Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), imewataka Wananchi kuelewa kuwa Michezo ya kubahatisha haipaswi kuchukuliwa kama ajira au chanzo cha mapato ya kudumu, bali ni burudani inayodhibitiwa kisheria na inapaswa kufanyika kwa kiasi.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Huduma wa GBT, Daniel ole Sumayan, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, katika kikao kazi cha Wahariri na waandishi wa habari kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina. Lengo ni kueleza mafanikio na mwelekeo wa bodi hiyo chini.
“Michezo hii haina ujuzi maalum hii ni bahati tu, na ni burudani siyo ajira inapaswa kufanyika kwa kiasi, ili isigeuke mzigo kwa familia na jamii,” amesema Sumayan,
Aidha amesema kuwa sekta ya michezo ya kubahatisha inakua kwa kasi kutokana na mwitikio wa jamii na kuongeza kuwa michezo hiyo imegawanywa katika makundi mawili ikiwemo ya kibiashara inayoendeshwa na kampuni zenye leseni na zinazolipa kodi na isiyo ya kibiashara inayotumika katika kampeni za kukuza bidhaa na miradi ya kijamii.
Aidha amebainisha kuwa utoaji wa leseni unafuata mchakato mkali unaojumuisha uchunguzi wa historia ya waombaji, uwezo wao kifedha na kiufundi, pamoja na uadilifu wa washirika wao wa kibiashara.
“Maeneo yanayoruhusiwa kuendesha michezo hiyo ni yale yaliyopimwa na kukaguliwa kuhakikisha hayapo karibu na shule au nyumba za ibada.”Amesema
“Sekta hii imekuwa na mchango mkubwa kiuchumi ambapo mapato ya kodi yameongezeka kutoka shilingi bilioni 131.99 mwaka 2020/21 hadi bilioni 260.21 mwaka 2024/25 ukiwa ni ushahidi wa ukuaji unaoleta tija kwa taifa” amesema.






No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇