifugo na upatikanaji wa maji umeendelea kuwa mzuri katika
maeneo yote nchini.
Kuimarisha
Kilimo cha Umwagiliaji
51.
Mheshimiwa
Spika, katika kipindi cha mwaka 2015
hadi 2020, Serikali imefanikiwa kujenga na kukarabati skimu za umwagiliaji
179 ambazo zimeongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 461,000
mwaka 2015 hadi hekta 694,715 mwaka 2020 sawa na ongezeko la asilimia
50.7. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Taifa wa
Umwagiliaji wa mwaka 2018 (yaani Revised National Irrigation Master Plan - RNIMP
2018) ambao umeainisha hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa kilimo cha
Umwagiliaji.
52.
Mheshimiwa
Spika, vilevile,
Serikali imekamilisha ujenzi wa maghala 14 ya kuhifadhia mavuno katika skimu za
umwagiliaji za Ngana na Makwale (Kyela), Magozi na Tungamalenga
(Iringa), Mbuyuni-Kimani, Ipatagwa, Kongolo-Mswiswi
na Motombaya (Mbarali), Lekitatu (Arusha), Mombo (Tanga), Uturo
(Mbeya), Bagamoyo (Pwani), Mkindo na Mkula (Morogoro).
53.
Mheshimiwa
Spika, katika hatua ya
kuongeza mnyororo wa thamani kwenye uzalishaji wa mazao ya kilimo, kati ya
maghala hayo, maghala 6 yamewekewa na vinu vya kukobolea mpunga.
54.
Mheshimiwa
Spika, nimeamua kusema
haya ili Waheshimiwa Wabunge na Watanzania kwa ujuma wafahamu kwamba tunatambua
umuhimu wa kilimo cha umwagiliaji na tunachukua hatua.
Upatikanaji wa pembejeo za kilimo na uzalishaji wa mbegu
55.
Mheshimiwa
Spika, Serikali
imeweka mikakati ya kuhakikisha pembejeo zinawafikia wakulima kwa wakati ambayo
ni pamoja na kupata mahitaji halisi ya pembejeo za kilimo kutoka kila mkoa kabla
ya msimu wa kilimo kuanza na kuwasiliana na Makampuni ya pembejeo na kuyahimiza
kusambaza pembejeo hizo mapema kulingana na mahitaji ya kila mkoa.
56.
Mheshimiwa
Spika, pia, Serikali inaboresha mifumo ya uzalishaji, uagizaji
na uthibiti wa mbegu bora na viuatilifu hapa nchini ikiwemo kuimarisha
uzalishaji wa pembejeo hizo ndani ya nchi ili kukidhi mahitaji na upatikanaji wake
kwa wakati.
57.
Mheshimiwa Spika, katika kufikia malengo, Serikali
itaongeza eneo la ASA la uzalishaji wa mbegu kutoka hekta 4,925 (2019/2020)
hadi hekta 6,923 ifikapo 2025 na eneo la TARI kutoka hekta 1,033.2 hadi hekta 3,663.24
ifikapo 2025.
Huduma za Ugani
58.
Mheshimiwa Spika, uzalishaji na tija katika kilimo, pamoja na mambo
mengine huchangiwa na maarifa na ujuzi unaotolewa na Maafisa Ugani kwa
wakulima. Kwa mantiki hiyo,
Serikali inalenga kuhakikisha kuwa kila kijiji, mtaa na kata vinakuwa na Afisa Ugani
angalau mmoja ili kuwawezesha wakulima kupata maarifa na ujuzi wa kuzalisha
mazao kwa ufanisi na tija.
59.
Mheshimiwa
Spika, idadi ya Maafisa Ugani
waliopo nchini ni 6,704 ikilinganishwa na mahitaji 20,538. Aidha, katika
kukabiliana na changamoto ya uhaba wa Maafisa Ugani, Wizara inaendelea
kusomesha Maafisa Ugani tarajali katika ngazi ya Cheti na Diploma ambapo
kuanzia mwaka 2015 hadi 2020 jumla ya wataalamu wa kilimo 8,657 walihitimu
katika vyuo vya mafunzo ya kilimo ngazi ya Cheti na Diploma.
UWEZESHAJI WANANCHI KIUCHUMI
Mifuko na Programu za Uwezeshaji
Wananchi Kiuchumi
60.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyotangulia kueleza, suala la uwezeshaji
Wananchi iwe kwenye sekta ya kilimo au ujasiriamali na biashara ndogo na za
kati ni miongoni mwa hoja zilizoibuliwa na Waheshimiwa Wabunge. Suala hilo, pia
limejitokeza wazi wazi kwenye hotuba ya Dkt. John Pombe Joseph Magufuli,
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoitoa tarehe 13 Novemba, 2020 wakati
akifungua Bunge la 12.
61.
Mheshimiwa Spika, katika hotuba hiyo, Mheshimiwa Rais aliielekeza
Ofisi ya Waziri Mkuu kuhakikisha kuwa inaimarisha uratibu na usimamizi wa
Mifuko na programu za uwezeshaji wananchi kiuchumi ili Watanzania waifahamu ilipo,
vigezo vya kutolea mikopo na aina ya mikopo. Lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi
wananufaika na mikopo hiyo ili kuinua vipato vyao, kupunguza umaskini na tatizo
la ajira.
62.
Mheshimiwa Spika, licha ya changamoto zinazokabili mifuko na programu
za uwezeshaji wananchi kiuchumi, katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka
2015/2016 hadi 2019/2020, mifuko na programu za uwezeshaji za serikali
zimefanikiwa kutoa mikopo yenye thamani zaidi ya shilingi trilioni 2.22,
kunufaisha zaidi ya watu milioni 4.9 na taasisi 5,499.
63.
Mheshimiwa Spika, vilevile, kupitia mifuko ya uwezeshaji wa makundi
maalumu ya Vijana, Wanawake na Watu wenye Ulemavu Halmashauri 185 zimefanikiwa kutoa shillingi bilioni
93.3. Fedha hizo, zimewezesha upatikanji wa mikopo yenye masharti nafuu kwa
vikundi 32,553 kote nchini.
64.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha malengo hayo yanafikiwa napenda
kuliarifu Bunge lako tukufu kwamba tumeanza kuchukua hatua zenye kulenga kuboresha
huduma za mifuko na programu za uwezeshaji. Tarehe 17 Novemba, 2020
tulianza zoezi la tathmini ya utendaji wa programu na mifuko takriban 20.
Aidha, tayari taarifa ya awali kutoka ngazi ya Wataalamu imekamilika na
kuwasilishwa kwenye mamlaka husika.
65.
Mheshimiwa Spika, tarehe 9 Februari 2021 nilifungua wiki ya maonesho
ya nne ya mifuko na programu za uwezeshaji kwa kanda ya Kaskazini yanayofanyika
kwenye viwanja vya Sheikh Amri Abeid, Arusha. Ni Matumaini yangu kwamba kupitia
maonesho hayo wananchi wa mkoa wa Arusha, mikoa ya kanda ya Kaskazini pamoja na
wananchi kutoka sehemu mbalimbali nchini watapata uelewa mpana kuhusu shughuli
za mifuko na programu za uwezeshaji.
Mabenki na Mifuko ya Fedha Kuchangia Kilimo
66.
Mheshimiwa Spika, wakati tukiendelea na mkutano huu, Waheshimiwa
Wabunge walieleza kwa kina kuhusu changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima
na wafanyabiashara wetu hususan wadogo katika shughuli zao za kiuchumi na
kujiongezea kipato hususan masuala ya uzalishaji, masoko, ufungashaji bora wa
bidhaa, huduma za fedha, elimu ya ujasiriamali, teknolojia n.k.
67.
Mheshimiwa Spika, ni dhahiri kwamba mchango wa sekta ya fedha hususan
mabenki na mifuko ya hifadhi za jamii kwenye kilimo bado ni mdogo kwani
hadi sasa upo kwenye asilimia 8.5
sawa na shilingi trilioni 1.65. Kwa msingi huo, Serikali inaendelea kufanya
mazungumzo na Benki na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuona namna ambavyo watachangia
katika shughuli za kilimo na mnyororo mzima wa thamani.
Uwezeshaji wa Wajasiriamali
Wadogo (Machinga)
68.
Mheshimiwa Spika, Serikali
inatambua na kuthamini sana mchango mkubwa unaotolewa na wafanyabiashara wadogo
(Wamachinga) katika kukuza uchumi, kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja, kuondoa
umaskini na kuleta maendeleo endelevu nchini. Sekta hii ya wafanyabiashara wadogo nchini inakadiriwa kuwa na wajasiriamali
milioni 3.1 ambao wameajiriwa sawa
na takriban asilimia 23.4 ya nguvu
kazi ya Taifa.
69.
Mheshimiwa Spika, katika kuhakikisha wadau wa sekta hii
wanaendesha shughuli zao bila kubughudhiwa, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph
Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliamua kugawa vitambulisho
vya wajasiriamali wadogo. Hata hivyo, licha ya mafanikio makubwa ya vitambulisho hivyo,
vimeonesha kuwa na changamoto mbalimbali ambazo zinahitaji maboresho hususan katika
kuwasaidia kupata mikopo na mitaji kutoka kwenye taasisi za fedha ili waweze
kuendesha shughuli mbalimbali za ujasiriamali.
70.
Mheshimiwa Spika, katika kuwasadia wajasiriamali wadogo kupata mitaji kwa urahisi kupitia taasisi
za fedha, Serikali imeanza taratibu za kuboresha Vitambulisho vya
Wafanyabiashara Wadogo kwa mwaka 2021. Vitambulisho hivyo vitakuwa vya
kielektroniki na vitaboreshwa zaidi
hatua kwa hatua ili viwawezesha wafanyabiashara wadogo kukopa kutoka taasisi za
fedha ikiwemo programu na mifuko ya uwezeshaji.
71.
Mheshimiwa Spika, tarehe 28 Januari,
2021 nilipata fursa ya kufungua Kongamano la Wafanyabiashara Wadogo (maarufu
Wamachinga) lililofanyika Jijini Dar es Salaam. Lengo la Kongamano hilo, pamoja
na mambo mengine lilikuwa ni kuwashirikisha wadau hao kuhusu namna nzuri zaidi
ya kuboresha vitambulisho vya wafanyabiahara wadogo (Wamachinga) ili waweze
kuvitumia kupata mitaji au mikopo kutoka kwenye mabenki na taasisi za fedha.
72.
Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kuwapongeza wafanyabiashara wadogo
(Wamachinga) kwa kutekeleza vyema jukumu la usambazaji wa bidhaa nchini kwa bei
nzuri wanazozimudu wananchi hasa wale wa kipato cha chini. Aidha, nitoe rai kwa
Machinga wote kuepuka
kushirikiana na wafanyabiashara wakubwa wanaowatumia kukwepa kodi; kwa kuwapa
bidhaa nyingi bila kutoa risiti za kielektroniki zenye kiwango halisi cha bei
ya kununulia bidhaa husika.
73.
Mheshimiwa Spika, wakati tunaendelea na zoezi la
kuboresha vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo, naagiza viongozi na
watendaji wa Serikali za Mitaa washirikiane na viongozi wa wafanyabiashara
wadogo kwenye maeneo yao ili kupata orodha yao na kuwaandalia maeneo ya kufanyia
biashara zao.
MICHEZO
74.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi cha hivi karibuni nchi yetu imepata mafanikio mbalimbali hususan
katika mpira wa miguu. Nitumie nafasi hii kutoa pongezi zangu kwa Waziri wa
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) kwa mafanikio makubwa yanayojitokeza kwa upande wa soka na
michezo mingine kama ngumi hapa nchini. Mathalan, katika kipindi hiki
tumeshuhudia Tanzania ikishiriki fainali za mashindano ya Afrika ya Mpira wa
Miguu kwa wachezaji wanaocheza ligi ya ndani (CHAN) ambayo yamekamilika hivi
karibuni huko Cameroon.
75.
Mheshimiwa
Spika, nizipongeze pia timu za Taifa
za umri wa chini ya miaka 20 na 17 ambazo zimefuzu kushiriki katika mashindano
ya Fainali za Bara la Afrika kwa mwaka 2021. Timu hizi zitakwenda kushiriki
katika fainali za michuano hiyo katika nchi za Morocco kwa U-17 na Mauritania
kwa timu ya U-20. Vilevile, naipongeza timu
ya Wanawake U-17 kushinda kombe la COSAFA kwa mashindano yaliyofanyika Afrika
Kusini, Novemba 2020.
76.
Mheshimiwa
Spika, kwa upande wa
soka la vilabu, naipongeza Namungo FC kwa kufanikiwa kuvuka hatua mbili za
awali kuelekea kwenye makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika na pia niwatakie kila
la heri kwenye mchezo wao utakaochezwa kesho Jumapili huko nchini Angola.
77.
Mheshimiwa
Spika, nawapongeza pia
mabingwa wa Soka Tanzania, timu ya Simba
Sports Club kwa kufanikiwa kufuzu kuingia hatua ya makundi katika mashindano ya
Klabu Bingwa Afrika, na jana kushinda mchezo wake wa kwanza katika hatua ya
makundi wakiwa ugenini dhidi ya Klabu ya AS Vita huko Jamhuri ya Kidemokrasia
ya Kongo. Nitumie nafashi hii kumpongeza Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, mwanadada
Barbra Gonzalez kwa ubunifu na kushirikisha Wizara ya Maliasili na Utalii na
hivyo kulipa heshima Taifa letu kwa kulitangaza kupitia jezi yao kwa maneno
VISIT TANZANIA huu ni uzalendo wa hali ya juu ambo unapaswa kupongezwa na
kuigwa.
78.
Mheshimiwa Spika, mchambuzi maarufu wa michezo nchini Bw. Ali Kamwe,
kupitia ukurasa wake wa instagram, ameeleza vizuri maana ya matumizi ya neno
VISIT TANZANIA na namna nchi yetu itakavyonufaika na ubunifu huo. Kwa
mujibu wa maelezo yake, neno VISIT TANZANIA linakadiriwa kutazamwa na wapenzi
wa soka takriban milioni 500 kutoka sehemu mbalimbali duniani. Wapenzi hao wa
mpira kupitia vituo vya Televisheni vya Canal Algérie, BeIN Sports, Eurosport,
ESPN, Arryadia, GTV ya Ghana, MENA beIN Sports na West Africa Canal+ wameshuhudia
mchezo wa jana. Kwa lugha nyingine ni kwamba neno 'VISIT TANZANIA' lililopo
sehemu ya kifuani mwa jezi ya Klabu ya Simba litaonekana kupitia chaneli hizo
kwa kila dakika 90 ambazo Simba itashuka dimbani iwe dhidi ya Al-Ahly (Misri), El-Mereikh
(Sudan) au dimba la nyumbani kwa Mkapa (Tanzania). Tutavuta watalii wengi
kuifuatilia Nchi yetu.
79.
Mheshimiwa Spika, nchi yetu imeendelea kung’ara pia kwenye medani ya
masumbwi. Kwa upande huo wa masumbwi, nawapongeza mabondia Mfaume Mfaume kwa
kufanikiwa kutetea ubingwa wa East and Central Africa mwezi Decemba 2020; Bondia
Ibrahimu Class Mgendera kwa kushinda Ubingwa wa World Boxing Federation
Intercontinental lightweight (WBF). Vilevile, nawapongeza Bondia Tonny
Rashidi aliyefanikiwa kutetea mkanda wake wa African Boxing Union (ABU) na
Bondia Shabani Hamadi JONGO aliyeshinda ubingwa wa WBF International Cruiserweight
mwishoni mwa Januari 2021. Bila kuwasahau Mabondia walioonesha uwezo mkubwa wa
kina Hassan Mwakinyo, Twaha Kiduku na Dulla Mbabe ambaye atapanda ulingoni tarehe
26 Februari, 2021.
HITIMISHO
80.
Mheshimiwa Spika, nihitimishe hotuba yangu kwa kuwashukuru tena Waheshimiwa
Wabunge kwa michango yenu muhimu mliyoitoa kwa lengo la kuboresha maisha ya
wananchi wetu. Nimshukuru Katibu wa Bunge, wasaidizi wake na watumishi wote wa
Bunge kwa huduma nzuri na msaada mkubwa ambao wamekuwa wakitupatia kwa kipindi
chote tulichokuwa tukitekeleza majukumu yetu ya Mkutano wa Pili wa Bunge la 12.
81.
Mheshimiwa Spika, nawashukuru pia viongozi na watendaji wa Serikali
na taasisi zake ambao wameendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, umahiri
na ufanisi mkubwa. Hongereni sana kwani juhudi zenu zimekuwa chachu ya
kufanikisha shughuli zilizopangwa kwenye Mkutano huu wa Pili wa Bunge la 12. Vilevile,
nitakuwa mchoyo wa fadhila endapo sitowashukuru wanahabari kwa uchambuzi mzuri wa
hoja na mwenendo mzima wa Bunge na kuwahabarisha wananchi.
82.
Mheshimiwa Spika, vilevile, nivishukuru vyombo vya ulinzi na usalama
kwa huduma ambazo wamekuwa wakizitoa kwa washiriki wa Bunge hili. Pia,
niwashukuru madereva wote waliotuhudumia wakati wote tukiwa hapa Bungeni na ninawatakia
heri katika safari ya kurejea nyumbani.
83.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, sasa naomba kutoa hoja
kwamba Bunge lako tukufu liahirishwe hadi tarehe 30 Machi 2021 siku ya Jumanne saa tatu kamili asubuhi katika ukumbi huu hapa Jijini Dodoma.
84. Mheshimiwa Spika, sasa naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇