LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

May 19, 2022

WIZARA, BRELA, BPRA LINDENI KAZI ZA WABUNIFU



Makamu wa Kwanza wa Rais–Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman (kulia) akimsikiliza Ali Masoud Kipanya kuhusu gari aliloliunda linalotumia umeme alipokuwa akikagua mabanda ya wabunifu wakati wa ufunguzi wa Wiki ya Ubunifu Kitaifa jijini Dodoma Mei 16, 2022.

Kaimu Mkurugenzi wa Miliki Bunifu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Seka Kasera kulia akikabidhi vyeti vya Usajili wa Majina ya Biashara kwa baadhi ya wadau waliokamilisha  usajili katika banda la BRELA kwenye maonesho ya  Wiki ya  Kitaifa ya Ubunifu  (MAKISATU) yanayoendelea katika uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma.

Makamu wa Kwanza wa Rais–Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman ametoa Wito kwa Wizara zinazosimamia masuala ya ubunifu pamoja na taasisi  zikiwemo  Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) na  Wakala wa Usajili wa Biashara na Mali (BPRA) ya Zanzibar, kuhakikisha kuwa zina andaa mikakati maalumu ya kulinda kazi mbalimbali za wabunifu.   

 Mhe Othman ametoa agizo hilo tarehe 16 Mei, 2022  wakati wa ufunguzi  wa Wiki ya Kitaifa ya Ubunifu (MAKISATU) inayoambatana na maonesho ya Wabunifu, katika uwanja wa Jamhuri  Jijini Dodoma.

 Amesema kuwa, nchi mbalimbali zimepata maendeleo makubwa kwasababu ya kuwa na mikakati madhubuti ya kulinda kazi za wabunifu, kwa hivyo ni vema kuwasaidia wabunifu na lazima kuwa na mikakati ya kuwasaidia, kujua ni namna gani na hatua gani za kulinda  kazi  hizo.

“Siku hizi vitu vingi vinafanyika kwa udanganyifu na ujanja mkubwa umekuwa ni wa kuchukua kazi za wengine, hivyo tunapaswa kuwa na mikakati ya kulinda kazi za wabunifu,” amefafanua Mhe. Othman.

Mhe. Othman amefafanua kuwa,  kazi za ubunifu zisipolindwa zitakuwa hazina maana, na hii itawafanya wavuje jasho lakini bila kuwa na tija inayotokana na jasho lao, hivyo kuna haja ya kutilia mkazo suala hili  kwa kuweka mikakati madhubiti.


Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Miliki Bunifu Bw. Seka Kasera ameeleza kuwa, kama kaulimbiu inavyo sema, “Ubunifu kwa Maendeleo Endelevu,”amewataka wabunifu waliosajiliwa  kuendeleza bunifu zao kwa kuziboresha kulingana na mahitaji ya jamii.  


“Katika maonesho haya nimetembelea mabanda ya wabunifu na kuziona bunifu nyingi ambazo zinahitaji kuendelezwa kwa kuziboresha zaidi badala ya kuziacha kama zilivyo,” alifafanua Bw. Kasera.

Akirejea kauli ya Mgeni rasmi kuwa tangu mwaka 2019 China ndio nchi inayoongoza kwa kutoa bunifu nyingi na inaongoza kwa kutoa bunifu endelevu kwakuwa wamekuwa wakiziongezea ubora mara kwa mara kulingana na mahitaji ya jamii. 

Bw. Seka  amewashauri wabunifu ambao bunifu zao bado hazijapata ulinzi lakini  zina sifa ya kupata ulinzi, kuwasiliana na BRELA kwa ajili ya kupata ulinzi  juu ya uvumbuzi walioufanya.  .   

BRELA imekuwa ikitoa elimu ya namna ya kuboresha bunifu zile ambazo zimesajiliwa na kuziendeleza na kuangalia jinsi  ya kushirikiana na taasisi nyingine za kikanda na kimataifa kuwasaidia kuzipatia  masoko. 

Maonesho haya ya  wiki ya  MAKISATU  yaliyoanza tarehe 15 Mei, 2022 yatahitimishwa tarehe 20 Mei, 2022.


No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages