LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Sep 23, 2019

RAIS MAGUFULI AMJULIA HALI ASKOFU MKUU WA JIMBO KUU KATOLIKI LA DAR ES SALAAM ANAYEPATIWA MATIBABU TAASISI YA MIFUPA MUHIMBILI (MOI)


 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana kwa furaha na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mhashamu Yuda Thadeus Ruwa’ichi ambaye anapatiwa matibabu katika Taasisi hiyo ya Mifupa Muhimbili (MOI) mara baada ya kufanyiwa upasuaji wa Kichwa 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiongoza sala ya kumuombea Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mhashamu Yuda Thadeus Ruwa’ichi ambaye anapatiwa matibabu katika Taasisi hiyo ya Mifupa Muhimbili (MOI)

 
Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam Mhashamu Yuda Thadeus Ruwa’ichi akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alienda kumjulia hali katika Taasisi hiyo ya Mifupa Muhimbili (MOI). Wakwanza kulia ni Askofu Msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, kushoto ni Padre Dkt. Alister Makubi Paroko wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro Parokia ya Oysterbay jijini Dar es salaam 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa na Askofu Msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam kulia, Padre Dkt. Alister Makubi kushoto, Paroko wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro Parokia ya Oysterbay jijini Dar es salaam wakifurahia jambo pamoja na Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam Mhashamu Yuda Thadeus Ruwa’ichi ambaye hali yake imezidi kuimarika mara baada ya kufanyiwa upasuaji katika taasisi hiyo ya MOI. PICHA NA IKULU.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 23 Septemba, 2019 amemjulia hali Askofu Mkuu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam Mhashamu Yuda Thaddaeus Ruwa’ichi anayepatiwa matibabu katika Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) Jijini Dar es Salaam. 

Mhe. Rais Magufuli amemkuta Baba Askofu Mkuu Ruwa’ichi akiwa anaendelea vizuri tofauti na hali ilivyokuwa alipomtembelea tarehe 10 Septemba, 2019 siku aliyoletwa MOI akitokea Hospitali ya KCMC Mkoani Kilimanjaro alikougua ghafla baada ya kupatwa na ugonjwa wa kiharusi. 

Akiwa MOI, Baba Askofu Mkuu Ruwa’ichi amefanyiwa upasuaji na timu ya Madaktari Bingwa wa ubongo na mishipa ya fahamu kwa mafanikio na sasa anaendelea vizuri. 

Mhe. Rais Magufuli ameeleza kufurahishwa kwake na kuimarika kwa hali ya Baba Askofu Mkuu Ruwa’ichi na amewapongeza Madaktari Bingwa wa MOI kwa kumtibu kwa mafanikio makubwa. 

Aidha, Mhe. Rais Magufuli, Baba Askofu Mkuu Ruwa’ichi, Baba Askofu Mkuu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mhashamu Eusebius Nzigilwa na Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Petro Padre Dkt. Alister Makubi wamesali sala ya pamoja ya kumshukuru Mungu kwa uponyaji na kuwaombea wagonjwa wote wapone haraka. 

Baada ya kutoka MOI, Mhe. Rais Magufuli amewajulia hali wagonjwa waliolazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) akiwemo Baba Mzazi wa Daktari wa Rais, Mzee Wilson Ngwale aliyelazwa hospitalini hapo. 

Kabla ya kutembelea wagonjwa, Mhe. Rais Magufuli amekwenda Msasani Jijini Dar es Salaam kumpa pole Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (JWTZ) Jen. Venance Salvatory Mabeyo ambaye amefiwa na mwanae Nelson Venance Mabeyo (aliyekuwa Rubani) ambaye amefariki dunia leo asubuhi baada ya ndege aliyokuwa akiiendesha kupata ajali muda mfupi baada ya kuruka kutoka uwanja mdogo wa ndege wa Seronera Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara. 

Mapema leo asubuhi, Mhe. Rais Magufuli ameongoza kikao cha Baraza la Mawaziri kilichofanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam. 


Gerson Msigwa 
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU 
Dar es Salaam 
23 Septemba, 2019

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages