Shirika la Kimaendeleo la Kusini mwa Afrika – SADC- limeitaka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ihesabu tena upya kura za uchaguzi wa rais kufuatia utata ulioibuka.
Mgombea urais ambaye ametangazwa kushika nafasi ya pili, Martin Fayuli anadai kuwa alipata ushindi wa kishindo katika uchaguzi na kwamba aliyetangazwa mshindi, Felix Tshisekedi, alifikia mapatano ya siri na Rais Joseph Kabila ili atangazwe mshindi. Tshisekedi na Kabila wamekanusha tuhuma hizo.
Katika taarifa SADC imesema kuna haja ya kuhesabu upya kura za uchaguzi huo wa Disemba 30 ili kuwapa hakikisha washindi na washindwa.
SADC, ambayo inajumuisha waitifaki wa Rais Kabila kama vile Angola na Afrika Kusini, imependekeza kuundwe serikali ya umoja wa kitaifa inayowajumuisha vyama vya Kabila, Fayulu na Tshisekedi ili amani idumu nchini humo. SADC imewataka wanasiasa wa Kongo waangazia namna serikali za umoja wa kitaifa zilivyoundwa katika nchi kama vile Kenya, Afrika Kusini na Zimbabwe.
Fayulu, ambaye anaungwa mkono na mahasimu wa Kabila, siku ya Jumamosi aliwasilisha kesi katika Mahakama ya Katiba mjini Kinshasa kwa lengo la kulalamikia matokeo ya uchaguzi.
Tume ya Uchaguzi ilimtangaza Tshisekedi mshindi, kwa kupata asilimia 38.57 ya kura zote zilizopigwa huku Fayulu akiwa wa pili kwa asilimia 34.8.
Mgombea wa chama tawala Emmanuel Ramazani Shadary, aliambulia asilimia 23.8
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇