LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Aug 23, 2022

KANISA HALISI KUUNGURUMISHA IBADA YA KILELE CHA SHEREHE YA KUMTOLEA CHANZO HALISI MATUNDA YA SHAMBA LAKE, JUMAPILI, AGOSTI 28, 2022 (LANGO LA 12 ABU, 1)

Tegeta, Namanga Dar es Salaam
Kanisa Halisi la Mungu Baba lenye Makao yake Makuu Tegeta Namanga, Jijini Dar es Salaam, Jumapili ya Agosti 28, 2022 (Lango la 12 Abu, 1) litafanya Ibada kubwa na ya kipekee katika kilele cha Sherehe ya kumtolea Chanzo Halisi Matunda (sadaka) ya Shamba lake.

Taarifa iliyotolewa na Kanisa hilo, imesema, ibada ya kilele cha Sherehe hiyo inayotarajiwa kuhudhuriwa na Makuhani na Mamia ya Uzao (Waumini) wa Kanisa hilo, itaongozwa na Kiongozi Mkuu wa Kanisa Halisi la Mungu Baba ambaye ni Baba Halisi na itaanza mapema saa moja asubuhi na kuendelea hadi saa 6 mchana.

Katika mwaliko, Kanisa Halisi la Mungu Baba limesema, watu wote wa nyumba mbalimbali za Ibada wanakaribishwa kuhudhuria Ibada ya kilele cha sherehe hiyo kwa kuwa Kanisa hilo ni la Mungu Baba hivyo halibagui yeyote.

"Shiriki kwenye sherehe ya kumletea Chanzo Halisi matunda ya shamba lake, itakayofanyika lango la 12 Abu, 1 (Majira Halisi) au 28 Agosti, 2022.

Sherehe hii ilianza 3 Abu, 1 (Majira Halisi) au 19 Agosti, 2022 na kilele chake ni hilo lango la 12 Abu, 1 (Majira Halisi), yaani 28 Agosti, 2022 katika Ukumbi wa Kao kuu la Kanisa Halisi la Mungu Baba, kuanzia saa Moja asubuhi hadi saa Sita mchana. 

Ukishiriki sherehe hii ya Kumletea Chanzo Halisi Matunda, utapona kila eneo", imesema Taarifa hiyo.

Tafadhali soma mwaliko wenyewe kama ulivyotumwa kwetu. SOMA HAPO👇

KADI YA MWALIKO KWA JAMII  KWENYE SHEREHE YA KUMLETEA CHANZO HALISI MATUNDA YA SHAMBA LAKE (MATHAYO 21:43)


12 Abu, 1(Majira Halisi), yaani 28 Agosti, 2022. Katika Ayubu 41:11, imeandikwa kuwa “ni nani aliyetangulia kunipa ili nimlipe?” jibu ni kwamba hakuna aliyetangulia kumpa MUNGU BABA ambaye ndiye CHANZO HALISI chochote, maana yeye ndiye aliyeumba vyote. Yeye alitangulia kutupa pumzi, Uhai, Maisha, vyakula, vinywaji, mavazi, ulinzi na kila kitu kizuri tunachohitaji (Mwanzo 1:29-31).

Anaposema katika Kumbukumbu 12:5-7, kuwa tupeleke matunda yetu (sadaka), mahali alipopachagua haina maana kuwa anahitaji chochote kutoka kwetu; bali ni kama mama anayenyonyesha mtoto kumuomba mwanaye ampe ziwa lake yeye mwenye ili ajue mtoto wake ana ukarimu kiasi gani ndani yake. Hivyo, tunawajibika kumletea matunda CHANZO HALISI ili aone yale aliyotutendea tumeyapokea kwa kiasi gani!

Najua kila mmoja ana nyumba yake ya Ibada. Ila ninachosema hapa kinahusu Efeso 4:6, ambayo inakiri kuwa MUNGU BABA Aliyeumba vyote ni mmoja na vyote ni vyake, yuko juu ya wote na ndani ya wote na yote. Si hivyo tu, ninasisitiza kuwa Sauti yake ambayo ina mfululizo wa kupokelewa na: Moyo wa Mwanzo (Mwa.1:1); Kerubi (Eze.28:15); Adamu (Mwa.2:15); Musa (Kut.3:10); Eliya Mtishbi (I Fal.17:1); Yesu (Matendo 10:38); Adamu wa Pili (I Kor.15:44-49); Miaka 1000 (Isa.33:6); na Nafsi ya Kwanza (I Yoh.:8); sasa iko Tanzania, kwa mujibu wa Mathayo 21:43 (kama nitakavyothibitisha hapo mbele).

Katika majira zote zilizopita, MUNGU BABA ambaye ndiye CHANZO HALISI, hakuletewa Matunda ya shamba lake. Sasa amekuja kuyachukua mwenyewe kama alivyoahidi katika Mika 1:2-6 kuwa atakuja juu ya nchi kuyeyusha milima na vilima kama nta inayokutana na moto. Vilima na milima ni matatizo na shida ambazo sisi wenyewe tulikuwa hatuwezi kuviondoa kama vile ugonjwa wa korona uliokuwa umefuta utalii na biashara zingine. Baada ya CHANZO HALISI kutuponya korona bila kubagua yeyote, biashara ya utalii imerejea tena kwa kasi kubwa mno.

Ni wajibu wetu kumshukuru kwa kumfanyia sherehe ya kumletea matunda ya shamba lake.
Shamba lake ni kila kazi na biashara ya halali na haki tunayofanya. Tumletee hayo matunda ambayo nitafafanua hapo mbele kidogo.

Watalii huwa hawaishii kwenda kwenye mbuga za wanyama na kustarehe mahotelini peke yake; huwa pia wananunua madini na vitu vingine kama vile batiki na kadhalika.

Sote tumletee CHANZO HALISI matunda ya shamba lake. Kubwa kuliko ni Amani ambayo tunaisoma katika Isaya 2:4. Tumesoma huo mstari kwa muda mrefu katika nyumba za Ibada na majumbani kwetu, ila hatukujua ni wapi na ni wakati gani mstari huo utatimia. Kwa wale wanaofuatilia masuala ya kimataifa, baada ya Sauti ya MUNGU BABA, ambaye ndiye CHANZO HALISI kusikika Kigoma Tanzania kwa mfululizo wa: Mwaka 2003 (Sauti ya Majira ya sita); Mwaka 2015 (Sauti ya Majira ya saba); Mwaka 2019 (Sauti mpya ambayo ni zaidi ya zile sauti saba); na Mwaka 2020 (Sauti ya moyo), Amani imetamalaki katika mataifa yote. Hivyo, jamii yote ya kimataifa tumletee CHANZO HALISI Matunda ya shamba lake, maana amani tumepata sote.

Kumletea CHANZO HALISI matunda ya shamba lake ni jambo la thamani kubwa:
(1) Ukimletea fungu la kumi la mtaji wako na baadaye fungu la kumi la faida ya biashara yako (Lawi 27:30), hutafilisika maisha yako yote. Ina maana biashara hiyo inamilikiwa na CHANZO HALISI mwenyewe. Kwa kuwa CHANZO HALISI utakayemletea matunda alikuwepo kabla ya chochote (Kolosai 1:16-17a), alaye biashara yako hatapata tena nafasi;

(2) Ukimletea Shukrani kwa sababu ya makubwa uliyotendewa: utapata maongezeko maisha yako yote (Yoh.6:11-13); milango ya biashara yako itakuwa wazi maisha yote (Zaburi 100:4); na vitu vizuri vilivyokuwa vimekufa, vitafufuka;

(3) Ukimletea malimbuko ya biashara au mifugo yako au shamba lako, CHANZO HALISI atajua umemheshimu naye ataheshimisha maisha yako (Mithali 3:9). Basi kwa kuwa kila kinachofungua tumbo ni mali yake, mletee hayo malimbuko ya mali zako;

(4) Ukimletea matunda ya kubariki Chanzo cha Sauti, utafanikiwa katika kila kitu unachofanya katika maisha yako (II Nyakati 20:20);

(5) Ukimletea CHANZO HALISI matunda ya jamii, bidhaa zako zitapata kibali au soko kila mahali utakapoziuza (Isaya 58:7-11); na (6) Ukimletea matunda ya kujenga moyo mmoja, basi hutalia kama Esau alivyolia baada ya kukosa baraka alipokuta Yakobo ameshabarikiwa (Mwa.27:27-39).

Shiriki kwenye sherehe ya kumletea CHANZO HALISI matunda ya shamba lake, itakayofanyika lango la 12 Abu, 1 (Majira Halisi) au 28 Agosti, 2022. Sherehe hiyo ilianza 3 Abu, 1 (Majira Halisi) au 19 Agosti, 2022. Kilele chake ni hilo lango la 12 Abu, 1 (Majira Halisi), yaani 28 Agosti, 2022 katika ukumbi wa Kao kuu la KANISA HALISI LA MUNGU BABA kuanzia saa Moja asubuhi hadi saa Sita mchana. Ukishiriki sherehe hii ya Kumletea CHANZO HALISI matunda, utapona kila eneo.

 ©August 2022 CCM Blog/Bashir Nkoromo

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages