Duru za habari nchini Afghanistan zimearifu kwamba wanachama 38 wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) wamejisalimisha kwa maafisa usalama wa serikali ya nchi hiyo, katika jimbo la Nangarhar, mashariki mwa nchi.
Wizara ya Ulinzi ya Afghanistan imesema kuwa, baadhi ya magaidi wa kundi hilo wenye uraia wa Pakistan wamejisalimisha kwa jeshi hilo kupitia operesheni ya maafisa usalama iliyofanyika katika mji wa Achin wa jimbo hilo. Hii ni katika hali ambayo Shah Mahmood Miakhel, gavana wa jimbo la Nangarhar amewaambia waandishi wa habari kwamba magaidi wengine 29 wa kundi hilo maarufuu kwa kutenda jinai, wamejisalimisha katika mji wa Jalalabad, ambao ndio makao makuu ya jimbo hilo. Kwa upande wake Masood Andrabi, Kaimu Waziri wa Mambo ya Ndani wa Afghanistan akiwa katika sherehe za kumtambulisha kamanda mpya wa polisi wa jimbo la Nangarhar ameelezea kushindwa kundi hilo la ukufurishaji na kusema kuwa, asilimia 95 ya maeneo ya jimbo hilo yamekombolewa kutoka mikononi mwa wanachama wa kundi hilo.
Katika upande mwingine Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afghanistan imetoa taarifa ya kugunduliwa na kuteguliwa mabomu 50 katika makao makuu ya jimbo la Sar-e Pol kaskazini mwa nchi hiyo. Hii ni katika hali ambayo jeshi la polisi mjini Herat limetangaza kutokea miripuko miwili ya mabomu katika mji wa Pashtun Zarghun jimboni humo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇