Wawakilishi wa bunge la Afghanistan na waangalizi wa uchaguzi, wamekosoa hatua ya kucheleweshwa kutangazwa matokeo ya uchaguzi huo.
Ali Akbar Ismi, mwakilishi wa bunge na naibu mkuu wa kamisheni ya masuala ya ulinzi katika bunge la Afghanistan amesema kuwa, wafanyakazi kadhaa wa tume huru ya uchaguzi nchini humo wametapakaa ufisadi na kwamba wamehusika na kuwaomba hongo wagombea. Ameongeza kuwa ufisadi wa kifedha katika tume hiyo ya uchaguzi pia umesababisha kucheleweshwa kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa bunge katika baadhi ya majimbo. Naye Marwah Amini, msemaji wa idara ya ndani inayoshughulikia uangalizi wa uchaguzi nchini Afghanistan, amesema kuwa kurefushwa mwenendo wa kutangazwa matokeo ya uchaguzi uliopita, kunahusiana na ufisadi wa kifedha. Kadhalika Abdullah Qarlake, mwakilishi wa bunge la Seneti nchini humo anaamini kwamba uchakachuaji uliopindukia na udhaifu katika kusimamia uchaguzi wa bunge ukiwemo wa Kabul, mji mkuu wa nchi hiyo, umesababisha tume huru ya uchaguzi ishindwe kutangaza matokeo hayo wakati uliopangwa.
Kucheleweshwa kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa bunge ambako kumechukua kipindi cha miezi mitatu sasa tangu kujiri zoezi hilo, kumeibua ukosoaji mkubwa kutoka kwa shakhsia mbalimbali nchini humo. Madai ya baadhi ya wawakilishi wa bunge nchini Afghanistan juu ya watumishi wa tume ya uchaguzi kuomba rushwa yanajiri katika hali ambayo ufisadi ni moja ya changamoto kubwa zinazotajwa kuuathiri mfumo mzima wa utawala nchini humo. Kwa kuzingatia uzito uliopo kuhusiana na uchaguzi na matokeo yake katika kila mfumo wa kisiasa, kutuhumiwa watumishi wa tume huru ya uchaguzi nchini Afghanistan kuomba rushwa ili kutoa matokeo, ni suala linalotoa udharura wa kuchunguzwa tume huru ya uchaguzi ya Afghanistan na asasi za uangalizi na vyombo vya mahakama ili kuishtaki au kuisafishia jina tume hiyo. Mbali na kuwa, kutangazwa matokeo ya uchaguzi kumechukua muda mrefu sambamba na kuibua wasiwasi katika uga huo, suala hilo pia limewapelekea wananchi kutilia shaka suala zima la demokrasia na chaguzi nchini humo. Hasa kwa kutilia maanani kwamba, hivi sasa Afghanistan imbayo ilikuwa inajiandaa kwa ajili ya uchaguzi ujao wa rais ambao ulikuwa umepangwa kufanyika mwezi Aprili mwaka huu, sasa itasubiri zaidi kabla ya kushiriki zoezi hilo kwa kuwa uchaguzi huo umecheleweshwa kwa miezi mitatu mingine.
Kuhusiana na suala hilo, Samiullah Saihun, mtaalamu wa masuala ya kisiasa wa Afghanistan anasema, "kucheleweshwa kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa bunge, kunauvunjia itibari mwenendo wa demokrasia nchini Afghanistan." Mwisho wa kunukuu. Aidha kucheleweshwa kutangazwa matokeo ya uchaguzi wa bunge, kunaweza kupelekea pia kupungua ushiriki wa wananchi katika uchaguzi ujao wa rais. Ucheleweshaji wenye kuibua maswali kuhusiana na uchaguzi nchini Afghanistan na pia hali isiyo ya kawaida katika kutangaza matokeo na ambayo bado inaendelea, imesababisha kuporomoka itibari ya uchaguzi na pia ushiriki wa wananchi katika kuainisha mustakbali wa taifa lao. Inatazamiwa kwamba viongozi wa serikali na asasi nyingine za nchi hiyo, hazitaacha kuangalia upya mwenendo wa usimamizi na utekelezaji wa mfumo wa uchaguzi nchini, suala ambalo ni lenye umuhimu mkubwa. Katika hatua nyingine uamuzi uliotangazwa hivi karibuni wa kufanyika uchaguzi wa rais ujao ambao umeelezwa kwamba umetokana na mashinikizo ya Wamagharibi hususan Marekani, licha ya kwamba umekabiliwa na ukosoaji mkubwa wa vyama vya siasa na kutambuliwa na fikra za walio wengi kuwa unaenda kinyume na katiba ya nchi hiyo, umetathminiwa kuwa unaopingana na maslahi ya taifa la Afghanistan.
No comments:
Post a Comment
MAONI (COMMENTS)👇