Apr 3, 2025

HIKI NI KIKAO CHA MAFUNDO, MAZINGATIVU, MSIGWA AWAAMBIA MAAFISA HABARI

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, amewataka Maafisa Habari wa Serikali kutambua kwamba, ujio wao Zanzibar katika Kikao Kazi ni kwa ajili ya kufundwa na kuzingatia yote yatakayoelekezwa na kukumbushwa juu ya utekelezaji wa majukumu yao.


Bw. Msigwa ametanabahisha hayo wakati wa ufunguzi wa Kikao Kazi cha 20 cha Maafisa Habari wa Serikali kinachofanyika katika Hoteli ya New Amaan Zanzibar, leo Aprili 3, 2025.

"Hiki ni kikao cha mafundo na mazingativu, tunafundana na kuzingatia mafundo kwa Maafisa Habari, Mawasiliano, Uhusiano na Itifaki wa Serikali" amesisitiza Bw. Msigwa

Aidha, ametaja malengo ya Kikao Kazi hicho kwa Maafisa Habari wa Serikali kuwa ni kuimarisha mawasiliano ya Serikali kwa umma kupitia programu za kujenga uwezo kwa watumishi pia kuimarisha Muungano na kubadilishana uzoefu.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Mhe. Tabia Maulid Mwita, ameshukuru kukubaliwa ombi lake la Kikao Kazi hicho kufanyika Zanzibar na kutaja sababu kuu ya kufanya hivyo ikiwemo Maafisa Habari kujionea shughuli mbalimbali za utalii, michezo na maendeleo makubwa ndani ya Zanzibar. 

"Lengo kubwa la kuomba Kikao Kazi hiki kufanyika Zanzibar ni kuendelea kuimarisha Muungano wetu, pili ni kuwawezesha Maafisa Habari kuja kuiona Zanzibar ya sasa ya Dkt. Hussein Ali Mwinyi, hivyo watapata kibali cha kuisemea Zanzibar kule Tanzania Bara na duniani kote" - Mhe. Tabia

Vile vile ameahidi kwamba, Wizara yake ya Habari Tanzania Zanzibar itaendelea kushirikiana na Wizara ya Habari Tanzania Bara katika nyanja zote zinazohusu sekta ya Habari nchini.

Wakati mafundo hayo yakiendelea, kikao hicho kimetoa fursa ya upimaji wa afya bure kwa wadau wote wa habari wanaoshiriki kikao hicho na wananchi watakaofika katika viwanja vya Hoteli ya New Amaan ambapo madaktari bingwa kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili, MOI, JKCI na Lumumba wanaendelea kutoa huduma za afya za kibingwa kuanzia leo Aprili 3, 2025 hadi ukomo wa kikao hicho Aprili 6, 2025.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa akizungumza katika mkutano huo;








 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Pages