Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imesema makumi ya Wanajeshi wa nchi hiyo walijeruhiwa na kupatwa na matatizo ya kisaikolojia kufuatia shambulizi la makombora la Iran dhidi ya kambi mbili za kijeshi za nchi hiyo huko Iraq mapema mwezi huu, licha ya utawala wa Washington hapo awali kudai kuwa hakuna askari wake hata mmoja aliyeuawa au kujeruhiwa katika shambulizi hilo
Katika kikao na waandishi wa habari mjini Washington jana Ijumaa, Jonathan Hoffman, msemaji wa Pentagon alisema, "askari 34 hivi sasa wanapatiwa matibabu kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kisaikolojia, msongo wa mawazo na madhara mengine ya ubongo kufuatia shambulizi la Iran la Januari 8. Wanane waliopelekwa Ujerumani wameletwa katika Hopitali ya Kijeshi ya Walter Reed (karibu na Washington) na wengine tisa wamebaki huko Ujerumani."
Maafisa wa Marekani wanaendelea kukiri hatua kwa hatua juu ya kujeruhiwa wanajeshi wa nchi hiyo na makombora ya Iran, licha ya hapo awali kukataa
Awali Kamandi ya Jeshi la Marekani Asia Magharibi (CENTCOM) ilidai kuwa askari 11 wa nchi hiyo waliojeruhiwa Iraq katika makombora ya Iran wanatibiwa mjini Landstuhl nchini Ujerumani na katika kambi ya Arifjan nchini Kuwait.
Masaa machache baada ya Iran kuvurumisha makombora na kupiga kambi mbili za Marekani nchini Iraq, Rais Donald Trump alijitokeza mbele ya vyombo vya habari na kudai kuwa, "ni furaha kuwatangazia Wamarekani kuwa hakuna askari wetu hata mmoja aliyeuawa au kujeruhiwa katika shambulizi la makombora la Iran nchini Iraq."
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇