Kiongozi mmoja katika jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa manowari ya USS Abraham Lincoln ya Marekani imesimamishwa katika Bahari Arabu na haijafika katika Ghuba ya Uajemi na kwamba askari wake wameondolewa ndani ya meli hiyo ya kubeba ndege za kivita.
Kwa mujibu wa habari hiyo, eneo la Ghuba ya Uajemi litaendelea kutokuwa na manowari hiyo. Ripoti kutoka kituo cha mawasiliano na taarifa za kiulinzi cha jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, imesema kuwa afisa mmoja jeshini amefafanua harakati za kijeshi za Marekani katika eneo na kuongeza kuwa harakati hizo zilikuwa na lengo tu la kulinda majeshi yake katika eneo hili. Amebainisha kwamba masuala mengine yaliyotajwa na White House 'yaani operesheni za kisaikolojia za adui' yalikuwa na lengo la kuathiri fikra za walio wengi ndani na nje ya Marekani. Amesema kuwa kwa mujibu wa taarifa za upelelezi na kijeshi, kile ambacho kimekuwa kikitangazwa na vyombo vya habari vya adui na baadhi ya serikali rafiki za Marekani, kuhusiana na harakati za kijeshi za nchi hiyo katika eneo la Asia Magharibi, kimsingi hakina ukweli wowote na badala yake ni kwamba Washington ilikuwa na lengo la kulinda askari wake walioko katika eneo kutokana na hatari tarajiwa na si kitu kingine.
Afisa huyo amebainisha kuwa, udhaifu wa Wamarekani na nchi washirika wake katika kuanzisha harakati zozote za kijeshi dhidi ya Iran umebainika wazi katika misimamo ya viongozi wa nchi hizo ambapo mara kadhaa wamekiri kuwa, hawana nia ya kuingia vitani na Iran, lakini suala hilo limekuwa likitumiwa katika mbinu za operesheni za kisaikolojia. Afisa huyo wa jeshi la Iran amesisitiza kuwa, kiuhalisia Washington haina nia yoyote ya kuingia vitani kutokana na udhaifu ilionao na kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama nchi yenye usalama na amani, haijawahi kuanza vita na haitoanzisha vita, lakini jeshi la nchi hii limejiweka imara kwa ajili ya kukabiliana na njama zozote kama ambavyo litaendelea kujiimarisha na kujiweka tayari na kwamba Marekani na washirika wake wanalifahamu vyema suala hilo.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇