Siku chache baada ya kujiuzulu Waziri wa Afya wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo akidai kuingiliwa majukumu yake, baadhi ya wanasiasa wameeleza wasiwasi walionao kuhusu taarifa za kuanza kutumika chanjo mpya ya Ebola ambayo haijafanyiwa majaribio.
Wakati wasiwasi wa kuenea Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ukiongezeka, mbunge mmoja wa mashariki mwa nchi hiyo ameibuka na kuwataka wananchi wake kutokubali kupewa chanjo hiyo ambayo haijathibitishwa.
Muhindo Nzangi Butondo amekuliwa akisema kuwa, hataki kuona wananchi wake wanatibiwa kama nguruwe wa Guinea. Mbunge huyo amesisitiza kuwa, anachotaka kwanza ni kuona chanjo mpya iliyoanza kutolewa inathibitishwa.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, chanjo pekee iliyokubaliwa na bodi ya maadili ya DRC na Shirika la Afya Duniani (WHO) ni ile ya Merck ambayo imeonesha kuwa na ufanisi kwa asilimia 95.7 kutibu Ebola, lakini sasa kuna dawa nyingine 2 inasemekana zimeanza kutumika.
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa watu zaidi ya 1,700 wameaga dunia ndani ya miezi 11 iliyopita kutokana na ugonjwa hatari wa Ebola tangu uripuke upya nchini Kongo DR mwezi Agosti mwaka jana 2018.
Mfumuko mkubwa zaidi wa ugonjwa wa Ebola ulitokea baina ya Disemba 2013 na Aprili 2016 na kuua zaidi ya watu 11,000 katika nchi za magharibi mwa Afrika za Guinea, Liberia na Sierra Leone.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇