Friday, December 4, 2015

MAUZAUZA

(Dkt. MUHAMMED SEIF KHATIB)
Mwanadamu ameumbwa na milango ya fahamu.  Milango hiyo ya utambuzi humsaidia mtu kuelewa kitu au jambo liliopo.  Huweza kutambua kitu kwa kukishika, kukisia, kufikiria au kudhani.  Lakini kwa vile  milango hiyo ni mingi, binadamu anao uwezo wa kugusa, kuonja, kunusa au kusikia.  Hata hivyo, mwanadamu huweza kumghilibu binadamu mwingine au kumdanganya kwa kutumia milango hiyo ya utambuzi na hatimaye kumpotosha.  Upo uwezo wa kudanganya macho ili yaone mambo kinyume na yalivyo.  Mtindo huo huitwa “mauzauza” au “kiinimacho”.  Katika Bunge la Tanzania, hivi majuzi kambi ya upinzani walionesha mchezo huo wa “mauzauza” au “kiinimacho” mbele ya Rais  wetu na viongozi kadha wa  kitaifa.

Na kwa vile vyombo vya habari vilitangaza na kuonesha vituko na viroja vyao, hali ilikuwa  dhahiri shahiri.  Viongozi wa genge la upinzani walisimama na kutaka Rais halali wa Zanzibar Dkt.  Shein eti asiingiye Bungeni kwa kudai kuwa si Rais halali wa Zanzibar na muda wake wa uongozi umekwisha.  Kama hilo halitoshi, walionesha ujinga wao na ushenzi wao  kwa kuzomea Bungeni na kufanya fujo.  Nia yao ni ilikuwa kumtetea Maalim kuwa ndiye aliyeshinda wakati Tume ya Uchaguzi chombo halali hakijamtangaza. Maalim  alifanya makosa makubwa  kwa kujitangazia ushindi wa Urais wa Zanzibar.

Nilidhani kambi ya  upinzani wakati wanasema Dkt. Shein siyo Rais halali wa Zanzibar basi na wakati huo huo mshirika wao wa UKAWA Maalim naye angeandika barua rasmi ya kujiuzulu nafasi yake ya Umakamo wa Kwanza wa Rais kwani na yeye muda wake umekwisha.  Hawawezi wapinzani kumtaka Dkt. Shein Rais wa Zanzibar aondoke  Ikulu lakini UKAWA wanapata kigugumizi  cha kumwambia  Makamo wa Kwanza na yeye atoke Ikulu!  Nilikuwa Zanzibar juzi, nilishtuka na kushangaa nilipomwona Maalim amepanda gari yenye nembo ya serikali ya Zanzibar pembeni mwa gari hiyo ipo bendera inapepea ya SMZ.  Mbele ya gari ya Maalim  ipo pikipiki ya polisi na gari za polisi za Serikali ya Muungano.  Nyuma ya gari yake wapo askari na sare zao wameshika silaha za ulinzi.

Niliambiwa kuwa gari ile ilikuwa inatokea ofisini pake Migombani ambayo imeandikwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.  Mlangoni hapo ofisini pake walinzi wake wakampa saluti ya nguvu ya heshima.  Naye bila kuchelewa huku akikenya akaipokea.  Baada ya udadisi wangu nikaambiwa bado anaishi katika jengo linalolipiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.  Hata huduma za nyumbani kwake bado zinabebwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.  Hata safari zake; za kwenda nje ya Unguja kama Pemba na Dar es Salaam, ndege aitumiayo hulipwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Sina hakika kama mshahara wa mwezi wa Novemba kama atapokea au la! Ni dhahiri bado anahudumiwa kiofisi na kimasilahi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.  Analindwa na Serikali ya Muungano.

Nini tunajifunza? Wanayoyasema UKAWA siyo wanayoyatenda.  Kama bungeni walikataa Dr. Shein asiingiye bungeni kwa sababu siyo Rais halali wa Zanzibar kwa nini hao hao wasimtake Maalim aandike barua ya kujiuzulu umakamo?  Kwa nini wasimtake aache kuishi Ikulu, akataye ulinzi, asitumie gari la serikal na  bendera?  Kwa nini asiache kutumia ndege za serikali na akitaka kwenda Pemba apande  jahazi? 

Hivi wale wabunge wa kambi ya upinzani waliokuwa Dodoma si wanatakiwa wamwombe radhi Rais Magufuli, Rais Shein na Watanzania kwa utovu wao wa adabu?  Waombe radhi kwa kuwadanganya Watanzania kusema kuwa Rais Shein siyo Rais halali wakati mshirika wao wa UKAWA Maalim bado anang’ang’ania Ikulu na kufaidi huduma  za kimasilahi na ulinzi kwa fedha za walipa kodi?  UKAWA waungame kuwa walichofanya ni “mauzauza” na “kiinimacho” tu.

Share:

KUCHAGUA LUGHA

IDADI YA WATU AMBAO HUTEMBELEA BLOGU HII

KUMBUKUMBU ZA POSTI ZOTE

JISAJILI UPATE TAARIFA KWA EMAIL

Jisajili ili upate taarifa kwa email

Google+ Followers

Powered by Blogger.