Mgeni rasmi katika kilele cha Lamadi Utalii Festival, Mbunge wa Busega
Dkt. Rafael Chegeni akipokea sanamu yenye sura ya Rais wa jamhuri wa
Muungano wa Tanzania,Dkt. Joseph Pombe Magufuli iliyotengenezwa na
Ndumisali Lema (mwenye rasta). Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Busega,Tano
Mwera
NA ANDREW CHALE, BUSEGA.
MBUNGE wa Jimbo la Busega lililopo Mkoani Simiyu, Dkt. Rafael Chegeni amewataka Vijana kuchangamkia fursa za kiuchumi zitokanazo na Utalii kupitia tamasha la kukuza na kuendeleza Utalii Wilaga ya Busega la 'Lamadi Utalii Festival' lililokuwa likifanyika kwa siku nne katika shule ya Msingi Itongo, mjini Lamadi.
Akizungumza wakati alipokuwa mgeni rasmi katika kilele cha tamasha hilo, Dkt. Rafael Chegeni alieleza kuwa, vijana wengi wapo tu mitaani bila kujishughulisha wakiwemo wengine kucheza 'pooltable' hivyo ni wakati sasa kuanza kubuni vitu mbalimbali vitokanavyo na fursa katika Utalii.
"Huu ni mwanzo tu. Tamasha la Lamadi Utalii liwe chachu kwenu. Mji utakuwa kwa kasi zaidi kama miji mingine ya kitalii kama ilivyo Karatu hivyo mchangamkie fursa na nyie hapa Lamadi.
Muanze kubuni na kutengeneza vitu mbalimbali ili hata watalii wanaoweza kuja hapa waweze kuviona na kuvutiwa waweze kununua, wakiweza kununua namna hii mtapata kipato kwa hiyo wito wangu kwa vijana wote sasa sio muda wa kulala ni muda wa kuchapa kazi" alisema Dkt. Chegeni.
Aidha, katika hatua nyingine, Dkt. Chegeni kupitia ofisi yake ya Mbunge, ameahidi kutoa kiasi cha Tsh. Laki Tano kwa ajili ya kusaidia mafunzo kwa vijana wote watakaopenda kujifunza mambo ya kuongoza watalii 'Tour guide' kwa muda mfupi.
"Niseme tu. Naomba vijana mchangamkie fursa. Hapa tunae mtaalam wa kuongoza watalii Nelson Machibya. Naomba ajitolee kuwasaidia na yupo tayari kwa hilo lakini mimi natoa Shilingi Laki Tano za kufanikisha hilo." Alisema Dkt. Chegeni.
Hata hivyo alitumia wasaha huo kuomba wadau kuja Lamadi kuwekeza Vyuo ama shule za mambo ya Utalii ilikuongeza fursa zaidi."Lakini kama itawezekana watu wachangamkie fursa kuja kuwekeza mafunzo ya kutembeza watalii.
watu wachangamkie hilo na tupo tayari kuwasaidia mji bado una maeneo makubwa ya fursa" alieleza Dkt Chegeni.
Katika kufunga tamasha hilo, Dkt. Chegeni aliweza kupokea sanamu yenye sura ya Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt. Joseph Pombe Magufuli ikiwa ameshika Mwenge wa Uhuru ambayo ilitengenezwa na moja ya kundi la vijana wabunifu wa mji huo.
"Maisha siku hizi ni ya kuangaika, nawapongeza vijana hawa kwa kubuni vitu vya kisanaa ikiwemo sanamu ili lenye sura ya Rais ambalo limepokelewa kwa shangwe na wananchi wote hapa baada tu ya kuliona hii inaashiria Rais wetu anapendwa muda wote na Watanzania.
Hii iwe msukumo kwa vijana wengine na fundisho kwao hiyo ni sehemu kwamba vijana sasa sio muda wa kukaa na kulalamika kwamba tuna njaa, hatuna chakula, kazi ya mikono yao ndio itawapa ridhiki ya kuweza kuishi na kuweza kuamka katika maisha yao." Alisema Dkt. Chegeni
ambapo kwa kutambua hilo, la kusaidia vijana, aliwahakikishia kupitia ofisi yake kusaidia kupata watalaam wawape zaidi ujuzi wa kuweza kuboresha kazi zaidi huku akiwashauri waweze kujisajili kama kikundi.
"Lakini niwashauri kikundi chenu kisajiliwe ili kiweze kutambulika rasmi, mukitawanyika huku sio lahisi kufikiwa na fursa.Mkisajiliwa itakuwa rahisi kusaidiwa hata rasilimali za kifedha" alieleza Dkt. Chegeni.
Dkt. Chegeni pia aliweza kugawa vyeti vya ushiriki na kutambua mchango kwa wadau wote kwa ushiriki wao.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Busega ambaye pia ndie Mwenyekiti wa Tamasha hilo, Tano Mwera alisema tamasha lijalo litakuwa na muamko mkubwa huku akiwataka wananchi na wadua kuendelea kuliunga mkono.
Tamasha hilo lililokuwa la siku nne huu ni msimu wake wa kwanza kufanyika katika viunga vya Mji unaokuwa kwa kasi wa Lamadi huku likidhaminiwa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA).
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇