Dar es Salaam, Tanzania
MSIMU wa sikukuu za mwisho wa mwaka umefika, kwa mwaka huu wa 2023. Sikukuu hizi ni Krismas ambayo inaadhimishwa na Wakristo Disemba 25 kukumbuka kuzaliwa kwa Mwokozi wao Yesu Kristo.
Sikukuu nyingine ni ya mkesha wa mwaka mpya ambayo inafanyika usiku wa Disemba 31 na baadhi ya watu hukesha hadi Januari Mosi kusheherekea Mwaka mpya.
Hizi ni sikukuu ambazo zinasheherekewa duniani kote. Baadhi ya familia hufanya safari za utalii ndani ya nchi zao, lakini wengine husafiri hadi nchi nyingine kutokana na mapendekezo yao.
MSIMU WA KUJIPA RAHA
Kwa ujumla ni msimu ambapo watu hasa wale wenye uwezo, wanajipa raha katika maeneo wanayopenda. Kuna michezo mbali mbali ikiwemo kuogelea, muziki, kwenda mbugani kuangalia wanyamapori, kadhali na kadhalika.
Hapa kwetu Tanzania, kuna mikoa 31, na Watanzania wana uhuru mkubwa wa kuishi katika mkoa wo wote wanaoupenda, iwe katika mikoa ile mitano ya Zanzibar au 26 ya Tanzania Bara, kote huko ni ruksa kuishi ni utashi wako tu.
Lakini, unapofika msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka, baadhi huamua kwenda kusalimia ndugu, jamaa na marafiki katika mikoa yao ya asili waliyozaliwa, au walikozaliwa wazazi na mababu.
Tanzania ina zaidi ya makabila 100 katika mikoa yake, ila kabila moja ambalo linaongoza kwa sifa ya kwenda kwenye mkoa wake wa asili ni Wachaga.
SENSA NA HIJA
Utasikia Mchaga mwenyewe akisema, "lazima Krismas hii niende Moshi". Lakini hata vijiweni utawasikia watu wakizungumza kwa kutaniana, "wee Mchaga hujaenda kwenu kuhesabiwa, wee hujaenda kuhiji", ili mradi ni mazungumzo yanayotawala.
Miaka nenda, miaka rudi, sikukuu hizi zimekuwepo. Kuna miaka imekuwa ya neema na kuna miaka imekuwa migumu kwa maisha wakati msimu wa sikukuu hizi.
Tanzania, mwaka, ambao wananchi walikuwa na wakati mgumu, kusheherekea Krismas ilikuwa ni 1974. Mapema, mwaka huo, serikali ilipiga marufuku petroli kuuzwa siku za mwishoni mwa wiki, Jumamosi, Jumapili na siku za sikukuu. Sababu ya marufuku ilikuwa ni kukabiliana na ongezeko la bei ya petroli duniani.
Kutokana na mzunguko wa majira na kalenda, hutokea mara chache, sikukuu za Krismas na Idd el Haj hugongana kwa kuadhimishwa siku moja ama moja kutangulia kwa siku moja na siku inayofuata hufuata nyingine.
KRISMAS NA IDD ZAGONGANA
Mgongano wa sikukuu za Krismas na Idd el Haj ulitokea mwaka 1974. Disemba 24 mwaka huo Waislamu waliadhimisha Sikukuu ya Idd el Haj na siku iliyofuata ikawa Krismas.
Nilieleza mapema, kwamba serikali ilipiga marufuku uuzaji wa petroli siku za sikukuu na mwishoni mwa wiki. Basi siku za sikukuu za Krismas na Idd mwaka 1974 zilikuwa chungu kwa wananchi kwa kukosa huduma ya kupata petroli.
Uchungu kwa wananchi kusheherekea siku za mwisho wa mwaka na Idd ulitokana na serikali kutoa tangazo kukumbusha maagizo yake ya kupiga marufuku uuzaji wa petroli.
"Watanzania hii leo Disemba 24,1974 watakuwa wakisheherekea sikukuu ya Idd el Haj na hapo kesho Sikukuu ya Krismas wakati habari zilizopatikana kutoka ofisi ya Mkurugenzi wa Maendeleo wa Dar es Salaam zinasema petrol haitauzwa kutokana na sheria ya serikali inayoendelea hivi sasa". taarifa ilisema siku hiyo.
PETROLI HAITAUZWA
Msemaji wa ofisi ya Mkurugenzi alieleza kwamba, labda tangazo maalum litolewe kuhusu petroli, lakini ukweli ni kwamba hakutakuwa na uuzaji wa petroli kama kawaida ya Jumapili na siku za sikukuu.
Alisema kufuatana na sheria hiyo, pia wenye magari wanaweza kutumia magari yao kama kawaida.
Katika kutafuta njia mbadala kukabiliana na upandaji wa bei ya petrol katika soko la dunia, mafundi wa karakana ya serikali ya magari walijitahidi kuwa wabunifu kutengeneza gari lisilotumia petrol.
MAFUNDI WABUNIFU
Meneja wa karakana ya magari ya serikali (M.T Depot) mjini Dar es Salaam, Ndugu K.C. Lim na mafundi M. Zavala na Mohamed Matengwa walishirikiana kujenga mitambo ya matumizi ya makaa ya mawe ili kuliwezesha gari litumie nishati hiyo kutembea.
Gari hilo aina ya Landrover ambalo lina mwendo kasi kiasi cha asilimia 75 cha gari linalotumia petrol, linaendeshwa kwa makaa ya mawe na limerekebishwa kwa gharama ya sh. 200 tu.
“Imetuchukua kiasi cha mwezi mmoja kurekebisha gari hili ambalo pia linaweza kutumia kuni, makaa ya mawe, mavi ya ng’ombe na takataka nyingine zinatoa hewa aina ya carbon monoxide zikichomwa moto,”walieleza mafundi.
Gari hilo la aina yake, lilionyshwa kwa Waziri wa Ujenzi, Ndugu Job Lusinde, Disemba 6,1974. Waziri Lusinde aliwapongeza wafanyakazi hao na kusema gari hilo ni ufunguo mpya wa tatizo la uhaba wa petroli.
Siku ya Jumapili ambapo magari hayaruhusiwi kutembea kuanzia saa nane alasiri, gari la makaa ya mawe lililobuniwa, litatembea mitaani tangu saa nane ili kuwapa fursa wananchi kujionea wenyewe ‘maajabu’ hayo.
Waziri Lusinde alisema angelitumia gari hilo kwenda kwenye gwaride rasmi la kuadhimisha miaka 13 ya Uhuru wa Tanganyika.
Hatua za serikali ya Awamu ya Kwanza chini ya Rais Mwalimu Julius Nyerere kukabiliana na uhaba wa petroli zilikuwa zinachukuliwa kila ilipoonekana ulazima wa kufanya hivyo.
AINA KUMI ZA MAGARI
Kuanzia Disemba Mosi, mwaka 1976, serikali ilitangaza kwamba ni aina 10 tu za magari zitakazoruhusiwa kuagizwa kutoka nje.
Msemaji wa Ikulu alieleza kwamba serikali imechukua hatua hiyo katika kupunguza matatizo mengi yanayoikabili nchi katika kuyatunza magari ya aina 45 yanayoagizwa.
Uamuzi huo ambao unaihusu serikali, mashirika ya umma na watu binafsi, ni miongoni mwa masuala kadhaa yaliyoamuliwa na Baraza la Mawaziri katika mkutano wake uliofanyika Novemba 30,1976.
Aina ya magari yaliyokubaliwa kuagizwa ni Volkswagen, Peugeot, Dutsan, Isuzu, Ford Transit, Bedford, Fiat, Scania, Leyland na Rang Rover/Land Rover.
Baadhi ya magari maarufu yaliyozuiwa kuagizwa ni Mercedes Benz,Toyota, Volvo na Ikarus. Msemaji wa Ikulu alieleza kwamba hatua hiyo itarahisisha upatikanaji wa spea na utengenezaji wa magari utakuwa rahisi. Miongoni mwa sababu muhimu za hatua hiyo kuchukuliwa ni ukosefu wa mafundi.
Miaka karibu 50 baada ya hatua hizo za serikali ya Awamu ya kwanza kukabiliana na kupanda kwa bei ya petrol, mambo yamebadilika. Sheria ya kupiga marufuku magari kutembea kuanzia saa nane alasiri Jumapili hadi saa 12 asubuhi Jumatatu ilifutwa Septemba mwaka 1987.
MACHUNGU YAMETOWEKA
Kuna uhakika kwa wananchi kusheherekea sikukuu za mwisho wa mwaka bila vikwazo vya kukosa petroli. Kuanzia miaka michache iliyopita, biashara ya petroli inazidi kunawiri. Vituo vya petroli mijini na katika barabara kuu zinazounganisha mikoa vinachipuka kila siku.
Sanjari na hilo, baadhi ya wenye magari, wameyabadilisha mfumo kutoka wa petroli na kuweka wa kutumia gesi kuendesha magari yao.
Nishati nyingine ya kutumia kuendesha gari, badala ya petroli ni solar. Kuna magari yameanza kutumia solar kwa kuendesha magari. Hivyo Krismas na mwaka mpya sasa zinasheherekewa bila machungu ya kukosa petroli.
Na Joe Nakajumo WhatsApp: 0784291434 email: nakajumoj@gmail.com |
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇