(Dkt. MUHAMMED SEIF KHATIB)
Mwanadamu ameumbwa na milango ya
fahamu. Milango hiyo ya utambuzi
humsaidia mtu kuelewa kitu au jambo liliopo.
Huweza kutambua kitu kwa kukishika, kukisia, kufikiria au kudhani. Lakini kwa vile milango hiyo ni mingi, binadamu anao uwezo wa
kugusa, kuonja, kunusa au kusikia. Hata
hivyo, mwanadamu huweza kumghilibu binadamu mwingine au kumdanganya kwa kutumia
milango hiyo ya utambuzi na hatimaye kumpotosha. Upo uwezo wa kudanganya macho ili yaone mambo
kinyume na yalivyo. Mtindo huo huitwa “mauzauza”
au “kiinimacho”. Katika Bunge la
Tanzania, hivi majuzi kambi ya upinzani walionesha mchezo huo wa “mauzauza” au
“kiinimacho” mbele ya Rais wetu na
viongozi kadha wa kitaifa.
Na kwa vile vyombo vya habari vilitangaza na
kuonesha vituko na viroja vyao, hali ilikuwa dhahiri shahiri. Viongozi wa genge la upinzani walisimama na
kutaka Rais halali wa Zanzibar Dkt.
Shein eti asiingiye Bungeni kwa kudai kuwa si Rais halali wa Zanzibar na
muda wake wa uongozi umekwisha. Kama hilo
halitoshi, walionesha ujinga wao na ushenzi wao kwa kuzomea Bungeni na kufanya fujo. Nia yao ni ilikuwa kumtetea Maalim kuwa ndiye
aliyeshinda wakati Tume ya Uchaguzi chombo halali hakijamtangaza. Maalim alifanya makosa makubwa kwa kujitangazia ushindi wa Urais wa Zanzibar.
Nilidhani kambi ya upinzani wakati wanasema Dkt. Shein siyo Rais
halali wa Zanzibar basi na wakati huo huo mshirika wao wa UKAWA Maalim naye
angeandika barua rasmi ya kujiuzulu nafasi yake ya Umakamo wa Kwanza wa Rais kwani
na yeye muda wake umekwisha. Hawawezi
wapinzani kumtaka Dkt. Shein Rais wa Zanzibar aondoke Ikulu lakini UKAWA wanapata kigugumizi cha kumwambia Makamo wa Kwanza na yeye atoke Ikulu! Nilikuwa Zanzibar juzi, nilishtuka na
kushangaa nilipomwona Maalim amepanda gari yenye nembo ya serikali ya Zanzibar pembeni
mwa gari hiyo ipo bendera inapepea ya SMZ.
Mbele ya gari ya Maalim ipo
pikipiki ya polisi na gari za polisi za Serikali ya Muungano. Nyuma ya gari yake wapo askari na sare zao
wameshika silaha za ulinzi.
Niliambiwa kuwa gari ile ilikuwa inatokea
ofisini pake Migombani ambayo imeandikwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar. Mlangoni hapo
ofisini pake walinzi wake wakampa saluti ya nguvu ya heshima. Naye bila kuchelewa huku akikenya akaipokea. Baada ya udadisi wangu nikaambiwa bado anaishi
katika jengo linalolipiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hata huduma za nyumbani kwake bado zinabebwa
na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Hata safari zake; za kwenda nje ya Unguja kama Pemba na Dar es Salaam,
ndege aitumiayo hulipwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Sina hakika kama
mshahara wa mwezi wa Novemba kama atapokea au la! Ni dhahiri bado anahudumiwa
kiofisi na kimasilahi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Analindwa na Serikali ya Muungano.
Nini tunajifunza? Wanayoyasema UKAWA siyo
wanayoyatenda. Kama bungeni walikataa
Dr. Shein asiingiye bungeni kwa sababu siyo Rais halali wa Zanzibar kwa nini
hao hao wasimtake Maalim aandike barua ya kujiuzulu umakamo? Kwa nini wasimtake aache kuishi Ikulu, akataye
ulinzi, asitumie gari la serikal na bendera?
Kwa nini asiache kutumia ndege za serikali na akitaka kwenda Pemba apande
jahazi?
Hivi wale wabunge wa kambi ya upinzani waliokuwa
Dodoma si wanatakiwa wamwombe radhi Rais Magufuli, Rais Shein na Watanzania kwa
utovu wao wa adabu? Waombe radhi kwa
kuwadanganya Watanzania kusema kuwa Rais Shein siyo Rais halali wakati mshirika
wao wa UKAWA Maalim bado anang’ang’ania Ikulu na kufaidi huduma za kimasilahi na ulinzi kwa fedha za walipa
kodi? UKAWA waungame kuwa walichofanya
ni “mauzauza” na “kiinimacho” tu.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇