Jul 26, 2019

TRUMP AUPIGA VETO MUSWADA WA CONGRESS WA KUPIGA MARUFUKU UUZAJI SILAHA KWA SAUDIA NA IMARATI

Ikiwa ni katika kuwaunga mkono washirika wake wa Asia Magharibi na pia kunufaika kiuchumi, Rais Trump alitangaza hali ya hatari nchini Marekani ili kupata mwanya wa kukwepa idhini ya Congress ya nchi hiyo katika kuziuzia silaha za thamani ya dola bilioni 8 nchi za Saudi Arabia, Imarati na Jordan. hatua hiyo ya Trump iliwakasirisha sana wabunge wa Marekani ambao katika kipindi hiki chote wamekuwa wakifanya juhudi za kupitisha muswafa wa kuzuia mauzo hayo makubwa ya silaha.
Pamoja na hayo, Jumatano usiku Trump alitumia uwezo wake wa veto au turufu kupinga muswada uliokuwa umepitishwa na bunge la Congress kwa ajili ya kusimamishwa mauzo hayo ya silaha na vilevile kutangazwa hali ya hatari nchini. Ili kuutengua uamuzi huo wa Trump Congress sasa inahitaji kupata thuluthi mbili ya kura za bunge hilo, jambo linaloonekana kuwa mbali kwa kutilia maanani kwamba baadhi ya wabunge wa chama cha Republican katika bunge hilo wanaunga mkono siasa za Trump kuhusiana na Saudia.
Trump alitangaza hali ya hatari nchini Marekani kwa kisingizio cha kuongezeka mvutano baina yake na Iran, na hivyo kuamua kuziuzia Saudi Arabia, Imarati na Jordan kiwango hicho cha silaha. Kwa kutangaza hali ya hatari nchini, rais wa Marekani anaruhusiwa kupuuza baadhi ya sheria zinazohusiana na udhibiti wa mauzo ya silaha na kuuza silaha hizo bila ya kupata idhini ya Congress.
Congress ya Marekani
Mwezi Aprili mwaka huu pia wabunge walipitisha muswada wa kuitaka Marekani isitishe ushirikiano wake na Saudia katika mashambulio ya nchi hiyo dhidi ya Yemen. Kuhusiana na suala hilo, Seneti ya Marekani ilipitisha muswada wa kumkemea Trump kutokana na hatua yake ya kuipuuza Congress katika masuala yanayohusiana na usalama wa taifa na kutangazwa hali ya hatari nchini. Waungaji mkono wa muswada huo wa Congress wanaamini kwamba ni Congress hiyo ndiyo inayopaswa kuchukua uamuzi wa mwisho kuhusiana na Marekani kushiriki katika vita vyovyote nje ya mipaka ya nchi na sio rais.
Kupitia muswada huo wabunge wa vyama vyote viwili vikuu vya Marekani yaani Democrat na Republican walionyesha kuchukizwa kwao na msimamo wa Trump wa kutoiadhibu Saudi Arabia kutokana na mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi mkosoaji mkubwa wa utawala wa Saudia aliyeuawa kinyama mwezi Oktoba mwaka uliopita katika ubalozi mdogo wa nchi hiyo huko Istanbul Uturuki.
Kwa mujibu wa gazeti la New York Times, hakuna suala jingine lolote linalozusha mvutano mkali katika siasa za nje kati ya Trump na Congress, kama lilivyo suala la Saudia.
Kama alivyofanya siku ya Jumatano usiku, tarehe 16 Aprili mwaka huu pia Trump aliupiga veto muswada wa Congress uliotaka kusimamishwa mara moja uungaji mkono wa Marekani kwa muungano wa kijeshi wa Saudi Arabia dhidi ya Yemen. Kwa hatua yake hiyo, Trump amewathibitishia wabunge wa Congress na hasa wa chama cha Democrat kuwa uamuzi wa mwisho kuhusiana na masuala ya usalama wa taifa na mauazo ya silaha uko mikononi mwa rais wa nchi na sio congress.
Uhusiano mkubwa wa Trump na watawala wa Saudia
Siasa za utawala wa Trump zimejengeka katika msingi wa kuunga mkono kwa hali na mali utawala wa Saudia. Nchi hiyo ya kifalme inahesabiwa kuwa mshirika wa kistratijia wa Marekani katika Asia Magharibi na moja ya nchi zinazonunua kwa wingi silaha za Marekani. Imarati pia ni miongoni mwa nchi zinazonunua kwa wingi silaha za Marekani. Kwa msingi huo Marekani haiko tayari kukata uhusiano huo kwa hali yoyote ile. Kuhusiana na suala hilo, tovuti ya Marekani ya Concervative imeandika kwamba Saudi Arabia ni mfano mzuri wa jinsi mauzo ya silaha za Marekani yanavyoharibu usalama wetu na wa Asia Magharibi. Si tu kwamba wanazitumia silaha hizo kuua maelfu ya watu wasio na hatia nchini Yemen, bali kwa msaada wa Imarati katika baadhi ya sehemu, silaha hizo hupewa manamgambo na washirika wao wa kigaidi.
Licha ya ukosoaji wa iana hiyo, lakini Trump anazitazama nchi hizo na hasa Saudia kwa jicho la biashara ambapo amekuwa akiidhalilisha mara kwa mara kwa kuitaja kuwa ni sawa na ng'ombe wa kukamwa anayepaswa kukamwa hadi mwisho wake

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Pages