LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 6, 2023

KILOMBERO WAMPONGEZA RAIS DK SAMIA, WAOMBA AWAMURIKE BAADHI YA VIONGOZI

Na Dismas Lyassa, Ifakara


WANANCHI katika kata na vijiji mbalimbali vya eneo la Bonde la Kilombero ambalo linahusisha wilaya na halmashauri  za Malinyi, Mlimba, Kilombero, Ulanga na Ifakara wamefurahishwa na kitendo cha Rais wa Jamhuri ya Muungano Dk Samia Suluhu Hassan kutangaza kuchukuliwe hatua ya kulinda bonde hilo.

ATHARI ZA MIGOGORO BONDE LA KILOMBERO
(Makaburi ya baadhi ya watu waliouawa kutokana na migogoro)




Katika siku za hivi karibuni eneo la Bonde la Kilombero ambalo limekuwa haliruhusiwi kutumika kwa shughuli za ufugaji, lilivamiwa na mifugo mingi kutoka mikoa mbalimbali ambayo imekuwa ikilalamikiwa kuharibu vyanzo vya maji na uoto wa asili, hivyo kuhatarisha uhai wa bonde hilo linalotegemewa na Taifa kwa masuala mengi ya maendeleo ikiwamo kukusanya maji kwa ajili ya mradi mkubwa wa Umeme wa Nyerere. 

Uharibifu mkubwa wa uoto wa asili umekuwa ukisababisha wananchi na wadau wa mazingira kupiga kelele wakiomba Serikali kuchuku hatua za haraka.

 Kauli ya hivi karibuni ya Rais Dk Samia, aliyoitoa akizindua kazi ya kujaza maji kwenye bwawa la Mwalimu Julius Nyerere kwa ajili ya mradi wa umeme, alisema bila kujali ni nani anaharibu mazingira ni lazima hatua za haraka zichukuliwe ili kuhakikisha vyanzo vya maji vinalindwa na kuheshimiwa.

 “Tumefurahishwa sana na Rais Samia,”anasema James Mbanile na kuongeza kuwa lililo la msingi sasa ni kuhakikisha maagizo haya yanafanyiwa kazi kwa vitendo, kwani miaka kadhaa nyuma kumewahi kutolewa maagizo kama haya lakini viongozi wa chini wamekuwa sio watekelezaji.

 Baadhi ya wananchi wanasema kuna umuhimu wa kuwamurika viongozi wa chini kwani hata utitiri wa mifugo katika eneo hilo unajua maswali ya nani aliruhusu wakati inajulikana wazi kwamba Bonde la Kilombero ni oevu na haliruhusiwi kwa sheria za kimataifa kutumika kwa shughuli za mifugo au kilimo au uvuvi holela.

 “Tujiulize imekuwaje hali imekuwa mbaya kiasi hiki? Viongozi wa wilaya na mkoa hawajui kama kuruhusu mifugo kwenye Bonde oevu ni kosa?” anasema mwananchi mwingine Halina Mliga mkazi wa Ifakara.

Baadhi ya wananchi pia wanaomba kuundwa kwa tume ya siri kuchunguza vitendo vya utesaji raia na hata mauaji ambayo yamekuwa yakitokea katika Bonde hilo kutokana na migogoro baina ya wafugaji na wakulima, huku kukilalamikiwa kutochukuliwa dhabiti.

 “Kuna wanaoumizwa na hata kuuawa, lakini hatuoni hatua thabiti za kisheria zikichukuliwa dhidi yao, tunashindwa kuelewa ni kwanini? Serikali kuu iingie yenyewe kwenye Bonde hili na kujiridhisha, mfanio katika kata ya Mofu kuna zaidi ya watu 19 ambao kwa nyakati tofauti walikatwa mapanga na wengine kufa, kuundwa kwa tume kutasaidia kujua uhalisia wa mambo,” anasema James.

Anton Chikongoti ni mkazi waKitongoji cha Igumbati,  Ifakara (Simu yake 068499884) ambaye analalamikia kuuawa kwa ndugu zake watatu na kuomba Serikali kuingilia kati kuwasaidia kwani kinachoendelea hadi sasa hakiwafurahishi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Musilim alipoulizwa kuhusiana na malalamiko ya wanaoteswa au kuuawa kutuchukuliwa alisema anachofahamu jeshi lake linafanya kazi kulingana na sheria zinavyowataka na kwamba atafuatilia zaidi ili kujiridhisha. 

Baadhi ya wananchi wanaamini wanaumizwa lakini hatua hazichukuliwi kwa sababu ya rushwa kauli ambayo Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Morogoro, Manyama Tungaraza alisema kama ni kweli kuna rushwa watoe taarifa ofisini kwake atachukua hatua.

“Inawezekana ni dhana tu, lakini kama ni kweli kuna wanaoumizwa na hatua hazichukuliwi kwa sababu ya rushwa, naomba wawasilishe malalamiko ili tufuatilie na kuchukua hatua stahiki,” alisema Manyama.

 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages