Na Dismas Lyassa
WANANCHI katika Kata ya Pangani, halmashauri ya Mji Kibaha mkoani Pwani wameipongeza kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi(CCM) katika kata hiyo kwa mfumo wake wa kufanya ziara za kutembelea miradi ya maendeleo huku ikishirikiana wenyeviti na makatibu wote wa matawi.
“Ni jambo zuri sana kufanya ziara, lakini ni jambo zuri zaidi kufanya ziara shirikishi, ziara inayoshirikisha wengi, kwani kupitia umoja na uwazi ndio unasaidia kuharakisha maendeleo katika kata yetu,” anasema mwananchi mmoja mkazi wa Mtaa wa Kidimu ambaye hakupenda jina lake liandikwe.
“Lengo langu sio jina langu lijulikane, bali azma yangu kuu ni kuwapongeza na kuwatia moyo viongozi wajue kwamba kufanya ziara kutembelea miradi ni suala la msingi sana, lakini tabia yao waliyoianzisha ya kushirikisha viongozi wa CCM wa matawi ni nzuri zaidi kwa sababu nao inawapa ufahamu ili waweze kujibu maswali pale wanapoulizwa na wanachama au wananchi kwenye maeneo yao,” anasema.
Wiki iliyopita Kamati ya siasa ya CCM Kata ya Pangani ilifanya ziara ya kutembelea miradi mitano ya maendeleo ambayo ni Shule ya Sekondari Pangani, Shule ya Sekondari ya Kidimu, Shule ya Msingi Mkombozi, Kituo cha Afya cha Kata Pangani na majengo ya zahanati ya Vikawe, azma kubwa ikiwa ni kuangalia maendeleo ya miradi hiyo.
Katibu Mwenezi wa Kata hiyo, James Mgaya anasema chama ni cha wote ni hii ndio sababu kwanini wamekuja na mpango huo wa kufanya ziara kwa uwazi na shirikishi ili kushirikiana kwa pamoja katika kuimarisha maendeleo kwenye kata.
Katibu wa CCM Kata Pangani, Masoud Seleman anasema wamejipanga kuhakikisha maendeleo yanapatikana kwa kasi katika kata hiyo kwa kuisimamia kwa karibu Serikali na viongozi wake.
Stanley Eliya ni mwenyekiti wa CCM Kata Pangani ambaye ameshukuru kwa ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi wenzake wa CCM na wananchi kwa ujumla na kuomba waendelee kushirikiana hivyo kwani anasema siku zote ushirikiano ndio unaozaa maendeleo kwa kasi.
“Niwapongeze wote kwa ushirikiano wenu, naomba sana tuendelee hivyo” anasema Eliya huku akishangiliwa.
Wengine walioshiriki ziara hiyo ni Augustino Mdachi ambaye ni Diwani wa kata hiyo, Omary Kafufi katibu wa CCM tawi la Kidimu, Rehema Saidi Mjumbe wa kamati ya Siasa kata, Tatu Bumba Mwenyekiti wa CCM tawi la Miwale, Pili Mbonde Katibu wa CCM Tawi la Mtakuja, Eliza Shija Subi Mwenyekiti wa CCM tawi la Pangani, Julius Kuduka Katibu wa CCM tawi la Pangani.
Walikuwepo pia Sanai Harison Mwenezi wa tawi la Lumumba, Fredi Mbilu Katibu wa CCM tawi la Lumumba, Lucia Gambila Katibu wa CCM tawi la Darajani, Amir Msangi Mwenyekiti wa Wazazi Kata Pangani, Mohammed Issa Rajabu Mwenyekiti wa CCM Tawi la Darajani, Bida Muya katibu wa CCM tawi la Vikawe Shule, Amos Mkwawa Mjumbe wa kamati ya siasa kata Pangani, David Lameck kaimu katibu wa CCM tawi la Mkombozi, Ismaili Maila Mwenyekiti wa CCM tawi la Vikawe Shule, Yohana Kajoro Mwenyekiti wa UVCCM Kata Pangani, Alphonce Moyo Mwenyekiti wa CCM tawi la Mtakuja na Ismail A. Maunda Mjumbe wa kamati ya siasa kata ya Pangani.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇