LATEST HEADLINES👉

Your Ad Spot

Jan 26, 2020

PENTAGONI YAKIRI MAKUMI YA ASKARI WA MAREKANI KUPATWA NA MADHARA KATIKA SHAMBULIO LA MAKOMBORA LA IRANI

Japokuwa Rais Donald Trump wa Marekani amedai kuwa shambulio hilo halikuua au kujeruhi mtu yeyote lakini sasa Washington inakiri taratibu na hatua kwa hatua kwamba wanajeshi wake walijeruhiwa katika shambulio hilo. 
Kuhusiana na suala hilo Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) imekiri kuwa, makumi ya askari wa nchi hiyo walijeruhiwa na kupatwa na matatizo ya kisaikolojia kufuatia shambulizi la makombora la Iran dhidi ya kambi mbili za kijeshi za nchi hiyo huko Iraq mapema mwezi huu. Jonathan Hoffman, msemaji wa Pentagon alisema, "askari 34 hivi sasa wanapatiwa matibabu kutokana na kukabiliwa na matatizo ya kisaikolojia, msongo wa mawazo na madhara mengine ya ubongo kufuatia shambulizi la Iran la Januari 8. Wanane waliopelekwa Ujerumani wameletwa katika Hopitali ya Kijeshi ya Walter Reed (karibu na Washington) na wengine tisa wamebaki huko Ujerumani." Hii ni katika hali ambayo kabla ya Marekani kukiri uhakika huo, Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo, Mark Esper alikuwa amekwepa kutoa taarifa na takwimu sahihi kuhusu hasara na maafa yaliyosababishwa na shambulio la makombora la Iran. Awali Rais Donald Trump alikuwa amewaambia waandishi wa habari kwamba: "Nimesikia kuwa, wanajeshi hao walikuwa wakisumbuliwa na maumivu ya kichwa na matatizo mengine. Kitu ambacho naweza kueleza na kukitolea taarifa ni kwamba, hakukuwa na tatizo kubwa." Awali Trump alidai kuwa, hakuna mwanajeshi wa Marekani aliyedhurika katika shambulio la makombora la Iran huko Ain al Asad. 
Ikiwa zimepita siku kadhaa sasa tangu kutekelezwa shambulio hilo, Pentagon kwanza kabisa ilikuwa imekiri kuwa wanajeshi wasiopungua 16 walijeruhiwa kwenye shambulio hilo. Kamandi ya wanajeshi magaidi wa Marekani katika eneo la magharibi mwa Asia maarufu kwa jina la CENTCOM  pia ilitangaza kupitia taarifa yake kwamba wanajeshi 11 wanahitaji kupata matibabu nje ya Iraq. 
Takwimu mpya zilizotolewa na Pentagon kuhusiana na kadhia hii zinaonesha kuwa, kinyume na madai ya awali ya Trump, idadi kubwa ya wanajeshi wa Marekani wamepatwa na madhara tena makubwa kulikko ilivyosemekana hapo awali. Ili kulinda "hadhi" ya Marekani, Trump amefanya jitihada za kuficha na hata kukana ukweli wa hasara zilizosababishwa na shambulizi la makombora ya Iran katika kambi ya Ainul Asad, mashambulizi ambayo yanatambuliwa kuwa ya kwanza ya jeshi la nchi nyingine kulenga kambi ya jeshi la Marekani tangu baada ya Vita vya Pili vya Dunia.
Sababu nyingine iliyomfanya Donald Trump afiche hasara zilizosababishwa na mashambulizi ya makombora ya Iran huko Ainul Asad ni kuepuka kuingia kwenye vita ya moja kwa moja na Iran; suala ambalo lingekuwa na madhara makubwa sana kwa serikali ya Washington na washirika wake. Pamoja na hayo mienendo ya Trump kuhusiana na kadhia hii inaendelea kukosolewa sana hususan na Wademocrati. Akizungumzia suala la kuongezeka idadi ya askari wa Marekani waliojeruhiwa katika shambulizi la makombora ya Iran huko Ainul Asad, seneta wa chama cha Democratic, Chris Murphy, ameelezea uongo uliofanywa na serikali ya Trump kuhusu hasara iliyoipata kambi hiyo ya kijeshi ya askari wa Marekani na kusema: "Hakuna mtu anayeweza kupelekwa Ujerumani kwa matibabu eti kwa sababu tu ya kuumwa kichwa, bali watu wanapelekwa Berlin wakiwa na hali mbaya sana."
Murphy amuumbua Trump
Seneta Elizabeth Warren wa chama cha Democtatic ambaye pia anawania tiketi ya chama hicho kwa ajili ya kugombea urais mwaka huu wa 2020 amekemea sera za Trump za kuficha hasara zilizosababishwa na shambulizi la makombora ya Iran huko Ainul Asad na kusisitzia ulazima wa kukomeshwa vita vya Marekani. Ameandika kwenye mtandao wa Twitter kwamba: "Trump amechochea mapigano na Iran kisha ameficha na kudogesha majeraha na hasara walizopata wanajeshi wetu. Suala hili linatisha sana.."
Kutolewa kiduchu kiduchu na hatua kwa hatua takwimu za hasara zilizosababishwa na shambulizi la makombora ya Iran dhidi ya kambi kubwa zaidi ya jeshi la Marekani nchini Iraq ni kielelezo cha jinsi serikali ya Donald Trump inavyofanya kila iwezalo kuficha hasa za shambulizi hilo. Joe Biden anayetarajiwa kuwakilisha chama cha Democratic katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa rais wa Marekani baadaye mwaka huu pia amekosoa jitihada za Trump za kutaka kuficha hasara zilizosababishwa na shambulizi hilo na kusema: "Hatua ya Trump ya kujaribu kulidhihirisha jambo hilo kuwa ni dogo inatia kichefuchefu."
Joe Biden
Hapana shaka kuwa, siku za usoni zitafichua mengi zaidi kuhusu hasara za kipigo hicho, na kadhia hii itaendelea kuwa fedheha kubwa kwa Trump hususan katika kampeni za uchaguzi wa rais zitakazojikita katika kufichua uongo unaosemwa na kiongozi huyo kuwahadaa Wamarekani. 

No comments:

Post a Comment

MAONI (COMMENTS)👇

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages