Kauli hiyo ameitoa wakati akijaribu kutuliza hofu ya jumuia ya kimataifa kuhusu kuongezeka mvutano unaohofiwa unaweza kuzidisha mzozo kati ya Marekani na Iran.
Akizungumza katika mkutano wa pamoja na waandishi habari na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, katika mji wa Sochi, Urusi, Pompeo amesema Marekani haitafuti vita na Iran na kwamba Marekani imeweka bayana kwamba iwapo Iran itatishia maslahi ya nchi hiyo, basi kitisho hicho bila shaka kitajibiwa kwa njia inayoeleweka.
''Tunaitaka Iran ifanye mambo yake kama nchi ya kawaida, hilo ndilo tunaloliomba. Tumeweka shinikizo katika uongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili kulifanikisha hilo. Kimsingi hatutafuti vita na Iran,'' alisema Pompeo.
Pompeo amesema kuwa jana alizungumza na Lavrov na siku ya Jumatatu mjini Brussels, Ubelgiji alizungumza na washirika wake wa Ulaya kuhusu kitisho ambacho Marekani inakiona kutoka kwa Iran.
Matamshi yake yametolewa baada ya Marekani kupeleka manowari ya kubeba ndege za kivita pamoja na ndege za mashambulizi aina ya B-52 katika eneo la Mashariki ya Kati, ingawa Rais Donald Trump amekanusha taarifa kwamba anafikiria kuwapeleka wanajeshi 120,000.
Akizungumza na DW mjini Brussels, mjumbe wa Marekani kwa ajili ya Iran, Brian Hook amesema Ulaya ina dhamana ya kuhakikisha kuwa eneo la Mashariki ya Kati lina amani na utulivu.
Iran na kitisho cha mashambulizi
Hook amefafanua kuwa Iran imekuwa ikitishia kufanya mashambulizi, hivyo hawana budi kuchukua hatua za kujihami. Amesema tatizo lililopo sasa ni kwamba imekuwa vigumu kuifikiria Mashariki ya Kati yenye amani, bila ya kuiwaza Iran yenye amani, na hivyo wanaisihi Iran kuwa kama taifa la kawaida lenye utulivu.
Wakati huo huo, kiongozi wa juu kabisa wa Kidini nchini Iran, Ayatollah Ali Khamenei, amesema hakuna vita vyovyote na Iran wala mazungumzo mapya na Marekani na kwamba suala hilo haliwezi kutokea.
Akizungumza kupitia televisheni ya taifa ya Iran, Khamenei amesema Iran imechagua njia hiyo ambayo ina uhakika kwamba mwisho wa siku itaibuka mshindi. Kiongozi huyo wa kidini amesema wana nia thabiti na imani kubwa ya kidini.
Mvutano kati ya Iran na Marekani uko juu na Rais wa Iran, Hassan Rowhani alisema wiki iliyopita kwamba nchi yake itaanza kujiondoa kwenye baadhi ya vipengele kutoka katika mkataba wa nyuklia uliofikiwa mwaka 2015 kati ya mataifa yenye nguvu duniani na Iran, ambayo yalidhibiti shughuli zake zenye utata za nyuklia.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇