Mlezi wa Mtandao wa kuwasaidia watoto wa kike kupata maendeleo ya Elimu (FAWE) Zanzibar Mama Shadia Karume amezitaka Jumuiya zisizo za kiserekali kuwasaidia watoto wa kike wanaoishi katika mazingira magumu ili kufikia malengo waliojiwekea.
Mama Shadya Karume aliyasema hayo huko Haileselassie Mjini Unguja wakati akifungua Mkutano wa Tisa wa Jumuiya hiyo.
Alisema kwamba kumpatia elimu mtoto wa kike ni msingi mzuri katika kulinda familia hivyo ni muhimu Taasisi za kiraia kushirikiana na Serikali kuwapatia elimu hasa masomo ya Sayansi na Teknolojia ili waweza kujitegemea na kujikwamua katika hali ngumu yamaisha.
Aidha alisema kuwa program ya Tuseme ni muhimu sana kwa wanawake kwani inawafanya watoto wa kike kujiamini na kuwasaidia katika kujieleza kuwa yeye ni nani na anataka nini .
Mama Shadia aliongeza kuwa masomo ya Sayansi yanawasaidia vijana kiuchumi na kijamii hivyo ameipongeza Jumuiya ya FAWE kwa kuanzisha program ya Stemp kwa wanaume na wanawake.
Mama Shadya alizishauri Taasisi za Kiraia kuisaidia Jumuiya hiyo na kuwataka vijana kujiunga na FAWE ili waweze kunufaika na elimu inayotolewa.
Mratibu wa Jumuiya ya FAWE Hinda Abdallah Ajmy alisema kuwa wameamua kuwashirikisha watoto wa kike wengi zaidi kuliko wanaume kutokana na woga walionao na itahakikisha inawasaidia kuwajengea uwezo wa kujiamini.
Alisema wamekuwa wakitoa ushauri kwa Wizara ya Elimu ili kuhakikisha kuwa mtoto wa kike anasaidiwa kupata elimu hata wale ambao uwezo wao wa kusoma ni mdogo kutokana na mazingira yasiyorafiki ya maisha.
Aidha alifahamisha kuwa wameanzisha mradi wa fadhili watoto mayatima na kuwasaidia watoto zaidi ya 200 wanaishi katika mazingira magumu wanume na wanawake Unguja na Pemba.
Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo Dkt, Mwatima Abdallah aliwaomba viongozi waliochaguliwa kuendelea kuwa na moyo wa kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu ili na wao wapate elimu.
Akitoa ushuhuda, mwanafunzi Amina Omar Kitwana kutoka Klabu ya Tuseme alisema kuwa mafunzo aliyopatiwa yamemsaidia kuwa na uwelewa kuweza kujiamini popote.
Sambamba na hayo wanafunzi ambao wamefadhiliwa kimasomo na FAWE wameahidi kuyafanyia kazi waliyoyaahidi wakati walipotaka ufadhili huo.
Fawe imenzishwa mwaka 1998 na ina wanachama 140 kutoka Unguja na Pemba ambapo Kauli mbiu ni FAWE ZANZIBAR KUWA KARIBU NA WASHIRIKI WA MAENDELEO KUMUENDELEZA MTOTO WA KIKE KIELIMU.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇