Walimu nchini Kenya waingiwa na kiwewe cha mashambulio ya wanamgambo wa al-Shabab
Jan 15, 2020 12:42 UTC
Wasiwasi wa walimu huo umekuja siku chache baada ya watu wanaosadikiwa kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la al-Shabab kuwashambulia na kuwauwa wenzao wanne na kuwajeruhi wengine kadhaa mwishoni mwa wiki iliyopita katika Kaunti ya Garissa.
Chama cha Walimu nchini Kenya (KNUT) nacho kimetoa wito kikiitaka serikali ya Kenya kuchukua hatua madhubuti ili kuwahakikishia usalama wa walimu hao.
Shambulizi lililofanywa na wanagmabo wa al-Shabab dhidi ya Shule ya Msingi ya Kamuthe katika Kaunti ya Garissa, limezua hasira na wasiwasi mkubwa miongoni mwa walimu katika eneo hilo linalopakana na nchi ya Somalia. Gavana wa Garissa, Ali Korane amevitaka vyombo vya usalama kuimarisha ulinzi katika eneo hilo.
Kundi la kigaidi la al-Shabab ni tawi la mtandao wa kigaidi al-Qaeda nchini Somalia na limefanya mashambulizi mengi ya kigaidi katika nchi jirani ya Kenya likilenga idara za serikali, askari, magari ya abiria na mahoteli.
Mauaji ya kigaidi katika Chuo Kikuu cha Garissa, ni shambulio kubwa zaidi kuwahi kufanywa nchini Kenya na wanamgambo hao tangu mwaka 1998. Watu 148 waliuwa wengi wao wakiwa wanafunzi wa chuo hicho katika shambulio hilo la kivamizi la al-Shabab la Aprili Pili mwaka 2015
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇