Na Said Mwishehe,Michuzi TV
TAASISI ya Amani kwa Waislamu Tanzania (TIPF) kupitia Mwenyekiti wake Sadiki Godigodi imeipongeza hotuba ya Rais Dk. John Magufuli ambayo ameitoa siku za karibuni kuhusu hali halisi ya janga la ugonjwa wa Covid-19 nchini.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo ni kwamba hotuba ya Rais Magufuli imejaa matumaini hususn katika matumizi ya dawa za kujifukiza huku akiwataka wataalamu wa kitaifa na kimataifa kuhakikisha wanafanyia kazi dawa hizo za asili zilizoonesha matumaini kwenye kutibu gonjwa hilo na si kuwakatisha tamaa wananchi kwani hata dawa za kisasa nyingi zinatengenezwa na mimea asili.
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam GodiGodi amesema kuwa watanzania wanatakiwa kuendelea kufanya ibada kama alivyoagiza Rais katika kukabiliana na janga hilo kwa kumlilia Mungu kila mmoja na imani yake.
Amefafanua mbali na ibada ni vema pia kutumia maarifa kama alivyosema Rais Magufuli kwa wataalamu kutopuuza matumizi ya dawa hizo kama walivyofanya katika nchi ya Madagascar kwani dawa inayoleta nafuu katika tatizo hilo la dunia ni vema kufanyiwa kazi kitaalamu na si kukatisha tamaa.
Godigodi ameongeza katika kipindi hiki ambacho Waislamu wameingia katika ibada ya funga,wajitahid kumuomba Mungu ili atuepushee na janga hilo la Corona na In shallah Watanzania watashinda vita hiyo na huku akisisitiza umuhimu wa kuendelea kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya
Pia amewataka wananchi kuwapuuza wote wanaobeza juhudi za Rais kwani vita hiyo ni kubwa hata mataifa makubwa yameshindwa na kumuachia Mungu na kamwe watanzania wasikubali kuyumbishwa na habari za mitandao ya kijamii.
"Wananchi wanatakiwa kusikiliza wataalamu wa afya pamoja na wasemaji rasmi walioteuliwana Serikali kuhusu janga hilo wanaojitahidi kutoa habari sahihi kwa wakati huku viongozi wotewakishikamana bila kujali tofauti za kisiasa au kidini kwenye mapambano hayo,"amesema.
Amempongeza Rais kwa kutoliweka karantini Jiji la Dar es Salaam kwani ingeweza kusababisha taharuki kwa wananchi wa kawaida na kuyumbisha uchumi wa nchi na kwamba hayo ni maamuzi magumu ambayo kiongozi wa nchi ameamua kuyachukua kwa maslahi mapana yataifa.
Hivyo, lazima Rais auungwe mkono na Watanzania wote na kusisitiza umuhimu wa kushirikiana katika hili kwani kuna watu wamezuia watu wake kutoka nje ya nchi zao,nyumba zao pamoja na kufunga nyumba za ibada.
" Rais wetu tunakupongeza kwenye hili kwani umeonesha namna ambavyo unajali wananchi wako kwa kuwataka kuchukua tahadhari lakini kubwa zaidi kuruhusu wananchi kuendelea na shughuli zao za kiuchumi.Ahsante Rais ,Watanzania tuko pamoja nawe."
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇