Jan 12, 2025

MKUTANO WA 'MISSION 300', RC CHALAMILA AKOLEZA MAANDALIZI DAR, ATOA ONYO KALI KWA VIBAKA, AHIMIZA USAFI UTAMALAKI KILA ENEO

Na Bashir Nkoromo, CCM's Blog, Dar es Salaam
Wakati maandalizi ya Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika (Mission 300) utakaofanyika kwa siku mbili kuanzia Januari 27, 2025, yanazidi kupamba moto, Jiji la Dar es Salaam ambamo utafanyika mkutano huo limezidi kukaa mguu sawa kuhakikisha unafanyika kwa amani, upendo na usalama.

Katika kuhakikisha hayo, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila, ameendelea kutoa maelekezo kwa wananchi wa kada mbalimbali kujiandaa na kufanyika mambo mbalimbali ikiwemo kuimarisha usalama, usafi wa mazingira na kuutumia mkutano huo kama fursa ya maendeleo.

RC Chalamila ametoa baadhi ya maelezo hayo jana, Jumamosi, Januari 11, 2025, alipokuwa na timu yake, katika kufanya usafi kwenye maeneo mbalimbali ya jijini Dar es Salaam ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano huo na pia kutekeleza ufanyaji usafi kila Jumamosi ya kwanza ya kila mwezi.

Akizungumza na wafanyabisahara wa Soko la Samaki la Feri, RC Chalamila aliwataka wananchi mbali na kwamba usafi ni jambo la muhimu wakati wote lakini kuelekea mkutano huo ni muhimu zaidi kuhakikisha wanazingatia kufaya usafi katika maeneo ya shughuli zao ili wageni watakapofpata fura ya kuyatembelea wakute yanavutia.

RC Chalamila alitoa onyo kali kwa yeyote hasa vibaka wakataojaribu kujihusisha na uhalifu huo, akisema atachukuliwa hatua kali za kisheria tofauti na wakati mwingine wowote ambapo alisema, wakati mwingine huwa kuna kusamehe au kuchukulia hatua  ndogondogo lakini katika siku za kuelekea mkutano huo na nyakati za mkutano wenyewe atakayethubu atakiona cha moto.

"Natoa onyo, natoa onyo, nasema tena natoa onyo, kibaka yeyote atakayethubutu kufanya ukibaka wake wakati huo, nasema kichwa chake kitageuzwa 'skeletoni' ambayo itatumia kufundishia wengine ubaya wa kuwa kibaka. Nasema mkiwapata nasema msiwaue, lakini hakikisheni mnachukua sherika kali", akasema RC Chalamila.

Alisema, baadhi ya barabara kama inayotoka Feri hadi Hyati Hotel zitafungwa kutumiwa na baadhi ya vyombo vya usafiri ikiwemo bajaji na bodaboda, na taa za barabarani zitaboreshwa ili kuwezesha viongozi na wageni mbalimbali watakaohitaji kufanya mazoezi wafanye katika mazingira mazuri.

“Rais, Dk. Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa  kuitangaza Tanzania kimataifa, hii imefanya taasisi za kimataifa, Kampuni na Wawekezaji kuona Tanzania ni sehemu sahihi ya kufanya biashara na uwekezaji na mfano halisi ni hili la Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo Afrika kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huu mkubwa wa kimataifa utakahudhuriwa viongozi kutoka nchi 54 barani Afrika, hivyo lazima tuone fahari na kumuunga mkono Rais kwa kuuenzi mkutano huu.”  akasema RC Chalamila.

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamika akizungumza na wananchi katika soko kuu la samaki, Feri jana.

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Pages