Na Richard
Mwaikenda, Dodoma
HOSPITALI ya Uhuru iliyopo wilaya ya Chamwino, Dodoma
tayari imeanza kutoa huduma kwa wagonjwa tangu Desemba 21, mwaka jana.
Akizungumza
na waandishi wa habari hospitalini hapo jana, Mganga Mfawidhi wa hospitali
hiyo, Dkt. Pius Kagoma, amesema kuwa hadi juzi Januari 11, wamehudumia takribani
wagonjwa 239.
Amesema hadi sasa watumishi 50 wamesharipoti kazini
na wengine wanaendelea kuwapokea kwa ajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa
hospitalini hapo.
Aidha, Dkt.
Kagoma amesema licha ya miundominu michache kuwa katika hatua za mwisho kukamilishwa,
lakini hadi sasa asilimia 99 hospitali
hiyo imekamilika na wanasubiri ufunguzi rasmi.
Dkt. Kagoma
ametaja wagonjwa wanaoendelea kuwatibia kuwa ni; wagonjwa wanachama wa Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF), na wagonjwa wanaotibiwa bure ambao ni wazee,
wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano pamoja na wananchi wengine.
Kuhusu vifaa
vya tiba, Dkt. Kagoma amebainisha kuwa vipo vya kutosha vikiwemo vya vifaa vya mionzi,
madawa na vya kujifungulia na kwamba vingine vinaendelea kuletwa.
Alitaja
baadhi ya changamoto zilizopo kuwa ni; kutokamilika kwa ujenzi wa barabara ya
kuingia hospitalini hapo, baadhi maboma ya maji kutotoa maji lakini anaamini kwa
muda mchache uliobakia mambo yote yatawekwa sawa.
Hospitali
hiyo ambayo imejengwa baada ya Rais John
Magufuli kuelekeza huko fedha zilizotakiwa kutumika katika maadhimisho ya
Sikukuu za Uhuru na gawio la serikali
kutoka Kampuni ya Simu ya Airtel, itakuwa na uwezo wa kuhudumia wagonjwa
kati ya 500,000 hadi 1,000,000 kwa mwaka.
Dkt. Kagoma
amesema kuwa kwa asilimia kubwa itakuwa inahudumia watumishi wa Ikulu ya
Chamwino, watumishi kutoka Mji wa Kiserikali wa Mtumba, wananchi wa vijiji jirani pamoja na wananchi wote kwa ujumla.
Alisema
amefurahi sana kuwa miongoni mwa watumishi wa kwanza kuhudumia hospitali hiyo
mpya na kuahidi kwamba yeye na watumishi walioko chini yake watafanya kazi kwa
bidii ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais Magufuli za kufanikisha
hospitali hiyo kujengwa.
Kwa uhondo zaidi wa tukio hili naomba uendelee kusikiliza kupitia kwenye video hii....
IMEANDALIWA NA;
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇