LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 13, 2021

MBUNGE MWAKANG'ATA AKABIDHI MSAADA WA MASHINE ZA KUSAGA NA KUKOBOA KWA UWT SUMBAWANGA


 

MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Rukwa, Bupe Mwakang’ata ametoa msaada wa mashine za kusaga na kukoboa kwa Umoja wa Wanawake (UWT) Wilaya ya Sumbawanga Mjini. Mkoa Rukwa.

 

 Katika hafla hiyo iliyofanyika hivi karibuni mjini Sumbawanga, mbunge huyo alisema kuwa mashine hizo maalumu kwa mradi wa UWT  zimegharimu sh. milioni 4.5.

 

Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo, Mbunge Mwakang’ata, alisema  ameamua kufanya hivyo ikiwa ni shukrani kwa wananchi waliomwezesha kushika wadhifa huo, lakini pia kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli za kuwawezesha wanawake kiuchumi.

 

Baadhi ya wanachama wa UWT, walimshukuru Mwakang’ata kwa msaada huo mkubwa na kuahidi kuutunza na kuutumia vizuri ili uwaletee mafanikio kwa lengo la kuwakomboa kiuchumi.


Katibu wa UWT Wilaya ya Sumbawanga Mjini, Algla Salinyambo alimshukuru Mbunge Mwakang'ata kwa msaada huo mkubwa na kwamba kitendo hicho ni sawa  na kuwavisha wanawake nguo kwani walikuwa hawana hata mradi mmoja.


"Tumejisikia vizuri na kujawa na faraja, kwa msaada wa mashine hizo, tuna imani alichokitoa kitainufaisha UWT , kwani tulikuwa hatujui pa kugusa, tulikuwa hatuna hata mradi mmoja, tunafurahi tumeupata, ametuvisha nguo wanawake, Mungu amzidishie pale alipotoa,"alishukuru Salinyambo.


Sainyambo anasema wamejipanga vizuri kuhakikisha mradi huo unakuwa endelevu na kuleta tija ya kuwaendeleza kiuchumi wanawake. Pia amesema wanaweka mambo sawa ili mradi huo uanze kufanya kazi mapema iwezekanavyo.


Naye, Katibu wa CCM Wilaya ya Sumbawanga Mjini, Tabu Hussein, alisema kuwa wamejisikia faraja kupata mradi huo na kumshukuru Mbunge Mwakang'ata kwa kuwakomboa wanawake kwa kutimiza lengo la chama la kujitegemea kiuchumi kuliko kuwa ombaomba.

 

Katika hafla hiyo, Mwakang’ata pia alitoa mifuko 200 ya saruji yenye thamani ya sh. milioni 12 kwa shule 10 za msingi zilizofanya vizuri katika mitihani ya darasa la saba na shule 10 zenye mahitaji maalumu katika manispaa ya Sumbawanga.

 

Vilevile, aliwazawadia vyeti,  katoni za sukari na zawadi zinginezo kwa walimu ambao shule zilifanya vizuri.

 

Lakini pia, alikabidhi madawati 50  yenye thamani ya  sh. Milioni 3.5 kwa Shule ya Msingi Manzitiswe iliyopo Manispaa ya Sumbawanga.

 

Akipokea madawati hayo, Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Lasko Manase alisema yeye na wajumbe wa  kamati ya shule, wameupokea msaada huo kwa furaha kubwa kwani umepunguza kwa kiasi kikubwa upungufu wa madawati shuleni hapo.

 

 Mwalimu Manase amewaomba wadau wengine akiwemo mbunge wa Sumbawanga Mjini, Aishi Hillary na wabunge wengine kuunga mkono juhudi za Mwakang’ata kwa kutoa msaada wa mabawati yaliyobakia.

 

Naye Afisa Elimu Msaidizi wa Manispaa ya Sumbawanga, Graseana Killenga alimshukuru sana Munge Mwakang’ata kuwapatia  msaada huo na kuulinganisha kama lulu na kwamba saruji hiyo itasaidia sana kupunguza uhaba wa matundu ya vyoo na kusaidia ujenzi wa baadhi ya vyumba vya madarasa katika shule hizo kumi.


Kwa undani zaidi sikiliza yaliyojiri kupitia video hii....

IMEANDALIWA NA; 
RICHARD MWAIKENDA 
MHARIRI BLOG YA TAIFA YA CCM 
0754264203

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages