MBUNGE wa Viti Maalumu kupitia kundi la wafanyakazi. Dkt. Alice Kaijage ameishauri serikali kuiongezea fungu la fedha za bajeti Wakala wa Serikali Mtandao (eGA) ili iweze kusimamia vizuri mifumo ya utendaji kazi katika utumishi wa umma na taasisi za umma.
Amesema kuwa mifumo hiyo ambayo kwa sasa imeunganishwa katika Taaisi za serikali 433 kati ya 522, ikisimamiwa vizuri itasaidia kuongeza ufanisi katika maeneo ya kazi, kuboresha maslahi ya watumishi, hivyo kupunguza upendeleo, uonevu na unyanyasaji.
Dkt. Kaijage ametoa ushauri huo alipokuwa akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora bungeni Dodoma Aprili 19, 2023.
"Mifumo hiyo ukiwemo wa utoaji taarifa za utumishi wa umma na mishahara itaongeza ubora wa kazi, ufanisi na kuwatia moyo wafanyakazi lakini pia itapunguza upendeleo, uonevu pamoja na unyanyasaji," amesema Dkt. Kaijage huku akishangiliwa na wabunge kwa kugonga meza.
Ameutolea mfano mfumo wa utoaji taarifa za utumishi na mishahara kuwa umerahisisha sana mchakato ambapo awali ilikuwa inachukua siku takribani 14 kukamilisha lakini hivi sasa kazi hiyo ya kusambaza mishahara inachukua siku moja.
Aidha, Dkt Kaijage amesema kuwa mfumo huo ambao umeunganishwa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Rita na mifuko ya jamii itakuwa ni rahisi kulihamisha jina la mtumishi mstaafu kwenye listi ya mishahara na kulipeleka 'automatically' kwenye mifuko ya pensheni hivyo kupunguza ulipaji mishahara hewa.
Awali akitoa ushauri wake huo, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuujali utumishi wa umma pamoja na kuwa na keki ndogo.
Pia amempongeza Waziri wa ofisi hiyo, George Simbachawene, Naibu Waziri, Ridhiwani Kikwete pamoja na aliyekuwa waziri wa ofisi hiyo, Jenista Mhagama kwa utendaji wao mzuri.
Mdau, nakuomba uendelee kusikiliza kupitia clip hii ya video, Dkt. Kaijage akitoa pongezi kwa Rais Samia na kuelezea umuhimu wa mifumo hiyo...
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇