TAMKO RASMI LA UWT LA KUMPONGEZA MWENYEKITI WA CCM NA RAIS DKT SAMIA SULUHU HASSAN KWA KUIMARISHA DEMOKRASIA NCHINI
Ndugu wanahabari
Ndugu Viongozi mbalimbali mliopo
Mabibi na Mabwana
Nawasalimu kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Awali ya yote niwapongeze wanahabari wote kwa jitihada zenu za dhati za kuutaarifu Umma kila siku kuhusu maendeleo mbali mbali yanayofanywa na Serikali yetu chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan
Ndugu waandishi wa Habari,
Mimi Mwenyekiti wa UMOJA WA WANAWAKE TANZANIA Nimewaita hapa leo Kwa niaba ya viongozi, watendaji, wanachama wa UWT na wanawake wote wa Tanzania kwa ajili ya kutoa salamu za pongezi zinazotokana na matokeo ya Mkutano baina ya Mwenyekiti wa CCM na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan na Vyama vya Siasa vyenye usajili wa kudumu uliofanyika jana tarehe 3/1/2023 .
UWT inampongesa sana Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kufanya maamuzi yaliyoleta furaha isiyo na kifani kwa wananchi wa TANZANIA NA WAPENDA AMANI DUNIANI kote na kwa kutoa majawabu ya vikwazo vya Demokrasia yetu. Sisi kama UWT tumekoshwa sana na hatua hiyo ya kihistoria ya;
1. Kuondoa zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa.
2. Kukwamua mchakato wa kupata Katiba Mpya.
3. Kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali ili kupanua wigo wa demokrasia hapa nchini . Maamuzi haya ya Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan yameleta faraja hususan kwa vyama mbalimbali vya siasa nchini Tanzania na imewezesha kufikiwa kwa hatua kubwa ya kidemokrasia Nchini kwetu .
Mhe Rais Dkt. Samia ameendelea kuonesha uthabiti wa kauli zake na matendo ambapo hata pale alipohutubia Taifa mara baada ya kuapishwa 19/3/2021 Mhe Rais Samia alisema nanukuu “Huu si wakati wa kutizama mbele kwa mashaka bali kutazama mbele kwa matumaini“ mwisho wa kunukuu na hakika kwa maamuzi aliyofikia Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kupitia mchakato wa maridhiano kuanzia kuundwa kwa Kikosi Kazi na pia mazungumzo kati ya Vyama vya Siasa na Vyama Vya CCM na CHADEMA yameleta matumaini mapya katika kujenga demokrasia ya kuaminiana baina ya Vyama vyote vya Siasa Nchini ambayo ni chachu katika ujenzi wa Taifa lenye umoja , amani na utulivu .
Ndugu waandishi wa Habari,
Ni wazi Falsafa ya Rais wetu Dkt Samia ya Kujenga upya Nchi yenye Umoja katika ujenzi wa Taifa inaongozwa na falsafa yake ya 4R (maridhiano,ustahamilivu,mabadiliko na kujenga upya Nchi yetu). Hadi sasa Falsafa hii imefanikiwa kwa 100% si tu kwa kuleta mafanikio makubwa ya kisekta aliyoyatekeleza Rais Samia kwa muda mfupi wa chini ya miaka miwili madarakani licha ya kuipokea Nchi ikiwa na hali tete kutokana na majanga ya Corona, vita ya Ukraine na kufiwa na Mtangulizi wake mwaka 2021. Bali Falsafa hizi zinahimiza siasa za kistaarabu zenye kuwaweka watu pamoja, kujenga hoja za ushawishi kupitia majadiliano na mazungumzo na kuhusisha Vyama vya Siasa katika uendeshaji wa nchi. UWT tunampongeza sana Rais wetu, hakika Wanawake wanaweza.
Ndugu wanahabari , Umoja wa Wanawake wa Tanzania unaungana na wito Mhe Rais Samia Suluhu Hassan kwa wanasiasa kutumia ruksa ya Mikutano ya hadhara ya vyama vya vizuri kwa kufanya siasa za kistaarabu , siasa za kupevuka na zenye kujenga na kuacha matusi na kashfa.
Ndugu wanahabari
Rais na Mwenyekiti wetu wa Chama cha Mapinduzi Dkt Samia ni Kiongozi msikivu, mkweli na mpenda haki na ndio maana Maamuzi matatu yaliyochukuliwa na Rais Samia jana kwa Vyama vya Siasa, ni mwelekeo Mpya wa Nchi yetu katika kuihami Demokrasia yetu. UWT tunasema hakika Mama Samia ni Neema kutoka kwa Mungu. Nani kama mama!!??
Ndugu Waandishi wa Habari,
Kilio chetu UWT siku zote ni kuona Nchi yetu ikiwa na Utulivu, Amani na yenye haki baina ya wananchi wake na Serikali yao, Rais Samia amechonga palio, wajibu wetu sote wanasiasa na wananchi wote ni kulifuata kwa unyenyekevu hilo palio, tusimkatishe tamaa. Si vijana, Akina mama wala wazee, sote tuwe wamoja tujenge Nchi yetu.
UWT inawasihi Viongozi Wanawake ndani ya Vyama vya Siasa kuonyesha mfano katika hili kwa kutanguliza ustaarabu, kuheshimiana, utu wakati wote wa Mikutano hiyo ya hadhara na kamwe pasitokee Viongozi wa Vyama Vya Siasa kubeza na kutweza utu wa mwanamke au wa mtu mwingine katika Mikutano hiyo ya Vyama vya Siasa .
Ndugu wanahabari UWT inawahimiza viongozi wanawake wa vyama mbalimbali kuandaa mikutano mingi ya hadhara ili kuweza kupokea changamoto mbalimbali zinazowagusa Wanawake kwa kuwa Wanawake wa Tanzania wanakabiliwa na changamoto zinazofanana bila kujali itikadi zao na pia katika Mikutano hiyo tupendekeze hatua mahususi za kuchukua kwa Serikali ili kumkomboa Mwanamke Kiuchumi , Kijamii na Kisiasa.
Ndugu wana habari kama UWT tumefurahishwa na uamuzi wa Serikali hii ya Awamu ya Sita ya kuridhia mapendekezo ya Kikosi kazi ya kufanya marekebisho ya sheria kadhaa ndani ya nchi kwa nia ya kuimarisha Demokrasia zaidi ambayo yatahusisha wananchi . Tunaimani marekebisho hayo pia yatazingatia masuala ya Usawa wa Kijinsia katika kuongeza uwakilishi wa wanawake kwenye Siasa na Uongozi kuanzia kwenye Vyama vya Siasa kama ambavyo tunashuhudia namna Rais wetu Dk Samia Suluhu Hassan anavyojitahidi kuongeza ushiriki wa wanawake kwenye uongozi ndani ya Serikali yake na Chama anachoongoza cha CCM .
Ndugu wanahabari, Kwa niaba ya wanawake wa Tanzania tunaunga mkono uamuzi wa Kukwamua mchakato wa marekebisho ya Katiba ya Tanzania na hivyo tunahimiza amani na utulivu wakati wote wa kusubiri Serikali kukamilisha taratibu zote za kuanza mchakato huu kama alivyoeleza Mhe Rais Samia Suluhu Hassan katika hotuba yake jana.
Ndugu wanahabari, UWT inahimiza viongozi wake wa Jumuiya kuanzia ngazi za Tawi ,Kata/Wadi ,Jimbo, wilaya , Mkoa mpaka Taifa pamoja na Madiwani,wawakilishi na Wabunge Wanawake kufanya mikutano ya hadhara kwa kufuata taratibu zote ,mikutano hiyo ilenge kuelezea utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025 , kusikiliza kero za wananchi na kujibu hoja mbalimbali zitakazopotoshwa kwa lugha ya kistaarabu na kwa kutumia takwimu sahihi , sisi Viongozi wa UWT Taifa tutaonyesha mfano kwa kutumia fursa hii iliyotolewa na Mhe Dk Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania .
Mwisho lakini sio kwa umuhimu UWT tunaendelea kuwaomba Watanzania kuendelea kumuamini Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kumuunga mkono kwani ana dhamira njema ya kujenga Taifa linaloongea lugha moja , na ambalo kila mmoja anashiriki katika ujenzi wa Taifa lake .
Kwa kuhitimisha niendelee kuwatakia kheri ya Mwaka Mpya wa 2023,Na ukawe ni Mwaka wa Neema na wenye mafanikio kwa kila Mtanzania.
Ahsanteni kwa kunisikiliza.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇