1.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kwamba, Bunge lako Tukufu likae kama
Kamati ya Mipango ili kupokea na kujadili mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi
ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka
2021/22.
2.
Mheshimiwa Spika, napenda kumshukuru Mwenyezi
Mungu kwa kuendelea kutujalia uhai na afya njema na kutuwezesha leo hii
kukutana ili kupokea na kujadili Mapendekezo ya Mwongozo
wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa
kwa Mwaka 2021/22.
3.
Mheshimiwa Spika, naomba kuchukua fursa hii kutoa pole kwa ndugu, jamaa na
marafiki na kwako wewe Mheshimiwa Spika na Waheshimiwa Wabunge wote kwa kifo
cha Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum (CCM).
Tunamwomba Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake kwa amani.
4.
Mheshimiwa
Spika, kipekee kabisa napenda kumpongeza Mheshimiwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Joseph Magufuli kwa
kuchaguliwa tena kwa ushindi wa kishindo kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania. Aidha, ninampongeza Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa
kuchaguliwa tena kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Vile
vile, napenda kumpongeza Waziri Mkuu Mheshimiwa
Kassim Majaliwa Majaliwa na Waheshimiwa Mawaziri wote kwa kuteuliwa
kushika nafasi hizo muhimu katika uongozi wa nchi yetu. Uongozi wao madhubuti
unaozingatia maslahi mapana kwa Taifa ulikiwezesha Chama Cha Mapinduzi kupata
ushindi katika majimbo 256 kati ya majimbo 264 yaliyopo.
5.
Mheshimiwa Spika, napenda pia kutoa shukrani za dhati kwa Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango, Mheshimiwa Mwanaidi
Ali Khamisi (Mb), na watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango
wakiongozwa na Katibu Mkuu, Bw. Doto Mgosha James kwa ushirikiano walionipa
katika maandalizi ya hotuba hii na vitabu vya Mapendekezo ya Mpango na Mwongozo.
Aidha, ninawashukuru sana Wizara, Taasisi, Idara za Serikali, Sekta Binafsi na
wadau mbalimbali waliotoa maoni na michango yao katika kukamilisha Mapendekezo
ya Mpango na Mwongozo.
6.
Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kuishukuru Kamati ya Kudumu ya
Bajeti chini ya Mwenyekiti Mheshimiwa Sillo Daniel Baran, Mbunge wa Babati
Vijijini (CCM) na Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa
Omari Mohamed Kigua, Mbunge wa Kilindi (CCM) kwa maoni yao wakati wa
majadiliano ya vikao vya kamati. Maoni hayo yamezingatiwa katika kuboresha
Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya
Mpango na Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2021/22.
Aidha, napenda kuhakikishia kuwa maoni yatakayotolewa na Bunge lako Tukufu,
yatazingatiwa katika kuboresha Mwongozo na Mpango huu. Hivyo, ninawasihi
Waheshimiwa Wabunge katika nafasi yenu ya uwakilishi wa wananchi, mtumie weledi
na uzoefu wenu katika kutoa maoni, ushauri kuhusu maeneo muhimu na miradi
inayopendekezwa.
7.
Mheshimiwa Spika, Mapendekezo ya Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti
ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka 2021/22 yamezingatia:
Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango Elekezi wa Maendeleo wa Muda Mrefu
2011/12 – 2025/26; Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika kipindi cha mwaka 2020
hadi 2025; Hotuba za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt.
John Pombe Joseph Magufuli wakati akizindua Bunge la 11 na 12 la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Novemba, 2015 na 2020 mtawalia; Sera na Mikakati
mbalimbali ya Kisekta.
8.
Mheshimiwa Spika, Kitabu cha Mapendekezo ya Mpango kimegawanyika katika
sura saba (7): Sura ya kwanza ni utangulizi; Sura ya pili inaainisha mapitio ya
hali ya uchumi; Sura ya tatu inaelezea mapitio ya utekelezaji wa Mpango wa
mwaka 2019/20 na nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21; Sura ya nne inaelezea maeneo
ya kipaumbele kwa mwaka 2021/22; Sura ya tano inaelezea ugharamiaji wa Mpango; Sura
ya sita inaainisha mfumo na utaratibu wa ufuatiliaji, tathmini na utoaji
taarifa za utekelezaji wa Mpango; na Sura ya saba ni viashiria hatarishi vya
utekelezaji wa Mpango na hatua za kukabiliana navyo.
2.0
MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI
2.1 Mwenendo
wa Viashiria vya Uchumi
9.
Mheshimiwa Spika, uchumi wa Taifa umeendelea kuwa imara ambapo katika
kipindi cha miaka minne (2016 – 2019), Pato halisi la Taifa lilikua kwa wastani
wa asilimia 6.9. Ukuaji huu umeiwezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kipato
cha kati wa chini (lower-middle income) kutoka kundi la nchi masikini kwa
kufikisha wastani wa pato la mtu mmoja mmoja la shilingi 2,577,967 (sawa na
dola za Marekani 1,080) mwaka 2019, ambalo ni zaidi ya kigezo cha dola za
Marekani 1,036 cha kuingia katika kundi hilo. Pato la Taifa lilikua kwa asilimia 7.0 mwaka 2019.
10.
Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha Julai hadi Septemba 2020,
Pato Halisi la Taifa lilikua kwa asilimia 4.5 ikilinganishwa na ukuaji wa
asilimia 8.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Aidha, Katika kipindi cha Januari hadi Septemba 2020, Pato la Taifa
lilikua kwa asilimia 4.7 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 7.3 katika
kipindi kama hicho mwaka 2019. Kupungua kwa kasi ya ukuaji katika kipindi
husika kumechangiwa na mvua zilizozidi wastani zilizosababisha mafuriko ambayo
yaliharibu miundombinu ya usafirishaji nchini na kuchelewesha utekelezaji wa
baadhi ya miradi pamoja na athari za mlipuko wa ugonjwa wa homa kali ya mapafu
ulioenea katika nchi nyingi ambazo ni washirika wetu wakubwa wa biashara.
Aidha, athari kubwa za kiuchumi zilizojitokeza zaidi katika robo ya pili ya
mwaka 2020 (Aprili hadi Juni) ambapo shughuli za kiuchumi za hoteli, biashara
na elimu zilikuwa na ukuaji hasi kufuatia hatua zilizochukuliwa kwa muda na
Serikali za kusitisha baadhi ya shughuli za kiuchumi hasa mikusanyiko ikiwemo
kufungwa kwa safari za anga pamoja na kusitishwa kwa shughuli zote za sanaa na
burudani ikiwemo michezo. Kwa kipindi cha miezi tisa ya mwanzo wa mwaka 2020
(Januari hadi Septemba), sekta zilizokua kwa viwango vikubwa ni pamoja na Sekta
ya Ujenzi (asilimia 13.6); Madini na Mawe (asilimia 9.9); Habari na Mawasiliano
(asilimia 9.0); Uchukuzi na Uhifadhi wa Mizigo (asilimia 8.9); na Shughuli za
kitaalamu,Sayansi na Ufundi (asilimia 8.8). Hata hivyo, Tanzania ni miongoni
mwa nchi chache zinazotarajia kuwa na ukuaji chanya mwaka 2020 kutokana na hatua za Serikali za kutowafungia watu ndani
(lock down) na kuwaruhusu waendelee na shughuli za kiuchumi na kijamii wakati
wa mlipuko wa homa kali ya mapafu.
11.
Mheshimiwa Spika, mfumuko wa bei ulikuwa wastani wa asilimia 3.3 katika
kipindi cha mwaka unaoishia Desemba 2020 ikilinganishwa na asilimia 3.4 katika
kipindi kama hicho mwaka 2019. Kuimarika kwa mfumuko wa bei kulitokana na
upatikanaji wa mazao ya chakula cha kutosha katika masoko ya ndani na nchi
jirani.
12.
Mheshimiwa Spika, urari
wa malipo nje ya nchi umeendelea kuimarika, licha ya kuwepo kwa changamoto za
kudorora kwa shughuli za kiuchumi duniani kutokana na athari za COVID-19. Katika kipindi cha Julai hadi Desemba 2020, nakisi ya urari wa biashara ya
bidhaa, huduma na uhamisho mali nchi za nje (current account deficit) uliimarika
kufikia nakisi ya dola za Marekani milioni 331.3, ikilinganishwa na nakisi ya
dola za Marekani milioni 344.3 kwa kipindi kama hicho mwaka 2019/20. Akiba ya fedha za kigeni
imeendelea kuwa ya kutosha kuweza kukidhi mahitaji kwa ajili ya uagizaji wa
bidhaa na huduma. Hadi Desemba 2020, kulikuwa na akiba ya fedha za kigeni ya
dola za Marekani milioni 4,767.7, ambayo inatosheleza kuagiza bidhaa na huduma
nje ya nchi kwa kipindi cha takriban miezi
5.6. Kiwango hiki ni zaidi ya lengo la nchi la kukidhi miezi 4.0 na
zaidi ya lengo la miezi 4.5 kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
13.
Mheshimiwa Spika, Sekta
ya benki imeendelea kuimarika ikiwa na mtaji na ukwasi wa kutosha kukidhi
mahitaji ya kila siku ya wenye amana na wakopaji. Kwa mwezi Desemba 2020, kumekuwa na ongezeko la mapato na faida
kutokana na uwekezaji katika rasilimali na mtaji ikilinganishwa na kipindi kama
hicho mwaka 2019. Katika kipindi cha Julai hadi Desemba
2020, faida ya benki
itokanayo na mali (Returns on Asset - ROA) ilifikia wastani wa asilimia 2.03
ikilinganishwa na asilimia 1.82 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Faida ya
benki itokanayo na mtaji (Returns on Equity - ROE) ilifikia wastani wa asilimia
7.92 Desemba, 2020 kutoka asilimia 6.80 katika kipindi kama hicho mwaka 2019. Mikopo kwa sekta binafsi ilikua kwa wastani wa asilimia
8.1 kwa mwaka 2019/20 ikilinganishwa na ukuaji wa wastani wa asilimia 6.8 mwaka
2018/19, ikiashiria kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi zikichagizwa na
uwekezaji wa sekta ya umma.
14. Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2019/20 thamani ya Shilingi ya Tanzania dhidi ya fedha za kigeni
imeendelea kuwa tulivu. Kwa mwaka 2019/20, dola moja ya Marekani ilibadilishwa
kwa wastani wa shilingi 2,289.1 ikilinganishwa na shilingi 2,282.3 mwaka
2018/19. Hii inamaanisha kuwa thamani ya shilingi ilipungua kwa kasi ndogo ya
wastani wa asilimia 0.30 mwaka 2019/20 ikilinganishwa na asilimia 1.73 kwa
mwaka 2018/19. Aidha, katika kipindi cha nusu ya kwanza
ya mwaka 2020/21 dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa shilingi
2,309.83 ikilinganishwa na shilingi 2,299.97 kipindi kama hicho mwaka 2019/20. Hali
hii inatokana na usimamizi thabiti wa Sera za Fedha na Bajeti.
15. Mheshimiwa
Spika, hadi Desemba
2020, deni la Serikali lilikuwa shilingi trilioni 59.01,
sawa na ongezeko la asilimia 7.6 ikilinganishwa na shilingi trilioni 54.85
kipindi kama hicho mwaka 2019. Kati ya kiasi hicho, deni la nje ni shilingi trilioni
42.83 na deni la ndani ni shilingi trilioni 16.18. Ongezeko la deni limetokana
na: ukopaji kwa ajili ya kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo
ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme na maji; na
malimbikizo ya riba ya deni la nje hususan nchi zisizo wanachama wa kundi la Paris Club ambazo Serikali inaendelea
kujadiliana nazo. Tathmini ya uhimilivu wa deni iliyofanyika Novemba, 2020 imeonesha
kuwa deni la Serikali ni himilivu katika kipindi cha muda mfupi, wa kati na
mrefu kwa kuzingatia ukomo unaokubalika kimataifa kwa viashiria vyote muhimu.
Kwa mwaka 2020/21 thamani ya sasa ya deni la Serikali kwa Pato la Taifa ni
asilimia 27.9 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 70; thamani ya sasa ya deni
la nje kwa Pato la Taifa ni asilimia 17.3 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia
55; na thamani ya sasa ya deni la nje
kwa mauzo ya nje ni asilimia 113.2 ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 240.
Aidha, ulipaji wa deni la nje kwa mauzo ya bidhaa nje ni asilimia 13.7
ikilinganishwa na ukomo wa asilimia 23.
16.
Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu mwenendo wa viashiria vya
uchumi yanapatikana katika Sura ya Pili
ya Kitabu cha Mapendekezo ya Mpango na Sehemu
ya Kwanza, Sura ya Pili ya kitabu cha Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na
Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2021/22.
2.2 Utekelezaji
wa Bajeti ya Mwaka 2019/20
17.
Mheshimiwa Spika, katika mwaka
2019/20, mapato ya ndani yalifikia shilingi trilioni 20.29, sawa na asilimia
88.0 ya lengo. Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 17.62 mapato ya kodi yaliyokusanywa
na Mamlaka ya Mapato Tanzania, sawa na
asilimia 92.3 ya lengo. Aidha, shilingi trilioni 1.95 ni mapato yasiyo ya kodi,
sawa na asilimia 85.9 ya lengo na
shilingi bilioni 717.2 ni mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, sawa na
asilimia 93.7 ya lengo.
18.
Mheshimiwa Spika, katika kipindi hicho, fedha za misaada na mikopo nafuu
zilizopokelewa zilikuwa shilingi trilioni 3.52 sawa na asilimia 126.3 ya lengo.
Kuvuka
lengo kwa misaada na mikopo nafuu kulitokana na Washirika wa maendeleo kuongeza
viwango vya misaada waliyoahidi awali kutokana na mahusiano mazuri kati ya nchi
yetu na Washirika hao wa maendeleo. Mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara
iliyopatikana ni shilingi trilioni 1.82 sawa na asilimia 78.7 ya lengo. Kutofikiwa kwa lengo kumetokana na masharti magumu
katika soko la mitaji la kimataifa. Mikopo iliyopatikana kutoka soko la ndani ni shilingi trilioni
4.96 sawa na asilimia 100 ya lengo.
19.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2019/20, mapato yaliyokusanywa kutoka vyanzo vyote
vya ndani na nje ni shilingi trilioni 30.59, sawa na asilimia 92.4 ya lengo la
mwaka la shilingi trilioni 33.11. Aidha, Serikali ilitoa ridhaa ya matumizi ya
shilingi trilioni 28.57, sawa na asilimia 86.3 ya lengo. Kati ya kiasi hicho,
shilingi trilioni 20.21 ni za matumizi ya kawaida sawa na asilimia 96.9 ya
lengo. Matumizi ya kawaida yanajumuisha shilingi trilioni 8.11 zilizotumika
kulipa madeni ya fedha zilizokopwa kugharamia utekelezaji wa miradi mbalimbali
ya maendeleo, shilingi trilioni 7.30 kwa ajili ya mishahara ya watumishi na
shilingi trilioni 4.80 kwa ajili ya matumizi mengineyo. Aidha, shilingi trilioni
8.37 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo kwa fedha zilizopitia Mfuko Mkuu wa
Serikali sawa na asilimia 68.3 ya bajeti ya maendeleo. Vile vile, jumla ya
shilingi trilioni 1.46 ni fedha za
Washirika wa Maendeleo zilizopelekwa moja kwa moja kwenye utekelezaji wa miradi
na hivyo kufanya utekelezaji wa bajeti ya maendeleo kufikia asilimia 80.2.
2.3 Utekelezaji
wa Bajeti kwa Kipindi cha Nusu ya Kwanza ya Mwaka 2020/21
20. Mheshimiwa Spika, katika
kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21, mapato yaliyokusanywa kutoka
vyanzo vyote vya ndani na nje ni shilingi trilioni 13.84 sawa na asilimia 87.3
ya lengo. Kati ya mapato hayo, mapato ya ndani yalifikia shilingi trilioni 10.45,
sawa na asilimia 88.9 ya lengo. Kati ya mapato ya ndani: shilingi trilioni 9.05
zilikusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania, sawa na asilimia 89.5 ya lengo;
shilingi trilioni 1.03 ni mapato yasiyo ya kodi, sawa na asilimia 84.0 ya lengo; na shilingi bilioni
376.5 ni mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa, sawa na asilimia 89.0 ya lengo.
Serikali itaendelea kuchukua hatua
mbalimbali za kuhakikisha kuwa malengo ya mapato ya ndani yanafikiwa ikiwemo:
Kuendelea kuimarisha mifumo ya kielektroniki ya kukusanyia mapato, kuhimiza
matumizi sahihi ya mashine za kielektroniki za kutolea stakabadhi (EFD),
kusimamia ukusanyaji kwa mfumo wa vitalu (Block management) na kuimarisha elimu
na huduma ya walipakodi.
21.
Mheshimiwa
Spika, Misaada na mikopo nafuu ilifikia shilingi bilioni 971.2,
sawa na asilimia 63.1 ya lengo na mikopo kutoka masoko ya ndani shilingi trilioni
2.41, sawa na asilimia 94.6 ya lengo. Mapato yanayokusanywa na Mamlaka ya
Mapato Tanzania yalifikia kiwango cha juu ambacho hakijawahi kutokea cha
shilingi trilioni 2.09 Desemba 2020.
22.
Mheshimiwa
Spika, ridhaa ya matumizi iliyotolewa katika kipindi
kilichoishia Desemba, 2020/21 ilikuwa shilingi trilioni 13.12, sawa na asilimia
82.8 ya lengo. Kati ya kiasi kilichotolewa, shilingi trilioni 10.52 ni fedha za
matumizi ya kawaida, sawa na asilimia 95.2 ya lengo na shilingi trilioni 2.60
ni fedha za maendeleo, sawa na asilimia 54.2 ya lengo. Fedha za matumizi ya
kawaida zilizotolewa zinajumuisha: shilingi trilioni 3.79 kwa ajili ya
mishahara, sawa na asilimia 97.7 ya lengo; shilingi trilioni 4.02 kwa ajili ya
kugharamia deni la Serikali kwa fedha ambazo zilitumika kugharamia miradi ya
maendeleo, sawa na asilimia 92.9 ya lengo; na shilingi trilioni 2.71 kwa ajili
matumizi mengineyo (ikijumuisha shilingi bilioni 177.8 zitokanazo na vyanzo vya
ndani vya mapato ya Mamlaka za Serikali za Mitaa), sawa na asilimia 95.3 ya
lengo. Aidha, fedha za maendeleo zilizotolewa zinajumuisha shilingi trilioni 2.51
fedha za ndani na shilingi bilioni 86.2 fedha za nje. Vile vile, kiasi cha
shilingi bilioni 734.1 ni fedha za
Washirika wa Maendeleo zilizopelekwa moja kwa moja kwenye utekelezaji wa miradi
na hivyo kufanya utekelezaji wa bajeti ya maendeleo kufikia asilimia 69.5.
23.
Mheshimiwa Spika, Maelezo ya kina kuhusu Utekelezaji wa Bajeti ya Mwaka
2019/20 yanapatikana katika Sehemu ya
Kwanza, Sura ya Pili ya kitabu cha Mwongozo.
2.4 Utekelezaji
wa Baadhi ya Miradi ya Maendeleo kwa Mwaka 2019/20 na Nusu ya Kwanza ya Mwaka
2020/21
24.
Mheshimiwa Spika, hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi ya
maendeleo mwaka 2019/20 na nusu ya kwanza ya
mwaka 2020/21 ni
pamoja na:
(i)
Reli: Serikali inaendelea na ujenzi wa reli ya kati ya kiwango cha Kimataifa (Standard
Gauge Railway- SGR) ambapo ujenzi wa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (km
300) umefikia asilimia 90 na kipande cha Morogoro – Makutupora (km 422)
umefikia asilimia 49.2, kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa kipande cha Mwanza -
Isaka (km 341) wenye thamani ya shilingi trilioni 3.07; na kuendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa vipande vya
Makutupora – Tabora (km 294) na Tabora – Isaka (km 133). Katika mwaka 2019/20
shilingi bilioni 901.8 zimetumika na shilingi bilioni 351.0 zimetumika katika
nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21. Aidha, ukarabati wa miundombinu ya reli ya kati kutoka Dar es Salaam -
Isaka (km 970) sehemu ya Dar es Salaam - Kilosa (km 283) umefikia asilimia 94.0
na Kilosa – Isaka (km 687) asilimia 99.8;
kukarabati na kurejesha huduma za reli ya Tanga hadi Arusha (km 439); na
kununuliwa kwa vichwa vipya 11 vya treni na kukarabatiwa kwa mabehewa 347 ya
mizigo na mabehewa 20 ya abiria;
(ii)
Uboreshaji
wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL): Kununuliwa kwa ndege mbili (2)
aina ya Boeing 787-8 Dreamliner na Bombardier Dash 8 Q400 ambazo zimeanza
kufanya kazi; na malipo ya awali ya ununuzi wa ndege mpya tatu (3) yamekamilika
kwa asilimia 90 ambapo ndege mbili (2) ni aina ya Airbus A220-300 na moja (1)
ni aina ya De Havilland Dash 8-400. Ununuzi huo umeifanya ATCL kuwa na jumla ya ndege 12. Katika
mwaka 2019/20 shilingi bilioni 315.2 zimetumika na shilingi bilioni 2.5
zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21;
(iii)
Viwanja
vya Ndege na Rada: Kuendelea na ujenzi wa viwanja vya ndege vya Geita
(ambao utekelezaji umefikia asilimia 86), Songea (asilimia 91) na Mtwara (asilimia
49.0); kukamilika kwa maandalizi ya mradi wa ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha
Kimataifa cha Msalato ambao utagharimu dola za Marekani milioni 330, sawa na
shilingi bilioni 759; uzinduzi wa ujenzi na upanuzi wa viwanja vya ndege vya
Shinyanga, Kigoma, Tabora na Sumbawanga vinavyogharimu Euro milioni 50 sawa na
shilingi bilioni 136.85; kuanza kwa ujenzi na upanuzi wa uwanja wa Musoma; kukamilika kwa ukarabati wa karakana
ya matengenezo ya ndege; kupanuliwa kwa barabara ya kuruka na kutua ndege
katika kiwanja cha ndege cha Dodoma; kufungwa kwa mifumo ya kuongoza ndege
(AGL) katika viwanja vya ndege vya Dodoma, Tabora na Mwanza; na kupanuliwa na
kukarabatiwa kwa viwanja vya ndege vya Bukoba, Mwanza, Arusha, Nachingwea na
Iringa. Katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni 56.1 zimetumika na shilingi
bilioni 4.5 zimetumika katika nusu ya
kwanza ya mwaka 2020/21.
Kununuliwa kwa rada nne (4) za
kuongoza ndege za kiraia na kufungwa katika viwanja vya ndege vya Julius
Nyerere, Kilimanjaro, Songwe na Mwanza na hivyo kuongeza kiwango cha usalama wa
abiria katika viwanja vya ndani. Katika mwaka 2019/20 na nusu ya kwanza ya
mwaka 2020/21 jumla ya shilingi bilioni 12.5 zimetumika;
(iv)
Mradi wa Kufua Umeme wa Maji - Julius Nyerere MW 2,115: Kuendelea na
ujenzi wa Mradi wa Kufua Umeme wa Maji – Julius Nyerere ambapo utekelezaji
umefikia asilimia 25.8. Utekelezaji wa mradi huu ulitumia shilingi
bilioni 693.2 katika mwaka 2019/20 na shilingi bilioni 128.9 zimetumika katika nusu
ya kwanza ya mwaka 2020/21;
(v)
Miradi
Mingine ya Umeme: hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa miradi mingine ya
umeme ni: Kukamilika kwa asilimia 100 kwa miradi ya kuzalisha umeme ya
Kinyerezi I MW 150, Kinyerezi II MW
240 na mradi wa njia ya kusafirisha umeme kV 220 kutoka Makambako hadi Songea; kukamilika kwa asilimia 73 ya
utekelezaji wa mradi wa Kufua Umeme wa
Rusumo MW 80; kukamilika kwa asilimia 98 ya ujenzi na upanuzi wa vituo vya
kupoza umeme pamoja na njia za kusafirisha umeme katika Mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa Msongo wa kV 220 Bulyanhulu –
Geita; kuendelea na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa kV 400 Singida – Arusha –
Namanga ambapo utekelezaji umefikia asilimia 76, kuendelea na
utekelezaji wa mradi wa Kinyerezi I Extension MW
185 ambapo utekelezaji umefikia asilimia 84; kukamilika kwa usanifu wa
miradi ya Kakono MW 87 na Malagarasi MW 45; kuendelea na kuhuisha
upembuzi yakinifu na usanifu wa miradi ya Kufua Umeme wa Maji ya Ruhudji MW 358 na Rumakali MW 222; kukamilika kwa upembuzi yakinifu na kuendelea na maandalizi
ya mradi wa Njia ya Kusafirisha Umeme wa
Msongo wa kV 400 Rufiji – Chalinze – Dodoma na Chalinze – Kinyerezi; na
kuunganishwa umeme kwa jumla ya vijiji
10,018 kati ya vijiji 12,317 hadi Desemba 2020, sawa na asilimia 81.3. Katika
mwaka 2019/20, shilingi bilioni 328.9 zimetumika na shilingi bilioni 172.9
zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21;
(vi)
Mradi wa Ujenzi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima
(Uganda) hadi Tanga (Tanzania): Kukamilika kwa tathmini ya athari za mazingira;
kuendelea na utoaji wa elimu kwa umma kwa maeneo ya pembezoni mwa eneo la
mradi; kukamilika kwa majadiliano ya maeneo mawili (2) kati ya matatu (3) ya
mikataba ikiwemo ya Nchi Hodhi na wawekezaji, mkataba wa ubia, mkataba wa
bandari na mkataba wa pango la ardhi;
(vii)
Mradi wa Kuchakata na Kusindika Gesi Asilia – Lindi: Kukamilika kwa ulipaji wa fidia kwa wananchi
watakaopisha mradi; na kuendelea na majadiliano baina ya Serikali na kampuni za
uwekezaji kuhusu Mikataba Hodhi ya utafutaji na uendelezaji wa mradi. Hadi
kufikia Desemba 2020, shilingi bilioni 6.0 zimetumika katika maandalizi ya
mradi, ikiwa ni pamoja na kulipa fidia kwa wananchi watakaopisha mradi;
(viii)
Ujenzi
wa Barabara na Madaraja Makubwa: Kujengwa kwa mtandao wa barabara kwa kiwango cha lami
wenye urefu wa kilomita 3,537 (barabara kuu na za mikoa kilomita 2,209 na
barabara za halmashauri kilomita 1,328) na hivyo kufanya mtandao wa barabara uliojengwa
kwa kiwango cha lami hadi mwaka 2019/20 kufikia kilomita 13,044 ambapo kilomita
10,939 ni barabara kuu na kilomita 2,105 ni barabara za mikoa; Kuzinduliwa na kuanza kutumika kwa barabaya ya juu (Interchange) ya Ubungo;
kukamilika kwa ujenzi wa madaraja makubwa 12 ambayo ni Magufuli (Morogoro),
Nyerere (Dar es Salaam), Magara
(Manyara), Kavuu (Katavi), Ruvu Chini (Pwani), Mlalakuwa (Dar es Salaam), Momba
(Rukwa), Lukuledi (Lindi), Lukuledi II (Lindi), Mara (Mara), Sibiti (Singida)
na Mtibwa (Morogoro); na kuendelea
na ujenzi wa madaraja ya Ruhuhu (Ruvuma) asilimia 95, Daraja jipya la Tanzanite (Dar es Salaam) asilimia 55.2, Kitengule
(Kagera) asilimia 50 na New Wami
(Pwani) asilimia 41.4; kuendelea na ujenzi wa daraja la Kigongo – Busisi (Mwanza) lenye urefu
wa kilomita 3.2 na upana wa mita 28.45 ambapo utekelezaji umefikia asilimia 5.8.
Katika mwaka 2019/20, shilingi trilioni 1.93 zilitumika na shilingi bilioni
398.6 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21;
(ix)
Uendelezaji
wa Bandari: Katika Bandari
ya Dar es Salaam shughuli zilizofanyika ni: Kuboreshwa kwa gati namba 1 – 4
(gati namba 1-3 kwa ajili ya mizigo mchanganyiko na gati namba 4 kwa ajili ya
mizigo ya kichele mfano ngano na mbolea); kukamilika kwa ujenzi wa gati la
kupakia na kushushia magari (RoRo); na kuendelea na uboreshaji wa gati na 5
hadi 7 (gati namba 5 kwa ajili ya mizigo ya kichele na gati namba 6-7 ni kwa
ajili ya makontena). Katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni 207.6 zimetumika na
shilingi bilioni 42.6 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21.
Katika Bandari
ya Mtwara ujenzi wa gati jipya lenye urefu wa mita 300 na yadi ya kuhudumia
makasha umekamilika ambapo katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni 43.6
zimetumika na shilingi bilioni 44.9 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka
2020/21. Katika Bandari ya Tanga
ujenzi wa kina cha lango la bandari kutoka mita 4 hadi mita 13 na ujenzi wa
gati mbili kwenye kina kirefu umekamilika. Katika mwaka 2019/20 shilingi
bilioni 66.5 zimetumika na shilingi bilioni 20.4 zimetumika katika nusu ya
kwanza ya mwaka 2020/21;
(x)
Usafiri wa Abiria na Mizigo
katika Maziwa Makuu: Ziwa
Victoria: Kukamilika kwa ukarabati wa meli mbili (2) za New Butiama Hapa
Kazi Tu na New Victoria Hapa Kazi Tu; kuendelea na ujenzi wa meli mpya ya MV
Mwanza Hapa kazi Tu yenye uwezo wa kubeba abiria 1,200 na tani 400 za mizigo
ambao umefikia asilimia 35; kukamilika kwa ujenzi wa Chelezo cha kujengea na kukarabati
meli katika Bandari ya Mwanza; na kupatikana kwa makandarasi kwa ajili ya
ukarabati wa meli za MV Umoja na MV Serengeti na kukamilika kwa maandalizi ya
mikataba kwa ajili ya ukarabati wa meli hizo; na kukamilika ukarabati wa meli
za MV Clarias na ML Wimbi. Aidha, shughuli nyingine zilizokamilika ni: Ujenzi
wa magati ya Lushamba, Ntama, Nyamirembe, Magarine na Gati la majahazi
Mwigobero; ununuzi wa vifaa vya kuhudumia mizigo na meli; ukarabati wa majengo
na ofisi za bandari za Ziwa Victoria; kuboresha eneo la kushukia abiria Mwanza
North; na ukarabati wa ‘Link Span’ ya bandari ya Mwanza South. Vile
vile, katika Ziwa Tanganyika,
mikataba kwa ajili ya Ujenzi wa Meli Mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na
tani 400 imesainiwa pamoja na ukarabati wa meli ya MV Liemba; na ukarabati wa
meli ya MT. Sangara. Katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni 56.2 zimetumika
kutekeleza miradi yote katika Ziwa Victoria na Tanganyika na shilingi bilioni
12.8 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21.
Ziwa Nyasa: Kukamilika kwa ujenzi wa
matishari mawili (2) yenye uwezo wa kubeba tani 1000 kila moja; na ujenzi wa
meli moja mpya ya MV Mbeya II yenye uwezo wa kubeba abiria 200 na mizigo tani
200 umekamilika na kuanza kufanya kazi. Katika mwaka 2019/20 shilingi milioni
233.9 zimetumika na shilingi bilioni 1.5 zimetumika katika nusu ya kwanza ya
mwaka 2020/21;
(xi)
Uendelezaji
wa Viwanda:
Kujengwa kwa jumla ya viwanda vipya 8,477 kati ya mwaka 2015 – 2019, ambapo
viwanda vikubwa ni 201, vya kati 460, vidogo 3,406 na vidogo sana 4,410. Ujenzi
wa viwanda hivyo umeongeza idadi ya viwanda nchini kutoka 52,633 mwaka 2015
hadi 61,110 mwaka 2019. Katika mwaka 2019/20 na nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21
shilingi bilioni 5.5 zimetumika katika uratibu wa shughuli za viwanda;
(xii)
Kiwanda cha Sukari Mkulazi: kuendelea na utekelezaji wa mradi ambapo shughuli
zilizofanyika ni pamoja na: kulimwa na kupandwa miwa eneo lenye hekta 2,061
kwenye shamba la Mbigiri; kukamilika kwa ufungaji wa mifumo ya umwagiliaji
shamba la Mbigiri kwenye eneo la hekta 700 na kuanza eneo lingine lenye ukubwa
wa hekta 756. Vile vile, shughuli nyingine zilizofanyika ni kupatikana kwa
mshauri elekezi wa mifumo ya umwagiliaji na mitambo ya kiwanda katika eneo la
Mkulazi I.
(xiii)
Kilimo: Kujengwa na
kuboreshwa kwa miundombinu ya umwagiliaji ambayo imeongeza eneo la
kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 461,376 mwaka 2015 hadi hekta 694,715 mwaka
2020; kuendelea na ujenzi wa
miundombinu ya umwagiliaji katika skimu za Kigugu – Mvomero yenye hekta 200
ambapo utekelezaji umefikia asilimia 98, Mvumi – Kilosa yenye hekta 249 (asilimia 100), Msolwa Ujamaa – Morogoro yenye hekta
675 (asilimia 98), Njage – Kilombero yenye hekta 325 (asilimia 100), Shamba la
Mbegu Kilangali – Kilosa yenye hekta 400 (asilimia 80); kuongezeka kwa
uzalishaji wa mbegu bora kutoka tani 36,614 mwaka 2015 hadi tani 71,000 mwaka
2020; kukamilika kwa ujenzi wa maabara
ya mbegu katika Makao Makuu ya Wakala wa Mbegu za Kilimo – Morogoro. Katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni
45.9 zimetumika na shilingi bilioni 28.7 zimetumika
katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21;
(xiv)
Mifugo: Kujenga kiwanda kipya cha Kilimanjaro International Leather Industries Co Ltd chenye uwezo wa
kuzalisha jozi na soli za viatu 1,200,000 kwa mwaka na kuchakata ngozi futi za
mraba 13,000,000 kwa mwaka; kuimarisha kituo cha Taifa cha Uhimilishaji cha National
Artificial Insemination Center - NAIC kilichopo USA River Arusha kwa kununua kifaa (Chiller) kwa ajili ya mtambo wa
kuzalisha kimiminika cha naitrojeni; kujengwa kwa viwanda vipya vya kimkakati
vya nyama vya Tanchoice (Pwani), Elia Food Oversees Limited (Arusha) na Binjiang Company Limited (Shinyanga);
kujengwa kwa kiwanda cha maziwa cha Galaxy
Food and Beverage Company Limited
(Arusha); kujengwa kwa kiwanda cha kuzalisha chanjo cha Hester Bioscience Africa Limited
(Pwani) chenye uwezo wa kuzalisha chanjo aina 37; kuendelea kuboresha huduma za
malisho ya mifugo na majosho; na kuendelea kukamilisha ujenzi wa machinjio ya
kisasa Vingunguti. Katika mwaka
2019/20 shilingi bilioni 2.76 zimetumika na shilingi bilioni 1.77 zimetumika
katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21;
(xv)
Uvuvi: Kuongezeka kwa uzalishaji wa samaki katika maji ya asili
kutoka tani 362,645 zenye thamani ya shilingi trilioni 1.48 mwaka 2015/16 hadi
tani 497,567 zenye thamani ya shilingi trilioni 2.34 mwaka 2019/20; kuongezeka
kwa usindikaji wa minofu ya samaki aina ya Sangara kutoka tani 23,000.58 mwaka
2015/16 hadi tani 27,596.27 mwaka 2019/20; kuongezeka kwa huduma za
usafirishaji wa mazao ya uvuvi kwenda
masoko ya Ulaya ambapo katika mwaka 2019/20, jumla ya kilo 777,750.0 za mabondo
zilisafirishwa; na kuendelea na maandalizi ya ujenzi wa Bandari ya Uvuvi
(Mbegani) na ununuzi wa meli nne (4) za uvuvi. Katika mwaka 2019/20 shilingi
milioni 426.3 zimetumika na shilingi milioni 606.7 zimetumika katika nusu ya
kwanza ya 2020/21;
(xvi)
Madini: Kupitia na kutunga Sheria, Sera na mikataba ya madini;
kuanzishwa kwa Kampuni mpya ya Twiga
Minerals Corporation inayomilikiwa kwa ubia kati ya Tanzania (hisa asilimia
16) na Kampuni ya Barrick (hisa asilimia 84) ambapo imetoa gawio la shilingi
bilioni 100; kusainiwa kwa mkataba wa ubia wa kampuni ya LZ NICKEL na Serikali
ya Tanzania kwa ajili ya kuendeleza na kuchimba madini ya Nickel ambapo chini
ya mkataba huo imeundwa kampuni ya ubia inayoitwa Tembo Nickel Corporation
Limited (kwa umuliki wa hisa 84% kwa Kampuni ya LZ Nickel na Serikali ya
Tanzania Hisa 16%); kujengwa kwa masoko 39 ya madini na vituo 41 vya kuuzia
madini; kukamilika kwa ujenzi wa vituo vinne (4) vya umahiri katika maeneo ya
Bariadi, Musoma, Bukoba na Handeni na kuendelea na ujenzi wa vituo vya Songea,
Mpanda na Chunya; kuimarishwa kwa ulinzi wa rasilimali za madini kwa kujenga
ukuta wenye mzingo wa kilomita 24 wa Mirerani Manyara pamoja na kujenga One Stop Centre, kufunga vifaa vya
ulinzi ikiwa ni pamoja na taa na CCTV
Camera kuzunguka ukuta na barabara ya kuzunguka ukuta wa ndani; na
kukamilisha ujenzi wa vituo vitatu (3) vya Mfano vya uchenjuaji wa madini ya
dhahabu kwa ajili ya wachimbaji wadogo katika maeneo ya Lwamgasa (Geita),
Katente (Bukombe) na Itumbi (Chunya). Katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni
3.08 zimetumika na shilingi bilioni 3.3 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka
2020/21;
(xvii) Miradi ya Afya: Kuendelea kutoa huduma za kupandikiza uloto (bone marrow transplant) na kukamilika kwa
ujenzi wa jengo la wodi namba 18 ya Sewa Haji pamoja na ujenzi wa wodi za
kulaza wagonjwa binafsi katika Hospitali
ya Taifa ya Muhimbili; Kukamilika kwa ujenzi wa jengo la huduma za dharura
na ukarabati wa jengo la X-ray katika
Hospitali ya Rufaa Dodoma;
kukamilika kwa asilimia 98.2 ya ujenzi wa Hospitali
ya Uhuru – Dodoma; kununuliwa kwa
mashine za digital X-ray na ultrasound, vifaa vya maabara na mashine
za uchunguzi wa kifua kikuu kwa kuotesha vimelea BACTEC 960 (Mycobacteria Growth Indicator Tube - MGIT) na Blood culture
machine katika Hospitali ya Rufaa ya
Magonjwa ya Kifua Kikuu – Kibong’oto; ununuzi wa mashine ya Positron Emmission Tomography (PET Scan) kwa ajili ya Hospitali ya Ocean Road; kujenga na
kuboresha miundombinu ya hospitali za rufaa za Mara, Geita, Songwe, Katavi,
Sekou Toure (Mwanza), na hospitali za rufaa za kanda ya kusini Mtwara na kanda
ya nyanda za juu kusini Mbeya na Hospitali ya Kanda ya Kaskazini (KCMC) na Hospitali ya Kanda ya Ziwa ya Burigi
(Geita).
Vile vile, Serikali inaendelea na utekelezaji wa miradi
ya sekta ya afya ambayo imefikia hatua mbalimbali ikiwemo: kufikia asilimia 98
ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali
ya Rufaa Mwananyamala; kukamilika na kuanza kutumika kwa jengo la wagonjwa
wa nje na kufikia asilimia 73 ya ujenzi wa jengo la maabara katika Hospitali ya Rufaa Njombe; na ujenzi wa
jengo la ghorofa moja la huduma za upasuaji, radiolojia na maabara na kufikia
asilimia 50 ya ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya Rufaa Simiyu. Katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni
321.24 zimetumika na shilingi bilioni 64.6 zimetumika katika nusu ya kwanza ya
mwaka 2020/21;
(xviii) Miradi ya Maji Mijini
na Vijijini:
Kukamilika
kwa miradi 1,423 ya maji iliyotekelezwa mijini na vijijini ambayo imewezesha
wananchi zaidi ya milioni 25 kupata huduma ya maji safi na salama. Baadhi ya
miradi iliyotekelezwa na hatua zilizofikiwa ni: kukamilika kwa miradi ya maji
katika miji ya Geita, Njombe na Songwe na kuendelea kwa ujenzi wa mradi wa maji
katika mji wa Kigoma (asilimia 90); utekelezaji wa Mradi mkubwa wa Maji wa Ziwa Victoria kwenda katika miji ya Isaka, Tinde, Kagongwa, Tabora,
Igunga, Uyui na Nzega umefikia asilimia 98; kukamilika kwa asilimia
76 ya ujenzi wa mradi wa maji katika Jiji la Mwanza; kukamilika kwa asilimia 62 ya ujenzi wa mradi wa maji katika Jiji la Arusha; na kuendelea na ujenzi wa mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe ambapo utekelezaji
wake umefikia asilimia 65. Aidha, katika eneo linalohudumiwa na DAWASA (mikoa ya Dar
es Salaam na Pwani) utekelezaji wa miradi umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90.
Katika mwaka 2019/20 shilingi bilioni 511.5 zimetumika na shilingi bilioni
226.7 zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21;
(xix)
Elimu: Kujengwa kwa miundombinu muhimu
katika shule 3,904 (Msingi 3,021 na Sekondari 883), mabweni 547, nyumba za
walimu 101, majengo ya utawala 25 na maktaba 43; kukamilika kwa ujenzi wa
maboma 2,815 katika shule za msingi 2,133; kuendelea kugharamia elimumsingi bila ada ambapo katika
mwaka 2019/20 shilingi bilioni 252.9 zimetumika na shilingi bilioni 124.8
zimetumika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21; kukarabatiwa shule kongwe 84 kati ya 89; kuboreshwa kwa miundombinu ya vyuo 54 vya Maendeleo ya
Wananchi; kutolewa kwa mikopo ya elimu ya juu jumla ya shilingi trilioni 2.26;
na kuimarishwa kwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji katika taaluma za Anga na
Chuo cha Ufundi Arusha katika taaluma ya Nishati. Katika mwaka 2019/20,
shilingi bilioni 734.9 zimetumika na shilingi bilioni 159.0 zimetumika katika
nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21; na
(xx)
Ajira: Kutokana na mafanikio
mbalimbali yaliyopatikana katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi
cha kuanzia mwaka 2016/17 hadi mwaka 2020/21, jumla ya ajira 12,773,126
zimezalishwa. Kati ya ajira hizo, ajira za moja kwa moja ni 11,891,772 na ajira
zisizo za moja kwa moja ni 881,354. Aidha, jumla ya vijana 65,008 katika
kipindi cha mwaka 2017 hadi 2020
wamepatiwa mafunzo ya ujuzi na stadi za kazi ikiwemo mafunzo ya uanagenzi katika fani za
ujenzi, useremala, umeme wa majumbani na viwandani, umeme wa jua, ufundi
magari, ufundi bomba, utengenezaji wa vifaa vya aluminium, uchomeleaji na
uungaji vyuma, kilimo na ufugaji, ushonaji, uchorongaji vipuli, uchapaji
nyaraka na TEHAMA. Serikali imeendelea kulinda ajira za wazawa kwa kuhakikisha
kuwa wageni wanaokuja kufanya kazi
nchini wanakidhi vigezo
vilivyoainishwa katika Sheria ya
Kuratibu Ajira za Wageni Na. 1 ya mwaka 2015.
25.
Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu utekelezaji wa miradi ya
maendeleo mwaka 2019/20 na nusu ya kwanza ya
mwaka 2020/21 yameainishwa
katika kitabu cha Mapendekezo ya Mpango
(Sura ya Tatu).
2.5 Changamoto
za Utekelezaji wa Mpango na Bajeti na Hatua na Kukabiliana nazo
26.
Mheshimiwa Spika, utekelezaji
wa Mpango na Bajeti kwa mwaka 2019/20 na nusu ya kwanza ya mwaka 2020/21
ulikabiliwa na changamoto mbalimbali katika utekelezaji. Baadhi ya changamoto
hizo ni pamoja na: uharibifu wa miundombinu uliosababishwa na mafuriko;
kupungua kwa shughuli za kibiashara duniani kutokana na athari za COVID-19; na ukwepaji
kodi kwa baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu hususan kupitia njia za
magendo, uhamishaji wa faida (transfer pricing) kwa kampuni zenye mtandao wa
kimataifa na kutokutoa na kudai stakabadhi za kielektroniki (EFD receipt)
wakati mauzo yanapofanyika.
27. Mheshimiwa
Spika, katika kukabiliana na
changamoto za utekelezaji wa Mpango na Bajeti, Serikali itaendelea kuchukua
hatua zifuatazo: kufanya ukarabati wa miundombinu iliyoharibiwa na mafuriko
pamoja na kuimarisha ukaguzi wake; kuendelea kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa
biashara duniani ili kutumia fursa zilizotokana na athari za COVID-19 kwa
manufaa mapana ya nchi pamoja na kuchukua hatua za kisera na kiutawala
kurejesha biashara zilizoathirika; na kuimarisha mifumo ya usimamizi na
ufuatiliaji wa mapato ili kudhibiti ukwepaji kodi pamoja na kuendelea
kuhamasisha umma juu ya matumizi ya stakabadhi za kielektroniki.
3.0
MWONGOZO WA MAANDALIZI YA MPANGO NA BAJETI YA SERIKALI KWA
MWAKA 2021/22
28.
Mheshimiwa Spika, masuala ya msingi yatakayowezesha kufikia shabaha za
uchumi jumla ni pamoja na: kuendelea kuwepo kwa amani, usalama, umoja, utulivu
wa ndani na nchi jirani ili kuwezesha kuendelea kwa shughuli za kiuchumi na
kijamii; kuimarika kwa uchumi wa dunia na utulivu wa bei katika masoko ya
kimataifa; kuhimili athari za majanga ya asili kama vile mafuriko na magonjwa
ya mlipuko; na hali nzuri ya hewa itakayowezesha uzalishaji wa chakula cha
ziada.
29.
Mheshimiwa Spika, shabaha na malengo ya uchumi jumla yatakayozingatiwa katika
muda wa kati ni pamoja na:
(i)
Kuongeza
kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 6.0 mwaka 2021 na
kuendelea kukua kwa wastani wa asilimia 6.3 ifikapo mwaka 2023;
(ii)
Kuendelea
kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha kuwa unabaki kwenye wigo wa
tarakimu moja ya wastani wa asilimia kati ya 3.0 - 5.0 katika muda wa kati;
(iii)
Mapato
ya ndani (ikijumuisha mapato ya Halmashauri) kufikia asilimia 15.9 ya Pato la
Taifa mwaka 2021/22 na asilimia 16.3 ya Pato la Taifa mwaka 2023/24;
(iv)
Mapato
ya kodi kufikia asilimia 13.5 ya Pato la Taifa mwaka 2021/22 kutoka matarajio
ya asilimia 12.9 mwaka 2020/21;
(v)
Kuhakikisha
kuwa nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) haizidi asilimia 3.0 kuendana na
makubaliano ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki; na
(vi)
Kuwa
na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango cha kukidhi mahitaji ya uagizaji wa
bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne (4).
3.1
Mfumo
wa Awali wa Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2021/22
30. Mheshimiwa
Spika, katika
mwaka 2021/22, Serikali inatarajia kukusanya na kutumia jumla ya shilingi trilioni
36.26. Kiasi hiki ni sawa na ongezeko la asilimia 4.0 ikilinganishwa na bajeti
ya mwaka 2020/21 ya shilingi trilioni 34.88. Ongezeko hili linatokana na:
Mahitaji ya Mfuko Mkuu wa Serikali ikijumuisha malipo ya deni la Serikali;
mahitaji ya upandishwaji wa madaraja ya watumishi na ajira mpya; na mahitaji ya
Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanzania National Parks
Authority - TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa
Wanyamapori Tanzania (Tanzania Wildlife Management Authority - TAWA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (Ngorongoro Conservation
Area Authority - NCAA). Mapato ya ndani (yakijumuisha mapato ya
Halmashauri) yanakadiriwa kuongezeka hadi shilingi trilioni 26.03 mwaka 2021/22
kutoka makadirio ya shilingi trilioni 24.07 mwaka 2020/21 na kukua kwa wastani
wa asilimia 8.6 katika muda wa kati. Uwiano wa mapato ya ndani kwa mapato yote
unatarajiwa kuongezeka kutoka asilimia 71.8 ya bajeti ya mwaka 2021/22 hadi
asilimia 76.7 ya makadirio ya bajeti ya mwaka 2023/24. Mapato ya kodi
yanakadiriwa kuongezeka hadi shilingi trilioni 21.47 mwaka 2021/22 kutoka
shilingi trilioni 20.14 mwaka 2020/21 na kukua kwa wastani wa asilimia 7.1
katika muda wa kati. Mapato yasiyo ya kodi (yakijumuisha mapato ya Halmashauri,
mapato ya utalii na mapato mengine yasiyo ya kodi yanayokusanywa na Mamlaka ya
Mapato Tanzania) yanakadariwa kuwa shilingi trilioni 4.56 mwaka 2021/22 na
kuongezeka kufikia shilingi trilioni 5.60 mwaka 2023/24.
31.
Mheshimiwa Spika, Washirika wa Maendeleo wanatarajiwa kuchangia shilingi trilioni
2.89 sawa na asilimia 7.9 ya bajeti yote mwaka 2021/22. Katika kipindi hicho,
Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 4.99 kutoka soko la ndani. Kati ya
kiasi hicho shilingi trilioni 3.15 ni
kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na kiasi cha
shilingi trilioni 1.84 sawa na asilimia 1.1 ya Pato la Taifa ni mikopo kwa
ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo. Aidha, mikopo ya masharti ya
kibiashara kutoka nje inatarajiwa kuwa shilingi trilioni 2.35 mwaka 2021/22.
32.
Mheshimiwa Spika, matumizi ya Serikali yanakadiriwa kufikia shilingi trilioni
36.26, ambapo shilingi trilioni 23.0 ni matumizi ya kawaida na shilingi trilioni
13.26 ni matumizi ya maendeleo, sawa na asilimia 37 ya bajeti yote. Matumizi ya
kawaida yanajumuisha mishahara shilingi trilioni 8.15 (sawa na asilimia 31.3 ya
makadirio ya mapato ya ndani), malipo ya riba na mtaji kwa deni la ndani na nje
shilingi trilioni 8.88 na matumizi mengineyo shilingi trilioni 5.97. Aidha,
matumizi ya maendeleo yanajumuisha shilingi trilioni 10.37 fedha za ndani na
shilingi trilioni 2.89 fedha za nje. Makadirio
ya matumizi ya maendeleo yamezingatia kukamilika kwa miradi mbalimbali kama
vile maboma ya shule na vituo vya kutolea huduma za afya ambayo yanahitaji
fedha za matumizi ya kawaida kwa ajili ya uendeshaji.
33.
Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu sera za mapato na matumizi katika
muda wa kati yapo katika Sehemu ya
Kwanza, Sura ya Tatu ya Kitabu cha Mwongozo.
3.2
Maelekezo
Mahsusi ya Mwongozo
34.
Mheshimiwa Spika, Mwongozo wa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2021/22
umeainisha maelekezo mbalimbali ambayo Maafisa Masuuli watatakiwa kuyazingatia wakati
wa uandaaji, utekelezaji, ufuatiliaji, tathmini na utoaji wa taarifa. Hivyo,
Maafisa Masuuli watatakiwa kutekeleza kikamilifu maelekezo yote yaliyopo kwenye
Mwongozo na kusimamia Sheria ya Bajeti, SURA 439 na Kanuni zake. Baadhi ya
maelekezo yaliyobainishwa katika Mwongozo huu ni kama ifuatavyo:
3.2.1 Uandaaji
(i)
Mamlaka za Serikali za
Mitaa kutenga angalau asilimia 40 ya mapato ya ndani yasiyolindwa kwenda kwenye
miradi ya maendeleo;
(ii)
Kuzingatia
matakwa ya Sheria ya Msajili wa Hazina, Sura 370 kwa kutenga na kuwasilisha
katika Mfuko Mkuu wa Hazina ya Serikali michango ya asilimia 15 ya mapato ghafi
ya Taasisi na asilimia 70 ya ziada ya mapato baada ya kutoa matumizi
yaliyoidhinishwa;
(iii)
Kupata
idhini kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya Fedha kabla ya kupokea
mikopo, misaada na dhamana kwa mujibu wa kifungu cha 15(1) cha Sheria ya
Mikopo, Dhamana na Misaada, Sura 134;
(iv)
Kuzingatia
viwango vya ukomo wa bajeti vitakavyotolewa na Serikali;
(v)
Kushirikisha
kikamilifu Kamati za Bajeti za kila Fungu katika maandalizi na utekelezaji wa
bajeti ili kuwepo kwa mipango na utekelezaji shirikishi katika Mafungu kama
ilivyobainishwa katika Kanuni ya 17(3) ya Kanuni za Sheria ya Bajeti za Mwaka
2015;
(vi)
Kutumia
Mfumo wa Kitaifa wa Kusimamia Miradi ya Maendeleo (NPMIS) katika kuandaa na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa
kuzingatia Waraka wa Hazina Na. 5 wa mwaka 2020/21; na
(vii)
Kutenga
fedha kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa kwa kuzingatia Waraka wa Hazina
Na. 3 wa mwaka 2019.
3.2.2 Utekelezaji
(i)
Kuhakikisha
mapato yote katika Wizara na Taasisi za Umma yanaendelea kukusanywa kupitia
Mfumo wa Government e-Payment Gateway (GePG);
(iii)
Kuzingatia
maelekezo ya Waraka wa Hazina Na. 2 wa Mwaka 2019 unaoelekeza utaratibu wa
kuomba, kuhamisha, kupokea, kutumia, kuhasibu na kutoa taarifa za utekelezaji
wa miradi ya D-Fund na matumizi ya Mfumo wa Usimamizi wa
Fedha Zinazopelekwa Moja kwa Moja kwenye Miradi;
(iv)
Kuhakikisha
ununuzi wa umma unafanyika kwa kuzingatia Sheria ya Ununuzi wa Umma, Sura 410
na Kanuni zake kwa kufanya ununuzi wa pamoja na kutumia Mwongozo wa Matumizi ya
Force Account wa Mei 2020 ili kupata thamani halisi ya fedha;
(v)
Kutumia Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma
(TANePS) katika ununuzi wa bidhaa, huduma na kandarasi za ujenzi;
(vi)
Kuhakikisha
Taasisi na Mashirika ya Umma yanaingia Mkataba wa Utendaji Kazi pamoja na
kuwasilisha utekelezaji wa Mikataba kila robo mwaka kwa mujibu wa Sheria ya
Msajili wa Hazina;
(vii) Kuepuka uzalishaji na ulimbikizaji wa madeni kwa
kuzingatia Waraka wa Hazina Na. 3 wa mwaka 2019; na
(viii) Kuhakikisha Wizara na Taasisi za Umma zinatumia Mfumo wa
Uhasibu Serikalini (MUSE) kwa ajili ya malipo na shughuli za kihasibu kwa
kuzingatia Waraka wa Hazina Na. 5 wa mwaka 2019.
3.2.3 Ufuatiliaji na Tathmini
(i)
Kuandaa mpango kazi na
mtiririko wa fedha wa utekelezaji wa bajeti kupitia mifumo ya CBMS na PlanRep;
(ii)
Kuandaa taarifa za
utekelezaji kwa kuzingatia muundo ulioainishwa katika Sura ya Pili ya Sehemu ya
Pili ya Mwongozo. Taarifa za utekelezaji za kila robo ya mwaka ziwasilishwe
katika muda wa siku 30 baada ya kukamilika kwa robo ya mwaka husika. Vile vile,
taarifa za utekelezaji za mwaka ziwasilishwe kabla ya tarehe 15 Oktoba kila
mwaka wa fedha;
(iii)
Kujenga uwezo wa watumishi
katika vitengo vya ufuatiliaji na tathmini na kuandaa mpango wa kurithisha
watumishi wapya maarifa ili kuwa na mfumo endelevu wa ufuatiliaji;
(iv)
Kujenga uwezo wa
wakaguzi wa ndani kufanya ukaguzi kupitia mifumo ya kielektroniki (system-based
auditing) ili kuongeza ufanisi; na
(v)
Kuongeza matumizi ya
TEHAMA katika shughuli za Serikali ili kuongeza ufanisi ikiwa ni pamoja na
kujenga uwezo wa wataalam wa ndani kwenye eneo la usalama wa mifumo.
35.
Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu maelekezo mahsusi ya Mwongozo
yanapatikana katika Sehemu ya Pili, Sura
ya Kwanza na Sura ya Pili ya Kitabu cha Mwongozo.
4.0
MAPENDEKEZO YA MPANGO WA MAENDELEO WA TAIFA WA MWAKA 2021/22
36.
Mheshimiwa Spika, Serikali
itatekeleza vipaumbele vilivyoainishwa katika Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa
Taifa wa Miaka Mitano (2021/22 – 2025/26) ambao ni wa mwisho katika utekelezaji
wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, wenye dhima ya “Kujenga Uchumi Shindani na Viwanda kwa Maendeleo ya
Watu”. Utekelezaji wa Mpango
wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22 utakuwa ni wa kwanza katika kutekeleza
maeneo ya kipaumbele ya Mpango huu. Aidha, utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya
Mwaka 2021/22 utajumuisha ukamilishaji wa miradi ya kipaumbele na kimkakati
ambayo utekelezaji wake haukukamilika katika Mpango wa Pili wa Maendeleo wa
Taifa wa Miaka Mitano 2016/17 – 2020/21. Maeneo ya kipaumbele pamoja na baadhi ya miradi
itakayopewa kipaumbele kwa mwaka 2021/22 ni kama ifuatavyo:
(i)
Kuchochea Uchumi Shindani na Shirikishi. Eneo hili linajumuisha miradi ambayo itajikita katika:
kujenga jamii yenye uwezo wa kushindana kikanda na kimataifa; kuimarisha
utulivu wa uchumi; kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji; kuimarisha
uvumbuzi na uhawilishaji wa teknolojia kutoka nje; na kuendeleza miundombinu na
huduma katika maeneo ya reli, barabara, madaraja, usafiri wa majini, usafiri wa
anga, TEHAMA, nishati, bandari na viwanja vya ndege;
(ii)
Kuimarisha Uwezo wa Uzalishaji Viwandani na Utoaji Huduma: Eneo hili linajumuisha kuendeleza viwanda vya
uzalishaji wa dawa kwa matumizi ya binadamu; miradi ya viwanda inayolenga
kuongeza thamani ya mazao ya kilimo, mifugo, uvuvi na madini pamoja na
kuzalisha bidhaa zitakazotumia malighafi na rasilimali zinazopatikana kwa wingi
nchini. Aidha, eneo hili linajumuisha pia miradi na programu inayolenga
kuboresha sekta ya utalii, huduma za fedha na bima;
(iii)
Kukuza Biashara: Eneo hili linajumuisha programu za kuimarisha masoko ya
ndani na kutumia fursa za masoko ya kikanda na kimatiafa. Aidha, masoko
yanayolengwa ni yale yatakayotoa fursa kwa bidhaa zinazozalishwa nchini ikiwemo
bidhaa zitokanazo na kilimo na viwanda;
(iv)
Kuchochea Maendeleo ya Watu: Eneo hili linajumuisha utekekelezaji wa miradi ambayo
inajikita katika kuboresha maisha ya watu ikiwemo kuboresha elimu na mafunzo
katika ngazi zote; afya na ustawi wa jamii; kinga ya jamii; huduma za maji na
usafi wa mazingira; mipango miji, na nyumba na maendeleo ya makazi; na
(v)
Kuendeleza Rasilimali Watu: Eneo hili linajumuisha
programu na mikakati inayolenga kuendeleza ujuzi wa rasimali watu nchini,
kuanzia ngazi za elimu ya awali hadi elimu ya juu ikiwemo kuwawezesha vijana
kujiajiri. Vile vile, eneo hili linajumuisha hatua za kuboresha viwango vya
utoaji wa elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi pamoja na ujuzi adimu kwa
lengo la kuongeza tija na ushindani wa wananchi katika kutumia rasimali
zilizopo nchini ili kuleta maendeleo.
Aidha, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Mwaka 2021/22
utajumuisha miradi ya kielelezo inayoendelea ambayo utekelezaji wake
unatarajiwa kuwa na matokeo makubwa na ya haraka katika uchumi. Baadhi ya
miradi hiyo ni: Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Julius Nyerere - MW 2,115;
Kuboresha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL); Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango
cha kimataifa (Standard Gauge); Makaa
ya Mawe - Mchuchuma na Chuma – Liganga ikijumuisha ujenzi wa reli kiwango cha
standard gauge kutoka Mtwara hadi Mbambabay na matawi yake ya Mchuchuma na
Liganga; Bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima (Uganda) hadi Tanga (Tanzania);
Mradi wa Kuchakata Gesi Asilia kuwa Kimiminika (LNG) – Lindi; Mradi wa Kufua
Umeme wa Maji wa Ruhudji (MW 358); Mradi wa Kufua Umeme wa Maji wa Rumakali (MW
222); Uchimbaji wa madini ya Nickel; Ujenzi wa Madaraja Makubwa na Barabara za
Juu (Interchange) za Daraja la Kigongo - Busisi (Mwanza), Tanzanite (Dar es
Salaam) na Interchange ya Kamata (Dar
es Salaam); Bandari ya Uvuvi (Mbegani) na Ununuzi wa Meli za Uvuvi; Kiwanda cha
Sukari Mkulazi; Utafutaji wa mafuta katika vitalu vya Eyasi Wembere na Mnazi
Bay Kaskazini; Mradi wa Magadi Soda – Engaruka; Kuongeza Rasilimali Watu yenye Ujuzi
Adimu na Maalumu (Ujuzi wa Kati na Wabobezi) kwa Maendeleo ya Viwanda na Ustawi
wa Jamii; Kanda Maalum za Kiuchumi.
Kwa kuzingatia umuhimu wa Sekta Binafsi katika ustawi wa
kiuchumi na kijamii, Mpango utajielekeza katika kuhakikisha Sekta Binafsi nchini
inashamiri. Mpango utaainisha vipaumbele vitakavyowezesha maendeleo ya Sekta
Binafsi kwa kuweka mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji. Aidha, Mpango
utaainisha mikakati mbalimbali ya uwekezaji na fursa zilizopo kwa ajili ya
uwekezaji kwa Sekta Binafsi.
37.
Mheshimiwa Spika, Maelezo ya kina kuhusu Maeneo ya Kipaumbele kwa mwaka 2021/22
yapo katika Kitabu cha Mapendekezo ya
Mpango (Sura ya Nne).
5.0 HITIMISHO
38.
Mheshimiwa
Spika, Mapendekezo haya yatawezesha
uandaaji wa Mpango na Bajeti ambao utazingatiwa na Maafisa Masuuli wote wakati
wa kuandaa Mipango na Bajeti za Mafungu yao kwa mwaka 2021/22. Kutokana na
Mapendekezo haya, Maafisa Masuuli wa Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala za
Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Taasisi na
Mashirika ya Umma wanaelekezwa kuzingatia maeneo ya kipaumbele yaliyoainishwa
katika Mapendekezo ya Mpango wakati wa kuandaa Mipango na Bajeti za Mafungu yao
kwa Mwaka 2021/22. Vile vile, Maafisa Masuuli wanaelekezwa kuzingatia kikamilifu
maelekezo yote yaliyopo kwenye Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Serikali kwa
Mwaka 2021/22 na kusimamia kikamilifu Sheria
ya Bajeti, SURA 439 na Kanuni zake.
39.
Mheshimiwa
Spika, nawaomba Waheshimiwa Wabunge
wajielekeze zaidi katika kutoa maoni, ushauri na mapendekezo yanayohusu masuala ya Kitaifa kwa maslahi
mapana ya nchi yetu ikijumuisha wananchi tunaowawakilisha. Maoni na ushauri wa
Waheshimiwa Wabunge yatakuwa na mchango mkubwa katika uandaaji wa Mpango wa
Maendeleo na Bajeti kwa ajili ya kuchochea maendeleo ya nchi.
40. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa Bunge lako Tukufu
lipokee, lijadili na kutoa maoni na kuishauri Serikali kuhusu Mapendekezo ya
Mwongozo wa Maandalizi ya Bajeti ya Serikali na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa
Mwaka 2021/22.
41. Mheshimiwa
Spika, naomba kutoa hoja.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇