Imeelezwa kuwa Serikali ya Awamu ya sita, inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ushirikiano wa ufadhili wa Benki ya Dunia kupitia mpango dharura ( CERC PROJECTS), imetoa kiasi cha Shilingi Bilioni 45.6 kutekeleza miradi mitano (5).
Miradi hiyo ni pamoja na Daraja la Kyanyabasa (mita 105), Daraja la Kalebe (mita 60), Daraja la Kamishango (mita 45),Daraja la Kyetema (mita 45) na Daraja la Kanino (mita 30) pamoja na barabara unganishi ambazo zinatekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya leo tarehe 12 Januari 2025, Mkoani Kagera wakati akikagua miradi iliyoathiriwa na mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya.
“Nimshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kukubali kutoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 45 ili kujengwa kwa miradi hii ambayo imeathiriwa na mvua za El-nino na kuweza kujengwa upya”, amesema Mhandisi Kasekenya.
Aidha, Mhandisi Kasekenya ameongeza kwa kusema kuwa miradi ya dharura ikianza kujengwa haisimami kwa sababu inatekelezwa kwa njia ya dharura na kukamilika ndani ya muda uliopangwa wa miezi 12 kwa kujali ubora na viwango vya juu.
Vilevile, amewataka Wakandarasi wazawa walioaminiwa kujengewa uwezo kutekeleza miradi hiyo mikubwa kwa wakati uliopangwa na kwa ubora.
Naye, Mbunge wa Bukoba Vijijini, Dkt. Jason Rweikiza amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweza kutoa fedha za kujenga miradi hiyo ambayo iliathiriwa na mvua za el-nino kwani kukamilika kwa miradi hiyo ya dharura kutasaidia wananchi wa Bukoba mjini na vijijini kupita kwenye madaraja hayo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS, Mkoa wa Kagera, Mhandisi Ntuli Mwaikokesya, amesema miradi hii ni sehemu ya juhudi za Serikali katika kuboresha miundombinu ya usafiri na kuhakikisha maendeleo endelevu kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya akitoa maelekezoalipokuwa akikagua miradi iliyoathiriwa na mvua za El-Nino na Kimbunga Hidaya mkoani Kagera.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇