LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 11, 2025

TBN: SHERIA ITUMIKE VILIVYO DHIDI YA 'MANABII' WANAOTABIRIA KIFO VIONGOZI

Mtandao wa Mabloga Tanzania (TBN) umeiomba serikali kusimamia vema sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, ikiwemo kuwachukulia hatua kali manabii ambao wamekuwa wajinadi majukwaani na katika mitandao ya kijamii kutabiria vifo viongozi.


Ombi hilo limetolewa na Mabloga katika kikaokazi cha mafunzo ya mabloga hao kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, kilichofanyika, Makao Makuu ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), jijini Dar es Salaam, leo Agosti 11, 2025.


Baada ya mjadala mpana kuhusu kadhia hiyo, kikao kazi hicho kiliifanya kuwa ndilo azimio, hivyo kuamua kwa pamoja kupaaza sauti ili vitendo hivyo vya ukiukwaji sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi ikomeshwe.


Mjadala wa kadhia hiyo uliibuka baada ya mmoja wa washiriki kutaka kujua kwa nini wanaojiita manabii, wachungaji na wengine ambao wamekuwa wakitangza taarifa za kutabiria vifo viongozi hawachukuliwi hatua ilihali kitendo hicho kinaweza kuzua taharuki katika taifa hasa nyakati za Uchaguzi mkuu.


Hatimaye Mabloga hao wakaiomba serikali kupitia Mamlaka ya TCRA na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) kushirikiana kuwasaka na kuwachukulia hatua kali wale wote wanaohusika na vitendo hivyo.


Katika kikao hicho, mabloga walibainisha kuwa kumeibuka kundi la watu wanaodai kuwa ni manabii na kutoa kauli zinazokiuka sheria za nchi na kuleta taharuki kuelekea uchaguzi. 


Walisisitiza kuwa baada ya kuchambua Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (Personal Data Protection Act), walibaini kwamba 'utabiri' wa namna hiyo mbali na kuweza kusababisha taharuki unaingilia na kuvuruga haki ya msingi ya faragha ya familia na ya anayetabiriwa kifo.


Mapema akitoa mada Innocent Mungy, kutoka PDPC alibainisha kuwa sheria inakataza mtu kuzungumziwa kuhusu afya yake, mwenendo, au taarifa zake binafsi kutolewa bila ridhaa yake na kwamba sheria hiyo ina adhabu kali na lazima ifuatwe na kila mtu, si tu Mabloga na Waandishi wa Habari.


Mafunzo hayo yaliyoratibiwa na TCRA, yalilenga kuwaandaa mabloga kuripoti habari za uchaguzi kwa weledi na uadilifu. 


Pamoja na mada ya ulinzi wa taarifa binafsi iliyotolewa na Mungy, mada nyingine zilizotolewa ni pamoja na Mwongozo wa Waandishi wa Habari katika Uchaguzi na Matumizi ya Akili bandia (AI) katika uandishi wa habari.


Lengo kuu la mafunzo haya ni kuongeza uwezo wa mabloga kuhakikisha wanafuata sheria na maadili ya uandishi, jambo linalotazamiwa kuchangia mazingira ya uchaguzi yenye amani na utulivu.


No comments:

Post a Comment

Tupia Comments👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages