Mganga wa tiba asili na tiba mbadala, Huasi Mohamed aliyevaa shuka nyeupe ambaye ameepata mafunzo ya kuwaibua na kuwahisi wagonjwa wa kifua kikuu wanaofika katika kilinge akiwa katika picha ya pamoja na mratibu wa kifua kikuu,ukoma na tiba asili katika Hospitali ya wilaya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole wa pili kushoto na baadhi ya wazazi wake,Mganga huyo amekuwa msaada mkubwa katika kuwaibua wagonjwa wa kifua kikuu wanaofika kwake kwa ajili ya kupata huduma ambapo wale wanaohisiwa wanapewa rufaa ya kwenda Hospitali kwa ajili ya uchunguzi na matibabu.
Na Mwandishi Wetu, Tunduru
BAADHI ya wananchi wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wameipongeza Serikali kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma Hospitali ya wilaya ya Tunduru kuanza kuwatumia waganga wa Tiba asili na tiba mbadala waliosajiliwa kuibua wagonjwa wa kifua kikuu na kutoa rufaa ya kwenda hospitali kupata matibabu.
Wananchi hao waliokutwa katika kitongoji cha Mdingula kijiji cha Namasalau wakipata tiba katika moja ya kilinge cha mganga maarufu wa tiba asili na tiba mbadala Hausi Mohamed wakipata huduma, wameishauri Serikali iendelea kuwaamini na kuwaunga mkono waganga hao kwani wana mchango mkubwa katika kutokomeza ugonjwa huo na kuokoa maisha ya watu.
Rahim Hussen na Mohamed Abdala walisema, iwapo Serikali itawatumia waganga wa Tiba asili kwenye kampeni na mkakati dhidi ya ugonjwa wa kifua kikuu, mafanikio yake yatakuwa makubwa kutokana na kuwepo kwa idadi kubwa ya watu kutoka maeneo mbalimbali wanaofika kwa waganga hao kwa ajili ya kupata huduma kutokana na shida zao.
Rahim alisema, kwenye vilinge vya waganga wa tiba asili kuna makundi makubwa ya watu kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na visiwani na hata nchi jirani ya Msumbuji.
Alisema,ushiriki wao katika kuibua wahisiwa wa kifua kikuu wanaofika katika vilinge vyao na kuwapa rufaa ya kwenda Hospitali kwa ajili ya vipimo na matibabu wataokoa maisha ya wananchi wengi wenye maradhi hayo wanaokimbilia kwa waganga wa tiba asili.
Mohamed Abdala alisema, jamii kubwa inaaamini sana tiba mbadala kama suluhisho la matatizo waliyonayo kwani baadhi ya maradhi hayana tiba za kitaalam,lakini wanapofika kwa waganga wanapona kabisa na kuungana na familia zao na kushiriki katika kazi za maendeleo.
“sisi kama wananchi tunashukuru sana katika kijiji chetu kupata mganga wa tiba asili ambaye amekuwa mkombozi mkubwa wa shida zetu,tulikuwa na shida ambazo tulikwenda hospitali lakini hatukupona, na mara baada ya kuja kwa mganga afya zetu zimeimarika,naiomba Serikali iendelea kuwatumia na kushirikiana na waganga kwani ni msaada mkubwa kwetu sisi wananchi”alisema.
Kwa upande wake Mratibu wa kifua kikuu na ukoma Hospitali ya wilaya Tunduru Dkt Mkasange Kihongole alisema, tayari kuna waganga wa tiba asili zaidi ya arobaini wamepata mafunzo ya namna ya kuwaibua wagonjwa wenye maambukizi ya kifua kikuu na kuwapa rufaa kwenda Hospitali kwa ajili ya uchunguzi.
Dkt Kihongole ambaye ni mratibu wa tiba asili na tiba mbadala alisema,kutokana na tatizo kubwa la kifua kikuu katika jamii yetu Serikali imeona umuhimu wa kuwatambua na kuwashirikisha waganga hao katika kampeni yake ya kutokomeza TB ifikapo mwaka 2035.
Alieleza kuwa, lengo la kuwashirikisha waganga hao ni baada ya kubaini asilimia sitini kati ya mia moja ya Watanzania wanaamini na kukimbilia kwa waganga hao kupata matibabu kulingana na shida walizo nazo na asilimia arobaini tu ndiyo wanaofika Hospitali.
Alisema, moja kati ya mkakati wa Serikali katika kutokomeza TB ni kushirikiana na waganga ambao utasaidia kuwahisi wale wenye vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu na kuwapa rufaa kwenda Hospitali kwa ajili ya matibabu zaidi badala ya kuwakumbatia jambo ambalo ni hatari kubwa kwa maisha ya waganga wenyewe na watu wengine.
Aidha Kihongole,amewataka waganga hao kuacha kufanya shughuli zao kwa kujificha bali wafanye katika mazingira rafiki, bora na safi ili kufikiwa kwa urahisi na watu wengi zaidi.
Alieleza wananchi waliokutwa katika Kilinge hicho kuwa, tiba asili ni salama kwani ilianza kutumiwa tangu enzi za Yesu Kristo na kuwataka viongozi kuanzia ngazi ya kijiji kuweka utaratibu mzuri utakao wezesha vijiji vyao kupata fedha kutokana na uchimbaji mizizi na miti dawa inayotumika kwa ajili ya tiba, badala ya kuwaachia waganga na watu kutoka nje ya wilaya hiyo wakinufaika na rasilimali za mitidawa inayopatikana kwa wingi katika wilaya ya Tunduru.
Mmoja wa Waganga wa tiba asili Hausi Mohamed(Babu Manjenje), ambaye ni mingoni mwa waganga waliopata mafunzo ya kuwaibua wagonjwa wa kifua kikuu, ameishukuru Serikali kwa kuwatambua na kuona umuhimu wa kushirikisha katika kampeni ya kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu.
Alisema, kuna watu wengi wenye shida mbalimbali wanaofika katika Vilinge vyao kwa ajili ya kupata tiba, hivyo uamuzi wa Serikali kuwatumia waganga katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo utasaidia kuokoa maisha ya Watanzania wengi ambao wako hatarini kupoteza maisha kwa ugonjwa wa TB huku baadhi yao wakihusisha maradhi yao na Imani za kishirikina.
Babu Manjenje alisema, waganga wa tiba asili katika wilaya hiyo wote kwa pamoja wamekubali kushiriki kikamilifu katika kampeni ya kutokomeza ugonjwa huo ili kuokoa maisha ya watu Watanzania wenzao ambao bado wanaendelea kutokana na kukosa tiba sahihi ya magonjwa yanayowasumbua.
Ameipongeza Hospitali ya wilaya kwa kutoa mafunzo kwa waganga kwani yatasaidia wao kuwatambua wagonjwa wenye viashilia vya ugonjwa huo wanaofika katika vilinge kupata tiba na kusisitiza kuwa,mafunzo hayo yataepusha waganga wa tiba asili kuuwa watu wanaofika katika vilinge huku wakiwa na matatizo ambayo matibabu yake ni ya kitaalam.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇