Rais Dk. John Magufuli akilihutubia Taifa wakati akizindua Bunge la 12 la Tanzania, Bungeni jijini Dodoma, leo, Nov.13, 2020. Tafadhali, soma hotuba yote hapo kama tulivyoipokea kutoka kurugenzi ya mawasiliano ya Rais Ikulu.👇
HOTUBA
YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JOHN POMBE JOSEPH
MAGUFULI, WAKATI WA KUZINDUA RASMI BUNGE
LA
12 LA JAMHURI YA MUUNGANO
WA
TANZANIA DODOMA, 13 NOVEMBA 2020
Mheshimiwa Spika;
Mara ya mwisho
nilipoingia kwenye Ukumbi huu Kulifunga Bunge la 11, tulibahatika kuwa na
Marais wetu Wastaafu watatu. Lakini leo, wapo wawili. Mmoja, Mheshimiwa
Benjamin William Mkapa, Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, ametangulia mbele za
haki. Hivyo basi, kabla ya kuanza hotuba yangu, nawasihi sote tusimame
tumkumbuke pamoja na wabunge wote waliofariki dunia tangu kufungwa kwa Bunge la
11. Mwenyezi Mungu aiweke roho ya Marehemu Mzee Mkapa pamoja na marehemu wetu
wote mahali pema peponi. Amina.
Mheshimiwa Spika;
Baada
ya utangulizi huo, napende niseme kwamba, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Ibara ya 91 Ibara ndogo ya kwanza imempa dhamana Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kulifungua rasmi Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ni kwa sababu hiyo, nimekuja hapa leo kulihutubia Bunge hili kwa lengo la
kutimiza masharti hayo ya Kikatiba.
Napenda nianze kwa kumshukuru
sana Mwenyezi Mungu aliyetujalia neema ya uhai na kutuwezesha kuiona siku ya
leo. Aidha, nakupongeza wewe, Mheshimiwa Job Ndugai, Mbunge wa Jimbo la Kongwa
kwa kuchaguliwa, kwa mara nyingine, kuliongoza Bunge hili ukiwa Spika. Hongera
sana. Nampongeza pia Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson kwa kuchaguliwa kwa mara
nyingine kuwa Naibu Spika; tena mara hii akiwa Mbunge wa kuchaguliwa kutoka
Jimbo la Mbeya Mjini. Hongera sana Mheshimiwa Dkt. Tulia. Huu ni uthibitisho kwamba,
nchi yetu, kupitia Serikali inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi, inawaamini sana
wanawake.
Kama mnavyofahamu,
Makamu wetu wa Rais, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, naye ni mwanamama. Aidha, Bunge
hili la 12 nalo lina Wabunge wengi wanawake. Kwa msingi huo, napenda nitumie fursa
hii kuahidi kuwa, Serikali ninayoingoza, itaendelea kuwaamini wanawake katika kushika
nafasi mbalimbali za uongozi. Wanawake na akinamama Oyee!!!
Napenda pia kuwapongeza
Waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchaguliwa kwenu kuwa Wabunge wa Bunge hili la 12.
Mmechaguliwa kwa vile wananchi wana imani kuwa mna uwezo wa kuwawakilisha
vizuri. Hivyo basi, nawasihi msiwaangushe wananchi waliowachagua. Watanzania
wana imani kubwa sana na Bunge hili.
Nitumie fursa hii pia
kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kuridhia na kumpitisha Mheshimiwa Kassim
Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Ahsanteni
sana.
Mheshimiwa Spika;
Nimekuja kulizindua
Bunge hili baada ya nchi yetu kufanikiwa kumaliza Uchaguzi Mkuu uliofanyika
tarehe 28 Oktoba, 2020 kwa uwazi amani na utulivu mkubwa. Kwa msingi huo,
napenda nirudie kuipongeza Tume yetu ya Taifa ya Uchaguzi kwa kusimamia vizuri
zoezi la Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu; kuanzia kwenye uandikishaji wapiga kura;
uchukuaji na urejeshaji fomu za wagombea; usimamizi wa kampeni na pia zoezi la
kupiga kura na utoaji matokeo mapema. Kwa hakika, Tume imedhihirisha uwezo
mkubwa katika kusimamia Uchaguzi bila kutegemea misaada kutoka nje. Mheshimiwa
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Mstaafu Semistocles Kaijage;
Makamu Mwenyekiti wa Tume, Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud Hamid; Makamishna wa Tume; Mkurugenzi
wa Uchaguzi, Dkt. Wilson Mahera pamoja na Watendaji wote wa Tume; hongereni
sana kwa kazi nzuri.
Lakini, kwa namna ya
pekee, nawapongeza kwa namna mlivyotumia vizuri fedha mlizotengewa. Kama
inavyofahamika, Uchaguzi wa Mwaka huu uligharamiwa na Serikali kwa asilimia 100, ambapo kiasi cha shilingi bilioni 331 kilitengwa. Hata
hivyo, mpaka Uchaguzi umekamilika, Tume imetumia shilingi bilioni 262 tu. Hii ni ishara ya uadilifu mkubwa walionao
Viongozi na Watendaji wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Hongereni sana. Natoa rai
kwa Taasisi nyingine kuiga mfano mzuri wa Tume hii.
Kwa moyo wa dhati
kabisa, narudia kuwashukuru Viongozi wetu wa Dini kwa kutuongoza vyema kwa sala
na dua katika kipindi chote cha Uchaguzi; na hatimaye tumeweza kumaliza
Uchaguzi wetu salama. Nawasihi endeleeni kuliombea Taifa letu ili libaki katika
mikono ya Mwenyezi Mungu.
Narudia pia kuvishukuru
vyombo vyetu vya Ulinzi na Usalama kwa kusimamia vizuri amani na utulivu wa
nchi yetu na mipaka yake wakati wote wa Uchaguzi. Hii ni ishara kuwa vyombo vyetu
vya ulinzi na usalama ni imara na vinafanya kazi kwa ueledi mkubwa. Hongera
sana kwa vyombo vyetu vya ulinzi na usalama.
Kwa namna ya pekee
kabisa, natoa shukrani nyingi kwa Watanzania wenzangu wote kwa kushiriki vizuri
na kuonesha utulivu mkubwa kwenye Uchaguzi uliopita; kuanzia kwenye zoezi la
uandikishaji wapiga kura, wakati wa kampeni, upigaji kura na kupokea matokeo.
Hakuna shaka, Uchaguzi wa Mwaka huu, kwa mara nyingine, umeuthibitishia ulimwengu
kuwa sisi Watanzania ni wapenda amani, tunajitambua, hatudanganyiki na tumekomaa
kidemokrasia. Ahsanteni sana Watanzania wenzangu.
Mheshimiwa Spika;
Masuala yote muhimu tuliyopanga kutekeleza kwenye miaka mitano ijayo,
tumeyaweka kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2020 – 2025 ambayo ina kurasa
303. Kwa bahati nzuri, Waheshimiwa Wabunge
wengi wa Bunge hili wanaifahamu vizuri Ilani hiyo kwa vile wameitumia katika kuomba
kura kwa wananchi kwenye Uchaguzi Mkuu uliomalizika.
Lakini, sambamba na masuala hayo yaliyomo kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi
wa mwaka 2020 - 2025, tutaendelea pia kutekeleza na kusimamia mambo yote
niliyoeleza wakati nikizindua Bunge la 11, tarehe 20 Novemba, 2015.
Kama mtakavyokumbuka, kwenye Hotuba hiyo ya kuzindua Bunge la 11
nilieleza mambo mengi sana, ambayo, kimsingi, yalitoa falsafa, dira na
vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Tano. Baadhi tumeyatekeleza vizuri; yapo
ambayo hatujayatekeleza kwa ukamilifu na mengine yapo kwenye hatua mbalimbali
za utekelezaji. Kwa hiyo, kwenye miaka mitano ijayo, tutaendelea kusimamia na
kutekeleza mambo yote niliyoyaeleza kwenye Hotuba ya Kuzindua Bunge la 11. Hii
ndiyo sababu nimeamua kuigawa tena Hotuba yangu ya Uzinduzi wa Bunge la 11
kwenu Waheshimiwa Wabunge ili mkaisome na hatimaye ikawaongoze katika
kutekeleza majukumu yenu vizuri.
Hata hivyo, pamoja na hayo yote, naomba Mheshimiwa Spika uniruhusu nitaje baadhi ya mambo muhimu tutakayoyapa
kipaumbele kikubwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Mheshimiwa Spika;
Jambo la
kwanza na muhimu tutakalolipa kipaumbele kikubwa kwenye miaka mitano ijayo ni
kuendelea kulinda na kudumisha tunu za Taifa letu, yaani Amani, Umoja na Mshikamano, Uhuru wa Nchi yetu, Muungano na
Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Na katika hilo, naahidi kushirikiana kwa karibu
sana na Rais mpya wa Zanzibar, Mheshimiwa Dkt. Hussein Mwinyi. Kamwe, hatutakuwa
na mzaha na yeyote mwenye kutaka kuhatarisha amani ya nchi yetu; mwenye nia ya
kuvuruga umoja na mshikamano wetu; na pia mwenye kutaka kutishia Uhuru wetu,
Muungano pamoja na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.
Napenda
pia kutumia fursa hii kumwahidi Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwamba,
kwenye miaka mitano ijayo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itatoa
ushirikiano mkubwa na kufanya kazi kwa karibu na Serikali ya Zanzibar. Kwa
kifupi, naweza kusema, tutafanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuleta maendeleo
kwa pande zetu zote mbili za Muungano. Na katika hilo, nampongeza sana
Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Mwinyi kwa hotuba nzuri aliyoitoa wakati wa
kuzindua Baraza la Wawakilishi. Kwenye hotuba yake alitoa dira, mwelekeo na kutaja
vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar. Hongera sana kwa Mheshimiwa
Rais Dkt. Mwinyi kwa hotuba nzuri. Kupitia Bunge hili, napenda nimwahidi
Mheshimiwa Rais Dkt. Hussein Mwinyi kuwa, nitampa ushirikiano wa kutosha katika
kutekeleza yote aliyoahidi wakati wa Uzinduzi Rasmi wa Baraza la Wawakilishi.
Mheshimiwa Spika;
Sambamba
na kulinda na kudumisha tunu za nchi yetu, kwenye miaka mitano ijayo, tutaendelea
kuimarisha utawala bora, hususan kwa kusimamia nidhamu kwenye utumishi wa umma
pamoja na kuzidisha mapambana dhidi ya rushwa, wizi, ufisadi na ubadhirifu wa
mali za umma. Kwenye miaka mitano iliyopita, tuliwachukulia hatua za kinidhamu watumishi
32,555 na kuiwezesha nchi yetu kushika
nafasi ya kwanza kati ya nchi 35 za
Afrika kwa kupambana na rushwa, kwa mujibu wa Transparency International; na pia kushika nafasi ya 28 kati ya nchi 136 duniani kwa matumizi mazuri ya fedha za umma kwa mujibu wa Utafiti
Jukwaa la Dunia (World Economic Forum) wa
mwaka 2019.
Hata hivyo, watumishi wazembe bado wapo; wala rushwa bado
wapo; na pia wezi na wabadhirifu wa mali ya umma bado wapo. Kwa hiyo, kwenye
miaka mitano ijayo, tutaendelea kushughulikia matatizo hayo. Na kwa kifupi, niseme,
utumbuaji majipu utaendelea. Hata hivyo, kwa upande mwingine, tutaendelea
kuboresha mazingira ya kazi pamoja na maslahi ya watumishi wetu wote ili yaendane
na hali halisi ya maisha ya Watanzania. Kwa hiyo, watumishi wasiwe na wasiwasi.
Mheshimiwa Spika;
Kwenye
miaka mitano ijayo pia, tumejipanga
kuendeleza jitihada za kukuza uchumi. Kama unavyofahamu, katika
kipindi cha miaka mitano iliyopita, tulijitahidi kusimamia vizuri uchumi wetu,
ambapo ulikua kwa wastani wa asilimia 7
kwa mwaka. Aidha, Pato ghafi la Taifa limeongezeka kutoka shilingi trilioni 94.349 mwaka 2015 hadi kufikia shilingi trilioni 139.9 mwaka 2019;
tulidhibiti mfumuko wa bei, kutoka asilimia
6.1 mwaka 2015 hadi kufikia wastani wa asilimia
4.4 na kuongeza akiba ya fedha ya kigeni kutoka Dola za Marekani bilioni 4.4 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 5.2 mwezi Julai, 2020 ambazo zinatuwezesha
kununua bidhaa na huduma kwa miezi 6.
Zaidi
ya hapo, kwenye miaka mitano iliyopita, tuliongeza mauzo yetu ya nje kutoka Dola za Marekani bilioni 8.9 mwaka 2015
hadi Dola za Marekani bilioni 9.7
mwaka 2019; na pia kuvutia uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 14.6, sawa na zaidi ya shilingi trilioni 30. Aidha,
tulifanikiwa kupunguza umasikini wa kipato hadi kufikia asilimia 26.4 kwa takwimu za mwaka 2017/2018. Mafanikio haya, bila
shaka, ndiyo yamewezesha, mwezi Julai 2020, nchi yetu kutangazwa kuingia kundi
la nchi za uchumi wa kati kutoka kundi la nchi masikini. Na mafanikio hayo
yamepatikana miaka mitano kabla ya muda uliopangwa, yaani mwaka 2025.
Kwa hiyo, kwenye miaka mitano ijayo tunakusudia
kuendeleza mafanikio ya kiuchumi yaliyopatikana na tutahakikisha ukuaji uchumi
unawanufaisha wananchi, hususan kwa kuinua vipato vyao, kupunguza umasikini na
tatizo la ajira. Na katika hilo, tunalenga kukuza uchumi wetu kwa wastani wa
angalau asilimia 8 kwa mwaka na pia
kutengeneza ajira mpya zipatazo milioni
8. Tutaendelea pia kuboresha
sera zetu za uchumi jumla na sera za fedha (yaani macroeconomic and monetary policies), na pia kuhakikisha viashiria
vyote vya uchumi; ikiwemo thamani ya sarafu yetu, mfumko wa bei pamoja na
viwango vya riba; vinabaki kwenye hali ya utulivu.
Tutaongeza pia jitihada za
kuwawezesha wananchi wetu kiuchumi kwa kuwapatia mikopo isiyo na riba ama yenye
riba nafuu, ikiwemo mikopo ya asilimia
10 inayotolewa na Halmashauri zetu; na pia kupitia Mifuko na Programu mbalimbali zilizoanzishwa na Serikali,
ambayo kwa idadi zipo 18. Baadhi ya
Mifuko hiyo ni Mfuko wa Maendeleo ya Vijana (YDF); Mfuko wa
Maendeleo ya Wanawake (WDF); Mfuko wa Taifa wa Kuendeleza Wajasiriamali (NEDF);
Mfuko wa Kutoa Mikopo kwa Wajasiriamali Wadogo (SELF Microfinance Fund), Mfuko
wa Kudhamini Mikopo ya Mauzo ya Nje; Mfuko wa Kilimo Kwanza. n.k. Tutaimarisha
usimamizi wa Mifuko hii na kuhakikisha Watanzania wanaifahamu.
Najua Mifuko hii mingi ipo chini ya
Ofisi ya Waziri Mkuu; hivyo basi, nakuagiza Mheshimiwa Waziri Mkuu, hii ikawe
kazi yako ya kwanza kuishughulikia; ikiwezekana, mwangalie uwezekano wa
kuiunganisha baadhi ya mifuko ili ifanye kazi kwa tija zaidi na kupunguza
gharama za uendeshaji. Nataka Mifuko hii ikiwasaidie wananchi wa kawaida,
wakiwemo machinga, akina baba na mama lishe pamoja na wajasiriamali wengine
wadogo.
Sambamba
na kutoa mikopo, tutaendelea kutekeleza Program mbalimbali za kukuza ujuzi na
maarifa, ikiwemo maarifa ya ujasiriamali, ili kuwapa ujuzi na uzoefu wananchi
wetu utakaowawezesha kujiajiri ama kuajirika ndani na nje ya nchi. Tutaendelea
pia kutekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili tuliouzindua
mwezi Februari 2020, ambao utagharimu takriban shilingi trilioni 2.032. Tutahakikisha fedha hizo zinawafikia
walengwa, ambao ni wananchi masikini.
Muhimu
zaidi ni kwamba, katika kipindi cha miaka mitano ijayo, sekta binafsi itapewa
umuhimu wa pekee sana. Tunataka mtu yeyote atakayetaka kuwekeza asisumbuliwe
kwa kuwekewa vikwazo vya aina yoyote. Watanzania ni matajiri lakini baadhi yao
wanasita kuwekeza hapa nchini kwa kuogopa kusumbuliwa na maswali yasiyo na
msingi. Tunahitaji kuwa na Mabilionea wengi wa Kitanzania. Nataka Watanzania
wote washiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa nchi yao.
Sambamba
na kuwekeza, Watanzania wahamasishwe kuweka fedha kwenye Benki za hapa nchini
ili kusaidia benki zetu kufanya biashara na kuimarisha mzunguko wa fedha na
kupunguza riba kwa wakopaji. Waheshimiwa
Wabunge na Watanzania mnaonisikiliza, wakati wa kufanya mambo bila woga ni
sasa. Kwenye miaka mitano ijayo pia tutafungua milango kwa sekta binafsi
kufanya majadiliano na Serikali ili kutafuta mwafaka ya migogoro ya biashara (business disputes) iliyopo kwa faida ya
pande zote mbili. Lengo letu ni kuona Tanzania inakuwa mahali pazuri pa kufanya
biashara duniani. Kwenye miaka mitano iliyopita, tumefuta tozo 168, ambapo 114 zitahusu kilimo, mifugo na uvuvi na tozo nyingine 54 za biashara.
Mheshimiwa Spika;
Mbali na hatua hizo; kwa lengo la kukuza uchumi, kupambana
na umasikini, na pia kukabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira, tunakusudia,
kwenye miaka mitano ijayo, kuweka mkazo mkubwa katika kukuza sekta zetu kuu za
uchumi na uzalishaji, hususan kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, madini, biashara
na utalii. Sekta hizi ndizo zenye kuajiri Watanzania wengi. Kwa hiyo, ni wazi,
tukifanikiwa kuzikuza, uchumi wetu utakua kwa kasi na hivyo kupunguza matatizo
ya umasikini na ukosefu wa ajira nchini.
Kwa msingi huo, kwenye KILIMO, tunakusudia kuongeza tija na kukifanya kilimo chetu kuwa
cha kibiashara. Lengo ni kujihakikishia usalama wa chakula, upatikanaji wa
malighafi za viwandani na pia kupata ziada ya kuuza nje. Ili kufanikisha hayo,
tutahakikisha pembejeo na zana bora za kilimo, ikiwemo mbegu, mbolea,
viatilifu/dawa na matrekta, vinapatikana kwa uhakika na kwa gharama nafuu.
Tutaongeza pia eneo la umwagiliaji kutoka hekta 561,383 hadi hekta milioni
1.2 mwaka 2025 ili kupunguza utegemezi kwenye mvua.
Tutaimarisha mifumo ya upatikanaji wa mitaji kwa wakulima
wadogo na wawekezaji kwa kushirikisha taasisi za fedha, ikiwemo Benki yetu ya
Maendeleo ya Kilimo pamoja na benki nyingine. Tutashughulikia pia tatizo la
upotevu wa mazao (yaani post harvest loss),
ikiwemo kwa kukamilisha ujenzi wa vihenge na maghala maeneo mbalimabli nchini
ambayo yataongeza uwezo wetu wa kuhifadhi mazao kutoka tani 190,000 za sasa hadi tani
501,000. Takwimu zinaonesha kuwa, kila mwaka, nchi yetu inapoteza wastani
wa kati ya asilimia 30 - 40 ya
mavuno yake kwa sababu mbalimbali, ikiwemo kukosekana kwa miundombinu ya
kuhifadhi. Zaidi ya hapo, tunakusudia kuanzisha
bidhaa mbalimbali za huduma ya Bima ya Kilimo na pia kuingia makubaliano ya
kibiashara na nchi walaji na wanunuzi wa mazao ili kupata soko la uhakika.
Mazao ya kimkakati tunayolenga kuyapa kipaumbele kikubwa
ni pamba, korosho, chai, kahawa, tumbaku, mkonge, michikichi, cocoa, alizeti na miwa; lakini pia mazao ya chakula. Nchi yetu kila mwaka inaagiza tani 800,000 za ngano na kwa ujumla, tunatumia wastani wa shilingi trilioni 1.3 kuagiza chakula
kutoka nje. Hii ni aibu kwa nchi kama Tanzania. Hivyo basi, ni lazima tutafute
majawabu ya suala hili. Na hii ndiyo ikawe kazi ya kwanza ya Waziri wa Kilimo
nitakayemteua.
Lakini, zaidi ya hapo, tutaweka mkazo mkubwa kwenye
kilimo cha mazao ya bustani (matunda, mbogamboga, maua na viungo), ambacho
kinakua kwa kasi kubwa nchini. Hivi sasa nchi yetu inashika nafasi ya 20 kwa kuzalisha kwa wingi mazao hayo
duniani na mauzo yetu ya nje yameongezeka kutoka Dola za Marekani milioni 412 mwaka 2015 hadi kufikia Dola za Marekani milioni 779 mwaka
2018/2019. Hii ndiyo sababu, hatuna budi kukiendeleza kilimo cha mazao hayo. Na
katika hilo, napenda kuriafu Bunge hili Tukufu kuwa, kwenye miaka mitano ijayo,
tunakusudia kununua ndege moja ya mizigo ili kurahisisha uzafirishaji wa mazao
ya bustani, lakini pia minofu ya samaki pamoja na nyama. Wakulima wetu ni
lazima watajirike na shughuli wanazozifanya; hivyo basi, Mawaziri wa Kilimo,
Biashara, Mambo ya Nje na Mabalozi wajipange vizuri kwa hili.
Kwa upande wa MIFUGO,
kama mnavyofahamu, nchi yetu inashika nafasi ya pili kwa mifugo Barani Afrika. Tuna ng’ombe milioni
33.4; mbuzi milioni 21.3; kondoo milioni 5.65; punda 657,389;
lakini pia tuna idadi kubwa ya kuku, bata, kanga, n.k. Hata hivyo, ukweli ni kwamba, sekta hii bado
haijatunufaisha vya kutosha.
Kwa kuzingatia hilo, kwenye miaka mitano ijayo,
tunakusudia kuikuza sekta ya mifugo ili ichangie ukuaji uchumi na kupunguza
matatizo ya umasikini na ukosefu wa ajira nchini. Tutaongeza maeneo ya ufugaji
kutoka hekta 2,788,901 za sasa hadi hekta 6,000,000. Tunataka wafugaji
wasiteswe na mifugo yao. Mifugo ni utajiri. Sambamba na hayo, tutahamasisha
ufugaji wa kisasa; tutaongeza vituo vya kuzalisha mbegu bora na pia kuongeza
uzalishaji wa chakula cha mifugo viwandani kutoka tani 900,000 hadi milioni 8.
Zaidi ya hapo, tutakamilisha ujenzi wa machinjio
saba unaoendelea maeneo mbalimbali nchini, ambapo, kwa pamoja, zitakuwa na
uwezo wa kuchinja ng’ombe 6700 na
mbuzi 11,000 kwa siku. Ujenzi wa machinjio
hizo sio tu utasaidia kupatikana kwa nyama bora itakayouzwa hadi kwenye masoko
ya kimataifa bali pia utawezesha upatikanaji wa ngozi bora kwa ajili ya
kutengeneza bidhaa za ngozi. Takwimu zinaonesha kuwa, takriban asilimia 90 ya ngozi inayozalishwa
nchini kwa sasa haina ubora unaohitajika; na sababu mojawapo ni uchinjaji wanyama
kienyeji. Kwa hiyo, machinjio yanayojengwa yatapunguza tatizo hilo.
Nitumie
fursa hii, kuikaribisha sekta binafsi kuwekeza kwenye viwanda vya kutengeneza
bidhaa za mifugo (nyama, ngozi, maziwa, kwato, n.k.). Na katika hilo, tunaahidi
kutoa vivutio maalum kwa watakaowekeza kwenye viwanda hivyo ambavyo vitasaidia
kuinua vipato vya wafugaji wetu na pia kuongeza fursa za ajira kwa Watanzania. Na
hapa, nataka niweke bayana kuwa, watendaji watakaokwamisha ujenzi wa viwanda
hivyo tutawashughulikia.
Mheshimiwa Spika;
Nchi yetu pia imebarikiwa kuwa na maeneo mengi yanayofaa kwa
shughuli za uvuvi, ikiwemo Ukanda wa Pwani, Maziwa, mito na mabwawa. Hali hii
inafanya sekta hii kuwa na nafasi ya kutoa mchango mkubwa kwenye kukuza Pato la
Taifa na pia kupambana na umasikini na tatizo la ajira. Hata hivyo, kwa sasa,
mchango wake bado ni mdogo. Hivyo basi, kwenye miaka mitano ijayo tunakusudia
kuikuza sekta hii, ikiwemo kuimarisha shughuli za uvuvi kwenye Bahari Kuu,
ambako tumekuwa tukipoteza mapato mengi. Kwa mujibu wa Ripoti ya Kamati ya
Bunge kuhusu Shughuli za Uvuvi wa Bahari Kuu ya Mwaka 2018; shughuli za uvuvi
kwenye Bahari Kuu zinaweza kuingizia Serikali mapato ya moja kwa moja ya
takriban shilingi bilioni 352.1 kwa
mwaka endapo mifumo ya usimamizi na udhibiti ingekuwa imara na samaki
wangechakatwa hapa nchini. Hata hivyo, mapato yaliyokuwa yamekusanywa kwa
kipindi cha miaka tisa (2009 hadi 2017) yalikuwa shilingi bilioni 29.79, sawa na shilingi bilioni 3.3 kwa mwaka.
Kiwango hiki cha mapato hakikubaliki.
Hii ndiyo sababu, tunataka, kwenye miaka mitano ijayo,
kuisimamia vizuri shughuli za uvuvi wa Bahari Kuu ili Taifa letu linufaike na
rasilimali zake, kwa kuhusisha sekta binafsi. Kwa bahati nzuri, tayari, mwaka
huu (2020) tumetunga Sheria Mpya ya Kusimamia na Kuendeleza ya Uvuvi wa Bahari
Kuu. Aidha, tumepanga kununua Meli 8
za Uvuvi kwa kushirikiana na Shirika IFAD (4
upande wa Zanzibar na 4 upande wa
Tanzania Bara) ili zishiriki katika uvuvi wa Bahari Kuu. Kama mnavyofahamu,
suala la uvuvi wa bahari kuu ni la Muungano. Tunakusudia pia kujenga Bandari
kubwa ya Uvuvi itakayotoa ajira zipatazo 30,000;
na tutaendelea kuihamasisha sekta binafsi kujenga viwanda vya kuchakata samaki.
Sambamba na kusimamia Bahari Kuu, tutakuza shughuli za
uvuvi kwenye Maziwa yetu Makuu (Victoria, Tanganyika na Nyasa) pamoja na Mito
yetu mikubwa. Tutahamasisha wavuvi wetu wadogo kujiunga kwenye vikundi ili
tuweze kuwapatia mitaji, ujuzi, vifaa na zana za uvuvi; na halikadhalika
tutapitia upya tozo na maeneo mbalimbali ili kuwapunguzia wavuvi kero na kuvutia
uwekezaji. Tutahamasisha pia watu binafsi kujenga mabwawa na kufuga kisasa kwa
kutumia vizimba. Sekta ya uvuvi ni lazima itoe mchango mkubwa kwenye uchumi wa
nchi yetu. Wateule wote wa sekta hii ni lazima walisimamie hili.
Mheshimiwa
Spika;
Ni ndoto kufikiria kwamba utaweza
kukuza uchumi au kupambana na umasikini pamoja na tatizo la ukosefu wa ajira
bila kuelekeza nguvu katika kukuza sekta ya viwanda. Duniani kote, sekta ya
viwanda ndiyo mhimili mkuu wa kukuza uchumi, kupambana na umasikini pamoja na
matatizo ya ajira. Kwenye miaka mitano iliyopita, tulifanikiwa kujenga viwanda
vipya takriban 8,477 ambavyo
vilitengeneza ajira zipatazo 480,000,
ambapo Mkoa wa Pwani uliongoza kwa kujenga viwanda vingi.
Hivyo basi, kwenye miaka mitano
ijayo, tutaendeleza jitihada za kukuza sekta hiyo. Mkazo mkubwa tutauweka
kwenye viwanda vyenye kutumia malighafi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini
(mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi); vyenye kuajiri watu wengi; na ambavyo
bidhaa zake zinatumika kwa wingi hapa nchini (nguo, bidhaa za ngozi, mafuta ya
kula, sukari, saruji, n.k.).
Ili kuvutia uwekezaji kwenye
sekta ya viwanda, tutaendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji,
ikiwemo kuangalia masuala ya kodi na kuondoa vikwazo na urasimu. Pamekuwepo na
urasimu mwingi na kusumbuliwa kwa wawekezaji kwa kuzungushwa zungushwa na hivyo
kuwafanya wakate tamaa. Mimi nataka mwekezaji mwenye fedha akija apate kibali
ndani ya siku 14. Kwa sababu hiyo,
nimeamua suala la uwekezaji ikiwa ni pamoja na Kituo cha Uwekezaji Tanzania
(TIC) kulihamisha kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kwenda Ofisi ya Rais ili hao
wanaokwamisha nikapambane nao mwenyewe. Lakini, zaidi ya hapo, tumepanga
kujenga Ukanda na Kongani (clusters)
za viwanda kila mkoa kulingana na mazao na maliasili zinazopatikana.
Mheshimiwa Spika;
Kwenye miaka mitano iliyopita
tumepata mafanikio makubwa kwenye sekta ya madini. Mapato yameongezeka kutoka shilingi bilioni 168 mwaka 2014/2015
hadi shilingi bilioni 527 mwaka
2019/2020. Mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia 3.4 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 5.2 mwaka 2019. Zaidi ya hapo,
kwa mara ya kwanza, katika historia ya nchi yetu, mwaka 2019, sekta ya madini
iliongoza kwa kutuingizia fedha nyingi za kigeni, Dola za Marekani bilioni 2.7. Nitumie fursa hii kulipongeza Bunge
la 11 kwa kutoa mchango mkubwa katika kupatikana kwa mafanikio haya.
Nina imani kuwa Bunge hili la 12
litafuata nyayo za Bunge la 11. Na katika hili, napenda niliarifu Bunge hili Tukufu
kuwa, kwenye miaka mitano ijayo, tutaendelea kuimarisha ulinzi na usimamizi wa
madini yetu, (kama tulivyofanya kwa kujenga Ukuta Mirerani) kwa kuimarisha
Sheria zetu ili madini yetu yasitoroshwe na Serikali kukoseshwa mapato. Aidha,
tunakusudia kuendelea kufanya majadiliano na wawekezaji wakubwa kwa kuzingatia
mfano wa Makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali na Kampuni ya Barrick
yaliyowezesha kuundwa kwa Kampuni ya Twiga
Minerals Corporation. Nchi yetu imebarikiwa kuwa na madini mbalimbali,
ikiwemo dhahabu, almasi, Tanzanite, chuma, bati, nickel, copper, n.k. Aidha,
tuna gesi aina mbalimbali, kama vile ethane, helium, ambayo hivi karibuni
zimepatikana futi za ujazo bilioni 138 kwenye Ziwa Rukwa, ambazo zinaweza
kuhudumia dunia kwa miaka 20. Hii ndiyo sababu, kila siku nimekuwa nikisema, sisi
sio masikini; sisi ni matajiri. Nchi yetu ni tajiri sana.
Lakini, kuhusu madini pia, kwenye miaka mitano
ijayo pia tutaendelea kuliimarisha Shirika letu la Taifa la Madini (STAMICO)
ili lishiriki kikamilifu kwenye shughuli za madini; kuwawezesha wachimbaji wetu
wadogo, ikiwa ni pamoja na kuwatengea maeneo ya uchimbaji, kuwapatia mafunzo,
mikopo pamoja na vifaa. Na katika natambua kuwa, wapo baadhi ya watu wamepewa
leseni za utafiti na uchimbaji lakini hawajazifanyia kazi; tutazifuta leseni
zao, na maeneo hayo kuyagawa kwa wachimbaji wengine, hususan wachimbaji wadogo.
Wachimbaji wadogo ni muhimu sana katika kukuza sekta ya madini.
Tutaendelea pia kuimarisha masoko ya madini pamoja
na kuhamasisha ujenzi wa viwanda vya uchenjuaji, uyeyushaji, usafishaji na utengenezaji
wa bidhaa za madini. Tunataka madini
yachimbwe hapa Tanzania, yachenjuliwe, yayeyushwe na kisha bidhaa za bidhaa za
madini zitengenezwe hapa hapa Tanzania; na ndipo ziuzwe nje ama watu kutoka nje
waje kununua bidhaa za madini hapa nchini. Ni imani yetu kuwa, kutokana na
hatua tulizopanga kuzichukua sekta ya madini itaweza kuchangia angalau asilimia 10 ya Pato la Taifa ifikapo
mwaka 2025.
Mheshimiwa Spika;
Utalii ni sekta nyingine ambayo tutaipa mkazo
mkubwa kwenye miaka mitano ijayo. Sekta hii imeajiri takriban watu milioni 4. Kwenye miaka mitano
iliyopita, ilikua kwa kiwango cha kuridhisha, ambapo idadi
ya watalii waliotembelea nchini iliongezeka kutoka watalii 1,137,182 mwaka 2015 hadi watalii 1,510,151 mwaka 2019. Mapato nayo yaliongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni 1.9 mwaka 2015 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 2.6 mwaka
2019. Nitumie fursa hii kuipongeza Hifadhi yetu ya Taifa ya Serengeti kwa
kuchaguliwa kuwa Hifadhi Bora Barani Afrika kwa mwaka 2020.
Kwenye miaka mitano ijayo, tumejipanga kuongeza
idadi ya watalii hadi kufikia milioni 5
mwaka 2025 na mapato kutoka Dola za
Marekani bilioni 2.6 za sasa hadi Dola
za Marekani bilioni 6. Hatua tutakazochukua ni pamoja na kupanua wigo wa
vivutio vya utalii, ikiwemo kukuza utalii wa mikutano na uwindaji wanyamapori;
kuimarisha utalii wa fukwe; kujenga miundombinu ya kuwezesha meli za utalii
kuzuru nchini na kuongeza kasi ya utangazaji wa vivutio vyetu. Vilevile,
tutazihamaisha taasisi na watu binafsi kuanzisha ranchi, mashamba na bustani za
wanyama, kama inavyofanyika nchi nyingine, ili kuzuia ujangili na kukuza utalii;
lakini pia kuongeza vipato na fursa za ajira kwa Watanzania. Na katika hilo,
napenda kuwaarifu Watanzania, kupitia Bunge hili Tukufu kuwa, tumepunguza bei
kwa ajili ya kupata wanyama wa mbegu. Mathalan, bei ya nyati wa mbegu imepungua
kutoka Dola za Marekani 1,900 hadi
kufikia shilingi laki mbili; Pofu
kutoka Dola za Marekani 1,700 hadi shilingi 310,000 na Swala kutoka Dola za Marekani 150 hadi shilingi 90,000. Hivyo basi, nawasihi
Watanzania wenzangu, popote walipo, kuchangamkia fursa hiyo; ambayo itachochea
pia uanzishaji wa butcher za wanyama
pori.
Zaidi ya hapo, tutaendelea kupitia upya kodi
na tozo mbalimbali ili kuzifuta ama kupunguza kodi zenye kero. Kwenye miaka mitano
iliyopita, tulipunguza ada ya leseni ya biashara ya utalii
kwa wakala wa kusafirisha watalii yenye idadi ya magari chini ya manne kutoka Dola za Kimarekani 2,000 hadi Dola za Marekani 500 na matokeo yake
idadi ya kampuni za Kitanzania zimeongezeka kutoka 643 mwaka 2015 hadi 1,687
mwaka 2020.
Mheshimiwa Spika;
Tuna imani, hatua hizi
nilizoeleza zitatuwezesha kufikia malengo tuliyojiwekea ya kukuza uchumi kwa
angalau asilimia 8 kwa mwaka, kuinua
vipato vya Watanzania, kupunguza umasikini na kutengeneza ajira mpya milioni 8. Hata hivyo, najua, ili
kufikia malengo haya, tunategemea sana kupata ushirikiano kutoka sekta binafsi.
Kama mnavyofahamu, sekta binafsi ndiyo injini ya kujenga uchumi wa kisasa.
Hivyo basi, narudia kuikaribisha sekta
binafsi ya hapa nchini na kutoka nje kuwekeza katika sekta nilizozitaja; na
ambazo sikuzitaja. Na napenda niwahakikishie watu wa sekta binafsi kuwa,
Tanzania ni mahali pazuri na sahihi pa kuwekeza. Nchi yetu ina amani na
utulivu; tumebarikiwa kuwa na fursa nyingi za uwekezaji; nchi yetu ipo kwenye
eneo la kimkatati; sisi pia ni Wanachama wa jumuiya mbili, EAC na SADC, ambazo
zina soko la watu takriban milioni 500.
Kwa hiyo narudia, kuikaribisha sekta binafsi kuwekeza hapa nchini. Na kwa
bahati nzuri, tangu mwaka jana, tumeanza kutetekeleza Mpango wetu wa Kuboresha
Mazingira ya Biashara nchini (yaani Blueprint
for Regulatory Reforms to Improve the Business Environment in Tanzania).
Hivyo basi, mazingira ya biashara na uwekezaji, kwenye miaka mitano ijayo,
yanatarajiwa kuwa bora zaidi.
Mheshimiwa Spika;
Ili kukuza uchumi pamoja na sekta
za uzalishaji ni lazima tuimarishe miundombinu, hususan ya usafiri na nishati
ya umeme. Kamwe, huwezi kukuza
sekta za kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda, uchimbaji madini na utalii bila kuimarisha
miundombinu na huduma za usafiri pamoja na upatikanaji wa huduma za umeme. Kwa
hiyo, kama ilivyokuwa kwenye miaka mitano iliyopita, tutaendelea kuweka mkazo
mkubwa kwenye ujenzi wa miundombinu ya usafiri na kuboresha huduma za
usafirishaji. Tutakamilisha miradi tuliyoianzisha na kuanza kutekeleza miradi
mipya. Na katika hilo, tumepanga, kwenye miaka mitano ijayo, kukamilisha ujenzi
wa kilometa 2,500 za barabara za
lami na kuanza ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilometa 6,006; ili
hatimaye tuweze kufikia lengo letu la kuunganisha mikoa na wilaya zote kwa
barabara za lami. Barabara hizo zimetajwa kwenye Ilani yetu ya Uchaguzi na
nyingine zinatokana na ahadi nilizotoa kipindi cha Kampeni. Tumepanga pia
kukamilisha ujenzi wa madaraja 7 na kuanza mengine 14, likiwemo Daraja la
Kigongo – Busisi, Wami na Pangani.
Zaidi ya hapo, tutaendelea kushughulia tatizo la msongamano wa magari
kwenye miji na majiji yetu, hususan Arusha, Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza na
hapa Dodoma, ambako tumepanga kujenga barabara ya mzunguko ya njia nne yenye
urefu kilometa 110; ambapo
Wakandarasi wawili tayari wamepatikana na ujenzi utaanza hivi karibuni.
Kwa upande wa usafiri wa reli, tumepanga kuendelea kuimarisha usafiri wa
Reli ya Kati na TAZARA. Aidha,
tutakamilisha ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Dar es Salaam – Dodoma na kuanza
ujenzi wa vipande vya reli ya Mwanza – Isaka; Makutopora – Tabora; Tabora –
Isaka – Tabora – Kigoma na Kaliua – Mapanda – Kalema. Zaidi ya hapo, tutanunua
vichwa vya treni ya njia kuu 39 na
kukarabati 31; tutanunua mabehewa ya
mizigo 800 na kukarabati 690; na pia tutanunua mabehewa 37 ya abiria na kukarabati 60.
Kuhusu usafiri wa majini, tumepanga kukamilisha upanuzi wa bandari zetu kuu
za Dar es Salaam, Tanga na Mtwara pamoja na zilizopo kwenye Maziwa yetu Makuu
(Victoria, Tanganyika na Nyasa). Tumepanga pia kununua meli mpya ya mizigo kwa
ajili ya kutoa huduma Bahari ya Hindi. Tutakamilisha ujenzi wa meli mpya,
kukarabati meli ya Mv. Butiama na kuanza ujenzi wa meli ya kubeba mabehewa (ferry wagon) Ziwa Victoria. Tutaikarabati
MV. Liemba na MT. Sangara pamoja na kuanza ujenzi wa meli mpya ya kubeba abiria
600 na mizigo tani 400; na nyingine kubwa ya kubeba mizigo tani 4,000 kwenye Ziwa Tanganyika.
Kuhusu usafiri wa anga, tutajenga kiwanja kipya cha Msalato, tutafanya
upanuzi na ukarabati wa viwanja vya ndege 11, vikiwemo vya Kigoma, Shinyanga,
Sumbawanga, Tabora, Mtwara na Songea na pia kujenga kwa kiwango cha lami njia
za kutua na kuruka ndege kwenye viwanja vya Iringa, Lake Manyara, Tanga, Musoma,
Lindi, Kilwa Masoko, Njombe, Singida na Simiyu. Zaidi ya hapo, tutanunua ndege
mpya tano, ambapo kama nilivyosema, moja itakuwa ya mizigo.
Ujenzi wa miundombinu hii ya usafiri pamoja na uboreshaji wa huduma za
usafirishaji sio tu utachochea shughuli za uchumi na uzalishaji lakini pia
itakuwa ni hatua nzuri ya kuelekea kufikia malengo yetu ya kuifanya nchi yetu
kuwa lango kuu la biashara kwenye Ukanda huu; na hivyo kuweza kunufaika na
nafasi ya kijiografia.
Mheshimiwa Spika;
Kuhusu sekta ya nishati, tutaendelea kuimarisha miundombinu ya nishati na
pia kuboresha upatikanaji wa huduma za umeme. Na katika hilo, tunakusudia
kukamilisha ujenzi wa Bwawa la kufua Umeme la Nyerere litakalozalisha Megawati 2,115 na kuanza ujenzi wa
miradi mingine ya umeme wa maji Ruhudji Megawati
358; Rumakali Megawati 222;
Kikonge Megawati 300 na pia umeme wa
gesi asilia Mtwara Megawati 300;
Somanga Fungu Megawati 330,
Kinyerezi III Megawati 600 na
Kinyerezi IV Megawati 300; pamoja na
miradi mingine midogo midogo. Aidha, tunakusudia kuzalisha umeme Megawati 1,100 kwa kutumia nishati
jadidifu (jua, upepo, jotoardhi).
Tumepanga pia kukamilisha Miradi wa kusafirisha umeme wa Msongo wa kilovoti 400 wa Singida – Arusha –
Namanga na Iringa – Mbeya – Tunduma ambayo itaunganisha nchi yetu na majirani
zetu wa Kenya na Zambia. Tutatekeleza mingine ya kuunganisha maeneo ya humu
nchini kwenye Gridi ya Taifa, ikiwemo Kigoma. Kwenye miaka mitano iliyopita,
tulitekeleza miradi mingi ya kusafirisha umeme na hivyo kupunguza matumizi ya
umeme wa mafuta; na tukaweza kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 719 kwa mwaka.
Kuhusu umeme pia, kwenye miaka mitano ijayo, tumepanga kufikisha umeme
kwenye vijiji vyote ambavyo bado havijafikishiwa umeme, ambapo idadi yake
haizidi 2,384. Kwenye miaka mitano
iliyopita, kwa takwimu za hadi jana, tumefikisha umeme kwenye vijiji 9,884; kutoka vijiji 2,018 mwaka 2016. Nchi yetu ina vijiji 12,280. Miradi hii yote ya umeme
itakapokamilika, sio tu itatuwezesha tuwe na umeme wa kutosha na kufikisha
umeme kwenye maeneo yote nchini, bali pia itatufanya tuwe na ziada ya kuweza kuuza
nje.
Sambamba na hayo, kuhusu nishati, kwenye miaka mitano ijayo, tutaanza
utekelezaji wa Miradi ya kielelezo (flagship
projects) ya Bomba la Mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga
lenye urefu wa kilometa 1,445 pamoja
na Mradi wa Kusindika Gesi Asilia (LNG) Mkoani Lindi. Zaidi ya hapo,
tutaendelea kuhamasisha matumizi ya gesi asilia na gesi ya mitungi majumbani,
kwenye taasisi, viwanda na magari ili kupunguza uharibifu wa mazingira na
athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Spika;
Dunia hivi sasa ipo kwenye Mapinduzi ya Nne ya Viwanda (yaani The Fourth Industrial Revoulution)
ambayo yanaongozwa na sekta ya mawasiliano (ICT). Shughuli nyingi duniani, kwa
sasa, zinafanyika kwa kutumia TEHAMA. Hivyo basi, sisi nasi hatuna budi
kwendana na kasi hiyo ya kukua kwa sekta ya mawasiliano. Kwa msingi huo,
tumepanga, kwenye miaka mitano ijayo, pamoja na masuala mengine, kufikisha
miundombinu ya Mkongo wa Taifa kwenye maeneo mengi ya nchi yetu, hususan
Wilayani, tutaongeza wigo wa matumizi ya mawasiliano ya kasi (yaani broadband) kutoka asilimia 45 ya sasa hadi asilimia
80 mwaka 2025. Aidha, tumepanga kuongeza watumiaji wa internet kutoka asilimia 43
ya sasa hadi asimilia 80 mwaka 2025
na pia kuboresha matumizi ya simu za mkononi ili kupatikana nchi nzima. Zaidi
ya hapo, tutatoa kipaumbele kwenye masuala ya utafiti na ubunifu kwenye TEHAMA;
tutawatambua na kuwasajili wataalam wote wa TEHAMA; na tunakusudia kuweka
anuani za makazi (postikodi) maeneo
mbalimbali nchini. Tutaimarisha pia usalama kwenye masuala ya Mawasiliano.
Sambamba na kukuza huduma ya mawasiliano, tunakusudia kuendelea kuboresha
huduma za jamii, hususan afya, elimu na maji. Kuhusu AFYA, kama unavyofahamu, kwenye miaka mitano iliyopita tumepata
mafanikio makubwa, ikiwemo kujenga
vituo vya kutolea huduma za afya 1,887 (zahanati 1,198, vituo vya afya 487,
hospitali za wilaya 99, Hospitali za Rufaa za Mikoa 10 na
Hospitali za Rufaa za Kanda 3). Vilevile, tumepunguza vifo vya
akinamama wajawazito kutoka wastani wa vifo 11,000 kwa mwaka mwaka 2015
hadi kufikia wastani wa 3,000 hivi sasa na halikadhalika rufaa za
kupeleka wagonjwa nje zimepungua kwa asilimia 90 baada ya kuimarisha
huduma za kibingwa.
Kwa msingi huo, kwenye miaka mitano ijayo, tunakusudia
kuendeleza ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za afya, hususan zahanati,
vituo vya afya na Hospitali za Wilaya kwenye maeneo ambako hazipo. Tutaimarisha
pia upatikanaji wa dawa, vifaa na vitendanishi na kuongeza watumishi wa afya
pamoja na kuimarisha Mifuko yetu ya Bima ya Afya ili kufikia lengo la
kuwawezesha wananchi wote kupata Bima ya Afya. Wakati wa ugonjwa wa corona, mbali na kumtunguliza mbele
Mwenyezi Mungu, tiba za asili au tiba mbadala zimesaidia sana. Hivyo basi,
kwenye miaka mitano, tunakusudia kuimarisha kitengo cha utafiti wa tiba
mbadala. Hatupaswi kudharau dawa zetu za asili ama tiba mbadala; na kwa sababu
hiyo, matibabu na maduka rasmi ya dawa za asili yataruhusiwa. Zaidi ya hapo, tutaimarisha huduma za matibabu
ya kibingwa na ubingwa bobezi ili kufikia viwango vya kimataifa. Tunataka
huduma zote za afya zipatikane hapa nchini; na ikiwezekana watu kutoka nje waje
kutibiwa hapa nchini. Na kimsingi, tayari wameanza kuja kutibiwa.
Kwenye ELIMU,
tutaendelea kutoa elimu ya msingi na sekondari bila malipo; tutaongeza bajeti
ya mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu ili kuongeza idadi ya wanufaika. Aidha,
tutaendelea kujenga na kukarabati miundombinu ya elimu, ikiwemo shule,
madarasa, mabweni, maabara, maktaba, ofisi na nyumba za walimu, hosteli pamoja
na kumbi za mihadhara. Tutahakikisha tunaendelea kuboresha elimu inayotolewa
ili iweze kutoa maarifa na ujuzi wa kutosha kwa wahitimu. Tutahimiza ufundishaji
wa masomo ya sayansi na hisabati, hususan kwa wanafunzi wa kike; ambapo
tunakusudia kujenga Shule moja ya Sekondari kwenye kila Mkoa kwa ajili ya
kufundisha masomo ya sayansi kwa wasichana. Tutaweka pia mkazo mkubwa kwenye
elimu ya ufundi. Na katika hilo, tunalenga kuanzisha vituo mahiri vya mafunzo kwa taasisi za elimu ili
kuzalisha vijana wenye uwezo unaohitajika Kitaifa, Kikanda na Kimataifa, ambapo
kiasi cha Dola za Marekani milioni 75
kimepangwa kutumika: Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam itabobea katika TEHAMA,
Taasisi ya Teknolojia Mwanza itabobea kwenye masuala ya Ngozi, Chuo cha Taifa
cha Usafirishaji kitakachobobea katika taaluma za usafiri wa anga na Chuo cha
Ufundi Arusha kitabobea katika nishati jadidifu.
Kuhusu MAJI,
mafanikio makubwa sana yamepatikana kwenye miaka mitano iliyopita. Tumetekeleza
miradi ipatayo 1422 yenye thamani ya takriban shilingi trilioni 2.2.
Hii imefanya upatikanaji wa maji
safi na salama uongezeke kutoka asilimia 47 mwaka 2015 hadi kufikia asilimia 70.1 mwaka 2020 kwa vijijini; na kwa mijini kutoka asilimia 74 mwaka 2015 hadi asilimia 84 mwaka 2020.
Hata hivyo, napenda nikiri, nilipokuwa kwenye
Kampeni moja ya changamoto kubwa niliyoelezwa na wananchi ilikuwa shida ya
maji, hususan maeneo ya vijijini. Kwa msingi huo, kwenye miaka mitano ijayo,
tutajitahidi kuelekeza nguvu zaidi katika kushughulikia, ikiwemo kwa
kuhakikisha fedha zinazopelekwa vijijini kutekeleza miradi ya maji zinatumika
vizuri. Nataka kuona miradi ya maji inayojengwa inakamilika kwa wakati.
Watendaji wawe wabunifu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea. Mito na Maziwa yetu
yatumike kikamilifu katika kuwafikisha maji kwa wananchi.
Kwenye miaka mitano ijayo pia, tutaimarisha
Mfuko wa Taifa wa Maji ili kuuongezea uwezo wa kifedha wa kutekeleza miradi ya
maji. Tutakamilisha pia miradi mikubwa, ukiwemo wa Miji 28 utakaogharimu shilingi trilioni 1.2; Mradi wa Maji wa
kutoa maji Ziwa Victoria unaogharimu takriban shilingi bilioni 600 na Mradi Mkubwa wa Arusha wenye thamani ya shilingi bilioni 520. Lakini, nitumie
fursa hii pia kuwasihi Watanzania kulinda vyanzo vya maji na miundombinu
inayojengwa. Na nitoe wito kwa viongozi wote, mkiwemo Waheshimiwa Wabunge,
kulifanya suala la kutunza vyanzo vya maji na miundombinu yake kuwa ajenda
muhimu katika shughuli zenu.
Mheshimiwa Spika;
Kwenye miaka mitano ijayo, tumejipanga kuendelea
kuimarisha na kukuza uhusiano wetu na nchi mbalimbali kwa kuzingatia Sera yetu
ya Mambo ya Nje inayoweka msisitizo diplomasia ya kiuchumi. Tutakuza urafiki na
ujirani mwema na pia tutashiriki kikamilifu kwenye shughuli za Kikanda, Kibara
na Kimataifa, hususan kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC); Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC); Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa.
Tutaendelea pia kushiriki kwenye shughuli za kulinda amani.
Halikadhalika, kwenye miaka mitano ijayo, tutaendeleza
jitihada za kukuza na kuimarisha demokrasia, kulinda uhuru na haki za wananchi
na vyombo vya habari. Hata hivyo, ningependa kukumbusha kuwa, lengo la
demokrasia ni kuleta maendeleo na sio fujo; na hakuna demokrasia isiyo na
mipaka. Aidha, Uhuru na Haki vinakwenda samabamba na wajibu. Hakuna uhuru au
haki isiyo na wajibu. Vyote vinakwenda sambamba.
Mheshimiwa Spika;
Kama nilivyoahidi wakati wa kipindi cha
Kampeni, kwenye miaka mitano ijayo tutaendelea kuboresha mazingira ya kufanya
biashara kwa wajasiriamali wadogo (machinga, mama lishe, baba lishe, waendesha
boda, bajaji, n.k.). Kama mnavyofahamu, kwenye miaka mitano iliyopita,
tulianzisha utaratibu wa kutoa Vitambulisho Maalum kwa wajasiriamali wetu
wadogo. Kwenye miaka mitano ijayo, tunakusudia kuviboresha vitambulisho,
ikiwemo kuweka picha na taarifa nyingine muhimu, kama ilivyo kwenye
Vitambulisho vya Taifa au Pasipoti. Hii itawawezesha wafanyabiashara
watakaotumia vitambulisho hivyo kutambulika, ikiwemo kwenye benki na hivyo
kupata mikopo kwa ajili ya kukuza biashara. Hii itawawezesha wafanyabiashara
wetu wadogo kukua na kutajirika. Na hilo ndilo lengo letu. Tunataka
wafanyabiashara wetu wadogo wawe wanakua na kutajirika; na sio siku zote wabaki
kuwa wafanyabiashara wadogo.
Kwenye miaka mitano ijayo pia, tutakuza sekta
ya sanaa, michezo na utamaduni ambayo inakua kwa kasi kubwa hivi sasa. Kama
nilivyoahidi wakati wa Kampeni, tutaikuza zaidi sekta hii, hususan kwa
kuimarisha usimamizi wa masuala ya Hati Miliki ili wasaniii waweze kunufaika na
kazi zao; tutahuisha Mfuko wa Utamaduni na Sanaa ili kuwasaidia wasanii wetu,
ikiwemo kupata mafunzo na mikopo. Tutaanza pia kutenga fedha kidogo kidogo kwa
ajili ya kuziandaa Timu zetu za Taifa. Na katika hilo, napenda kutumia fursa
hii kuitakia heri Timu yetu ya Taifa, Taifa
Stars, kwenye mechi yao dhidi ya Tunisia baadaye leo pamoja na
Mwanamasumbwi wetu, Hassan Mwakinyo, ambaye naye ana pambano letu. Watanzania tunataka
ushindi.
Mheshimiwa Spika;
Kwenye miaka mitano iliyopita, tumefanikiwa kuhamishia
Makao Makuu ya Serikali hapa Dodoma. Viongozi na Watumishi wote wa Serikali
wenye kustahili kuhamia Dodoma tayari wamehamia. Kwenye miaka mitano ijayo, tutakamilisha
ujenzi wa ofisi na pia kuendelea na ujenzi wa makazi ya watumishi. Zaidi ya
hapo, tutaendelea kutekeleza miradi ya miundombinu, ambayo tayari nimeitaja
(barabara ya njia nne, Uwanja wa ndege wa Msalato) na kushughulikia suala la
upatikanaji maji katika Jiji la Dodoma.
Masuala mengine ambayo tutayapa kipaumbele ni
kama ifuatavyo:
(i)
Uendelezaji na uboreshaji wa makazi wa
wananchi, ambapo tutahakikisha vifaa vya ujenzi vinapatikana kwa gharama nafuu
na mikopo ya ujenzi inapatikana kwa riba nafuu;
(ii)
Tutashughulikia pia masuala ya mabadiliko ya
tabianchi;
(iii)
Tutashughulikia masuala ya watu wa makundi
maalum, ikiwemo wazee na watu wenye ulemavu;
(iv)
Tutaendeleza vita dhidi ya biashara haramu ya
dawa za kulevya;
(v)
Tutaimarisha sekta ya misitu na nyuki, ikiwemo
kwa kuanzisha viwanda vya mazao ya nyuki ili sekta hiyo itoe mchango mkubwa
kwenye uchumi wa nchi yetu. Tutahamasisha pia ufugaji wa nyuki.
(vi)
Tutahakikisha wamiliki wa magari wanatoa
mikataba kwa madereva ili kuipa hadhi inayostahili kazi hiyo na kuchochea
shughuli za huduma za usafirishaji. Na katika hiyo, ikiwezekana, itatungwa
Sheria mahususi.
Tutashughulikia pia kero mbalimbali za
wananchi, ikiwemo migogoro ya ardhi, mirathi, n.k. Na katika hili napenda
kuwaagiza viongozi wa Serikali kuanzia ngazi za vijiji, kata, tarafa, wilaya na
mikoa kuhakikisha wanatenga siku maalum za kukutana na wananchi kwenye maeneo
yao ili kusikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi.
Mheshimiwa Spika;
Kwa ujumla, mambo tuliyopanga kutekeleza ni
mengi; ni mengi sana. Baadhi nimeyaeleza na yapo mengine mengi ambayo
yameelezwa vizuri kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM yenye kurasa 303, lakini kwa
sababu ya muda sitoweza kuyaeleza yote. Hivyo basi, nawaagiza Mawaziri
nitakaowateua pamoja na Watendaji kuisoma vizuri, kuielewa na kuitafsri vizuri
Ilani hiyo katika Sera na Mipango Kazi ya Utekelezaji kwenye Wizara au Taasisi wanazoziongoza
ili ikifika mwaka 2025, tuwe tumeitekeleza yote.
Lakini, najua, ili kuweza kutekeleza Ilani
yetu vizuri, tutahitaji sana kupata ushirikiano kutoka kwenye Bunge hili. Kama
mnavyofahamu, Bunge ni kiungo muhimu kati ya Serikali na Wananchi. Kwa hiyo,
nina uhakika, endapo tutashirikiana vizuri, miaka mitano ijayo itakuwa ya
maajabu na mafanikio makubwa kwa nchi yetu. Na binafsi, sina shaka kwamba,
Bunge hili litatoa ushirikiano wa kutosha kwa Serikali.
Hata hivyo, napenda niweke bayana kuwa,
ninaposema tunaomba ushirikiano haimaanishi kwamba tunataka muunge mkono kila
kitu. La hasha! Penye kukosoa kusoeni; lakini kwa hoja na kutoa mapendekezo ya
namna ya kushughulikia. Tunahitaji constructive
criticism na sio kukosoa kwa lengo la kukosoa tu. Na katika hilo, kwa
upande wetu Serikali, tunaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Bunge hili ili
kuliwezesha kutimiza majukumu yake ipasavyo. Tutatoa pia ushirikiano kwa
Mhimili wa Mahakama, ili nao uweze kutimiza majukumu yake ya kusimamia haki
nchini. Kama mnavyofahamu, Mahakama ni muhimu sana katika kuongoza Serikali. Ni
muhimu katika kujenga maelewano katika jamii, kudumisha amani na usalama na pia
kuchochea shughuli za kiuchumi.
Mheshimiwa Spika;
Kwa mujibu wa Katiba
yetu, mimi ni sehemu ya Bunge hili. Hivyo basi, kabla sijahitimisha, napenda
kutumia fursa hii kuwashukuru wageni wetu wote walioungana nasi kwenye tukio
hili. Baada ya kusema hayo, sasa natamka kwamba nimelifungua rasmi Bunge la 12
la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Asanteni kwa kunisikiliza!
Mungu libariki Bunge letu na Wabunge wake!
Mungu Ibariki Tanzania!
“Ahsanteni
sana kwa Kunisikiliza”
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇