Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimepongezwa kwa kufanya mkutano wake Mkuu Maalum kwa njia ya mtandao na kwamba kwa kufanya hivyo kimeonyesha njia kwenye teknolojia ya mawasiliano.
CCM imefanya Mkutano huo, leo Julai 26, 2025, jijini Dodoma ukiongozwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ambapo kutokana na kutano huo kufanyika kwa njia ya mtandao wajumbe wa mkutano huo nchini kote wameshiriki.
"Binafsi nimefarijika mno kusikia Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimefanya mkutano mkuu maalumu kupitia mtandao. Inahitaji kupongezwa kwa kuwa yapo manufaa makubwa ambayo nitayaeleza. Niwaase CCM kuwa hii isiwe tu kwa mkutano huu bali mikutano mingi", ameandika Yahya Msangi kwenye ukurasa wake wa Facebook.
Akieleza historia ya mikutano ya kimtandao (online conferences) Yahya Msangi ambaye amekuwa akihudumu katika mashirika mbalimbali ya Umoja wa Mataifa (UN) kwa miaka mingi amesema;
"Nikiwa mshiriki wa mikutano ya kimataifa haswa chini ya UN kuanzia 1972 (Stockholm Conference on Environment) nimeshuhudia hasara kubwa zitokanazo na hii mikutano ya uso kwa uso (face 2 face conferences).
Baadhi yetu tulianza kupinga hii mikutano chini ya kikundi kilichopinga ugonjwa tuliouita "Stockholm syndrome". Ugonjwa wa kuandaa mikutano kila tatizo au Kila jambo jipya lilipojitokeza.
Hakika dunia inaugua hili gonjwa kwa kiwango cha kutisha. Lakini kikundi chetu kilipingwa mno na wengi. Watu na nchi zinataka mikutano kwa sababu mbalimbali. Mikutano inafanyika matatizo hayaishi na mapya yanajitokeza".
Ni Nini madhara ya gonjwa la Stockholm Syndrome?
1. Matumizi makubwa ya fedha. Chukulia mkutano wa UNFCCC au UNCCD, au CBD. Hii hufanyika kila mwaka na huhudhuriwa takribani na wajumbe kati ya 30000-50000, ni fedha kiasi gani inatumika kugharamia malazi, usafiri na chakula?
Mikutano hii huchukua wiki mbili. Sasa angalia mkutano maalumu wa CCM? Wajumbe takribani 3000, kama kila mmoja ataenda Dodoma unadhani zitatumika kiasi gani kuwalipa posho? Na hii sio Kwa CCM pekee. Hebu fikiria mkutano mkuu wa ACT au CHADEMA? Wangeokoa kiasi gani kama wangeendesha kimtandao kama ambavyo CCM wanafanya leo?
2. Kuwaondoa watu maofisini au kwenye biashara na shughuli zao za kila siku.
Ni gharama kiasi gani nchi au chama au taasisi inaingia kwa kuwa tu watendaji wamesafiri? Fikiria watendaji woote wa CCM leo wangekuwa Dodoma? Fikiria mawaziri woote leo wasingekuwa maofisini? Fikiria wabunge woote leo wasingekuwa majimboni?
3. Mikutano kuongeza tatizo ambalo wanataka kulitatua.
Fikiria mkutano wa kudhibiti uharibifu wa mazingira aka UNFCCC Conference of Parties? Ni Moshi wa ndege tani ngapi utazalishwa na ndege zitakazopeleka wajumbe kuhudhuria mkutano? Wakifika watajadili namna ya kupunguza hewa mkaa (carbon) ambao wamezalisha mamilioni ya tani wakati wakija kwenye mkutano! Pale mkutanoni watakula na kuchafua mazingira pia! Na kama mkutano ni kuhusu janga la UKIMWI wataambukizana ndani ya hizo wiki. NImetaja madhara machache tu ili Makala isiwe ndefu saaana, lakini mwenye akili ataona faida ya kukutana kimtandao.
Sasa serikali na CCM na vyama vyote vijikite kwenye mikutano ya kimtandao kama huu wa CCM. Najua mtakumbana na watu watakaopinga kama ilivyo kimataifa. Watu wanataka safari ili wapate posho na watalii. Muwakatalie. Iwepo mikutano michache tu ya kukutana uso kwa uso. Hata vyama vya upinzani unakuta IT kwao ni kuandaa press conferences na post tu! Huoni wakifanya mikutano kimtandao wakati wengine kama CHADEMA wanaojiita CHADEMA DIGITAL! Mikutano wanatumia ANALOGUE!
Wizara nazo zitoe kipaumbele kwa online conferencing. Haina maana watu wa wizara moja wanaondoka kituo kimoja mfano Dodoma kwenda kujadiliana Morogoro au Arusha. Kuna maana gani kuwa na vitengo vya IT wizarani halafu vitengo hivyo havitumuki kuandaa mikutano kimtandao? Unakuta eti nao wanasafiri kwenda kusaidia ku install wifi na power point projectors kwenye kikao!
Hata bunge letu lianze sasa kukutana mara nyingi kimtandao. Tutanufaika mno kama Taifa. Hii mambo ya watu 400 kukaa mwezi Dodoma ni matumizi mabaya ya fedha za walipa Kodi. Mbunge awekewe vifaa ofisi ya Jimbo ili ashiriki kupitia mtandao. Kwanza kuna wengi hata hawaendi au wanaenda na kusaini halafu wanasepa na wanalipwa.
Kwa kuwa tuko kwenye uteuzi basi moja ya sifa ya mgombea iwe uwezo wa kushiriki mikutano kimtandao. Awe anajua kutumia platform kama zoom, go2meeting, webinar, n.k.
CCM: hii isiwe kama ebola inakuja na kuondoka. Liwe zoezi endelevu. Muachane na zama za kuandaa mikutano ya kuita wajumbe mkoa mmoja. Tuachane na CCM ya kina Polepole! CCM ANALOGUE. Maneno mengii matumizi ya TEKNOLOJIA sufuri
Binafsi ningependa secretariat ya CCM itoe tathmini ya gharama ambazo zimeepukika kwa kutumia online conference. Ili liwe funzo kwa wote.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiongoza Mkutano Mkuu Maalum wa Chama hicho uliofanyika kwa njia ya Mtandao katika ukumbi wa mkutano wa NEC (White House) Makao Makuu ya CCM, Jijini Dodoma tarehe 26 Julai, 2025. Chama cha Mapinduzi (CCM) kimefanya mkutano huo Mkuu kwa mara ya kwanza kwa njia ya mtandao na kuwakutanisha Wajumbe wote wa Mkutano huo kote nchini. Cde Yahya Msangi



No comments:
Post a Comment
Tupia Comments👇